Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 23 Februari 2023.
Mhe. Dkt. Tax ambaye ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama.
Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira; taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.
Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni umuhimu wa kukitangaza Kiswahili duniani kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli rasmi za Jumuiya.
Awali akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ezekiel Nibigira amesema kuwa Burundi kama mwenyekiti inaona fahari kuandaa Mkutano wa aina hiyo ambapo pia aliwakaribisha Mawaziri wenzake na washiriki wa Mkutano huo nchini humo na kueleza kuwa nchi hiyo imeendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote.
Mkutano huo ambao umefanyika kwa siku tano , ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama viilivyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Februari 2023.
Mbali na Mhe. Dkt. Tax ujumbe wa Tanzania pia uliwajumuisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko, Naibu Makatibu Wakuu akiwemo Bibi. Amina Khamis Shaaban Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kutunga sera za Jumuiya, kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa program mbalimbali za Jumuiya kwa maslahi mapana ya Nchi Wanachama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi saba za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.
Sehemu ya ujumbe wa Burundi wakishiriki mkutano |
Ujumbe wa Uganda na Sudan Kusin katika mkutano |
Ujumbe wa Kenya katika mkutano |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakishiriki Mkutano |
Ujumbe wa Rwanda katika Mkutano |
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kilichofanyika kabla ya kuanza Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. |
Kikao kikiendelea |