Friday, May 20, 2016

Dkt. Mahadhi Juma Maalim amtembelea Balozi wa Malawi Nchini Kuwait

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili Ubalozi wa Malawi na kupokelewa na mwenyeji wake, Mhe. Balozi Wilfred Ali (hayupo pichani). Dkt. Maalim alimtembelea Balozi huyo wa Malawi kwa lengo la kumshukuru kutokana na mchango mkubwa wa Ubalozi huo katika kufanikisha ufunguzi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kuwait. Hata hivyo, Balozi Maalim, alimuhakikishia  Balozi Ali utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na Malawi na jamii nzima ya kidiplomasia nchini Kuwait.   
Balozi Dkt. Mahadhi pamoja na mwenyeji wake Mhe. Ali wakiendelea na mazungumzo yao.

UN YAWAENZI WALINZI WAKE WA AMANI WALIOPOTEZA MAISHA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  Balozi Tuvako Manongi akiwa ameshika medali  ya  Dag Hammarskjold waliyotunukiwa  mashujaa watatu watanzania ambao wamepoteza maisha mwaka jana wakati wakihudumu katika Misheni za kulinda Amani  za Umoja wa Mataifa. kushoto kwa Balozi ni Luteni Kanal  George Ita'ngare, mshauri wa  masuala ya kijeshi  katika Uwakilishi wa Kudumu na  kulia ni  Bw,Herve Ladsous,  Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya  Operesheni za Ulinsi wa Amani  za Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, akimvisha Bibi Yacine Mar Diop medal maalum ya   Kapteni Mbaye Diagne ambaye alikuwa ni  mume wa Bibi Yacine, Kapteni Diagne aliuawa mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda. medali hiyo  maalum imebuniwa na  Baraza  la Usalama kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake na kujituma kwake kwa hali ya juu hadi  kupelekea kupoteza maisha.  Kapteni  Diagne anakumbukwa  kwa namna alivyookoa maisha ya mamia ya wanyarwanda kwa kuwaficha kwenye lori na kuwapeleka  mahali salama kabla ya  yenye mwenyewe kuuawa.
Balozi Tuvako Manongi  akiandika katika kitabu cha  kuwaeni walinzi wa amani wa  Umoja wa Mataifa waliopotea maisha mwaka jana. miongoni mwa mashujaa 129 waliokumbukwa  wapo watanzania watatu ambao ni Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis 
Sehemu ya  washiriki wa hafla ya siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa hafla hiyo ilifanyika  jana Mei 19.

=============================================



Na Mwandishi Maalum, New York

Umoja wa Mataifa,  jana   Mei 19 umefanya  hafla  maalumu ya  siku ya Kimataifa ya  Walinzi wa Amani  wanaohudumu  katika Misheni mbalimbali za Kulinda Amani chini  ya kofia ya  Umoja wa Mataifa.

Katika   hafla hiyo  jumla ya walinzi 129  wanajeshi na  polisi waliopoteza maisha  mwaka  jana  kwa kushambuliwa na  makundi ya wapiganaji wenye silaha, matukio ya kigaidi, ajali na kuumwa    walikumbukwa  na kuenziwa kwa mchango wao.

Miongoni mwa Mashujaa hao  129   kutoka  nchi   50, wapo mashujaa watatu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashujaa hao ni  Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl. John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis. 

Hafla  hiyo maalum ya kutambua mchango wa  walinzi  hao  wa Amani na ambao wamejitolea maisha  yao kwaajili ya  kuwalinda na kuokoka maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia   katika  nchi zinazokabiliwa na vita na  migogoro ya wenyewenye  kwa wenyewewe iliongozwa na Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon.

Mwakilishi wa Kudumu wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,  ndiye aliyepokea medali maalum za mashuja hao watatu kwa niaba ya familia zao.  Medali    waliyotunukiwa  mashujaa hao na  wengine inatambuliwa kama  medali   ya  Dag Hammarskjold.

Hafla ya mwaka huu,   pamoja na  kutambua mchango wa mashujaa hao 129 ,  pia  ilitambua kwa namna ya pekee  na kwa  mara ya kwanza,  mchango  na kujitolea wa hali ya juu  ulikofanywa   na Kapteni  Mbaye Diagne raia ya  Senegal, aliyepoteza maisha mwaka 1994 wakati  akiokoa maisha ya  wanyarwada wakati wa  mauaji ya kimbali.

Kapteni Mbaye Diagne ameeziwa rasmi katika maadhimisho ya mwaka  huu kwa kupewa medali maalum iliyopewa  jina  la  Medali ya  Mbaye Diagne, medali ambayo alikabidhiwa mjane wa Mbaye  Bibi Yacine Mar Diop  huku akishuhudiwa na watoto  wake wawili.

