Wednesday, December 21, 2016

Kikao cha Kwanza cha Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na UAE chafanyika Abu Dhabi





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Balozi Augustine Mahiga (kushoto) kwa pamoja na  Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakisaini  Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga. Mkataba huo ulisainiwa wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi, Falme za Kiarabu tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharika, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Uchumi na Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE wakiwekeana saini baadhi ya makubaliano yaliyoafikiwa.
Mhe. Dkt. Mahiga na ujumbe alioongozana nao wakiwa katika kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano na ujumbe wa UAE kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Mratibu wa Mkutano kwa upande wa Serikali ya Tanzania kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hangi Mgaka akifuatilia mkutano.


Picha ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania na UAE mara baada ya kukamilisha kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UMOJA WA FALME ZA KIARABU ZAFANYA MKUTANO WA KWANZA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU YA USHIRIKIANO HUKO ABU DHABI. 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimefanya kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano huko Abu Dhabi makao makuu ya Umoja wa Falme za Kiarabu.  Kikao hicho kilifanyika tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.

Mkutano huo ulioshirikisha sekta mbalimbali za Serikali zote mbili uliongozwa na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania na Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). 

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo Tanzania na UAE zimekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya Kidiplomasia; Uchumi; Utalii; Nishati; Kilimo; Sayansi na Teknolojia; Usafirishaji; Miundombinu; Ulinzi na Usalama; Elimu pamoja na Kazi na Ajira. 

Sambamba na mkutano huo, Tanzania na UAE zimesaini Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga (Bilateral Air Service Agreement-BASA) na Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utalii. Vilevile Serikali zote mbili zimekubaliana kukamilisha na kusaini Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi za Mapato; Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji; pamoja na ushirikiano katika sekta ya Elimu, Afya, Ulinzi na Usalama, Ushirikiano katika Usafiri wa Majini,  Kazi na Ajira pamoja ushirikiano katika masuala ya Zimamoto na Uokoaji. 

Mkutano huo umekuwa ni chachu katika mahusiano ya kihistoria ya nchi hizi mbili ambapo umeweka mazingira rasmi ya ushirikiano sio tu kwa Serikali bali pia kwa sekta binafsi. 

Mheshimiwa Waziri Mahiga katika hotuba yake ya ufungaji alitoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla za Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu kuchangamkia fursa zinazopatikana katika nchi hizi mbili kuafuatia mkutano huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Desemba, 2016.


Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na ujumbe wa UNMICT



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (katikati) akizungumza na Bwana Samuel Akorimo, Mkuu wa Ofisi ya Arusha kutoka Mahakama ya Umoja wa Mataifa (UNMICT) iliyopo Arusha walipomtembelea  Wizarani kwa lengo la kushukuru kwa mchango wa Serikali na Wizara kufanikisha ujenzi na uzinduzi wa Majengo ya Umoja wa Mataifa Jijini Arusha, eneo la Lakilaki. Wengine katika picha ni Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria (kulia) na Bi.Bi Blandina Kasagama, Afisa Mambo ya Nje. Kushoto ni Bw. Samwel Algozin Afisa Sheria Mkuu kutoka (UNMICT)


Katibu Mkuu, Balozi Mlima na Ujumbe kutoka UNMICT wakiwa  katika picha ya pamoja baada ya kikao

Friday, December 16, 2016

Tanzania na Kenya zasaini Makubaliano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Dkt. Amina Mohammed wakisaini Makubaliano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.  Makubaliano hayo yamesainiwa kufuatia Kikao cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Kenya kilichofanyika tarehe 1 hadi 3 Desemba, 2016 ambapo masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yalijadiliwa na kukubaliwa. Masuala ya ushirikiano ni pamoja na kilimo, uchukuzi, utalii, nishati na madini na uvuvi. Hafla hiyo fupi ya uwekaji saini makubaliano hayo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini  Dar es Salaam tarehe 16 Desemba, 2016.
Waziri Mahiga na Waziri Mohammed wakibadilishana makubaliano hayo mara baada ya kusaini.
Waziri Mahiga akizungumza katika hafla hiyo.Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kenya na kwamba makubaliano yaliyosainiwa yataimarisha mahusiano hayo kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji, kurahisisha ufanyaji biashara na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa nchi hizi mbili.
Waziri Amina naye  akizungumza kwenye hafla hiyo. Katika hotuba yake aliahidi Kenya kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika masuala yote yaliyokubaliwa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi akitoa neno la shukrani katika hafla hiyo ya uwekaji saini Makubaliano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano
Sehemu ya wajumbe kutoka Kenya waliohudhuria  hafla ya uwekwaji saini wa Makubaliano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.  Kulia ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Chirau Ali Mwakwere
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania nao wakishuhudia uwekwaji  saini katika makubaliano ya tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya. Kushoto ni Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika akifuatiwa na Bw. Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masahriki
Mshereheshaji ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiwakaribisha wageni wakati wa hafla ya uwekaji saini Makubaliano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.
Sehemu ya maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waandishi wa Habari waliohudhuria  hafla hiyo.
Picha ya Pamoja

