Thursday, June 23, 2016

Ubalozi wa Kuwait watoa msaada wa madawati 300

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye Hafla ya kukabidhi Madawati 300 kutoka Ubalozi wa Kuwait hapa nchini. Balozi Jasem Al Najem ndio aliyokabidhi msaada huo wa madawati.
 Juu na Chini ni sehemu ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza kwa Makini Waziri Mahiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani)

Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al Najem akizungumza katika hafla hiyo.
Sehemu nyingine ya Wakuu Idara na Vitengo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Najem akiendelea kuzungumza
Waziri Mahiga (kulia), Balozi Najem na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Abdallah Kilima, kwa pamoja wakiwa wamekaa kwenye madawati yaliyotolewa na Ubalozi wa Kuwait hapa nchini.
Waziri Mahiga na Balozi Najem wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa Idara na Vitego mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ameupongeza Ubalozi wa Kuwait kwa kuwa wa  kwanza kuitikia maombi yake ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule za msingi na sekondari hapa nchini. 

Pongezi hizo alizitoa jana wakati wa hafla ya kupokea madawati 300 ambayo Ubalozi huo uliahidi kuipa Serikali. Hafla ilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Tumeanza kupokea madawati kutoka kwa rafiki zetu, huu ni mwanzo tu, na wengine watafuatia na taarifa ya kila dawati litakalokuwa linapatikana nitaiwasilisha kwa Mhe. Waziri Mkuu. Dkt. Mahiga alieleza.

Mhe. Waziri aliwaambia wahudhuriaji wa hafla hiyo kuwa katika utekelezaji wa malengo ya milennia, Tanzania ilifanya vizuri katika baadhi ya maeneo hususan, elimu na afya ya mama na mtoto. Licha ya idadi ya watoto kuandikishwa mashuleni iliongezeka, bado kulikuwa na changamoto ya kuboresha ubora wa elimu na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kama vile vitabu na majengo ya maabara na vifaa vyake.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutangaza elimu bure, udahili mashuleni umeongezeka maradufu na hivyo kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba mkubwa wa madawati. 

“Kufuatia hali hiyo, Serikali imejipanga kutumia mbinu mbalimbali kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwaomba marafiki zetu watusaidie. Hivyo, Kuwait imejitokeza kutusaidia na imeahidi kusaidia sio madawati tu bali, hata maeneo mengine yenye changamoto kwenye elimu”.

Kwa upande wake, Balozi wa Kuwait,  Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya jitihada za Serikali yake kuunga mkono mkakati wa Rais Magufuli wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.  

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.


Wednesday, June 22, 2016

Wadau wajadili utekelezaji wa Mradi wa Eneo la Viwanda la Bagamoyo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na anayefuatilia pembeni yao ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki katika Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi na Wakala zinazohusika katika mradi wa Bagamoyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam terehe 21 Juni 2016.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi na Wakala mbalimbali za Serikali zinazoshiriki katika kutekeleza mradi wa eneo la Viwanda la Bagamoyo wamekutana leo katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ambayo itawezesha miundombinu wezeshi kwa ajili ya kutekelezwa kwa haraka kwa mradi huo, eneo maalum la Viwanda la Bagamoyo lililo chini ya EPZA, linatarajiwa kujengwa kuwa mji wa Viwanda na Biashara.  Mkutano huo umefanyika chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mradi huu ili kuweza kukamilika kwa wakati utahitaji ushirikiano na uratibu wa karibu wa Serikali chini ya Wizara, taasisi na Wakala mbalimbali za Serikali. Hadi sasa kuna shughuli mbalimbali za mwanzo za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu wezeshi katika eneo hilo maalum.
Akiongea katika Mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema, ili mradi huu kuanza kutekelezwa ni vyema kila taasisi kuanza kutekeleza kwa haraka miradi ya miundombinu wezeshi ili wawekezaji katika mradi huu kupata imani ya kuweza kuwekeza katika eneo hilo. “Wawekezaji kutoka China wako tayari wanachosubiri ni kwa sisi kutekeleza kwa upande wetu yale ambayo tunapaswa kutekeleza ili kuwezesha mradi huu kuanza” alisema.
Kati ya shughuli hizo za msingi ni maandalizi ya miundombinu wezeshi kwa upande wa Bandari ya Bagamoyo ambapo TPA hadi sasa wameishafanya maandalizi ya kujenga lango kubwa la kuwezesha meli kuingia, lango hilo linatarajiwa kuwa na ukubwa wa Cubic Metre 25, 000,000, uchambuzi yakinifu ulifanyika Mwaka 2010 na hadi sasa TPA wameiishaanza kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa lango hilo.
Vilevile kwa upande wa miundombinu ya barabara, Wakala wa Barabara TANROADS wameanza hatua za utekelezaji wa awali wa ujenzi wa barabara tatu za kiwango cha lami ambazo ni Tegeta - Bagamoyo, barabara hii inatarajiwa kuwa na urefu wa Km. 43.2 ambapo barabara hiyo itapanuliwa na kuwa ya njia mbili kila upande, barabara nyingine ni ile ya Makofia- Mlandinzi hii itakuwa na jumla ya Km. 36.7 na barabara  ya Mbegani -  Bagamoyo yenye urefu wa km 7.2. barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kutoka bandarini kuunganisha na barabara kuu. Barabara hizi zote ni kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji kutoka na kwenda eneo la mradi.
Kwa upande wa reli, mradi huu unatarajiwa kujengewa reli itakayounganisha  njia nyingine za usafirishaji kutoka eneo la mradi. Jumla ya hekta 1,200 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha Standard gauge na reli hii itajengwa kutoka Mpiji hadi Bagamoyo, reli hii inakadiriwa kuwa na urefu wa Km 60.
Ili mradi huu wa Bagamoyo uweze kufanyakazi utahitaji umeme wa kutosha na hadi sasa TANESCO chini ya Wizara ya Nishati na Madini wanatarajia kupeleka umeme mkubwa chini ya mradi wa North East -3  ambao utaweza kutoa jumla ya 220 KV ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu umeme wa Zinga kwenda kwenye 132KV. Aidha, TANESCO wanatarajia  kuweka power plant eneo la Zinga yenye uwezo wa kuzalisha takriban Megawatt 200. Vilevile Wizara ya Nishati ili kuweza kuhakikisha umeme wa mradi huu wa uhakika unapatikana wanatarajia kujenga bomba la gas kutoka Tegeta hadi Bagamoyo eneo hilo la Viwanda,
Eneo hilo pia linatarajiwa kuwa na miundombinu ya uhakika ya maji ambapo DAWASCO wanatarajia kusambaza maji kutoka vyanzo vyake ikiwa ni pamoja na kujenga bwawa la maji katika mto Ruvu litakalo kuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya ujazo wa million 190 Lita.
Eneo hili vilevile linatarajiwa kuunganishwa na miundombinu ya Mawasiliano ambapo TTCL wataunganisha eneo hili la Viwanda kwenye Mkongo wa Taifa kwa upande wa kutoka Chalinze – Bagamoyo ikiwa ni pamoja na kuweka mawasiliano ya 4G kwa ajili ya matumizi ya ofisi na majengo katika eneo hilo la Viwanda la Bagamoyo.
Makatibu Wakuu pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali wanaohusika katika mradi huu wamemaliza mkutano kwa kuweka  maazimio mbalimbali ikiwa ni  pamoja na kusisitiza kila mdau katika mradi huu ahakikishe anatekeleza eneo lake kwa haraka kwani eneo hili likikamilika litaibadilisha Tanzania katika ramani ya dunia kwa upande wa biashara na Viwanda, pia litatoa ajira kwa Watanzania na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu na hivyo kufikia lengo la Nchi yenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 22 Juni 2016.



Tuesday, June 21, 2016

Dkt. Mlima akutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Aziz Mlima akiwa katika na mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India, Mhe. Amar Sinha, Mazungumzo hayo yalijikita katika kuboresha na kukuza mahusiano kati ya Tanzania na India hasa kwenye nyanja ya Viwanda ambayo itazalisha ajira kwa vijana na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.. 
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (wa kwanza kushoto), na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Ally Kondo na Bi. Mercy Kitonga wakinukuu mambo muhimu ya mazungumzo hayo.
Sehemu ya Ujumbe ulioambatana na Mhe. Sinha ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Dkt. Mlima na Mhe. Amar Sinha. Wa kwanza kulia ni Baloizi wa India nchini Tanzania, Mhe. Sandeep Arya
Mkutano ukiendelea.
Dkt. Aziz Mlima na Mgeni wake, Mhe. Amar Sinha wakiwa katika picha ya pamoja.