Thursday, September 9, 2021

UINGEREZA IMEIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA, UWEKEZAJI, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Uingereza imeipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, Haki za Binadamu na Utawala Bora, jambo ambalo limeimarisha ushirikiano baina ya Nchi hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge, ukiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ya awali kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri huyo alipofanya ziara hapa nchini

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kutokana na mazungumzo hayo Uingereza na Tanzania zimekubaliana kufanya kongamano kubwa litakalojumuisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uingereza ili kuja kuwekeza hapa nchini. 

Pia Balozi Mulamula ameishukuru Uingereza kwa kuiunga mkono Tanzania katika bodi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jambo lililoiwezesha Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na adhari za UVIKO 19.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami, ambapo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulisaidia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari.

“Ili shirika hili liendelee kuhudumia vyema wakimbizi ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa ikaendelea kutoa mchango wake, hasa kwa kuwaongezea bajeti UNHCR ambayo itawawezesha kutimiza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi” alisema Mheshimiwa Balozi Mulamula 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami kwa niaba ya Shirika hilo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa muda mrefu katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi. 

Ofisi ya Kikanda ya UNHCR iliyopo Kasulu, Kigoma inahudumia nchi Kumi na Moja (11) ambazo ni; Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, South Sudan, Tanzania and Uganda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami yaliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Gerald Mbwafu baada ya kumaliza mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara na Watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi.

Monday, September 6, 2021

SERIKALI YAAINISHA VIPAUMBELE SEKTA YA AFYA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali imeainisha vipaumbele vitakavyonufaika na mradi wa sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ufadhili wa Serikali ya Italia.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee Prof. Abel Makubi amevitaja hivyo alipokutana na madaktari kutoka Italia leo Jijini Dar es Salaam ambavyo ni mafunzo kwa wataalamu wa afya katika hospitali za mkoa, kanda na Taifa kwa ujumla, kununua vifaa vya matibabu vya kisasa, kujenga na kukarabati hospitali za kanda na taifa.

“Vipaumbele vingine ni kuanzisha na kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Italia, kuimarisha mifumo ya maabara katika hospitali na kuendelea kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 ikiwa ni pamoja na kuelimisha umuhimu wa chanjo” amesema Prof. Makubi.

Kwa upande wake Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amelipongeza Shirika la Maendeleo la Italia kwa kutenga Euro 1,250,000 za msaada wenye manufaa kwa sekta ya afya nchini.

“Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia ni wa muda mrefu na imara, naomba nikuhakikishie kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kwa maslahi ya pande zote mbili na kwetu sisi kama Italia huu ni mwanzo na tunaamini kuwa kupitia mradi huu uhusiano wetu utaendelea kuimarika zaidi,” amesema Balozi Lombardi.

Nae Dkt. Davide Bonechi, Daktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani amesema kuwa kupitia mpango wao wa kuboresha na kuimarisha sekta ya afya katika ukanda wa Afrika, mbali na Tanzania nchi nyingine zitakazo nufaika na mpango huo ni Kenya na Uganda.

 

“Lengo letu ni kuboresha sekta ya afya kwa ujumla pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kukabiliana na magonjwa mbalimbali yanayowapata binadamu,” amesema Dkt. Bonechi

Tarehe 3 September ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia uliwasili Tanzania kwa ziara maalum ya kutathmini na kufahamu mahitaji na vipaumbele vya Tanzania katika ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.

Ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia unaongozwa na Dkt. Davide Bonechi, Dkt. Giulia Dagliana, pamoja na Dkt. Beatrice Borchi, wote wakitoka katika Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.

Tanzania imekuwa ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ambapo ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa. Kuanzia wakati huo, Serikali ya Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya hapa nchini kama vile miradi ya kupambana na utapiamlo, afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya virusi vya ukimwi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea madaktari wa binadamu na wataalamu wa dawa za binadamu kutoka Italia ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kutoa huduma za matibabu. 

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akielezea jambo katika kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi (kulia) akiwaelezea vipaumbele vya Serikali sekta ya afya madaktari kutoka Italia. Madaktari hao wameambatana na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi.   


Mmoja kati ya madaktari kutoka Italia akieleza jambo wakati wa kikao


Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao


Kikao kikiendelea 



Friday, September 3, 2021

TANZANIA, UFARANSA NI UJUMBE WA UTULIVU NA AMANI DUNIANI

  Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Ufaransa zimetajwa kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo duniani na kwamba tukio la hivi karibuni katika ubalozi huo halikuathiri kwa namna yeyote mahusiano baina ya Nchi hizo.

Balozi wa Ufaransa hapa nchini mhe. Frederic Clavier ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana kwa mazungumzo pamoja na kumuaga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini na kuongeza kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake ameiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu,amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

“Katika kipindi chote cha uwakilishi wangu hapa Tanzania, nimeiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla,” Amesema Balozi Clavier.

Balozi Clavier ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Ufaransa na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, miundombinu biashara na uwekezaji umeendelea kukua kwa kiwango kikubwa na kwamba Ufaransa itaendela kukuza mahusiano hayo ya kihistoria baina ya nchi hizo mbili.

