Sunday, July 30, 2023

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza diplomasia ya uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi unaoendelea jijini Algiers, Algeria.

Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 1 Agosti 2023 nchini humo ambapo ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.).

Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo. Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni: Naibu Makatibu Wakuu kutoka sekta za Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati.

Aidha, kwa upande wa Serikali ya Algeria, Mkutano huo ulifunguliwa na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Selma Malika na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi kutoka nchini humo.

Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.

Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.

‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo.

Naye Balozi Selma Malika katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.

‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara, mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.

Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou ulilosababishwa na ongezeko la joto kali. 

Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara, viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia, mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.


===============================================


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akihutubia wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi, uliofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria. Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akifatilia  ufunguzi huo.



Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Balozi Selma Malika akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika  tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria. Kushoto ni Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mhe. Ahmed Djellal akifuatilia ufunguzi huo.


Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst) Jacob Kingu wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria.


Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakifatilia mkutano.


Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Isaac Kazi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria.


Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Bi. Lilian Mukasa akifuatilia Mkutano wa Tano wa JPC kati ya Tanzania na Algeria unaofanyika jijini Algiers, Algeria.


Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania


Mkutano ukiendelea.

Ujumbe wa Tanzania

Ujumbe wa Tanzania
Ujumbe wa Algeria ukifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Algeria.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.