Thursday, September 17, 2015

Tanzania na Norway kuimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akihutubia katika ufunguzi rasmi wa Semina ya Ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency ya Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad na wadau wengine katika sekta ya biashara na uwekezaji kutoka Norway na hapa nchini.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Maeland (kulia) akimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo. Kushoto ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula na katikati ni  Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Kaarstad. 
Waziri Membe akiendelea kuzungumza
Waziri wa Biasha na Viwanda nchini Norway Mhe. Monica Maeland naye alipata fursa ya kuzungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Maeland yupo nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania nchini Norway. Pia wakati wa ziara hiyo Mhe. Maeland amezindua mtambo wa mbolea wa Yara ulioko kwenye Bandari ya Dar es Salaam na pia atatembelea Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (kulia) na mmoja wa wadau katika semina hiyo Bw. John Ulanga (kushoto) wakifuatilia Hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa na Mhe. Membe na Mhe. Maeland (hawapo pichani). 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Tunsume Mwangolombe (katikati) naye akifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo.

Sehemu ya wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo 
Semina ikiendelea
Waziri Membe (katikati) na Waziri Maeland kwa pamoja na wajumbe waliofuatana nao wakiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kumaliza ufunguzi wa semina.
Waziri Membe (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya  faida ya semina hiyo ya wafanyabiashara wa Tanzania na Norway
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea


Picha na Reginald Philip
======================================================

TANZANIA NA NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameisifu Serikali ya Norway kwa kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa Tanzania hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.

Waziri Membe alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Abdallah Kigoda wakati akifungua rasmi semina kuhusu kuimarisha ushirikiano wa Kibiashara  na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam leo.

Katika ufunguzi huo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa kidiplomasia kwa miaka mingi lakini sasa nchi hizi zimeamua kushirikiana zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imefaidika na  ushirikiano na Norway katika sekta mbalimbali ambapo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuisaidia Tanzania kupambana na umaskini na kukuza uchumi. Hata hivyo alisema umefika wakati sasa nchi hizi mbili zinufaike kupitia biashara na uwekezaji ambapo nchi zote zina fursa nyingi katika maeneo hayo ikiwemo gesi na mafuta, kilimo na madini.

Mhe. Membe alisema kuwa kufanyika kwa semina hii itakayowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji itaongeza thamani katika uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Norway ambayo ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha zaidi gesi asilia na mafuta duniani. Hivyo aliwaasa Watanznaia kutumia semina hiyo kujifunza ili kuimarisha sekta ya nishati ya hapa nchini. 

“Semina hii ni fursa kwa Kampuni za Tanzania na Norway kujifunza na kubadilisha uzoefu na mawazo ya namna bora ya kuboresha sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili” alisema Waziri Membe.

Akizungumzia biashara inayofanyika kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania inatakiwa kuongeza biashara yake nje ya nchi ili kuimarisha uchumi wake. Alieleza kuwa kwa sasa biashara kati ya Tanzania na Norway imeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 6.9 mwaka 2014 kwa bidhaa zilizozwa Norway kutokea Tanzania ikiwemo kahawa, chai, viungo, maua, mbogamboga, mbao na madini.

Kwa upande wa bidhaa kutoka Norway, Tanzania imenunua kwa ongezeko la kutoka bilioni 22.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 73 mwaka 2014. Bidhaa hizo ni pamoja na dawa za binadamu na bidhaa za viwandani.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Monica aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji wa uchumi ambao umefikia asilimia 7. Alieleza kuwa Tanzania itafikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa vile inayo dhamira ya dhati na imejipanga kupitia uvumbuzi wa gesi na mafuta, nguvukazi ya vijana na mageuzi yaliyopo katika sekta ya uchumi.

Alieleza kuwa Norway ipo tayari kuendelea kuisadia Tanzania katika sekta ya gesi na mafuta kwa vile nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo hususan katika masuala ya teknolojia. Aidha, aliongeza kuwa Tanzania ni mshirika wa kweli wa Norway katika maendeleo hivyo nchi yake itashirikiana kikamilifu na Tanzania.
“Kuna msemo maarufu unasema kama unataka kwenda mbio nenda peke yako, lakini kama utanaka kufika mbali nenda pamoja na mwenzako. Hivyo Norway inataka kwenda pamoja na Tanzania ili kuziwezesha nchi hizi kufika mbali kimaendeleo” alisisitiza Mhe. Monica.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa nchi hizi mbili kukuza biashara kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu kwani ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu.

Semina hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Norway, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ilihudhuriwa na Makampuni 34 kutoka Norway na Tanzania na pia wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji.

-Mwisho-

Balozi Mulamula akutana na Balozi wa Uturuki nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Uturuki hapa nchini, Mhe. Yasemin Eralp, baada ya Balozi huyo kumtembelea Katibu Mkuu kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 17 Septemba, 2015.
Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakifuatilia mazungumzo hayo. Kulia ni Bw. Kondo Ally na Bw. Anthony Mtafya (kushoto).
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Yasemin Eralp mara baada ya mazungumzo.
======================================
PICHA NA REUBEN MCHOME.

