Saturday, July 8, 2023

TANZANIA, INDIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya India zimekubaliana kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, nishati, elimu, maji, afya, tehama na ulinzi.

Makubaliano hayo yameafikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar (Mb.) katika Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya Mkutano huo, Dkt. Tax amesema wameona kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika eneo la biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa hayo kwa kuwa India ni mbia mkubwa wa Tanzania kibiashara akiwa katika nafasi ya nne na mbia pia wa uwekezaji akiwa katika nafasi ya tano. 

 “Tumeona kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa pande zote mbili, na tumelekeza changamoto zinazoikabili sekta ya bishara na uwekezaji zifanyiwe kazi kwa uharaka na kuondolewa,” aliongeza Dkt. Tax.

Dkt. Tax ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika eneo la biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa hayo.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Tax aliongeza kuwa uamuzi wa Serikali ya India kufungua tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT), Zanzibar utasaidia kujengea uwezo, ubunifu na teknolojia kwa Watanzania.

“Taasisi hii ni taasisi ya kwanza ya teknolojia kuanzishwa na India nje ya taifa lao. Taasisi hiyo itatusaidia kutujengea uwezo, ubunifu na teknolojia na ilikubalika hadi kufikia mwezi Oktoba utekelezaji uwe umeanza,” alisema Dkt. Tax.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Jaishankar amesema kuwa Mkutano wa 10 wa Tume ya pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India umetoa fursa ya kujadili na kuona maeneo mapya ya ushirikiano kati ya mataifa hayo. 

Maeneo hayo ni pamoja na sekta za bishara na uwekezaji, sayansi na teknolojia, mafunzo, afya, kilimo, elimu na ulinzi kwa maslahi ya pande zote mbili. “India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu ulidumu kwa muda mrefu, hivyo ni imani yangu kuwa tutaendelea kushirikiana katika maeneo mapya,” alisema Dkt. Jaishankar 

 Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India – Zanzibar, Dkt. Jaishankar alisema kuwa kwa mara ya kwanza Serikali ya India imekusuadia kuanzisha tawi la taasisi hiyo Zanzibar ambayo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba 2023. 

“Tumefurahishwa sana na jambo hili kwani kwa mara ya kwanza Taasisi hii inaanzisha tawi lake nje ya India, kuanzishwa kwa tawi la taasisi hiyo Zanzibar ni imani yetu kuwa itasaidia kuboresha elimu na teknolojia nchini Tanzania,” alisema Dkt. Jaishankar

Makubaliano ya kuanzishwa kwa tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India nchini Tanzania yalisainiwa tarehe 05 July 2023 kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar na Taasisi ya IITM pamoja na Wizara ya Elimu ya India.

Aidha, kabla ya Mkutano huo, Dkt. Jainshankar aliwasilisha Ujumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasilisha Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kadhalika, Dkt. Jainshankar ailifanya ziara Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine, alikutana kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Husein Ali Mwinyi na kukubaliana kuendelea kuimalisha ushirikiano katika sekta za elimu na maji.

Vilevile, aliwasilisha alipata fursa ya kutembelea miradi wa maji wa Kidutani – Zanzibar, na Kibamba Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Technolojia Dar es salaam (DIT).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akielezea hatua zilizofikiwa katika Mkutano wa 9 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika mwaka 2019

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar wakionesha makubaliano ya maeneo mapya ya ushirikiano (Agreed Minutes) wakati wa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India ukiendelea 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India  

Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali za pande zote mbili



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.