Sunday, December 31, 2023
Wednesday, December 27, 2023
UMOJA WA MABALOZI WA AFRIKA WAKABIDHI MSAADA HANANG
Umoja wa Mabalozi wa nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania wamekabidhi msaada wa mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba kwa wananchi waliokumbwa na mafuruko na maporomoko ya udongo katika eneo la Katesh Wilayani Hanang mkoa wa Manyara.
Akikabidhi msaada huo kwa Serikali, Kiongozi wa Mabalozi hao na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed amesema kundi la Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao Tanzania lina mabalozi 24 ambao wameonesha kuguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kuona ni vyema kuwasaidia wananchi hao pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji.
Dkt. El Badaoui Mohamed amesema umoja wa Mabalozi wa Afrika nchini wameguswa na mafuriko yaliyotokea Katesh na kwa umoja wao wamechangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo la Katesh ili kurejesha makazi ya wananchi hao.
“Tunaendelea kuomba Mungu awajalie subira na kwa wale waliopoteza maisha wapumzike kwa amani. Kadhalika, kwa waliosalia basi msaada huo utawasaidia kujenga makazi yao na kuendelea na maisha kama ilivyokuwa awali,” alisema Dkt. El Badaoui Mohamed
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Serikali amewashukuru mabalozi hao kwa umoja wao na kwa msaada huo ambao utasaidia kurejesha makazi ya wananchi wa Katesh.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa baada ya kupokelewa utaratibu utafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa ili mifuko hiyo iwasilishwe katika Kijiji cha Katesh, Wilayani Hanang.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu, baada ya kutokea kwa maafa yale sote tunajua Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha maisha ya watu yanarejea katika hali ya kawaida. Msaada huu utasaidia katika ujezi wa nyumba zilizoathiriwa na mafuriko hayo,” alisema Mhe. Balozi Mbarouk.
Balozi Mbaorouk amesema msaada huo ni uthibitisho kwamba uhusiano kati ya Balozi zote zilizopo nchini hususan Balozi za Afrika ni mzuri na kwa msaada huo wameonesha ushirikiano mkubwa na Serikali ya Tanzania.
Tarehe 02 Disemba 2023 eneo la Katesh, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, lilikumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha vifo vya watu 89, kujeruhi wakazi wa eneo hilo na kuharibu makazi na mazao yao
Msaada huo walioukabidhi kwa Serikali ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa, tarehe 7 Disemba 2023, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba alipokutana na Jumuiya ya wana diplomasia nchini ili kuwapa taarifa rasmi ya Serikali juu ya tukio hilo na hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya kutokea kwa maporomoko ya tope kutoka mlima Hanang kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Mkoani Manyara tarehe 02 Disemba, 2023.
Thursday, December 21, 2023
TANZANIA YASAINI MKATABA MPYA WA UBIA NA NCHI ZA OACPS, EU
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na Mwakilishi kwenye Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) Mhe. Jestas Abuok Nyamanga, akisaini kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkataba Mpya wa Ubia baina ya Nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya (Mkataba wa Samoa). Hafla ya kusaini Mkataba huo ilfanyika tarehe 19 Desemba 2023 katika Makao Makuu ya OACPS Brussels Ubelgiji. Wanaoshuhudia tukio hilo ni maafisa waandamizi kutoka Sekretarieti ya OACPS na Umoja wa Ulaya. |
Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) Dkt. Ibrahim Richard akimpa mkono kumpongeza Mhe. Balozi Jestas Abuok Nyamanga baada ya kusaini mkataba huo kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wednesday, December 20, 2023
BALOZI MBAROUK ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO UBALOZI WA KUWAIT
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Kuwait Jijini Dar es Salaam kufuatia kifo cha Amir wa Kuwait, Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah.
Kiongozi huyo alifariki tarehe 16 Disemba 2023 akiwa na umri wa miaka 86 ambapo aliongoza taifa hilo kwa miaka mitatu iliyopita.
Balozi Mbarouk ametoa salamu za pole za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Alsehaijan ambapo amemuelezea kiongozi huyo atakumbukwa daima kama mwanadiplomasia na kiongozi imara aliyejitolea maisha yake katika masuala ya amani.