Ameongeza kuwa Ufaransa itaendelea kutoa kipaumbele katika kuendeleza uchumi wa buluu ambao kwa sasa umewekewa mikakati mahususi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama chanzo kipya cha kuongeza mapato ya serikali lakini pia kupunguza umasikini kwa Watanzania wote na kwamba anaporejea Ufaransa atahamasisha makampuni, wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemshukuru Balozi Frederic Clavier kwa kuimarisha na kuendeleza mahusiano baina ya Tanzania na Ufaransa.

Balozi Mulamula amempa pole Balozi huyo kwa tukio la kihalifu lililotokea hivi karibuni katika Ubalozi wa Ufaransa na kumhakikishia kuwa licha ya tukio hilo ambalo lilidhibitiwa na vyombo vya dola,Tanzania ni salama.

Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Maongezi baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  


Maongezi baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula (Mb) akitoa zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro kwa Balozi wa Ufaransa aliyemaliza muda wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Frederic Clavier  



Wednesday, September 1, 2021

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CANADA NCHINI


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, leo terehe 1 Septemba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pamela O’Donnell Balozi wa Canada nchini Tanzania, yaliyofanyika jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo hayo Balozi Sokoine na Balozi Pamela O’Donnell wamejadili masuala mbalimbali muhimu katika kudumisha na kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na ushirikiano katika masuala ya uchumi baina ya Tanzania na Canada. Kwa kipindi cha takribani miongo sita mahusiano ya Tanzania na Canada yamejikita katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii kama vile maendeleo ya viwanda, afya, kuendeleza rasilimali watu, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa mazingira. 

Tanzania ilianzisha mahusiano ya kidiplomasia na Canada mwaka 1961 mara baada ya uhuru. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell wakijadili jambo walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.
Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’Donnell akielezea jambo kwenye mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine. 

Mazungumzo yakiendelea




Umoja wa Mataifa umetangaza nafasi ya kazi ya Katibu Mkuu Msaidizi atakayeshughulikia masuala ya Amani (Assistant Secretary General for Peacebuilding Support). Fursa hii iko wazi kwa nchi wanachama wote wa Umoja wa Mataifa. 


Maelezo zaidi ya nafasi hiyo na jinsi ya kuwasilisha maombi yanapatikana kupitia  ukurasa wa Tovuti ya Umoja wa Mataifa wa https://www.un.org/peacebuilding/supportoffice.
 
Mwisho wa kupokea maombi hayo ni tarehe 20 Septemba 2021.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi hiyo.

Tuesday, August 31, 2021

UYOGA WA TANZANIA KUPATA SOKO NCHINI UHOLANZI

Balozi Irene Kasyanju (katikati) akiwa katika mazungumzo na uongozi wa LIMAX Group ulioongozwa na Mkurugenzi na Mmiliki wa Kampuni hiyo, Bw. Tom van WALSEM (wa pili kushoto) kuhusu soko la uyoga wa Tanzania nchini Uholanzi kwenye Ofisi za Kampuni hiyo zilizopo katika Mji wa Horst, Uholanzi. LIMAX Group inazalisha faida/pato kwa mwaka (annual turnover) la takriban Euro milioni 25. 

Balozi Irene Kasyanju (kulia) akiangalia namna uyoga unavyofungashwa kwenye makasha (packaging) tayari kwa kupelekwa sokoni huku akipatiwa maelezo ya mchakato mzima wa ufungaji kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa LIMAX Group, Bw. Rob Menheere (kushoto). Katikati ni Bw. Petro Mahuwi “intern” Mtanzania aliyeongozana na Balozi Kasyanju kwenye ziara hiyo.


Namna kitalu kimoja wapo cha uyoga uliopandwa na ambao unakaribia kuvunwa kinavyoonekana katika moja ya mashamba makubwa 4 ya LIMAX Group iliyoko Horst, Uholanzi.

Balozi Kasyanju (kushoto) akiwa na Mkurugenzi na Mmiliki wa LIMAX Group, Bw. Tom van WALSEM (wa kwanza kushoto); Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Rob Menheere (wa pili kushoto); na Meneja Biashara, Bw. Mark Duppen (wa tatu kushoto) wakikamilisha mazungumzo yao baada ya zoezi la kutembelea mashamba ya uyoga mjini Horst, Uholanzi kukamilika.


----------------------------

UYOGA WA TANZANIA KUPATA SOKO NCHINI UHOLANZI

Kampuni maarufu ya Uholanzi, LIMAX B.V. (LimaxGroup) imedhamiria kuwekeza kwenye Sekta ya Uyoga nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kusindika na kukausha uyoga Mkoani Iringa kwa thamani ya Euro milioni 2.1 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 5.5 za Tanzania. Hayo yameelezwa kufuatia Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju kutembelea kampuni hiyo tarehe 26 Agosti 2021 na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi na Mmiliki wa kampuni hiyo, Bw. Tom VanWalsem.

