Tuesday, April 21, 2015

Watanzania 18 warejeshwa nchini kutokea Yemen

Kiongozi wa Msafara wa Watanzania waliorejeshwa nchini kutokea Yemen Bw. Abdul Twahid Said akizungumza na Waandishi wa Habari  kwa niaba ya wenzake mara baada ya kuwasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Emirates. Bw. Said alitoa shukrani kwa jitihada za Serikali za kuwarejesha nchini Watanzania wote kufuatia machafuko yanayoendelea nchini Yemen.
 Bw. Sabri Hery Omari ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliorejea nae  akizungumza na Waandishi wa Habari huku sehemu nyingine ya Watanzania hao wakionekana kwa nyuma.
Watanzania waliurudishwa Nchini wakitokea nchini Yemeni kutokana na machafuko yanayoendelea huko wakifurahi kuwa nyumbani salama
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Mindi Kasiga akizungumza mara baada ya Watanzania hao kuwasili nchini. Anayeonekana pembeni mwenye miwani ni Bw. Elibariki Maleko, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alikuwepo wakati wa mapokezi hayo


Picha na Reginald Philip
============================================


Na. Reuben Mchome

Watanzania kumi na nane warejea kutoka Yemen.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwarejesha nyumbani jumla ya Watanzania kumi na nane kutoka nchini Yemen kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo ya wenyewe kwa wenyewe.

Watanzania hao ambao wamewasili nchini leo kwa ndege ya shirika la emirates namba EK 725 wameishukuru serikali kutokana na jitihada za haraka zilizofanywa kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Oman na kufanikiwa kuwarejesha salama pasipo gharama zozote .

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Watanzania hao Bw. Sabri Abeid Almaghi ambaye alikua anafanya biashara nchini Yemen amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa namna ya pekee kwa kuwajali wananchi wake bila kujali wapo nchini au nje ya nchi na kutoa msaada  kwa wakati.

“Tunaishukuru sana serikali yetu ya Tanzania kwa jinsi ambavyo wanajali wananchi wake bila kujali wapo ndani au nje ya nchi,  kweli kama sio jitihada za ubalozi wetu pale mjini Muscat, sijui leo tungekua katika hali gani, tunaomba shukrani zetu mzifikishe kwa Rais Kikwete, Waziri Membe na wahusika wengine wote waliofanikisha kuturejesha nyumbani” alisema Mzee Saleh Mbaraka Jabri mmoja wa watanzania hao waliorejea kutoka Yemen.

Aidha, akizungumzia hali ya usalama ilivyo nchini Yemen, Bw. Almaghi amesema kuwa hali ni mbaya sana kufuatia mapigano ya anga yanayoendelea hivi sasa na muda wowote yataanza mapigano ya ardhini. Aidha amesema kuwa kufuatia hali hiyo huduma zote za kijamii pamoja na biashara zimesimama.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea watanzania hao Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Bi. Mindi Kasiga amesema mpaka hivi sasa watanzania ambao wamesharejeshwa nchini kutoka Yemen ni 23, kati ya   Watanzania 69 ambao wamejiandikisha  na jitihada  zinaendelea.

“Awamu ya kwanza ya Watanzania waliorejeshwa na serikali kutoka nchini Yemen ni familia moja ya watu watano ambao walirudi wiki chache zilizopita” alimalizia Bi. Mindi Kasiga.

Hivi karibuni Serikali kupitia Waziri wa Mambo  na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe ilitangaza kuwarejesha nchini Watanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.


Tanzania yashiriki mkutano wa ushirikiano wa Afrika na Asia unaofanyika Indonesia

Mhe. Dkt. Mary M. Nagu (Mb) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Uratibu na Mahusiano akichangia hoja katika moja ya mijadala kwenye Mkutano wa Kuadhimisha miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Bara la Asia na Afrika unaoendelea jijini Jakarta nchini Indonesia kuanzia tarehe 19 hadi 24 Aprili 2015. Kulia kwa Waziri ni Mhe. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake ya kudumu nchini Malaysia, Bw. Khatibu Makenga, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Bw. Dismas Assenga, Afisa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia.
Mkutano huo kwa ngazi ya Mawaziri ukiendelea.
==============================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika kufanyika Indonesia

Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika pamoja na Miaka 10 ya Mkakati Mpya wa Ubia Kati ya Asia na Afrika umeanza tarehe 19 Aprili 2015 hapa Jakarta, Indonesia.

Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kinachojadili maazimio mbalimbali yaliyofikiwa mwaka 2005 pamoja na kutengeneza Agenda za Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali kuanzia tarehe 19 mpaka 24 Aprili 2015.

Kaulimbiu ya mkutano huu ni Kupanua wigo wa Ushirikiano kwa nchi wanachama “Advancing South - South Cooperation”.

Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili kwa kina na kupitisha maazimio yatakayodumisha ushirikiano miongoni kwa nchi wanachama katika masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na Afrika na Azimio la Palestina. Maazimio yote hayo matatu yalijadiliwa na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali za nchi wanachama na kisha kupitishwa na Mkutano wa Mawaziri.

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali utafanyika tarehe 22 na 23 Aprili 2015, ambapo Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo anatarajiwa kuufungua kwa kutoa hotuba kwa wageni kabla ya kupitisha na kusaini Maazimio tajwa hapo juu.

Aidha, pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia watajadili mustakabali mzima wa masuala mbalimbali yanayoendelea duniani katika Nyanja ya usalama, ubaguzi wa rangi, matabaka baina ya jamii, usafirishaji haramu wa binadamu, ugaidi na mengineyo. Siku ya mwisho, Mkutano unatarajia kukamilika kwa Wakuu wa nchi na Serikali kutembele jiji la kihistoria la Bandung ambako ndiko ulifanyika Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika miaka 60 iliyopita.

Ujumbe wa Serikali ya Tanzania kwenye mkutano huo, uliongozwa na Mheshimiwa Dkt Mary M. Nagu (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Balozi, Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake nchini Malaysia pamoja na Maafisa wengine katika taasisi hizo. 

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
Tarehe 21 Aprili, 2015

Monday, April 20, 2015

Hakuna Mtanzania aliepoteza Maisha kwenye vurugu nchini Afrika Kusini - Membe



Waziri Membe: Hakuna Mtanzania katika mauaji ya Wageni Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Benard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa Habari nchini kuhusiana machafuko yanayoendelea nchini Afrika ya Kusini.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Balozi Irene Kasyanju (wa kwanza kulia) akiwa na  Mkurugenzi Idara ya Amerika na Ulaya Balozi Joseph Sokoine (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Uswisi, Mhe. Modest Mero wakimsikiliza Waziri Membe (hayupo pichani) alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari.   
Waandishi wa Habari wakimsikiliza na kunukuu taarifa kutoka kwa Waziri Membe ambaye hayupo pichani
Waziri Membe akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nao wakimsikiliza Waziri Membe (Hayupo pichani) 
Mwandishi wa Habari mkongwe  Bw. Jackton Manyerere akiuliza swali kwa Mhe. Membe
Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la Mawio Bi. Pendo Omary naye akiuliza swali kwa Waziri Membe.
Waziri Membe akijibu Maswali yaliyo ulizwa na Waandishi wa Habari 
Mazungumzo yakiendelea

Picha na Reginald Philip

==============================

TAARIFA KWA  VYOMBO VYA HABAR

Waziri Membe: Hakuna Mtanzania katika mauaji ya Wageni Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouawa katika mashambulizi dhidi ya wageni huko Durban na Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.

Mhe. Membe amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Watanzania watatu wameuwawa katika mashambulizii hayo siyo za kweli.


"Nimehakikishiwa na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini, David Mahlobo, asubuhi hii kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland," ametaarifu Mhe. Waziri.

Amesema serikali ina taarifa kuwa kuna Watanzania watatu waliofariki dunia nchini Afrika Kusini, lakini hawakuuwawa katika mashambulizi ya wenyeji dhidi ya wageni.

"Watanzania hao ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa alipigwa risasi katika tukio la ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban; mfungwa Athumani China Mapepe, aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa vurugu za wafungwa, na Ali Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini kutokana na ugonjwa wa TB," alieleza Mhe. Membe.

Mwili wa marehemu Mohamed ulirejeshwa nchini jana kwa mazishi. Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna Watanzania 23 katika kambi iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko Durban kuhudumia wageni wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa utaratibu unafanywa kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. "Wawili wamesema hawako tayari kurudi."