“Kiongozi huyo atakumbukwa kama kiongozi mahiri wa Kuwait aliyeimarisha ushirikiano wa karibu kati ya Kuwait na Tanzania,” alisema Balozi Mbarouk.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapenda kutoa salamu zetu za pole kwa wananchi wa Kuwait kwa kuondokewa na kiongozi bora na mpenda amani. Roho yake Ipumzike mahali pema peponi,” aliongeza Mhe. Balozi Mbarouk
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Daima Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itamkumbuka Hayati Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah kama kiongozi imara na aliyependa amani.
Sunday, December 17, 2023
WAZIRI MAKAMBA ABAINISHA MAFANIKIO YA SERIKALI KWA MWAKA 2023 KUPITIA UTEKELEZAJI WA SERA YA MAMBO YA NJE
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ameainisha mafanikio yaliyopatikana kwa Taifa kutokana na utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine, kukua kwa biashara, uwekezaji na utalii na kuongezeka kwa ushawishi na sauti ya Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Mhe. Makamba ameanisha mafanikio hayo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2023 wakati akitoa Tathmini ya Mafanikio ya Wizara katika Kueneza, Kukuza na Kupanua Diplomasia ya Tanzania Kimataifa kwa mwaka 2023 pamoja na kutoa Mwelekeo na Matarajio ya Wizara kwa Mwaka 2024.
Mhe. Makamba amesema kuwa, Diplomasia ya Tanzania chini ya uongozi imara wa Mwanadiplomasia namba moja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali ambapo kupitia uratibu wa Wizara na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Tanzania katika kipindi cha mwaka 2023 imefanikiwa kuimarisha uhusiano ya uwili, kukuza biashara na uwekezaji, kuongeza ushawishi wa Tanzania katika masuala mtambuka yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa, kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati na kuongezeka kwa watalii.
Akifafanua kuhusu kuimarika kwa ushirikiano wa uwili kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na mashirika ya kimataifa, Mhe. Makamba amesema kupitia ziara mbalimbali zilizofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia, Viongozi Wakuu Serikalini na zile zilizofanywa na Marais na Wakuu wa Mashirika kutoka nje ya nchi hapa nchini zimeiwezesha Tanzania kunufaika kiuchumi kwa kuimarika zaidi kwa ushirikiano na nchi hizo pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa.
Kadhalika amesema kuimarika kwa ushirikiano huo kumeiwezesha Tanzania katika mwaka 2023 kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa ukiwemo Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mifumo ya Uzalishaji wa Chakula na Mkutano wa Kimataifa kuhusu masuala ya Rasilimali Watu.
Pia amesema Wizara imefanikiwa kuratibu Mikutano ya Tume ya Pamoja kati ya Tanzania na nchi mbalimbali zikiwemo Algeria, Comoro, Finland na Indonesia. Kupitia mikutano hiyo, Tanzania ilifanikiwa kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Kuhusu kukua kwa biashara na uwekezaji nchini, Mhe. Makamba amesema takwimu zinaonesha kwa kiasi kikubwa kazi imefanyika ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia ameongoza ushiriki wa Tanzania kwenye makongamano mbalimbali ya biashara na uwekezaji ikiwemo Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na India, Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Zambia pamoja na kuelekeza kufanyika kwa makongamano mbalimbali likiwemo lile la Tanzania na Uholanzi na Tanzania na Ufaransa yaliyomshirikisha Mhe. Waziri Makamba.
“Kwenye kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchini mbalimbali, takwimu zinaonesha kazi imefanyika kwa umahiri mkubwa. Mhe. Rais ameongoza kazi hii kama mwanadiplomasia namba moja na kushiriki kwenye makongamano ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India, Tanzania na Zambia lakini pia ameelekeza kufanyika kwa makongamano mengine ambayo tumeshiriki baadhi yetu sisi, Tanzania na Uholanzi, Tanzania na Ufaransa na Tanzania na Ungereza” amesisitiza Mhe. Makamba.
