Thursday, June 16, 2016

Dkt. Possi asisitiza umuhimu wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu

Mhe. Dkt. Abdallah Possi, (Mb) Naibu Waziri, Ofisi  ya Waziri Mkuu akichangia  majadiliano kuhusu  mada ya  kuwaondololea umaskini na   kukosekana kwa usawa kwa  watu wenye ulemavu. Mhe. Possi alikuwa mmoja wa wanajopo watano walioanzisha majadiliano kuhusu mada hiyo katika siku ya pili ya  Mkutano  wa Tisa wa Mkataba wa Watu  wenye Ulemavu unaoendelea hapa  Umoja wa Mataifa.
Naibu Waziri Possi  akibadilishana   mawazo na   Bi. Asa Regner Waziri wa Watoto, Wazee na Usawa wa Jinsia  kutoka Sweden muda mfupi  kabla ya kuanza kwa majadiliano kuhusu kuwaondolea umaskini na kukosekana kwa usawa kwa watu wenye ulemavu.
Ujumbe wa Tanzania ambao umeongoza na  Mhe, Naibu  Waziri katika  mkutano wa Tisa  wa  Mkataba kuhusu Watu wenye  Ulemavu.  kati ya wajumbe  hao ni,   kutoka kushoto mstari wa nyuma ni  Bi. Ngusekela Karen Nyerere ( Mambo ya Nje) Mhe. Stella Ikupa Alec ( Mb, CCM), Mhe. Riziki Said Lulinda( Mb,CUF) na Mhe. Dkt. Elly Marko Macha( Mb. CHADEMA)  aliyekaa mbele ni  Bi Josephine Makunzo Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu Watu wenye Ulemavu
sehemu ya  washiriki  wa  majadiliano kuhusu kuwaondolea umaskini na kukosekana kwa usawa  kwa watu wenye  ulemavu ikiwa ni sehemu ya  mwendelezo wa  majadiliano kuhusu  ajenda kuu ya mkutano wa tisa wa mkataba wa watu wenye ulemavu.

==================================
FURSA ZA KIUCHUMI  NI CHANGAMOTO KUBWA KWA  WATU WENYE ULEMAVU-MHE-POSSI

Mkutanowa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu ( CRDP), umeanza  tarehe 14 Juni, 2016,  katika  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  New York, Marekani.

Mada au  ujumbe wa Mkutano huu wa siku tatu ni “ Utekelezajiwa  Agenda  yaMaendeleoEndelevu (Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika Mkutano huu, unaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi( Mb). Wajumbe wengine ni Mhe. Riziki Lulinda (Mb), Mhe. Elly Macha (Mb), Mhe. Stella Ikupa (Mb) , Bi Josephine Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu watu wenye ulemavu na Bi. NgusekelaNyerere , Afisa Mambo yaNje, Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizugumza wakati wa majadiliano ya jumla mara baada ya hafla ya ufunguzi, Naibu Waziri. Dr. Abdallah Possi amesema, changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  ni fursa za kiuchumi.
“Licha ya mafanikio kadhaa yakiwamo ya utungaji wa sera,  sheria na mabadiliko mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa lengo la kuwapunguzia matatizo watu wenye ulemavu yakiwamo matatizo ya kutokuwa na fursa  sawa na kuondokana na umaskini”. Alieleza Naibu  Waziri.

Na Kuongeza kwamba, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine inakabiliwa pia na vipaumbele vinavyokinzana na ambavyo ni muhimu lakini vikiwaathiri zaidi watu wenye ulemavu.

Akavitaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi nasalama, chakula, huduma za afya, elimu na ukosefu wa ajira.

Vile vile Naibu Waziri ameleza kuwa mtazamo hasi kuhusu watu wenye ulemavu ni changamoto nyingine ambayo inatatiza ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika fursa mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambazo wangeweza kunufaika nazo bila ya kujali hali zao.

Akizungumzia kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania,  Mhe. Dr. Possi, ameeleza washiriki wa mkutano huu kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia mkataba wa watu wenye ulemavu kwamba,  watu wenye ulemavu nchini  Tanzania wanakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na vifaa saidizi ambavyo vingewasaidia na kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku.

Vivile akabainisha kuwa mwaka  2015, Tanzania ilikuwa moja ya wadhamini wa kuuwa Azimio kuhusu watu wenye ualibino, azimio ambalo pamoja na mambo mengine limelenga katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazo wakabili watu wenye ualibino katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya elimu, afya na ajira.

“ Bila ya kuwa na vifaa saidizi watu wenye ulemavu wa aina yeyote  ile wanashindwa kupata fursa anuai ambazo kwao zingewawezesha kuishi pasipo utegemezi na hivyo kuchangia katika maisha yao binafsi na maendeleo ya nchi yao” akasisitiza Naibu Waziri. Na akatumia fursa hiyo kwa kuhimiza upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujitegemea.
Awali akifungua mkutano wa tisa wa Mkataba wa Watu Wenye ulemavu,  Rais wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  Bw. Mogens Lykketoft, amesema nchi ambazo zimeridhia mkataba huo zinao wajibu wakuchukua hatua zote muhimu zikiwamo za maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“Kila nchi mwanachama wa mkataba huu na asiye mwanachama ana kazi ya kufanya, lakini katika dunia ya leo mafanikio hayamo katika mikono ya serikali pek eyake” akasisitiza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na kwasababu hiyo, ametoa wito kwa serikali zote pamoja na wadau mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuwawezesha watu wenye ulemavu zaidi ya bilioni moja.

Pamoja na hotuba kutoka kwa nchi wanachama, mkutano huu ambao ni wa siku tatu utakuwa na mijadala pembeni yenye mada tofauti. Mkutano huo pia  unashirikisha Asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu.








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.