Wednesday, December 14, 2016

Wizara ya Mambo ya Nje yapokea kifaa cha kutunza data za mtandao kutoka IOM

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine (katikati) akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  kupokea kifaa cha kulinda na kutunza data za mtandao (router) za   Wizara kutoka kwa Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) nchini Tanzania, Bw. Qasim Sufi ( kulia)Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbega.
 Balozi Sokoine (katikati) akizungumza na Bw. Sufi mara baada ya kupokea kifaa cha kutunza na kulinda data za mtandao wa Wizara (Router)
Balozi Mbega naye akichangia jambo wakati wa mazungumzo hayo
Picha ya pamoja

Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Dau awasilisha Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt Ramadhani Dau akikabidhi  hati zake za utambulisho kwa mfalme na mkuu wa nchi hiyo  Abdul Halim Mu'adzam Shah katika kasri ya Istana Negara jijini Kuala Lumpur  mapema mwezi huu.

Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt Ramadhani Dau akikabidhi  Hati za Utambulisho kwa Mfalme na Mkuu wa Nchi hiyo,  Abdul Halim Mu'adzam Shah katika kasri ya Istana Negara jijini Kuala Lumpur  mapema mwezi huu.



Kikosi cha askari kikitoa saluti wakati nyimbo za Taifa za Tanzania na Malayasia zikipigwa mara baada ya Balozi wa Tanzania nchini humo  Mhe. Dkt Ramadhani Dau kuwasili katika kasri ya Istana Negara jijini Kuala Lumpur kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Mfalme na Mkuu wa nchi hiyo aliyemaliza muda wake Abdul Halim Mu'adzam Shah mapema mwezi huu.

Tuesday, December 13, 2016

Wizara ya Mambo ya Nje yakutana uongozi wa Taasisi ya Aga Khan kujadili masuala ya ushirikiano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akitoa hotuba ya ufunguzi katika kikao cha wadau kilichoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa  ajili ya kujadili masuala ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Uongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan "The Aga Khan Development Network" (AKDN). Kikao hicho kilifanyika tarehe 13 Disemba, 2016 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa masuala ya Diplomasia katika Taasisi wa Maendeleo wa Aga Khan, Balozi Arif Lalani  akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Taasisi hiyo iliyopo nchini. Balozi Lalani alieleza kuwa wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na zenye ubora hususan katika sekta za Elimu, Afya na masuala ya Utalii sambamba na kuangalia namna ya kuanzisha maeneo mengine zaidi ya uwekezaji.
Waziri Mahiga akifuatilia ya taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Mratibu wa Mradi wa Chuo cha Aga Khan kinachotarajiwa kujengwa Jijini Arusha. Pembeni yake kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Balozi Baraka Luvanda.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga (kulia) pamoja na Bi Lilian Kimaro, Afisa Mambo ya Nje wakifuatilia kikao.
Sehemu nyingine ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao.
Kikao cha wadau kikiendelea.

Friday, December 9, 2016

Naibu Waziri ashiriki maadhimisho ya siku ya Kitaifa ya Japan


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Balozi wa Japan nchini, Tanzania Mhe. Masaharo Yoshida mara alipowasili kushiriki hafla fupi ya maadhimisho ya siku ya Japan iliyofanyika  nyumbani kwa Balozi huyo Oysterbay, Jijini Dar es Salaam 
Mkurugenzi na Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharn Yoshida alipowasili nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam kushiriki hafla fupi ya maadhimisho ya siku ya Japan
Kutoka kulia; Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Japan nchini Mhe.Masaharo Yoshida wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa unapigwa
Balozi wa Japan nchini Mhe.Masaharo Yoshida akiongea na hadhira iliyohudhuria hafla ya siku ya Japan 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akiongea na hadhira iliyohudhuria hafla hiyo