Thursday, August 3, 2023

TANZANIA YAFANYA UFUNGUZI RASMI WA UBALOZI JIJINI ALGIERS, ALGERIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wake jijini Algiers, Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf,  Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.

Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Akihutubia kwenye ufunguzi wa Ubalozi huo Waziri Tax ameeleza kuwa Tanzania na Algeria zimejidhatiti kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa lengo la kukuza ushirikiano wenye maslahi kupitia sekta za kipaumbele.

‘’Ni imani yangu kuwa Ubalozi huu utaendelea kuwa kiunganishi kati ya serikali zetu kwa kutoa huduma za kidiplomasia, kuhudumia Watanzania” alisema Dkt. Tax

Naye Mhe. Attaf ameeleza kuwa ziara ya Waziri Tax imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kuzungumza masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.

‘’Balozi zetu zitaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ili nia ya dhati ya kuimarisha na kukuza uhusiano iweze kuleta tija zaidi na kuziwezesha nchi zetu kunufaika kiuchumi,’’ alisema Mhe. Attaf.

Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa Hati 8 za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya. 

Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.

=====================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikata utepe kuashiria ufunguzi wa ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023 jijini Algiers. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf na kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst) Jacob Kingu wakishuhudia ufunguzi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf wakiwa katika ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipongezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf baada ya kukamilisha taratibu za ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.


Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (mwenye tai ya bluu) akifatilia hotuba zilizowasilishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Dkt. Tax na na Mhe. Attaf.


Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Algeria, Balozi Selma Malika na Balozi Djoudi wakifatilia hafla ya ufunguzi huo.

Picha ya pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf.

Picha ya Pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf na Watumishi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria na ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkabidhi zawadi Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023.

Wednesday, August 2, 2023

RAIS WA ALGERIA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA WAZIRI TAX

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune amekutana Kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipomtembelea Ikulu Jijini Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.

Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria unaofanyika kuanzia tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023. 

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na kidiplomasia ili kuweza kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi zao.

Aidha, katika kuendelea kuimarisha ushirikiano Waziri Tax pamoja na majukumu mengine, atazindua Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Agosti 2023 Jijini Algiers.

Uzinduzi wa ubalozi huo, ni hatua muhimu hasa wakati huu ambapo viongozi hao wamekubaliana kuinua sekta za uchumi ambazo ni pamoja na biashara, uwekezaji, nishati, madini, elimu, sayansi na teknolojia, afya na utalii.

======================================

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipomtembelea ofisini kwake Ikulu Jijini Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst) Jacob Kingu ambaye alifuatana na Waziri Tax Ikulu ya Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune akisalimiana na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mhe. Ahmed Djellal baada ya kuwasili Ikulu Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiongea mbele ya waandishi wa Habari katika Ikulu ya Algiers baada ya kumalizika kwa mazungumzo yake na Mheshimiwa Rais Abdelmadjid Tebboune Ikulu  Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023

Baada ya Kuwasili katika Ikulu ya Algiers, Algeria.


TANZANIA NA ALGERIA ZASAINI HATI 8 ZA MAKUBALIANO NA MIKATABA YA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesaini Hati 8 za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za umeme, gesi, biashara, viwanda na kilimo, utamaduni na sanaa, kumbukumbu na nyaraka, mafunzo katika vyuo vya diplomasia na ushirikiano katika taaluma na teknolojia.

Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria.

Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 30 hadi 31 Julai 2023.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati

Madhumuni ya mkutano huo ni kutathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye Mkutano wa Nne uliofanyika mwaka 2010 jijini Dar es Salaam.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Tax ameleza kuwa mkutano huu ni kielezo cha dhamira ya dhati kati ya Tanzania na Algeria kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka mfumo rasmi wa kujitathimini katika masuala mbalimbali yaliyokubalika.

‘’ Ni imani yangu kuwa wataalam wetu wamefanya kazi kubwa katika majadiliano kwa kuangalia maeneo muhimu na ya kipaumbele ili kuendelea kukuza ushirikiano kwa maslahi ya nchi zote mbili" alisema Dkt. Tax.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf katika hotuba yake ameeleza kuwa  mkutano huo umetoa fursa ya kujadili na kukubaliana maeneo ya kipaumbele kwa maslahi ya pande mbili. 

Pia ameeleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano ni ishara ya wazi kuwa nchi hizi zitaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo sanjari na kukuza ushirikiano kwenye maeneo mapya yenye tija. 

‘’Serikali ya Algeria itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi pamoja ili kufikia malengo tuliyojiwekea katika sekta mahsusi za ushirikiano,’’ alisema Mhe. Attaf.


Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Attaf wamewashukuru Wakuu wa Nchi wa pande zote mbili kwa utayari na jitihada zao wanazozifanya katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarishwa zaidi kwa maslahi mapana ya nchi mbili.

Mkutano huo umejadili na kutathimini utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano katika Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi na Afya, na Sanaa na Utamaduni.

Katika kuendelea kuhakikisha kwamba Tanzania na Algeria  zinatekeleza maazimio ya mkutano husika, nchi hizi mbili zimekubaliana kuitisha mkutano wa sita utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2025.

====================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria. Pembeni yake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.

Kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst) Jacob Kingu na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.

Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.

Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe pamoja na viongozi wengine Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika mafunzo ya diplomasia kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Diplomasia cha Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.
===========================

Matukio katika picha viongozi kutoka sekta za ushirikiano kati ya  Tanzania na Algeria wakisaini Hati za Makubaliano na Mikataba ya Ushirikiano wakati Mkutano
 wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria.




Sunday, July 30, 2023

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza diplomasia ya uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi unaoendelea jijini Algiers, Algeria.

Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 1 Agosti 2023 nchini humo ambapo ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.).

Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo. Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni: Naibu Makatibu Wakuu kutoka sekta za Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati.

Aidha, kwa upande wa Serikali ya Algeria, Mkutano huo ulifunguliwa na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Selma Malika na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi kutoka nchini humo.

Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.

Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.

‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo.

Naye Balozi Selma Malika katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.

‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara, mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.

Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou ulilosababishwa na ongezeko la joto kali. 

Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara, viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia, mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.


===============================================


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akihutubia wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi, uliofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria. Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akifatilia  ufunguzi huo.



Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Balozi Selma Malika akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika  tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria. Kushoto ni Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mhe. Ahmed Djellal akifuatilia ufunguzi huo.


Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst) Jacob Kingu wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria.


Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakifatilia mkutano.


Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Isaac Kazi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria.


Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Bi. Lilian Mukasa akifuatilia Mkutano wa Tano wa JPC kati ya Tanzania na Algeria unaofanyika jijini Algiers, Algeria.


Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania


Mkutano ukiendelea.

Ujumbe wa Tanzania

Ujumbe wa Tanzania
Ujumbe wa Algeria ukifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Algeria.


Friday, July 28, 2023

TANZANIA YAPONGEZWA KWA MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA AFYA

Serikali ya Tanzania imepongezwa kwa kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya pamoja na kutoa ushirikiano kwa mashirika ya kimataifa hususan Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses wakati wa kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 28 julai 2023.

"Ninaipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wenu ambao mmekuwa mkiutoa kwa Shirika la Afya Duniani, hakika tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika kuhakikisha kuwa tunaboresha na kuimarisha misingi ya sekta ya afya hapa Tanzania,” amesema Dkt. Sagoe-Moses

Dkt. Sagoe-Moses ameongeza kuwa juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na magonjwa ya mbalimbali hususan yale ya mlipuko ni nzuri na zinaridhisha, mfano mzuri ni jinsi Tanzania ilivyopambana na homa ya Marburg katika mkoa wa Kagera. 

“WHO tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukinga na kutibu magonjwa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa afya za watanzania zinakuwa bora wakati wote,” aliongeza Dkt. Sagoe-Moses.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amemhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.

Dkt. Tax amesema kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi na WHO ili kuhakikisha kuwa inaboresha na kuimarisha mifumo ya afya na Sekta ya afya kwa ujumla pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa sekta ya afya ili kuwawezesha kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoibuka katika jamii.  

“Tanzania na Shirika la Afya Duniani zimekuwa zikishirikiana katika kuimarisha na kuboresha sekta ya afya nchini, mchango wa WHO ni mkubwa na umeisadia Serikali kuboresha sekta ya afya na utekelezaji wa afua mbalimbali za mapambano dhidi ya magonjwa…..mfano mzuri tumekuwa tukishirikiana katika kutokomeza Malaria, Uviko 19 na magonjwa mengine kama vile HIV, ” alisema Dkt. Tax.

Tanzania imekuwa ikishirikiana na WHO pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa inaboresha mifumo ya afya na Sekta ya afya ili kuijengea uwezo nchi na wataalam wake katika kutambua na kudhibiti magonjwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses  katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dkt. Charles Sagoe-Moses  pamoja na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na watumishi kutoka WHO 


Wednesday, July 26, 2023

MHE. MARIAM CHABI TALATA AREJEA BENIN

Makamu wa Rais wa Benin, Mheshimiwa Mariam Chabi Talata ameondoka nchini na kurejea Benin baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Africa Human Capital Heads of State Summit) ulianza tarehe 25 na kumalizika tarehe 26 Julai 2023.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Mhe. Mariam Chabi amesindikizwa na Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb.), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.

Makamu wa Rais wa Benin, Mheshimiwa Mariam Chabi Talata akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kuondoka nchini Tanzania na kurejea Benin baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Africa Human Capital Heads of State Summit) ulianza tarehe 25 na kumalizika tarehe 26 Julai 2023


Makamu wa Rais wa Benin, Mheshimiwa Mariam Chabi Talata akizungumza na Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila kabla ya kuondoka nchini na kurejea Benin baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Africa Human Capital Heads of State Summit) ulianza tarehe 25 na kumalizika tarehe 26 Julai 2023