Kapten Mbaye Diagne alikuwa mwangalizi wa Amani nchini Rwanda, kwa ushujaa mkubwa na bila ya kujali  hatari iliyokuwa ikimkabili  alitumia lori kuwaficha na kuwapeleka  mahali  salama mamia ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda.

Kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake huo, Baraza la Usalama lilibuni   mwaka 2014 medali ya  Kapten Mbaye Diagne ambayo  watakuwa  wanatunukiwa wanajeshi,  polisi na raia ambao wameonyesha uthubutu na ushupavu wa hali ya juu kiasi cha kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumza wakati wa halfa  hiyo ambayo  ilibeba majonzi ya  aina yake,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  alieleza kwamba,  hadi kufikia mwezi   wa nne mwaka huu, jumla ya walinzi wa Amani  3,400 wakiwamo  wanajeshi, polisi na raia walikuwa wamepoteza maisha  tangu kuanzishwa wa  shughuli za ulinzi wa Amani kwa  kofia ya Umoja wa Mataifa miaka 70 iliyopita.

“Wakati leo tunawaenzi na  kuwakumbuka mashujaa hawa 129 kutoka mataifa 50 waliopoteza maisha  yao mwaka jana  wakati wakitekeleza  jukumu la kuwalinda  wananchi wengine,  jana ( Mei 18) walinzi wengine watano wanaohudumu huko   Mali  wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa”. Akasema Ban  Ki Moon kwa huzuni.

Thursday, May 19, 2016

Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumika katika Taasisi za Serikali

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ambapo alizungumzia matumizi ya Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Taasisi za Serikali.

Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia Dkt. Watengere Kitojo (kushoto) pamoja na Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Robi Bwiru. 
Bi. Mindi Kasiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia, Dkt. Watengere Kitojo naye akizungumza kuhusu Kozi zinazotolewa na chuo hicho ikiwemo Cheti, StaShahada, Shahada katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa
Sehemu ya Waandishi wa Habari waliojitokeza kwenye mkutano huo, katikati ni Afisa kutoka Habari Maelezo Bi. Immaculate Makilika akifuatilia kwa makini mkutano.
==================================================



Matumizi ya Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa wito kwa Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa zinatumia alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alama hizo zinatakiwa kutumika kwenye Ofisi za Serikali (Wizara, Idara zinazojitegemea,  mashirika ya umma na Wakala) sambamba na alama za Taifa yaani Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wimbo wa Taifa. 

Bendera ya Jumuiya inatakiwa kupepea sambamba na Bendera ya Taifa kwenye Ofisi za Serikali na Wimbo wa Jumuiya  nao unatakiwa kuimbwa sambamba  na Wimbo wa Taifa wakati wa shughuli rasmi za Kiserikali. 

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao katika kifungu cha 7(a) umesisitiza Jumuiya hii kuwa ni Jumuiya ya watu, hivyo wananchi wa Tanzania watahusishwa katika hatua zote za Mtangamano. Aidha,  Serikali ya awamu ya tano (5) chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itahakikisha kuwa Watanzania wanashirikishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za Jumuiya ili kuijua kwa madhumuni ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.

Matumizi ya alama hizi ni njia mojawapo ya kujenga uzalendo na kumfanya Mwananchi ajisikie kuwa sehemu ya Ushirikiano huu. Aidha, Taasisi binafsi hasa Mashule na Vyuo wanasisitizwa kutumia alama hizi kama sehemu ya kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaratibu zoezi la upatikanaji wa sampuli ya alama hizo kwa gharama za taasisi husika, hivyo Wizara, Taasisi na Ofisi za Serikali zinahimizwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa upatikanaji na matumizi ya alama hizo.

MAZUNGUMZO YA USULUHISHI WA MGOGORO WA BURUNDI

WAKATI HUOHUO, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataongoza mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yanayotarajiwa kuanza tarehe 21 hadi 24 Mei, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC – Arusha.
Katika mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifafanua kuwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni ataendelea kuwa  msuluhishi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuteua timu ya Usuluhishi ambayo itaongozwa na Mhe. Benjamin William Mkapa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Waandishi wa Habari wataruhusiwa kwenye siku ya Ufunguzi wa Mkutano huo na siku ya kufunga Mkutano tu. Aidha, waandishi wanahimizwa kujisajili ili kupata vitambulisho vya kuingia kwenye mkutano. Usajili utafanyika AICC-Arusha tarehe 20 Mei, 2016 saa 8:00 mchana chumba namba 541, ghorofa ya tano, upande wa Kilimanjaro.