Mhe. Membe amesema taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini inaonyesha kuwa hali ya utulivu imerejea Durban na Johannesburg katika saa 48 zilizopita kutokana na juhudi za Rais Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri aliyoiteua kushughulikia mashambulizi hayo.

Mapema jana, Mhe. Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis Mseleku,       na kuelezea kukerwa kwa Serikali na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha usalama wa Watanzania nchini Afrika Kusini.

Alisema Tanzania inaunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambayo imelaani vikali mashambulizi ya Waafrika kutoka nje ya Afrika Kusini. Hata hivyo, Rais Mugabe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja mwa Afrika (AU), amesifia hatua zinazochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na kurejesha utulivu.

Mhe. Membe aliwataka Watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko nje ya nchi, kujitambulisha kwenye Balozi zetu ili iwe rahisi kufuatilia usalama wao na kuwasaidia yatokeapo majanga.

"Hatuna takwimu sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa sababu wengi wao wamekwenda huko kwa njia za panya," alisema. Inakadiriwa kuna Watanzania 10,000 waishio Johannesburg na Durban. 

Akijibu swali, Mhe. Membe alisema Tanzania inapaswa kutumia utajiri mkubwa wa gesi asilia ilionao kuendeleza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia kwa vijana ili wasikimbilie nchi za nje na kuhatarisha maisha yao.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
20 Aprili, 2015.




Waziri wa Mambo ya nje akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) kwaajili ya kuzungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam
Waziri Membe akiingia katika ukumbi wa Mkutano kwaajili ya kuzungumza na waandishi we habari (hawapo pichani).
Waziri akizungumza na waandishi wa Habari  
Waziri Membe (Wa kwanza kulia) akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Radhia Msuya (Wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga 
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Membe akiongozana na Viongozi wa Wizara na baadhi ya Waandishi wa habari kuelekea nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere.

Friday, April 17, 2015

Waziri Membe akabidhi Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais kwenda kwa Sultani wa Oman

Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akimkabidhi Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Ujumbe Maalum kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda  kwa Mhe. Sultani Qaboos bin Said Al Said, Mtawala wa Oman. Mhe. Membe alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini humo
Makabidhiano yakiendelea huku Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Ali Ahmed Saleh akishuhudia. 
Waziri Membe akiwa kwenye mazungumzo na Mhe. Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman.

===========================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenda kwa Sultan Qaboos wa Oman

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amekabidhi ujumbe maalum kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Mhe. Sultani Qaboos bin Said Al Said, Mtawala wa Oman.

Ujumbe huo maalum ulikabidhiwa kwa Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje na mwenyeji wa ziara ya Waziri Membe nchini Oman, kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Muscat, Oman Alhamisi Aprili 16, 2015.

Makabidhiano hayo ya kihistoria nchini hapa, yalishuhudiwa na Mhe. Dkt. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Zanzibar , Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania Oman, na viongozi wengine wa nchi zote mbili na waandishi wa habari.

Baada ya makabidhiano, viongozi hao wawili na ujumbe wao walitumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Oman.

Viongozi hao waliahidi kukuza uhusiano na utamaduni wa nchi hizi mbili ambao unafanana kwa sababu za kihistoria. Mhe. Membe alimuelezea mwenyeji wake nia ya Serikali kujenga Ofisi za Ubalozi  kwenye kiwanja chake hapa Mascut kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuwa na majengo ya Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani.

Aidha mradi mkubwa wa bandari ya Bagamoyo pia ulizungumzwa na viongozi hao ambapo Serikali ya Oman ni mojawapo ya mdau wa mradi huo. Wahusika wengine wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni Serikali ya China na Tanzania.

Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Omani alimuhakikishia mgeni wake ushirikiano wa Serikali yake kwenye hatua zote hizi muhimu za kuendeleza na kukuza uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
17 Aprili 2015


Thursday, April 16, 2015

Serikali kuwarudisha nchini Watanzania waliopo Yemen


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwasili katika Hoteli ya Hyatt ya mjini Muscat, Oman mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania, Oman, Mhe. Ali Ahmed Saleh (kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, Bw. Abdullah bin Said al-Riyami. Wakati wa ziara hiyo Mhe. Membe alitangaza azma ya Serikali kuwarudisha nchini Wanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.
Mhe.  Membe akiwa na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman (kulia) na Bw. Abdullah bin Said al-Riyami, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika Mashariki wakimsikiliza Bw. Fahad al-Bulushi, Afisa Itifaki wa ujumbe wa Mhe. Membe mara baada ya kuwasili nchini Oman.
========================================= 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali kuwarudisha Watanzania waliopo Yemen

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametangaza hatua ya Serikali kuwarudisha Watanzania waishio nchini Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Akizunguza na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman siku ya Alhamis tarehe 16 Aprili 2015, Waziri Membe amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, wanarejea nyumbani salama.

Zoezi la kurudisha Watanzania hao lilianza siku chache zilizopita ambapo familia ya watu watano ilisaidiwa na kurudi nyumbani kupitia Oman, wakati zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha Watanzania likenddelea.

“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa salama nyumbani mara moja” alisema Mhe. Membe.

Watanzania hao ambao wengi wao hadi sasa wameshafika kwenye miji midogo ya Sarfat na Al-Mazyouna kwenye mkoa wa Salala mpakani mwa Oman na Yemen, walituma maombi ya dharura (distress call) kwenye Ofisi za Ubalozi Oman, kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili, na kuomba kurudishwa nyumbani.

“Kulingana na maelekezo ya Waziri Membe, zoezi la kuwarejesha Watanzania limeanza. Nimewapeleka maafisa wa ubalozi kule Salala ni kilometa takriban elfu moja kutoka Muscut, ambapo watahakiki na kukabidhiwa Watanzania wote sitini na nne (64) na wataruhusiwa kuingia nchini Oman na kuelekea Tanzania” alimaliza Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman.

Mgogoro wa Yemen unaoendelea baina ya maafisa wa polisi waaminifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, na makundi ya usalama yanayomuunga mkono rais wa sasa, Abed Rabbo Mansour Hadi, umeua mamia ya watu na kujerui maelfu.

Mhe. Membe ametoa rai kwa Watanzania wote wenye ndugu au jamaa nchini Yemen kuchukua tahadhari na kuwataarifu watafute msaada kupitia Ubalozini Muscat ili kujihakikishia usalama wao. Aidha ametoa tahadhari kwa Watanzania wanaotegemea kusafiri kwenda Yemen, kusitisha safari zao hadi hali ya usalama itakaporejea.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
16 Aprili, 2015


Wednesday, April 15, 2015

Ziara ya Mhe. Membe Kuwait katika Picha

Msafara wa Mhe. Membe ukiingingia Mjini Kuwait kwa ziara ya siku moja kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait.


Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwasili kwene hoteli ya Sheraton Jijini Kuwait kwa ziara ya siku moja nchini humo.


Mhe. Membe na ujumbe wake wakimsikiliza Mhe. Balozi Najib na kuangalia picha  mbalimbali za historia ya Mji wa Kuwait mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku moja. 

Waziri Membe akifuatiwa na Balozi Najeb na ujumbe wake wakiingia kwenye Ofisi za Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait  kwa mazungumzo ya pamoja na viongozi wa mfuko huo tarehe 14 Aprili 2015.

Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa na Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mkutano.
Bw. Peter Noni, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) akimuonyesha Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader kazi zinazofanywa na benki yake kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini Tanzania. 
Mazungumzo yakiendelea


Mhe. Membe akiagana na Mhe. Abdulwahab A. Al-Bader, mara baada ya mazungumzo hayo kumalizika. 

Msafara wa Waziri Membe ukielekea kwenye ofisi za Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait (jengo refu la kwanza kushoto)

Waziri Membe akiwasili na mapokezi yakiendelea





Waziri Membe akitambulisha ujumbe wake kwa Mhe. Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mkutano.

Mazungumzo yakiendelea



Ujumbe wa Mhe. Membe ulihudhuria pia chakula cha mchana pamoja na mwenyeji wake Mhe. Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait


Waziri Membe akiagana na mwenyeji wake Mhe. Sheikh Sabah Al-Khalid Al-Sabah,  Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait.
Mhe. Membe akiagana na Balozi Najeb kwenye Uwanja wa Ndege wa Kuwait baada ya kukamilisha ziara yake nchini humo.