Saturday, October 23, 2021

RAIS WA BURUNDI ATEMBELEA BANDARI KAVU – KWALA

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye amewasili leo mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla. Mhe. Ndayishime ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb).

Mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, Mhe. Ndayishimiye alielekea katika Stesheni ya Pugu na kapata taarifa fupi kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa kutoka Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora na Mwanza – Isaka ikiwa ni jumla ya Kilomita 1063 za njia kuu na njia za kupishania.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli, Bw. Masanja Kadogosa amemueleza Mhe. Ndayishimiye kuwa hadi sasa ujenzi wa SGR (kipande cha Pugu - Morogoro) umefikia asilimia 94 na kuwa unaendelea vizuri.

Aidha, mara baada ya kupata taarifa fupi kuhusu mradi wa ujenzi wa SGR, Mhe. Rais Ndayishimiye ametembelea bandari kavu eneo la Kwala Mkoani Pwani.

Mhe. Ndayishimiye amesema kuwa eneo la bandari kavu (Kwala) litakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi na litatusaidia kupunguza gharama za usafiri na fedha zitakazookolewa zitaenda kwenye miradi mingine.

“Mradi huu pia utapunguza gharama za bidhaa mbalimbali Nchini Burundi, kwetu sisi Burundi, mtu akikupa eneo amekuthamini sawa na kukuunga undugu kwenye familia yake,” amesema Mhe. Ndayishimie.

Awali akitoa taarifa ya eneo hilo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema eneo hilo lina ukubwa wa hekta 502, kati ya hizo hekta 10 zimetengwa kwa ajili ya Serikali ya Burundi.

“Dhumuni la kutenga eneo hili ni kupunguza msongamano wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam,” Amesema Prof. Mbarawa na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya eneo hili utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 37.23

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa kupitia mradi wa ujenzi wa bandari kavu eno la Kwala utasaidia kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Burundi pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla. mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar. Mhe. Ndayishime katika ziara yake ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb).


Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) na baadhi ya Mabalozi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Bw. Masanja Kadogosa alipokuwa akitoa taarifa fupi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wakati Mhe. Ndayishimiye alipowasili leo katika Stesheni ya Pugu ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu hapa nchini  


Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) na baadhi ya Mabalozi wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Tanzania Bw. Eric Hamissi alipokuwa akitoa taarifa ya eneo la Bandari Kavu (Kwala) mkoani Pwani leo


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa hotuba yake kwa wananchi wa Kwala kabla ya mkaribisha Rais wa Jamhuri ya Burundi kuongea na wananchi wa eneo la Bandari Kavu (Kwala) mkoani Pwani 


Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akihutubia wananchi wa Kwala wakati alipotembelea eneo la Bandari Kavu leo mkoani Pwani


Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akipokea nakala ya hati ya eneo lenye ukubwa wa hekta 10 zilizotengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Serikali ya Burundi kutoka kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb)




Dunia yatakiwa kujipanga kukabili magonjwa ya Mlipuko

Dunia yatakiwa kujipanga kukabili magonjwa ya Mlipuko

Ugonjwa wa Corona (UVIKO-19) umesababisha changamoto nyingi duniani katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, uchumi, usafirishaji, maji na utalii, hivyo dunia imetakiwa kuchukua changamoto hizo kama funzo ili kujipanga upya na namna ya kukabiliana na majanga ya mlipuko.

Hayo yemeelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokuwa anahutubia katika sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.

Dkt. Tax alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Kujijenga tena kwa kujenga mifumo ya afya bora” ni kielelezo cha wazi kuwa dunia haina budi kushirikiana ili kujenga mifumo madhubuti ya afya yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Lengo la mifumo hiyo ni kuhakikisha kuwa nchi hazipati athari kubwa zinazosababishwa na majanga kama hili la mlipuko wa UVIKO-19.

