Monday, October 28, 2013

MLINZI WA AMANI MTANZANIA APOTEZA MAISHA DRC


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ametuma salam za rambirambi kwa Familia na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Mlinzi wa Amani Mtanzania ambaye amepoteza maisha siku ya jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la waasi la M23 katika eneo la Kiwanja- Rushuru kilimita 25 magharibi ya mji wa Goma. katika shambulio hilo, Mlinzi mwingine ambaye pia ni Mtanzania amejeruhiwa. kumekuwapo na mapigano kati ya Majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na Kundi la M23.

Luteni Rajabu Ahmad Mlima Enzi ya Uhai Wake


Na Mwandishi Maalum

Kwa   mara nyingine  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon, amelaani vikali  tukio la kuuawa kwa mwanajeshi  wa kitanzania  aliyekuwa akihudumu katika Misheni ya  Umoja wa Mataifa ya  Kutuliza Amani katika Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).

Kifo cha mwanajeshi huyo mtanzania   kimetokea jana jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la M23 ambalo linapigana na majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya KONGO ( FARDC).

Katika salamu zake  rambirambi kwa  familia ya  marehemu  na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mkuu   huyo wa Umoja wa Mataifa, ameelaani vikali mauaji hayo na kuahidi kwamba  Umoja wa Mataifa utaendelea kutekeleza  majukumu yake ikiwa  ni pamoja na kuchukua  hatua   zote muhimu kuwalinda raia wa DRC.

“Ninalaani vikali mauaji ya  mlinda amani kutoka Tanzania ambaye alishambuliwa  na kundi la M23 katika eneo la    Mashariki ya  DRC, ninatoa  salamu zangu za  rambirambi kwa familia ya marehemu,  na  kwa Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania ” ananukuliwa Katibu Mkuu akisema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika  Umoja wa Mataifa,   siku  ya jumapili , zinaeleza kwamba Mlinzi huyo wa  amani aliyepoteza maisha  na ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa   anacheo cha  Luteni na kwamba alishambuliwa wakati  kikosi chake kikiwa katika harakati za kutoa ulinzi wa  raia katika eneo la Kiwanja- Rutushura  kilomita 25 kutoka  Magharibi mwa  mji wa Goma.

Katika mashambuli hayo mlinzi mwingine wa amani ambaye pia ni mtanzania amejeruhiwa.

 Aidha  taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  inaeleza kwamba Umoja wa Mataifa utachukua  hatua zote muhimu kwa mujibu wa Azimio namba 2098 ( 2013 )  kutimiza wajibu wake .

Ni kupitia Azimio hilo ambalo lilipitishwa mwezi Marchi  mwaka huu,  Baraza  Kuu la Usalama liliridhia kuanzishwa kwa Brigedi Maalum ( FIB) ambayo pamoja na mambo mengine imepewa  jukumu la kutumia nguvu pale inapobidi ikiwa  ni pamoja na kuwapokonya silaha makundi ya wanagambo wenye silaha likiwamo kundi  hilo la M23 na makundi mengine ambayo yamekuwa yakiendesha mapigano na machafuko katika DRC.

Mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya majeshi  ya serikali ya Kongo na kundi la M23 yamefuatia kuvunjia hivi  karibuni  kwa mazungumzo ya  Kampla  yaliyokuwa yakiendelea  kati ya pande  mbili. Hali inayolifanya eneo hilo la Mashariki ya Kongo kuzidi  kuwa tete.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.