Friday, July 21, 2023

NCHI WANACHAMA WA SADC ZARIDHIA KUMUUNGA MKONO DKT. TULIA NAFASI YA URAIS UMOJA WA MABUNGE DUNIANI

Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) imeridhia kwa kauli moja kumuunga mkono mgombea wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mgombea wa Kanda katika nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Luanda, Angola mwezi Oktoba 2023.

 

Hatua hiyo imefikiwa wakati wa Mkutano wa 25 wa Kamati hiyo uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 20 na 21 Julai 2023, baada ya Kamati hiyo kupokea na kuridhia ombi la Serikali ya Tanzania la kumuunga mkono Mhe. Dkt. Tulia lililowasilishwa kwao na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.

 

Aidha, wakati wa Mkutano huo, Jamhuri ya Zimbabwe ilitangaza kuwa imemuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho mgombea wake ambaye ni Spika wa Bunge la nchi hiyo, Mhe. Jacob Mudenda ili kumuunga mkono mgombea wa Tanzania kuwania nafasi hiyo.

 

Akizungumza mara baada ya hatua hiyo, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Zimbabwe na Kanda kwa ujumla kwa kumuunga mkono mgombea wa Tanzania na kueleza kuwa Kanda itawezesha mgombea huyo huyo kushinda nafasi hiyo.

 

Vile vile, Mhe. Dkt. Tax ameieleza Kamati hiyo kwamba Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) tayari ameungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU), Bunge la Afrika (PAP), Jukwaa la Maspika wa Mabunge ya Afrika Mashariki na Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC PF) katika kugombea nafasi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao umefanyika jijini Windhoek, Namibia  tarehe 20 na 21 Julai, 2023. Wengine wanaoishiriki ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa, kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kaspar Mmuya na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mnyepe (katikati), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kaspar Mmuya (mwenye vifaa vya kusikilizia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma (kulia)
Mwenyekiti wa  Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah akifunga Mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 20 na 21 Julai 2023
Meza Kuu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor naye ni miongoni mwa Mawaziri walioshiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
Taratibu za kufunga rasmi Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika zikiendelea ambapo wimbo wa Taila la Namibia na Wimbo wa SADC ziliimbwa
Hafla ya kufunga mkutano ikiendelea
Mhe. Dkt. Tax  (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Bashungwa (wa tatu kushoto) mara baada ya kushiriki Mkutanoi wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika Windhoek tarehe 20 na 21 Julai 2023. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Ulizni na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Mnyepe (wa tatu kulia), Katibu Mku wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mmuya (wa pili kushoto) na Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma (kushoto)
Picha ya pamoja

Picha ya pamoja


















 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.