Mhe. Makamba pia amesema kuwa, Tanzania imefanikiwa kupanua masoko ya bidhaa zake mbalimbali duniani ikiwemo kupatikana kwa soko la Mbaazi na Korosho nchini India na Vietnam na Mkonge nchini China na Brazil na Maparachichi nchini China na nchi za Ulaya. Amesema kupanuka kwa masoko ya bidhaa hizo kutaongeza uzalishaji, ajira na kipato na hatimaye kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kuhusu utafutaji fedha za kugharamia miradi ya maendeleo hapa nchini, Mhe. Waziri Makamba amesema jukumu hili limetekelezwa kikamilifu ambapo kupitia mawasiliano yaliyofanyika kati ya Tanzania na Mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayotoa misaada na mikopo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mfuko wa Kuwait, Shirika la Fedha Duniani na mengine yamefanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Waziri Makamba amesema kutokana na kazi za nzuri inayofanywa na Mwanadiplomasia namba moja, Mhe. Rais Dkt. Samia sauti na ushawishi wa Tanzania katika masuala mtambuka imeendelea kusikika huku akitoa mfano wa Mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Mambadiliko ya Tabianchi uliofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Desemba 2023 ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia alifanikisha kufanyika kwa mkutano wa pembezoni kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepuka ukataji wa miti hovyo.
Kadhalika amesema kutokana na Diplomasia ya Tanzania kuimarika, Mhe. Rais Dkt. Samia ameteuliwa kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo kuwa Championi wa Dunia kwenye masuala ya usawa wa kijinsia.
Pia Mhe. Makamba amesema kuwa, Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefanikiwa kuimarisha ujirani mwema na nchi mbalimbali, jumuiya za kikanda na kudumisha amani na usalama katika kanda.
“Tanzania ni mwenyekiti ajaye wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia nafasi hii Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika kuimarisha amani na usalama katika kanda hii” amesema Mhe. Makamba.
Akielezea mwelekeo na matarajio ya Wizara kwa mwaka 2024, Mhe. Makamba amesema Wizara itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayosisitiza katika Diplomasia ya Uchumi; Kukamilisha uandaaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ili iendane na mazingira ya sasa ya dunia; kukamilisha uratibu wa Hadhi Maalum kwa Diaspora; Kupanua uwakilishi wa Tanzania kwa kufungua Balozi mpya; Kuwa mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja; Kuratibu mikutano ya Tume za Pamoja za Ushirikiano na nchi mbalimbali; Kuandaa makongamano ya biashara kati ya Tanzania na nchi mbalimbali; Kuratibu na kuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya kikanda na kimataifa na kuratibu ziara za Mhe. Rais na Viongozi wengine wakuu wa Serikali.
Friday, December 15, 2023
TANZANIA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MAONESHO YA JUAKALI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Mjasiriamali kutoka Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza wa jumla kwenye Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Juakali yaliyomalizika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 15 Desemba 2023.
Mshindi wa pili ametokea Kenya huku mshindi wa tatu akitokea Uganda.
Mjasiriamali huyo, Dkt. Herieth Mkangaa maarufu kama Mama batiki ambaye
anamiliki Kampuni ya kutengeneza Batiki ya MoroBatiki ya mkoani Morogoro
ametangazwa mshindi wakati wa ufungaji rasmi wa Maonesho hayo ambayo
yamewashirikisha wajasiriamali 1,500 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Dkt. Mkangaa ni pia maarufu kwa kutengeneza vazi la batiki lililompatia
umaarufu la “Suti ya Samia” ikiashiria mtindo wa nguo unaopendelewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkanga amesema kuwa
amefurahia ushindi huo ambao ni mkubwa kwake na kwa Tanzania na kwamba tuzo
hiyo ni chachu kwake ya kuendelea kujituma zaidi na kutengeneza bidhaa nyingi
na zenye ubora ili kulikamata soko la Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa
ujumla.
Pia amewahamasisha wajasiriamali kote nchini kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara, masoko na uwekezaji zinazotangazwa na Serikali ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Wajasiriamali wawili wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar, Bw.
Abdul Kadir Amini Ahmed na Bw. Khamis Khamis Haji wanaojishughulisha na
utenegenezaji wa mikeka wamepongezwa na waandaji wa maonesho hayo kwa
kufanikiwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu licha ya hali ya ulemavu waliyo
nayo huku jamii ikitakiwa kuiga mfano wao wa kujituma katika kazi badala ya
kutegemea kuomba kusaidiwa.
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo
na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki”
hufanyika kila mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kutoka nchi moja kwenda nchi
nyingine ambapo maonesho ya 24 yanatarajiwa kufanyika nchini Sudan Kusini mwaka
2024.
Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya ufungaji wa maonesho hayo |
Jukwaa kuu |
Bi. Kisa akipokea zawadi ya mkeka mdogo kutoka kwa wajasiriamali wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar |
Kikundi cha ngoma maarufu ya Burundi wakitumbuiza wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo |
Shamrashamra za ushindi zikiendelea |