Au unaweza kutuma maelezo ya Press Card yako, picha ya ndogo (passport size) kwenye email ifuatayo; media@eachq.org, CC:oothieno@eachq.org.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 19 Mei 2016.




Press Release




PRESS RELEASE

VACANCY ANNOUNCEMENT FROM THE COMMONWEALTH SECRETARIAT

The Ministry of Foreign Affairs, East Africa, Regional and International Cooperation has received vacancy notification from the Commonwealth Secretariat inviting qualified Tanzanians to apply for the post of Director of Ocean and Natural Resources Advisory Division

Application details can be found on the Secretariat’s website, www.thecommonwealth.org. Closing date for application is Tuesday 31st May, 2016.

“The Ministry encourages qualified Tanzanians to apply”.



Issued by: The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation, 
Dar es Salaam.
19th May, 2016

Wednesday, May 11, 2016

Balozi wa Tanzania nchini Kenya akutana na Balozi Austria nchini Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule amefanya mazungumzo na Balozi wa Austria nchini Tanzania mwenye makazi yake Kenya, Mhe. Dkt. Harald Gunther kuhusu umarishaji wa ushirikiano baina ya nchi zao . Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ubalozi wa Tanzania Nairobi. Mazungumzo yalihusu pia masuala ya uwakilishi.
Austria ni mwanachama wa Kamati ya Ufadhili wa Maendeleo (DAC),ambayo inajumuisha nchi za Jumuiya ya Ulaya, Marekani, Japan na Australia.


Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro washiriki uangalizi wa uchaguzi Kisiwani Anjouan

Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, Bw. Mudrick Soragha akiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Mji wa Mrigou, Bw. Abdul  Latif wakati Bw. Soragha alipoongoza ujumbe wa Ubalozi kwenye Uchaguzi kwenye Kisiwa cha Anjouan.
Mmoja wa Wagombea kwenye uchaguzi huo Bw. Azali Othman (katikati) akiwa na timu yake kwenye Kampeni
Bw. Soragha (kulia) na Bw. Thabit Khamis wakiwa kwenye moja ya maeneo ya kampeni
Bw. Soragha na Wajumbe wengine kutoka Ubalozini wakiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Mji wa Sima, Bw. Abdallah Abdou (wa pili kulia)
=====================================================


Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro umeshiriki katika zoezi la uangalizi wa uchaguzi wa marejeo katika Kisiwa Anjouan. Uchaguzi huo unafanyika kufuatia Mahakama ya Katiba Visiwani Comoro kutoa amri ya kurejewa kwa uchaguzi wa majimbo 15 ambayo uchaguzi wake ulikumbwa na sintofahamu tarehe 10 Aprili 2016 ambapo zaidi ya wananchi 6305 kutoka Kisiwa hicho walishindwa kutekeleza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao.

Maeneo yanayorejea uchaguzi huo ni Mramani, Niamboimro, Mrijou, Bambini, Mjimandra na Bougoueni. 

Kwa kutambua umuhimu wa chaguzi hizi, Ubalozi wa Tanzania kama moja wapo ya nchi inayowakilisha jumuiya ya kimataifa iliyopo Comoro imetuma ujumbe unaoongozwa na Bw. Mudrick Soragha,  Mkuu wa Utawala na Fedha kwa lengo la kujiridhisha na kujionea hali halisi ya namna mchakato huo utakavyokuwa. Ikumbukwe kwamba Tanzania ina mahusiano ya muda mrefu na Muungano wa Visiwa vya Comoro.

Mahusiano hayo yalipata nguvu zaidi baada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mstari wa mbele katika Operesheni ya Kukikomboa Kisiwa cha Anjoun kutoka kwenye mikono ya mvamizi Kanali. Mohammed Bacar mwaka 2008 na kufanikiwa kukirejesha kisiwa hicho katika Umoja wa Visiwa vya Comoro.

Wakati ukiwa katika Kisiwa hicho, Ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana na wadau  mbalimbali wa Siasa hasa viongozi wa Tume ya Uchaguzi wa Kisiwa ijulikanayo kama CEII, Meya wa Miji pamoja na viongozi wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama wa Kisiwa cha Anjoun. Katika mazungumzo na viongozi hao wote walionyesha kutaka uchaguzi huo ufanyike katika mazingira ya amani na utulivu ili wananchi wa miji hiyo wapate fursa ya kutekeleza haki yao ya msingi ya Kidemokrasia.

Ni matarajio ya Ubalozi kuwa uchaguzi huo utapita salama kama zilivyopita chaguzi nyingine. Licha ya ujumbe wa Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro pia Umoja wa Afrika na Jumuiya nyingine za kimataifa na kitaifa zipo Kisiwani Anjoun kungalia uchaguzi huo.