Wednesday, June 15, 2016

Naibu Waziri Dkt. Possi ashiriki Mkutano wa Tisa wa nchi Wanachama wa Mkataba wa watu wenye Ulemavu


 Naibu Waziri, Ofisi  ya  Waziri Mkuu,(Masuala ya Walemavu)  Mhe. Dr. Abdallah Possi ( Mb) akizungumza wakati wa majadiliano ya jumla kuhusu  utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu. Mhe. Possi anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa  wa Nchi  Wanachama  wa Mkataba  wa Watu  Wenye Ulemavu. Mkutano huu wa siku tatu umeanza siku ya  Jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.  Wajumbe wengine katika  picha ni kutoka kushoto Mhe. Stella Ikupa Alex ( Mb), Mhe. Riziki Said Lulida ( Mb) na Mhe. Elly Marko Macha ( MB). 
Ujumbe wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa  Tisa wa Mkataba wa Watu  Wenye  Ulemavu,  ufunguzi wa mkutano  huu  ulifanyika katika  Ukumbi Mkuu wa Mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano huu wa siku tatu ajenda yake ni "Utekelezaji wa  Agenda  ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”. Unahudhuriwa na  Washiriki kutoka nchi 164   ambazo zimeridhia  Mkataba huu, Asasi zisizo za kiserikali pia  zinahudhuria katika  Mkutano  huu ambao ni  maalum kwa watu wenye ulemavu wa aina zote.

============================================

FURSA ZA KIUCHUMI  NI CHANGAMOTO KUBWA KWA  WATU WENYE ULEMAVU-MHE-POSSI

Mkutanowa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu ( CRDP), umeanza  Jumanne)  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  New York, Marekani.

Mada au  ujumbe wa Mkutano huu wa siku tatu ni “ Utekelezajiwa  Agenda  yaMaendeleoEndelevu (Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika Mkutano huu, unaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi( Mb). Wajumbe wengine ni Mhe. Riziki Lulinda (Mb), Mhe. Elly Macha (Mb), Mhe. Stella Ikupa (Mb) , Bi Josephine Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu watu wenye ulemavu na Bi. NgusekelaNyerere , Afisa Mambo yaNje, Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizugumza wakati wa majadiliano ya jumla mara baada ya hafla ya ufunguzi, Naibu Waziri. Dr. Abdallah Possi amesema, changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  ni fursa za kiuchumi.
“Licha ya mafanikio kadhaa yakiwamo ya utungaji wa sera,  sheria na mabadiliko mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa lengo la kuwapunguzia matatizo watu wenye ulemavu yakiwamo matatizo ya kutokuwa na fursa  sawa na kuondokana na umaskini”. Alieleza Naibu  Waziri

Na Kuongeza kwamba, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine inakabiliwa pia na vipaumbele vinavyokinzana na ambavyo ni muhimu lakini vikiwaathiri zaidi watu wenye ulemavu.

Akavitaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi nasalama, chakula, huduma za afya, elimu na ukosefu wa ajira.

Vile vile Naibu Waziri ameleza kuwa mtazamo hasi kuhusu watu wenye ulemavu ni changamoto nyingine ambayo inatatiza ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika fursa mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambazo wangeweza kunufaika nazo bila ya kujali hali zao.

Akizungumzia kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  Mhe. Dr. Possi, ameeleza washiriki wa mkutano huu kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia mkataba wa watu wenye ulemavu kwamba,  watu wenye ulemavu nchini  Tanzania wanakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na vifaa saidizi ambavyo vingewasaidia na kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku.

Vivile akabainisha kuwa mwaka  2015, Tanzania ilikuwa moja ya wadhamini wa kuuwa Azimio kuhusu watu wenye ualibino, azimio ambalo pamoja na mambo mengine limelenga katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazo wakabili watu wenye ualibino katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya elimu, afya na ajira.

“ Bila ya kuwa na vifaa saidizi watu wenye ulemavu wa aina yeyote  ile wanashindwa kupata fursa anuai ambazo kwao zingewawezesha kuishi pasipo utegemezi na hivyo kuchangia katika maisha yao binafsi na maendeleo ya nchi yao” akasisitiza Naibu Waziri. Na akatumia fursa hiyo kwa kuhimiza upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujitegemea.

Awali akifungua mkutano wa tisa wa Mkataba wa Watu Wenye ulemavu,  Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  Bw. Mogens Lykketoft, amesema nchi ambazo zimeridhia mkataba huo zinao wajibu wakuchukua hatua zote muhimu zikiwamo za maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“Kila nchi mwanachama wa mkataba huu na asiye mwanachama ana kazi ya kufanya, lakini katika dunia ya leo mafanikio hayamo katika mikono ya serikali peke yake” akasisitiza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.  

Na kwasababu hiyo, ametoa wito kwa serikali zote pamoja na wadau mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuwawezesha watu wenye ulemavu zaidi ya bilioni moja.

Pamoja na hotuba kutoka kwa nchi wanachama, mkutano huu ambao ni wa siku tatu utakuwa na mijadala pembeni yenye mada tofauti. Mkutano huo pia  unashirikisha Asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.