Friday, June 10, 2016

Naibu Waziri Kigwangalla ashiriki Mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI


 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na  Watoto,  Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla ( Mb) akizungumza   kwa niaba ya serikali kuhusu  mafanikio na changamoto ambazo  serikali imekuwa ikikabiliana nazo  dhidi ya  ugonjwa wa UKIMWI  katika Mkutano wa ngazi ya juu  wa Baraza Kuu la  Umoja wa  Mataifa kuhusu UKIMWI unaoendelea Umoja wa Mataifa New York-Marekani.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Kigwangalla (Mb) akiwa na baadhi ya wajumbe wa Tanzania Dkt.Hamis Mwinyimvua, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Policy & Coordination) na Mhe. Constantine Kanyasu Mbunge wa Geita na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya UKIMWI, katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu UKIMWI, ulioandaliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa na kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki Moon.
Naibu Waziri  Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla akiwa  katika picha ya pamoja na  sehemu ya ujumbe wa Tanzania  unaoshiriki mkutano wa   ngazi ya  juu  kuhusu  ukimwi,  mara tu baada ya kusoma hotuba yake katika Ukumbi Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambako mkutano huo unafanyika.

=====================================================

USHIRIKIANO BADO UNAHITAJIKA KUUKABILI   UGONJWA WA UKIMWI-TANZANIA.

Mkutano wa nganzi ya juu kuhusu UKIMWI jana ( alhamis) uliingia katika siku yake ya pili ambapo viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri na Manaibu waziri wanaohusika na masuala ya afya wameendelea kuelezea nini ambacho nchi zao zinatekeleza katika kukabili na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha UKIMWI pamoja na huduma wanazopatiwa watu ambao wamekwisha kuathirika na kuugua.

Mmoja ya nchi ambayo iliwasilisha mafanikio,  changamoto na mwelekeo wa baadaye katika kukabiliana na janga  la ugonjwa wa UKIMWI,   ambao jumuiya ya kimataifa umejiwekea lengo la  kuutokomeza ifikapo mwaka 2030 ilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Juhudi za Tanzania dhidi ya UKIMWI,  zilielezwa na Naibu Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Hamis A. Kigwangalla (Mb). Ambaye katika maelelezo yake amesema, Tanzania inaamini kuwa inawezekana kufikia hali ya kutokuwa na maambukizi mapya, kumaliza ubaguzi na unyanyapaa, na kuwa na kiwango sifuri   cha vifo vinavyohusiana na UKIMWI Ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo anasema, ilikufikia hatua hiyo au mafanikio hayo,  mambo   kadhaa yanapashwa kufanyika, yakiwamo ya uimarishwaji wa elimu ya kinga,  vijana na jumuiya kwa ujumla kufundishwa mbinu za kuepukana na tabia hatarishi ambazo zinachangia ongozeko la  waathirika na kuhakikisha upatikanaji kirahisi wa dawa na ambazo zitakuwa za gharama nafuu.

Kwa mujibu wa Naibu  Waziri ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, amekwenda mbali zaidi kwa kusema pia patahitajika kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi,  kujadili masuala ya jinsia pamoja na mila na tamaduni,  kutenga raslimali za kutosha kwaajili ya watu wenye mahitaji wakiwamo vijana, kuwa na viwanda vitakavyoweza kuzalisha dawa.

Akizungumza baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imekwisha kuyafikia katika kukabili tatatizo la ugonjwa wa UKIMWI, Naibu Waziri  ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka  140,000 mwaka 1990 hadi kufikia 63,000 mwaka 2014. Vilevile vifo vitokanavyo au vinavyo sababishwa na UKIMWI pia  vimepungua kwa asilimi 40 katika kipindi hicho.

Akaeleza pia kwamba hata watu wanaopatiwa huduma ya matibabu nayo imeongezeka kufikia asilimia 60 huku ongezeko likiwa kwa watoto na hasa baada ya kupitisha mpango unaotambulika kama Option B+  miaka sita iliyopita.

Kuhusu kupungua kwa raslimali fedha hususani kutoka kwa wafadhili, Dkt. Kingwangalla, amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, na kwa kuzingatia wito wa jumuiya ya kimataifa kupanua wigo wa mapato ya ndani,  serikali ya Tanzania ilianzisha Mfuko wa UKIMWI,  (AIDS Trust Fund) mfuko ambao alisema hadi sasa serikali ndiyo imekuwa mchangiaji mkuu, ingawa pia  kuna sekta binafsi nayo inatazamiwa kuchangia.

Akasema sehemu  au nusu ya fedha hizo (55%) itakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma na kuongeza kuwa juhudi hizo za serikali pia zimesaidiwa na ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine rafiki pamoja na mashirika ya kimataifa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wale  wote ambao wanachangia juhudi za serikali.

Kuhusu mipango mingine ambayo serikali inaendelea nayo ,  Naibu waziri alikuwa na haya ya kueleza “ baada ya kuwa tumeanza utaratibu wa kupima na kutibu kwa baadhi ya wilaya chache nchini, tunakusudia kuisambaza huduma hiyo lakini itakuwa ni kwa hatua ili kutoa nafasi ya kuwajengea uwezo watoaji wa huduma ya afya, kuhuisha mifumo ya usambazaji wa vifaa ikiwa ni pamoja na ushiriki wa jamii iliiweze kupokea na kuukubali mfumo huu mpya wa utoaji wa huduma” ameeleza Naibu Waziri.

Akasisitiza zaidi kwa kusema ingawa ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya nchi ambapo inakadiriwa watu milioni moja na nusu (1.5) wameathirika, huku mzigo mkubwa ukiwaelemea wanawake na vijana hasa watoto wa kike, serikali ya  Tanzania  itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha inafikia lengo  la kutokuwa na maambukizi mapya,  kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, na vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Katika hatua nyingine amesema ili kutorudisha nyuma mafanikio ambayo  Tanzania imeyafikia hadi sasa pamoja na nchi nyingine kusini mwa Jangwa la Sahara Jumuiya ya Kimataifa inaombwa kusaidia jitihada zinazofanywa na serikali za nchi hizo za kuwa na mapato yake yenyewe ya kugharamia huduma za afya kwa wagonjwa wa UKIMWI pamoja na huduma nyinginezo badala ya kuziachia kabisa jukumu hilo.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.