Dkt. Tax aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake katika sekta mbalimbali nchini na kuuahidi umoja huo na wadau wengine wa maendeleo kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana nao katika kukabiliana na janga la Corona. Alifafanua kuwa Serikali itaendelea kufuata miongozo yote inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na kujenga mfumo imara wa afya wenye kuhakikisha vituo bora vya afya, watumishi wa kutosha, vitendea kazi, dawa na miundombinu mingine ili kutoa huduma bora za afya nchini.

Alisema Serikali ilishaweka mikakati ya utekelezaji wa haya yote katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma hivi karibuni.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi kutumia fursa ya chanjo zilizopo nchini, kwa kuwa chanjo hizo zinapatikana kwa tabu na hadimu duniani.  

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic alisema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo, inaashiria kuwa Umoja wa Mataifa una dhamira ya dhati ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama za afya, elimu mazingira ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na wageni wengine waalikwa wakiwa wamesimama kwa ajili ya Wimbo wa Taifa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake ikiwa ni moja ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akishuhudia upandishaji wa Bendera ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni moja ya tukio muhimu katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi walioshiriki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa wakifuatilia hotuba za viongozi akiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Dua ya kubariki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa
Dua ya kubariki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zaitan Milišić akisoma Hotuba katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa jijini Dodoma.
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Lumumba ya mjini Zanzibar wakiimba ngonjera ya kuhamasisha watu kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo ya UVIKO-19.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Macocha Tembele akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuzungumza na wageni waalikwa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia mamia ya watu walioshiriki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umojha wa Mataifa jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka akitoa neno la shukurani kufuatia sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa kufanyika Dodoma.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea cheti kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zaitan Milišić.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari za Lumumba na Chinangali ambao waliimba ngonjera na shairi kwa ajili ya kuhamasisha chanjo ya UVIKO-19.

Friday, October 22, 2021

Rais Ndayishimiye aweka jiwe la msingi kiwanda cha mbolea cha ItraCom jijini Dodoma

 

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye akiwasalimia wananchi (hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa kiwanda cha Mbolea ya Asili cha ItraCom jijini Dodoma alipotembelea kiwanda hicho

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye akizindua kiwanda cha Mbolea ya Asili cha ItraCom jijini Dodoma

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika uzinduzi wa kiwanda cha Mbolea ya Asili cha ItraCom jijini Dodoma uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye .

Rais Samia ampokea Rais Ndayishimiye wa Burundi Ikulu Chamwino jijjini Dodoma


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkaribisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alipowasili ikulu ya Chamwino jijini Dodoma
 
Rais wa Burundi Mhe. Everiste Ndayishimye akiwa jukwaani na mwenyeji wake Mhe, Samia Suluhu Hassan wakati nyimbo za Taifa za mataifa ya Burundi na Tanzania zikipigwa kwa heshima yake baada ya kuwasili Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye akikagua gwaride la heshima katika viwanja vya Ikulu  Chamwino jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwatambulisha kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye viongozi mbalimbali waliofika kumlaki katika viwanja vya Ikulu Chamwino

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye wakiwa katika mazungumzo Ikulu Chamwino


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye wakifuatilia utaratibu wa kufuata kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari  katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

 Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza mbele ya waandishi wa habari kuhusiana na mazungumzo yao na ujumbe wa Burundi yaliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Everiste Ndayishimiye akimshukuru Mhe. Rais Samia baada ya kumaliza kuongea na waandishi wa habari  katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

 

 

RAIS NDAYISHIMIYE WA BURUNDI AWASILI NCHINI

      

Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye akiwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku tatu ya kitaifa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma.
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimtambulisha Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko kwa  Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma.
   
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimtambulisha Mkurugenzi Idara ya Afrika, Balozi Naimi Aziz kwa  Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwatambulisha viongozi mbalimbali walifika uwanjani kumlaki  Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma
Mhe. Rais Ndayishimiye akisalimia wananchi waliofika uwanjani  kumlaki alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma.
 
 

MAADHIMISHO YA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA KUFANYIKA DODOMA

 


Wednesday, October 20, 2021

SERIKALI YAZIHAKIKISHIA KAMPUNI ZA UFARANSA MAZINGIRA SALAMA UWEKEZAJI

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Tanzania imezihakikishia Kampuni za Kifaransa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni salama na kuwasihi kuwekeza kwa wingi hapa nchini.

Akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema Serikali imewahakikishia wafanyabishara na wawekezaji wa kampuni za Kifaransa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inajenga na inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuondoa kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wawekezaji hapa nchini.

“Serikali ya Awamu ya Sita iko serious….. na tuna azma kubwa ya kuhakikisha kwamba tunajenga mazingira rafiki ya kuweza kuwekeza na kuondoa kero zote ambazo zimekuwa zinajitokeza….na makampuni mengine yameeleza hizo kero lakini tunafurahi kuona kero hizo tayari zimeanza kuondolewa,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Wafaransa wamekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kwa muda mrefu na hivi sasa wamekuwa na shauku ya kufanya biashara na kuwekeza kwa wingi hapa nchini…..ambapo takwimu zinaonesha watalii kutoka Ufaransa kuja Tanzania kila mwezi ni zaidi ya watalii 7000 wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini, hivyo ni changamoto kwetu kuchangamkia fursa hii adhimu.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester amesema Ufaransa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mambo ambayo pia yanatiliwa mkazo na serikali ya Ufaransa.

“Ufaransa imedhamiria kuongeza ushirikiano na Tanzania na kama mlivyoshuhudia leo tumeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Paris hadi Zanzibar ambao ulisimama tangu mwaka 1974, huu ni mwanzo mzuri” amesema Mhe. Riester  

Mhe. Riester ameongeza kuwa wataendelea kuwaeleza na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Ufaransa juu ya fursa mbalimbali zinazopatika Tanzania ikiwemo katika sekta ya Nishati, Utalii, Viwanda, Usafirishaji pamoja na Uwekezaji ili kuja kuwekeza na kukuza ucbumi wa pande zote mbili.

Mawaziri wa Kisekta waliohudhuria kongamano hilo ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (Mb) Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) Waziri wa Uwekezaji – Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) na Waziri wa Ofisi ya Rais Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb).

Kampuni zilizoshiriki katika kongamano hilo ni pamoja na; CMA-CGM, Bolloré, Airbus, Thales, Lagardére, Total, Chama cha Wafanyabiashara wa Ufaransa-Tanzania, Engie pamoja na Maurel & Prom.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na washiriki wa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester akiongea na washiriki wa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam


Mawaziri wa Kisekta pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Ufaransa wakiendelea na Kongamano Jijini Dar es Salaam


Mawaziri wa Kisekta pamoja na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Ufaransa wakiendelea na Kongamano Jijini Dar es Salaam


Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Ufaransa wakiendelea na Kongamano Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb)  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester 



RAIS NDAYISHIMIYE WA BURUNDI KUZURU TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Oktoba, 2021.

Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesema Mhe. Rais Ndayishimiye atawasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma tarehe 22 Oktoba na kuelekea Ikulu ya Chamwino ambako atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Waziri Mulamula amesema baada ya kuwasili Ikulu ya Chamwino, Rais Ndayishimiye atakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake na baadae viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na kufuatiwa na mazungumzo rasmi.

Balozi Mulamula amesema akiwa jijini Dodoma tarehe 22 Oktoba mchana, Mhe.Rais Ndayishimiye atatembelea na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa madini ya phosphate na samadi kinachojengwa katika eneo la viwanda la Nala, kiwanda ambacho kinajengwa na Wawekezaji wa kampuni ya Itracom Fertilizers Limited (ITRACOM) kutoka nchini Burundi na baadaye jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa tarehe 23 Oktoba 2021 Mhe. Rais Ndayishimiye ataelekea Zanzibar ambako atapokelewa na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake huyo na baadaye ataelelekea Mkoani Dar es Salaam ambapo ataungana na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia .

Amesema akiwa jijini Dar es Salaam Rais Ndayishimiye anatarajiwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaoendelea nchini kutokea stesheni ya Dar es salaam hadi stesheni ya Kwala - Ruvu pamoja na kutembelea bandari kavu ya Kwala inayojengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania katika eneo hilo la Kwala mkoani Pwani ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu hiyo.

Akizungumzia ziara hiyo ya Rais Ndayishimiye nchini, Balozi Mulamula amesema ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Serikali za Tanzania na Burundi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa maslahi ya pande zote na itaendeleza na kukuza ushirikiano uliopo na kufungua fursa ya kuanzisha maeneo mingine ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Waheshimiwa Marais hao (wa Tanzania na Burundi) kufahamu hatua zilizofikiwa katika kutekeleza maagizo yao waliyoyatoa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Burundi tarehe 16 na 17 Julai, 2021.

Balozi Mulamula amesema Mhe. Rais Ndayishimiye na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini kurejea Burundi tarehe 24 Oktoba 2021 baada ya kumaliza ziara yake.

 

 


 

Tuesday, October 19, 2021

UFARANSA KUKARABATI UWANJA WA NDEGE “TERMINAL TWO”

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Tanzania na Ufaransa zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo ya kimkakati ikiwemo Nishati, Elimu, Kilimo na Miundombinu ambapo Ufaransa imekubali kukarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘Terminal Two’ Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester leo alipowasili Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku moja.   

Kumekuwa na Miradi ambayo Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lao la Maendeleo wamekuwa wakifadhili Miradi mbalimbali katika Sekta mbalimbali hapa nchini zikiwemo sekta za Nishati, Elimu, Kilimo na Miundombinu.

Mtakumbuka kuwa Ufaransa ndiyo waliojenga Uwanja wa Ndege wa “Termirnal Two” wa Julius Kambarage Nyerere sasa wanakuja na mradi wa kukarabati uwanja huo na kuufanya kuwa wa kisasa zaidi. Sasa hivi tu terminal three lakini terminal two imekuwa ikitumika na ndege zinazofanya safari zake za ndani hapa nchini……..mradi huu ni moja kati ya mradi mkubwa na utakamilika hivi karibuni.

Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester yupo nchini Tanzania kuzindua safari za Shirika la ndege la Ufaransa ‘Fance Airline’ kutoka Paris hadi Zanzibar ambapo mara ya mwisho kwa shirika hilo kufanya safari zake hapa nchini ilikuwa mwaka 1974.

Septemba 15, 2021 Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Nabil Hajlaouvi alisema Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la ndege ‘Fance Airline’ inategemea kuanzisha safari mpya ya ndege kutoka Ufaransa moja kwa moja hadi Zanzibar kuanzia 19 Oktoba 2021.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Colin Powell.

“Kwa kweli Serikali ya Tanzania tumeshtushwa sana na kifo chake………katika kipindi chake aliendeleza uhusiano wa Marekani na Mataifa mbalimbali, kwa kweli ni masikitiko makubwa tutamkumbuka daima,” Amesema Balozi Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester leo alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku moja


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) (wa saba kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester (kushoto kwa Balozi Mulamula) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wa tano kutoka kulia) pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku moja


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb).


Maongeza baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester yakiendelea. Maongezi hayo pia yamehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa Mhe. Samwel Shelukindo, Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania Mhe. Nabil Hajlaouvi pamoja na viongozi mbalimbali.    


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa Mhe. Samwel Shelukindo, pamoja na Mkurugezi wa Idara ya Amerika na Ulaya Balozi Swahiba Mndeme  wakifuatilia kikao cha Waziri Mulamula na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester akieleza jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa leo Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester leo Jijini Dar es Salaam


Mawaziri wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi leo Jijini Dar es Salaam