Balozi Kasyanju alieleza kuwa uwekezaji huo utakapokamilika, Tanzania itafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na mtiririko wa biashara ya uyoga kukua kwa kasi duniani ambapo kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), biashara hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 62.2 ifikapo mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani bilioni 42.4 mwaka 2018.

Balozi Kasyanju aliendelea kueleza kuwa Kilimo cha uyoga ni sekta inayostawi nchini Tanzania na thamani yake ya kila mwaka inakadiriwa kuwa Tsh. Bilioni 4. Hivyo, ni dhahiri kuwa uwekezaji wa LimaxGroup utakuwa na tija kubwa na wazalishaji wa uyoga nchini watafaidika na soko kubwa lililopo katika Jumuiya ya Ulaya likiongozwa na Uholanzi ikifuatiwa na Ujerumani na baadaye Poland.

Balozi Kasyanju akiwa katika kampuni hiyo alipata fursa ya kujionea mashamba ya kisasa ya uyoga unaozalishwa (sio wa asili) na namna zao hilo lenye faida kubwa kwa binadamu linavyosindikwa na kufungashwa (processed and packed) na kuelezea matumaini yake kuwa Tanzania itafaidika na uwezo, uzoefu na utaalam mkubwa wa biashara wa Kampuni  hiyo.

“Tanzania ni nchi yenye maeneo makubwa ya misitu yenye aina anuwai ya uyoga wa porini kwa ajili ya kula, na jamii zimekuwa zinategemea maarifa asilia kukusanya uyoga huo kwa matumizi na kuuza katika masoko ya ndani tu. Ni wakati muafaka sasa kufanya kazi pamoja kukuza ukuaji wa sekta hii kibiashara”., Balozi Kasyanju alisema.

LIMAXGroup itatoa mafunzo ya kuhifadhi na kuvuna uyoga wa porini kwa madhumuni ya biashara na kulinda mazingira pia. Aidha, ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Iringa kutawawezesha wakulima kuuza uyoga wanaozalisha moja kwa moja kiwandani, kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mnyororo wa thamani wa kilimo cha uyoga nchini. 


Saturday, August 28, 2021

BALOZI LIBERATA MULAMULA KATIKA KIKAO KAZI NA MAAFISA WA UBALOZI WA KUDUMU KATIKA UMOJA WA MATAIFA - NEW YORK, MAREKANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Uwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa New York,Marekani(hawapo pichani)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Uwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa New York,Marekani; kushoto kwa Balozi Mulamula ni Balozi wa Tanzania  katika umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Uwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa New York,Marekani

Baadhi ya Maafisa katika Ubalozi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa New York,Marekani wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb)





 

BALOZI MULAMULA AKIZUNGUMZA NA MHE. FLEMMING MOLLER MORTNSEN KWA NJIA YA MTANDAO KUHUSU UAMUZI WA KUFUNGA SHUGHULI ZA UBALOZI WA DENMARK

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza kwa nia ya mtandao (video conferencing) na Waziri Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Flemming Moller Mortensen kuhusu hamuzi wa Denmark kufunga shughuli za Ubalozi wake Nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza kwa njia ya mtandao (video conferencing) na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Flemming Moller Mortensen kuhusu uamuzi wa Denmark kufunga shughuli za Ubalozi wake Nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya Balozi Swahiba Mndeme (kushoto kwa Balozi Mulamula) pamoja na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Jean Msabila wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Flemming Moller Mortensen kuhusu uamuzi wa Denmark kufunga shughuli za Ubalozi wake Nchini Tanzania

 

Friday, August 27, 2021

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA BALOZI WA INDIA, ALGERIA NA SWEDEN

 Na Mwandishi wetu, Dar 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Sokoine amekutana kwa nyakati tofauti na mabalozi hao ambao ni Balozi wa India hapa nchini Mhe. Binaya Pradhan, Balozi wa Algeria hapa nchini Mhe. Ahmed Djellal pamoja na Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjöberg.

Pamoja na Mambo mengine viongozi hao wamejadili masuala ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ulipo baina ya Tanzania na mataifa hayo ambapo awali Balozi wa India Mhe. Pradhan ameahidi kuendeleza na kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya India na Tanzania.

“Nimemhakikishia Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Sokoine kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa yetu kwa maslahi ya pande zote mbili katika sekta mbalimbali ikiwemo Utalii, elimu, gesi, biashara na uwekezaji,” amesema Balozi Pradhan

Kwa upande wake, Balozi wa Algeria hapa nchini, Mhe. Djellal amesema kuwa mazungumzo yao yaligusia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Algeria na Tanzania.

“Tumekubaliana kuendelea kuimarisha diplomasia baina ya mataifa yetu kwa maslahi mapana……….na kwa maendeleo ya wananchi wetu,” amesema Balozi Djellal     

Nae balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Sjöberg amesema katika jitihada za kuendeleza uhusiano wa Sweden na Tanzania, Sweden itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Sokoine amewahakikishia mabalozi hao ushirikiano wa kutosha kutoka Tanzania.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Binaya Pradhan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Algeria hapa nchini Mhe. Ahmed Djellal akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjöberg akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam