Wednesday, June 22, 2016

Wadau wajadili utekelezaji wa Mradi wa Eneo la Viwanda la Bagamoyo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na anayefuatilia pembeni yao ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki katika Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi na Wakala zinazohusika katika mradi wa Bagamoyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam terehe 21 Juni 2016.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi na Wakala mbalimbali za Serikali zinazoshiriki katika kutekeleza mradi wa eneo la Viwanda la Bagamoyo wamekutana leo katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ambayo itawezesha miundombinu wezeshi kwa ajili ya kutekelezwa kwa haraka kwa mradi huo, eneo maalum la Viwanda la Bagamoyo lililo chini ya EPZA, linatarajiwa kujengwa kuwa mji wa Viwanda na Biashara.  Mkutano huo umefanyika chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mradi huu ili kuweza kukamilika kwa wakati utahitaji ushirikiano na uratibu wa karibu wa Serikali chini ya Wizara, taasisi na Wakala mbalimbali za Serikali. Hadi sasa kuna shughuli mbalimbali za mwanzo za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu wezeshi katika eneo hilo maalum.
Akiongea katika Mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema, ili mradi huu kuanza kutekelezwa ni vyema kila taasisi kuanza kutekeleza kwa haraka miradi ya miundombinu wezeshi ili wawekezaji katika mradi huu kupata imani ya kuweza kuwekeza katika eneo hilo. “Wawekezaji kutoka China wako tayari wanachosubiri ni kwa sisi kutekeleza kwa upande wetu yale ambayo tunapaswa kutekeleza ili kuwezesha mradi huu kuanza” alisema.
Kati ya shughuli hizo za msingi ni maandalizi ya miundombinu wezeshi kwa upande wa Bandari ya Bagamoyo ambapo TPA hadi sasa wameishafanya maandalizi ya kujenga lango kubwa la kuwezesha meli kuingia, lango hilo linatarajiwa kuwa na ukubwa wa Cubic Metre 25, 000,000, uchambuzi yakinifu ulifanyika Mwaka 2010 na hadi sasa TPA wameiishaanza kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa lango hilo.
Vilevile kwa upande wa miundombinu ya barabara, Wakala wa Barabara TANROADS wameanza hatua za utekelezaji wa awali wa ujenzi wa barabara tatu za kiwango cha lami ambazo ni Tegeta - Bagamoyo, barabara hii inatarajiwa kuwa na urefu wa Km. 43.2 ambapo barabara hiyo itapanuliwa na kuwa ya njia mbili kila upande, barabara nyingine ni ile ya Makofia- Mlandinzi hii itakuwa na jumla ya Km. 36.7 na barabara  ya Mbegani -  Bagamoyo yenye urefu wa km 7.2. barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kutoka bandarini kuunganisha na barabara kuu. Barabara hizi zote ni kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji kutoka na kwenda eneo la mradi.
Kwa upande wa reli, mradi huu unatarajiwa kujengewa reli itakayounganisha  njia nyingine za usafirishaji kutoka eneo la mradi. Jumla ya hekta 1,200 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha Standard gauge na reli hii itajengwa kutoka Mpiji hadi Bagamoyo, reli hii inakadiriwa kuwa na urefu wa Km 60.
Ili mradi huu wa Bagamoyo uweze kufanyakazi utahitaji umeme wa kutosha na hadi sasa TANESCO chini ya Wizara ya Nishati na Madini wanatarajia kupeleka umeme mkubwa chini ya mradi wa North East -3  ambao utaweza kutoa jumla ya 220 KV ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu umeme wa Zinga kwenda kwenye 132KV. Aidha, TANESCO wanatarajia  kuweka power plant eneo la Zinga yenye uwezo wa kuzalisha takriban Megawatt 200. Vilevile Wizara ya Nishati ili kuweza kuhakikisha umeme wa mradi huu wa uhakika unapatikana wanatarajia kujenga bomba la gas kutoka Tegeta hadi Bagamoyo eneo hilo la Viwanda,
Eneo hilo pia linatarajiwa kuwa na miundombinu ya uhakika ya maji ambapo DAWASCO wanatarajia kusambaza maji kutoka vyanzo vyake ikiwa ni pamoja na kujenga bwawa la maji katika mto Ruvu litakalo kuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya ujazo wa million 190 Lita.
Eneo hili vilevile linatarajiwa kuunganishwa na miundombinu ya Mawasiliano ambapo TTCL wataunganisha eneo hili la Viwanda kwenye Mkongo wa Taifa kwa upande wa kutoka Chalinze – Bagamoyo ikiwa ni pamoja na kuweka mawasiliano ya 4G kwa ajili ya matumizi ya ofisi na majengo katika eneo hilo la Viwanda la Bagamoyo.
Makatibu Wakuu pamoja na Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali wanaohusika katika mradi huu wamemaliza mkutano kwa kuweka  maazimio mbalimbali ikiwa ni  pamoja na kusisitiza kila mdau katika mradi huu ahakikishe anatekeleza eneo lake kwa haraka kwani eneo hili likikamilika litaibadilisha Tanzania katika ramani ya dunia kwa upande wa biashara na Viwanda, pia litatoa ajira kwa Watanzania na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu na hivyo kufikia lengo la Nchi yenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 22 Juni 2016.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.