Friday, February 24, 2023

DKT. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 43 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa  43 wa Kawaida wa  Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 23 Februari 2023.

 

Mhe. Dkt. Tax ambaye ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama.

 

Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira;  taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.

 

Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni umuhimu wa kukitangaza Kiswahili  duniani kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli  rasmi za Jumuiya. 

 

Awali akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ezekiel Nibigira amesema kuwa Burundi kama mwenyekiti inaona fahari kuandaa Mkutano wa aina hiyo ambapo pia aliwakaribisha Mawaziri wenzake na washiriki wa Mkutano  huo nchini humo na kueleza kuwa nchi hiyo imeendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote.

                                                                                           

Mkutano huo ambao umefanyika kwa siku tano , ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama viilivyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Februari 2023.

 

Mbali na Mhe. Dkt. Tax ujumbe wa Tanzania pia uliwajumuisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda,  Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko,  Naibu Makatibu Wakuu akiwemo Bibi.  Amina Khamis Shaaban   Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

 

Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kutunga sera za Jumuiya, kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa program mbalimbali za Jumuiya kwa maslahi mapana ya Nchi Wanachama.

 

Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi saba za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (katikati) akichangia jambo wakati wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika hivi karibuni jijini Bujumbura, Burundi. Mhe. Dkt. Tax aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo.

Mhe. Dkt. Tax akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto)na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) wakati wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
 


Mwenyekiti wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki nchini Burundi, Mhe. Balozi Ezekiel Nibigira akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano huo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda (kulia) akishiriki Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bibi Amina Khamis Shaaban
Sehemu ya ujumbe wa Burundi wakishiriki mkutano
Ujumbe wa Uganda na Sudan Kusin katika mkutano
Ujumbe wa Kenya katika mkutano
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakishiriki Mkutano

Ujumbe wa Rwanda katika Mkutano
Mkutano ukiendelea
Awali Mhe. Dkt. Tax aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Pichani Mhe. Dkt. Tax akizungumza wakati wa kikao hicho kilichomshirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kushoto)
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda akichangia jambo wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Pichani Mawaziri. Kulia ni Balozi Sokoine
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kilichofanyika kabla ya kuanza Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifafanua jambo kuhusu agenda za Mkutano kwa Waheshimiwa Mawaziri (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya na katikati ni Mhe. Balozi Maleko
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Japhary Kachenje akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kabla ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Haji Janabi akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.

Kikao kikiendelea

Thursday, February 23, 2023

BALOZI FATMA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA QATAR

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. 

Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali hususani ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Qartar ambapo Balozi Fatma amemhakikishia Balozi wa Qatar kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Qatar kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo viwanda, biashara na uwekezaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akizungumza na Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimsikiliza Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na Balozi wa Qatar nchini Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

BALOZI MBAROUK ATETA NA NAIBU KATIBU MKUU WA HUDUMA ZA NJE – EU

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Nje za Umoja wa Ulaya (EU), Bi Helena Konig katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ambapo Balozi Mbarouk amemhakikishia Bi. Konig kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika nyanja za biashara na uwekezaji, utunzanji wa mazingira hususan uchumi wa buluu, nishati, miundombinu pamoja na ushirikiano wa kikandaa na kimataifa kwa maslahi ya pande zote mbili. 

“Napenda kukuhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika sekta za biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, nishati, miundombinu kwa maslaahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuimarisha maeneo muhimu hususan biashara na uwekezaji kwa kuwa sekta hiyo ni muhimu kwa kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Nje Umoja wa Ulaya, Bi. Konig amesema licha ya changamoto ya uviko 19 kuikumba Dunia na vita ya Urusi na Ukraine, Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Afrika, hususan Tanzania kuimarisha na kuendeleza sekta za biashara na uwekezaji.

“EU tunaendelea kushikamana na kuimarisha nguvu zetu kwa pamoja ili kuhakikisha tunaendelea kuwekeza na kukuza biashara kati yetu na Tanzania kwa maslahi ya mataifa  yote,” alisema Bibi Konig.

Viongozi hao pia wamejadili masuala ya jinsia, digitali, ulinzi na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kijamii na kisiasa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Nje za Umoja wa Ulaya (EU), Bi Helena Konig katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimsikiliza na Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Nje za Umoja wa Ulaya (EU), Bi Helena Konig wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Huduma za Nje za Umoja wa Ulaya (EU), Bi Helena Konig



SERIKALI YAWASIHI WAFANYABIASHARA KUJIFUNZA, KUBADILISHANA UZOEFU WA BIASHARA

Serikali imewasihi wafanyabiashara na wawekezaji nchini kutumia fursa ya Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kujifunza, kubadilishana uzoefu na mawazo ya kibiashara ili kukuza na kuchochea maendeleo ya uchumi. 

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipofungua Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam. 