Wednesday, September 16, 2015

Mhe. Rais Kikwete awaapisha rasmi Balozi Mwakasege, Bundala, Kilima, Luvanda, Mbega na Shiyo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha Bi. Victoria Richard Mwakasege aliyekuwa Naibu Balozi wa Tanzania nchini Burundi. Balozi Victoria R. Mwakasege anaiwakilisha Tanzania nchini Malawi. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 16 September, 2015
Balozi Mwakasege akisaini kiapo chake mbele ya Mhe. Rais Kikwete
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Mwakasege vitendea kazi
Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mwakasege na familia ya Balozi Mwakasege
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha aliyekuwa  Kaimu Mkurugenzi  wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi.Zuhura Bundala kuwa Balozi na Msaidizi wa Rais (Diplomasia) anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Samweli Shelukindo. 
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Bundara vitendea kazi 
Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Bundala na familia ya Balozi Bundala
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha aliyekuwa  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Innocent E. Shiyo kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara hiyo
Balozi Shiyo akisaini kiapo chake mbele ya Mhe. Rais Kikwete
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Shiyo vitendea kazi
Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Shiyo na familia yake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha aliyekuwa Afisa Ubalozi Mkuu, Ubalozi wa Tanzania, Muscat, Oman, Bw. Abdallah Kilima kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Balozi Kilima naye akisaini kiapo chake mbele ya Mhe. Rais Kikwete
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Kilima vitendea kazi
Mhe. Rais Kikwete (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilima na familia yake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ubalozi wa Tanzania, Kampala, Uganda Bi. Anisa Mbega kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 

Balozi Mbega naye akisaini kiapo chake mbele ya Mhe. Rais Kikwete
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Mbega vitendea kazi
Mhe. Rais Kikwete (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mbega na wanafamilia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha aliyekuwa Mratibu wa Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu Bw. Baraka H. Luvanda kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Balozi Luvanda naye akisaini kiapo chake mbele ya Mhe. Rais Kikwete
Mhe. Rais Kikwete akimkabidhi Balozi Luvanda vitendea kazi
Mhe. Rais Kikwete (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Luvanda na familia yake

Balozi Irene Kasyanju (wa kwanza kulia), akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje Balozi Celestine Mushy (katikati) na wakwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Silima Haji Kombo walipokuwa katika hafla ya uapisho wa Mabalozi na wakurugenzi wapya

Wakurugenzi wasaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali watu wakifuatilia zoezi la uapisho wa Mabalozi na Wakurugenzi likiendelea
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Asha Rose Migiro (katikati) ambaye alikuwepo kwenye sherehe hizo akisalimiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Mindi Kasiga (wa kwanza kulia). Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula (Kushoto).
Balozi Mwakasege (kushoto),  Balozi Bundala (kulia) na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora Bi. Rosemary Jairo wakiwa katika picha ya pamoja na nyuso za furaha mara baada ya kumaliza kuapishwa kuwa Mabalozi 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Itifaki Bw. James Bwana (kushoto) akimpongeza Balozi Zuhura Bundala (kulia) mara baada ya kuapishwa kuwa Balozi.
Bi. Mindi Kasiga (kushoto) akimpongeza Balozi Mbega (kulia) mara baada ya kuapishwa kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mhe. Rais Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wapya pamoja na Waziri Membe, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mabalozi wapya wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Balozi Liberata Mulamula (wa nne kushoto mstari wa mbele), Naibu Katibu Mkuu Balozi Simba Yahya (wa tatu kutoka kushoto), Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 Juu na chini ni Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiwasubiri Mabalozi wapya kuwasili Wizarani hapo mara baada ya kuapishwa. 
Maafisa Mambo ya Nje wakiwa na maua wakisubiri  kuwakabidhi Mabalozi wapya kama ishara ya pongezi na kuwakaribisha Wizarani.
Sehemu nyingine ya watumishi wa Wizara hiyo wakiwatizama Mabalozi (hawapo pichani) wakiwasili Wizarani hapo mara baada ya kuapishwa Ikulu
Balozi Mwakasege akifuatana na Mabalozi wenzake kuteremka kwenye Basi maalumu lililoandaliwa kwaajili yao wakiwasili Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mara baada ya kuapishwa kuwa Mabalozi
Balozi Mwakasege (kushoto) akipokea maua kutoka kwa Afisa Mambo ya Nje Felista Rugambwa (kulia)
Balozi Samweli Shelukindo aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika naye akipokea maua kutoka kwa Afisa Mambo ya nje Eliet Magogo, mara baada ya kuwasili Wizarani.
Balozi Luvanda naye akipongezwa na Balozi Irene Kasyanju mara baada ya kuwasili Wizarani hapo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard  Membe (Mb.), katikati akipongezwa na Watumisho wa Wizra ya Mambo ya Nje kwa uongozi mzuri katika Wizara hiyo.
Waziri Membe akizungumza neno huku watumishi wa Wizara hiyo wakimsikiliza

Picha na Reginald Philip

Tuesday, September 15, 2015

Balozi Mulamula akutana na Balozi wa Canada hapa Nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Alexandre Leveque ofisini kwake katika mazungumzo ya kudumisha ushirikiano. 
 Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Alexandre Leveque akisisitiza jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula wakati wa mazungumzo hayo, kulia ni Afisa Mambo ya Nje wa Wizara hiyo Bw. Lucas Mayenga akifuatilia mazungumzo hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini.
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Alexandre Leveque, mara baada ya mazungumzo yao.
=========================
PICHA NA REUBEN MCHOME.