Monday, July 17, 2023

RAIS WA HUNGARY AWASILI TANZANIA

Rais wa Hungary Mheshimwa Katalin Novák, amewasili leo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nne itakayomalizika tarehe 20, Julai 2023.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Mheshimiwa, Novák amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) 

Akiwa nchini, tarehe 18 Julai 2023 Mheshimiwa Novák anatarajia kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kufanya mazungumzo rasmi na baadae viongozi hao kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Novák ni Rais wa kwanza mwanamke kuongoza Hungary ambapo alichaguliwa mwezi Mei, 2022. Aidha, ni Rais wa kwanza kutoka Hungary kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.

Ziara hiyo ni matokeo ya jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Mataifa mbalimbali duniani.

Tanzania na Hungary zimekuwa zikishirikiana katika sekta za biashara, elimu, utalii, kilimo, utangazaji na viwanda.

Viongozi wengine walioambatana na Dkt. Tax kumpokea Rais wa Hungary ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Muliro Jumanne, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayeiwakilisha pia Tanzania nchini Hungary, Mhe. Abdallah Possi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.








No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.