Friday, January 17, 2020

KAMPUNI YA ALRIFAI YA KUWAIT YATEMBELEA TANZANIA, KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI


Na Mwandishi wetu,

Kampuni ya Alrifai inayojihusisha na biashara ya mazao mchanganyiko iko nchini kwa lengo la kuangalia fursa za uwekezaji hususani kununua zao la korosho na kahawa na kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao la korosho nchini.

Ujumbe wa watu watatu (3) ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud, Meneja Viwango Bwn. Ahmed Mohamed Bahie pamoja na Meneja wa Manunuzi Bwn. M. K Hussin uko nchini tangu tarehe 13 Januari, 2020 kwa lengo kuu la kuangalia uwezekano wa Kununua korosho zilizokwisha chakatwa pamoja na kahawa zilizokobolewa na pia kuona maeneo ambayo wanaweza kuwekeza katika kiwanda cha kuchakata korosho.

Ujumbe huo ulifanya kikako na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Kahawa (TCB), Mamlaka ya Maendeieo ya Biashara Tanzania (TanTrade) pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko na kuweza kupata fursa ya kufahamu kwa undani juu ya taratibu za ununuzi wa mazao hayo pamoja na taratibu za uwekezaji wa kiwanda cha kuchakata korosho hapa nchini.

Akitoa maelezo juu ya uzalishwaji wa zao la Korosho nchini, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa TanTrade, Bi. Twilumba Mlelwa alisema kuwa korosho ghafi kwa mwaka huzalishwa kati ya tani 250,000 na tani 300,000 ambapo kiasi kikubwa huzalishwa Mtwara, Lindi, Ruvuma (Tunduru), Pwani (Mkuranga na Kibaha) pamoja na Tanga.

"Naomba niwatoe shaka juu ya zao la korosho kwani kwa sasa viwanda vya korosho ni 18 ambapo vinauwezo wa huhifadhi tani 63,000 za korosho lakini kwa sasa vinavyofanya kazi ni 13 na vina uwezo wa kubangua tani 43,000" Amesema Bi. Mlelwa

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud,ameushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Kuwait kwa ushirikiano alioupata kutoka ubalozini hadi kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuweza kuratibu zoezi la kukuagua zao la Korosho, kahawa pamoja na karafuu.

"Binafsi nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kwa viongozi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara, Bodi ya Mazao Mchanganyiko, TIC, TanTrade, Bodi ya Kahawa pamoja na Balozi Mhandisi Aisha Amour kwa namna alivyolisimamia jambo hili tangu likiwa wazo mpaka sasa tunapoelekea kwenye utekelezaji niwaahidi tu kuwa utekelezaji wa kununua mazao haya utaanza mara moja mara tu baada ya kufanya maamuzi na mikataba itasainiwa kwa mujibu wa sheria," amesema Bwn. Foaud

Aidha, mbali na maelezo ya uzalishaji wa zao la Korosho nchini, ujumbe huo pia ulipata fursa ya kuona zao la korosho lililohifadhiwa katika ghala la Serikali eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam na uliridhishwa na zao hilo na kuahidi kuwekeza nchini kwani korosho zinzazalishwa ni nzuri na bora.

Meneja Viwango Bwn. Ahmed Mohamed Bahie amesema "tumejionea wenyewe ubora wa korosho, kahawa na karafuu kwa kweli ni nzuri sana na sote tumeridhika na ubora huo. Tutajitahidi kukamilisha taratibu zote muhimu na kuanza mara moja uagizaji wa korosho na baadae kujenga kiwanda cha kuchakata korosho hapa Tanzania,".  

Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea maeneo kadhaa kwa lengo la kupata maelezo kuhusu taratibu na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini, maeneo hayo ni pamoja na mikoa ya Lindi, Mtwara na Kilimanjaro pamoja na Zanzibar ambapo waliweza kuona uzalishaji wa Karafuu.

Ujio wa kampuni hiyo ni matokeo ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini Kuwait ambapo ulifanya mazungumzo na Kampuni ya Alrifai inayojihusisha na biashara ya mazao mchanganyiko kuhusu nia yao ya kununua zao la korosho na kahawa na kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao la korosho nchini Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo akiwaelezea jambo viongozi wa Kampuni Alrifai juu ya upatikanaji wa zao la kahawa nchini

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud, akiongea na viongozi kutoka TIC, TCB, TanTrade pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wakati walipokutana katika mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Add caption

Meneja Viwango Bwn. Ahmed Mohamed Bahie akikagua korosho zinazozalishwa hapa nchini, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara TanTrade, Bi. Twilumba Mlelwa



Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud pamoja na Meneja wa Manunuzi Bwn. Hussain wakikagua korosho zilizohifadhiwa kwenye moja ya ghala hapa nchini, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi akimuonyesha Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud jinsi korosho zinavyohifadhiwa


 Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dkt. Anselm Moshi akimfafanulia jambo Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud pamoja na Meneja Viwango Bwn. Ahmed Mohamed Bahie


Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alrifai, Bwn. Abdellah Foaud akiuliza kitu wakati alipotembelea moja kati ya viwanda vya kubangua korosho Mkoani Mtwara


Ujumbe wa Kampuni ya Alrifai ukiwa katika moja ya kiwanda cha kubangua korosho mkoani Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bwn. Gelasius Byakanwa (kulia) akiwa ofisini kwake na Ujumbe wa Kampuni ya Alrifai ambapo ujumbe huo ulitembelea pia chuo cha utafiti wa Korosho Nariendele na baadhi ya viwanda vya kubangua korosho

Ujumbe wa Kampuni ya Alrifai ukiwa katika moja ya duka la kuuza karafuu Mjini Zanzibar 

Thursday, January 16, 2020

PROF. KABUDI ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO YA SULTAN WA OMAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokelewa na Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe.  Ally Abdallah Almahruqi katika ubalozi wa Oman - Tanzania. Prof. Kabudi amekwenda ubalozini hapo kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Sultan wa  Oman, Sultan Qaboos bin Said.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Oman uliopo Jijini Dar es Salaam kufutia kifo cha Sultan wa Oman, Sultan Qaboos bin Said. Waliosimama ni Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe.  Ally Abdallah Almahruqi akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Ramadhan Muombwa Mwinyi.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Oman uliopo Jijini Dar es Salaam kufutia kifo cha Sultan wa Oman, Sultan Qaboos bin Said. 
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe.  Ally Abdallah Almahruqi,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Ramadhan Muombwa Mwinyi na viongozi wa Ubalozi wa Oman hapa Nchini pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe.  Ally Abdallah Almahruqi,mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Sultan wa Oman,Sultan Qaboos bin Said.

Wednesday, January 15, 2020

SERIKALI YAAGIZA CHUO CHA DIPLOMASIA KUTOA ELIMU KWA VITENDO ZAIDI

Serikali imekitaka Chuo cha Diplomasia kutoa taaluma ya vitendo kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ili kuwawezesha wahitimu kuwa na mchango katika Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Akihutubia mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi katika mhafali hayo, amesema Serikali itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya stratejia, jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu hasa kwa muktadha wa kiafrika.

Waziri Kabudi ameongeza kuwa taaluma inayotolewa na Chuo hicho isiwe ya nadharia pekee bali iambatane na vitendo ili elimu hiyo itumike kusaidia kufafanua masuala ya Kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa yanayotokea duniani.

"Nakiagiza Chuo kuandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa vitendo ili tuangalie ni jinsi gani Wizara inaweza kusaidia. Aidha, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama ilivyopendekezwa ili kisipitwe na wakati. Dunia inabadilika kwa kasi. Nasi hatuna budi kwenda kwa kasi hiyo," Amesema Prof. Kabudi.  


Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ni vyema Chuo kikawa mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, na wafanyabiashara waliopo hapa nchini.

"Nimefarijika kusikia kuwa mmefanya mazungumzo na Chuo cha ISRI cha Angola kwa nia ya kufikia makubaliano ya kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili nchini Angola ambapo rasimu ya Hati ya Makubaliano imeandaliwa na inasubiri kusainiwa," Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba Balozi za Iran, Libya, Urusi, Indonesia na China zimekuwa zikitumia wigo huu wa ushirikiano na kubadilishana uzoefu, kutoa mada mbalimbali chuoni hapo. Aidha, alitumia fursa hiyo kuzikaribisha ofisi nyingine za kibalozi hapa nchini kutembelea Chuo cha Diplomasia na kutoa uzoefu wao kwa vinafunzi pamoja na wakufunzi. Hivyo basi, ni vyema menejimenti ya Chuo kutoa mwaliko kwa Balozi zote na wawakilishi wa kudumu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuja kutoa uzoefu wao kwani nayo itakuwa sehemu ya diplomasia ya ulimwengu.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Drkt. Faraji Mnyepe amesema wahitimu 453 wametunikiwa vyeti baada ya kupata mafunzo na kufuzu ambapo kati yao 98 ni wa ngazi ya Astashahada ya Msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa Shahada, 83 ni wa Stashahada ya Uzamili, 45 Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.

"Nina imani kuwa wahitimu wa leo kama wale wa miaka ya iliyopita, wameiva ipasavyo katika fani za mahusiano ya kimataifa, Diplomasia na Stratejia. Naamin pia kuwa mtakuwa rasilimali kubwa kwa Taifa letu katika fani mlizosomea" Amesema Dkt. Mnyepe.

Dkt. Mnyepe ameongeza kuwa, katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo kimeweza kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 1029 kwa 2018/19 hadi kufikia 1275 kwa mwaka wa masomo 2019/20 ambapo pamoja na mambo mengine juhudi zinaendelea katika kutanua wigo wa udahili kwa kuanziasha udahili wa mwezi Machi pamoja na kuanzisha program mpya.

 "Katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo pia kimeweza kupanua mawanda ya program zake kwa kuongeza idadi ya program za muda mrefu. Chuo kimeanzisha Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na Udhibiti wa Migogoro ambapo kwa sasa program hii inaendeshwa Dar es Salaam na Dodoma," Amesema Dkt. Mnyepe.

Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zetu mbili wa wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji. Kwa miaka yote hiyo, Chuo cha Diplomasia kimejikita kuwaandaa wanadiplomasia, wanastratejia na wabobezi wengi wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa.

Chuo kilitumika kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na baadae kilipanua huduma zake na kutumika kuwaandaa pia wapigania uhuru wa nchi za Angola, Zimbabwe, Namibia n.k.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akifungua rasmi Mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji Mnyepe akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), (katikati) akiwa katika picha ya ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji Mnyepe na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia  pamoja na wanafunzi walifaulu vizuri masomo yao


Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Faraji Mnyepe wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha Diplomasia. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akitoa hutuba yake wakati wa mhafali yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wanafunzi wakisubiri kutunikiwa 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akisoma hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe ili amkaribishe mgeni rasmi kufungua mahafali ya 22 ya chuo

Baadhi ya wahadhiri wa Chuo cha Diplomasia wakiwa wamesimama  huku wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mahafali
Baadhi ya Mabalozi na viongozi waandamizi wa Serikali wakiwa wanaimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja kati ya wanafunzi walifaulu vizuri masomo yake


 













Tuesday, January 14, 2020

NAIBU WAZIRI DKT NDUMBARO AFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI MKAZI WA ICRC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam,ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa ICRC  katika utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu hapa nchini hasa katika kambi za wakimbizi zilizopo hapa Nchini.

Amesisitiza kuwa Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa ICRC itaendelea kutimiza wajibu wake wa Kitaifa na Kimataifa na kwa kuzingatia Sheria za kimataifa  zilizopo chini ya ICRC,sheria za Tanzania na mkataba wa uenyeji (Head Quarter Agreement) kati ya Tanzania na ICRC uliosainiwa mwaka 2001.

Kwa upande wake Bw. Dubois ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuishirikisha ICRC katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususani ile inayohusu utoaji wa misaada ya kibinadamu (Humanitarian assistance) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu – Tanzania (Tanzania Red Cross Society – TRCS).

Ameongeza kuwa ICRC itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wengine katika utoaji wa huduma kwa wakimbizi walioko hapa nchini,wafungwa/mahabusu waliopo magerezani,mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama hususani wakati wa ulinzi wa amani (Training on International Humanitarian Law during peace keeping mission).

Bw. Dubois ameambatana na Bi. Andrea Heath mwakilishi Mkaazi wa ICRC – Tanzania. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akimsikiliza Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois.

Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) 

Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) Hayupo pichani. Pembeni yake anayeandika ni Bi. Andrea Heath mwakilishi Mkaazi wa ICRC – Tanzania

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam

Thursday, January 9, 2020

SERIKALI YAWATAKA MABALOZI KUZINGATIA SHERIA, TARATIBU ZA NCHI


Tanzania imewataka Mabalozi, Makaimu Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuzingatia sheria za nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao nchini kwa ufanisi na ufasaha.

Akiongea katika mkutano na Mabalozi, Makaimu Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yanajengwa katika misingi ya mkataba wa Viena, Mkataba wa umoja wa mataifa na sheria mbalimbali, hivyo ni vizuri mabalozi kuzingatia taratibu hizo.

"Sisi kama tumesisitiza kuwa ni vyema mabalozi na wawakilishi wa nchi zao wakafuata taratibu, mila pamoja na desturi zilizopo katika mikataba hiyo ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa Viena, mkataba wa umoja wa mataifa lakini pia kunga, mila na desturi za kibalozi," Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, Waziri Kabudi aliongeza kuwa Tanzania kupitia mkutano huo imeanza ukurasa mpya wa mahusiano na uendeshaji wa shughuli za Serikali na balozi pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania.

"………tunepata nguvu mpya baada ya mabalozi wote kueleza kuridhika kwao kwa hali ya juu sana na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imechukua kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha makusanyo ya kodi lakini pia kusimamia matumizi ya fedha za ndani pamoja na zile zinazotolewa na nchi mbalimbali katika maendeleo ya Tanzania,"  Amesema Prof. Kabudi.

Katika mkutano huo, Waziri Kabudi amewahamasisha mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuhusu kuhamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuwaeleza maendeleo yaliyofikiwa kuhusu ujenzi wa miundombinu mbalimbali muhimu na kwamba wakati umefika wa kuharakisha kuhamia Dodoma kwa wakati muafaka kwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa nayatoa fursa ya kuwawezesha wao kuhamia jijini Dodoma.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi hao hapa Nchini ambae pia ni Balozi wa Comoro Dkt. Ahamada Mohamed ameipongeza Tanzania kwa kuitisha mkutano huo mapema ikiwa ni siku tisa tu tangu kuanza kwa mwaka mpya wa 2020 kwa nia ya kubadilishana mawazo na kusikiliza changamoto za mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa pia kuwaelezea hatua za utekelezaji za masuala ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli jambo linalowapa fursa mabalozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi hapa nchini.

Nae balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu ambaye pia Kiongozi wa Mabalozi wa Bara la Afrika amesema wao kama mabalozi hawawezi kujua mipango, vipaumbele na changamoto za serikali bila ya kuelezwa na kutaka mikutano ya namna hiyo kufanyika mara kwa mara jambo ambalo linatoa uelewa na muelekeo wa utendaji kazi wa serikali  na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kutambua fursa na changamoto zilizopo.

Awali akiwakaribisha mabalozi katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu na kanuni za nchi ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.

"Nawasihi sana tufanye kazi kwa kuzingatia taratibu za nchi pamoja na sheria na mikataba kwa manufaa ya nchi yetu (Tanzania) na nchi zenu ili tuweze kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina yetu kwa maendeleo endelevu" Amesema Dkt. Mnyepe

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro,Katibu Mkuu Dkt Faraji Mnyepe na Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge, mabalozi 28, Makaimu Mabalozi 12 na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa 10.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akiongea na mabalozi, (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na mabalozi, manaibu mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam

Baadhi ya mabalozi wakifuaatilia mkutano baina yao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (katikati), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb),Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe na Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge wakiwa katika picha ya pamoja na mabalozi








Wednesday, January 8, 2020

PROF. KABUDI AKUTANA, KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA UNICEF NCHINI TANZANIA


...Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akutana, Balozi mteule wa Ujerumani nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi amemweleza Bi. Shalini Bahuguna kuwa UNICEF imekuwa na mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.

"Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho," Amesema Prof. Kabudi

Waziri Kabudi amemueleza Bi. Bahuguna kuwa tangu mwaka 2016 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa kuboresha sekta za elimu na afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe. 

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini, Bi. Bahuguna amesema kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kulinda haki za watoto.

"Haki za watoto katika taifa ni jambo muhimu sana, hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu," Amesema Bi. Bahuguna.

Katika tukio jingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa Tanzania na Ujerumani ambao ulijengwa tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambapo Tanzania na Ujerumani zina historia ndefu na zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika nyanja za kiutamaduni, kiuchumi na afya.

Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine, Mhe. Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ushirikiano unaolenga kuleta tija katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili.


Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipomtembelea na kufanya nae mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess wakati Balozi Hess alipomtembelea Naibu Waziri katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimkabidhi nakala ya Hati ya Utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




Tuesday, January 7, 2020

MFANYABIASHARA KUTOKA INDIA YUKO NCHINI KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI



MFANYABIASHARA KUTOKA INDIA YUKO NCHINI KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI

Dodoma, 7 Januari 2020

Mfanyabiashara kutoka nchini India, Bw.Vivek Agarwala yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia tarehe 6 hadi 12 Januari 2020. Bw. Agwarala ambaye amekuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini, atafanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na kutembelea maeneo kadhaa kwa lengo la kupata maelezo kuhusu taratibu na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Maeneo yatakayotembelewa na mfanyabiashara huyo ni Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) Dar es Salaam, Mkoa wa Simiyu ambapo ataangalia uwezekano wa kupata eneo la ekari elfu mbili (2,000) kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mpunga na ujenzi wa kiwanda zao hilo. Bw. Agarwala atatembelea maghala ya pamba ili kujiridhisha kabla ya kununua kiasi cha robota laki moja (100,000) ambayo aliahidi kununua wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB mwezi Desemba 2019. 

Bw. Agarwala pia atatembelea machimbo ya Tanzanite, mkoani Manyara, Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi kilichopo mkoani Iringa na kuangalia uzalishaji maparachichi ili kujenga kiwanda cha kusindika zao hilo kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi. 

Ujio wa mfanyabiashara huyo ni matokeo ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini India ambao uliratibu ziara ya kikazi iliyofanywa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji-Uendeshaji na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts iliyofanyika nchini India mwezi Desemba mwaka jana. Ziara hiyo ililenga kutafuta wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo soko la pamba nchini humo. 

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.