“Nawasihi wafanyabiashara wa Tanzania, kutumia fursa hii adhimu kujifunza, kubadilishana uzoefu na mawazo ya kibiashara ili kupiga hatua kama wenzetu na muweze kukuza na kuchangia katika uchumi wa taifa letu,” alisema Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alisema Serikali ya Tanzania inatoa kipaumbele katika sekta kilimo kwa kuwa ni moja ya sekta ambazo zina mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa. 

“Serikali imetoa msukumo wa kipekee katika kujenga uchumi wa nchi kwa kuwekeza kwenye kilimo biashara ili kuifanya sekta ya kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,” alisema Dkt. Mpango

“Serikali imechagua kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja kwa vijana ambacho kinahitaji uwekezaji wa kisasa, tunalenga uwekezaji mkubwa wa kibiashara kwenye kilimo cha miwa, ngano, alizeti, mahindi, zabibu, matunda, mbogamboga, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji na ufugaji wa Samaki,”alisema Dk Mpango

Amesema Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa muda mrefu wa EU kwa Tanzania ambapo imenufaika na msaada kwa programu mbalimbali za ushirikiano wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tatu ikiwemo msaada wa kukabiliana na janga la Uviko -19.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji alisema Jukwaa hilo ni muhimu kwa Tanzania kwakuwa linatoa fursa ya wafanyabiashara kutoka pande zote kujadili fursa za biashara na uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili.

“Jukwa hii ni muhimu kwa sababu linatoa fursa kwa wafanyabiashara kujadili na kubadilishana mawazo ya kibiashara hususan katika sekta za kilimo, utalii, nishati, na madini, tehama, miundombinu, fedha na nyinginezo, na kuwawezesha wafanyabiashara kuchochea maendeo yao na mataifa yao kwa ujumla" alisema Dkt. Kijaji 

Jukwaa hilo limehudhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 700 kutoka Tanzania na Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya unaongoza kwa uwekezaji hapa nchini katika sekta mbalimbali ambapo imewekeza kiasi cha Euro milioni 344.23.

Jukwaa hilo pia limehudhuriwa na Mabalozi wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya ambao ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestus Nyamanga, balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Balozi Caroline Chipeta.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam


Sehemu ya washiriki wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya washiriki wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk pamona na viongozi wengine wakifuatilia Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam

Viongozi mbalimbali wakifuatilia jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam


VACANCY AT INTERNATIONAL COTTON ADVISORY COMMITTEE


 

Wednesday, February 22, 2023

MAKATIBU WAKUU WAKAMILISHA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 43 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika  jijini Bujumbura, Burundi.

 

Mkutano huo ambao umetanguliwa na mkutano wa Wataalam uliofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Februari 2023 umepokea na kupitia taarifa, agenda na mapendekezo yaliyotokana na Mkutano wa wataalam hao kuhusu masuala mbalimbali ya Jumuiya ambazo hatimaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri tarehe 23 Februari 2023.

 

Taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na  taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo mbalimbali ya  biashara na forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira na utawala na fedha. Pia mkutano umepokea taarifa ya mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Jumuiya kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya; Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.

 

Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kukitangaza Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli  rasmi za Jumuiya. 

 

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

 

Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi,  Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu  Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko.

 

Wengine waliombatana naye ni Balozi Stephen  Mbundi, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Bernard Haule Mkurugenzi Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Haji Janabi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali. 

 

Mkutano huo ambao umefanyika chini ya uenyekiti wa Burundi, umehudhuriwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku Sudan Kusini wakishiriki kwa njia ya mtandao

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Burundi, Bw. Severin Mbarubukeye (katikati) akiongoza Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 22 Februari 2023 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 23 Februari 2023. Mkutano huo pamoja na mambo mengine umejadili na kupitisha agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Mawaziri. Kushoto ni Naibu katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kulia) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 22 Februari 2023 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la  Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 23 Fevruari 2023. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi. Amina Khamis Shaaban na katikati ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akichangia jambo wakati wa Mkutano wa makatibu Wakuu uliofanyika Bujumbura kuandaa Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akisaini Ripoti itakayowasilishwa kwenye Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mwenyekiti kutoka Burundi nae akisaini Ripoti hiyo
Mjumbe kutoka Rwanda nae akisaini Ripoti
Mjumbe kutoka Uganda akisaini Ripoti

Mjumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akisaini ripoti

Mjumbe kutoka Kenya akisaini ripoti

Balozi Sokoine akibadilisha kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Bw. Abdi Dubat na Mjumbe kutoka Uganda wakibadilishana mawazo wakati wa mkutano wa Makatibu Wakuu

Awali Timu ya maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Ngazi ya Wataalam wakisaini ripoti iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu. Ujumbe  Tanzania uliongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi (wa pili kushoto)

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko (kushoto) akishiriki moja ya vikao vya maandalizi
Wajumbe wengine kutoka Tanzania katika vikao vya maandalizi

Wajumbe wakifuatilia mikutano ya maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya  ya Afrika Mashariki

Mkutano ukiendelea


VACANCY ANNOUNCEMENT AT COMMONWEALTH SECRETARIAT