Monday, July 17, 2023

MKUTANO WA 25 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC KWA NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAANZA JIJINI WINDHOEK

Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utafanyika jijini Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 17 hadi 21 Julai, 2023

 

Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 17 na 18 Julai 2023 ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati hii unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Faraji Mnyepe.

 

Akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Balozi Penda Naanda amewakaribisha Wajumbe nchini Namibia na kuwaomba kujadili agenda zilizopo mezani kwa umakini ili hatimaye kuziwasilisha kwa Kamati ya Mawaziri kwa hatua zinazofuata.

 

Ameongeza kusema kuwa, vikao vya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ni muhimu kwani huzikutanisha nchi wanachama kwa ajili ya kujadili na kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama ya kanda, demokrasia na utawala bora kwa maslahi mapana ya nchi wanachama. 

 

“Nawakaribisha jijini Windhoek na katika kikao chetu hiki ili kwa pamoja tupokee na kujadili taarifa mbalimbali za vikao vilivyotangulia ili kutathimini hatua zilizofikiwa na kutoa mapendekezo yetu ya namna ya kuendeleza mtangamano wa Jumuiya yetu kupitia vikao hivi” alisema Balozi Naanda.

 

Akichangia hoja wakati wa Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Dkt. Samwel Shelukindo  amesema ni matarajio ya Tanzania kuwa, vikao hivyo ambavyo hufanyika kila mwaka vitaendelea kutoa mchango chanya katika kukuza na kuimarisha masuala mbalimbali ya Jumuiya ikiwemo demokrasia katika Kanda; hali ya Siasa, ulinzi na usalama; mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa, rushwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

 

Aidha, ametoa rai kwa Jumuiya ya SADC kuendelea kutilia maanani changamoto ya ongezeko la vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu na wimbi la utekaji nyara Watoto kwa kuwa ni changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya Kanda.

 

“Ni vyema Kanda yetu ikaendelea kujiwekea mikakati madhubuti ya kudhibiti changamoto hizi ikiwemo kutafuta fedha za kuwasafirisha wahamiaji haramu wanapomaliza vifungo vyao, manunuzi ya magari na vifaa kwa ajili ya kufanyia doria za pamoja za udhibiti wa mipaka na utoaji wa mafunzo kwa taasisi husika” alisisitiza Balozi Fatma.

 

Kuhusu athari zitokanazo na migogoro ya ndani na nje ya Afrika ikiwemo mgogoro wa Urusi na Ukraine ambao umeathiri usalama wa chakula, Balozi Fatma ameziomba nchi wanachama kuchukua hatua mbalimbali za kujitegemea kwa kuhakikisha zinazalisha chakula cha kutosha, kuimarisha mifumo ya ubora wa mazao, kuwa na soko la Kanda la kuuziana mazao na kuuza nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

 

Mkutano wa 25 unalenga pamoja na mambo mengine kupokea na kujadili agenda mbalimbali zikiwemo mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 24 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya kanda; masuala ya demokrasia; mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa, rushwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

 

Nchi Wanachama 16 za SADC zimeshiriki Mkutano huo wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Balozi Penda Naanda akifungua rasmi Mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 17 Julai 2023
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Balozi Penda Naanda akiwa na wajumbe wa meza kuu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kamati ya Makatibu Wakuu wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 17 Julai 2023
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC wakati wa mkutano uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 17 Julai 2023. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab.
Balozi Fatma Rajab wakati wa Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Balozi Fatma alitoa mchango wa Tanzania kuhusu umuhimu SADC kuendelea kutilia maanani changamoto ya ongezeko la vitenfo vya usafirishaji haramu binadamu na wimbi la utekaji nyara watoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri vijana ambao ni nguvu kazi ya kanda
Mjumbe wa Angola akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Botswana akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Lesotho akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Namibia akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Afrika Kusini akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,
Mjumbe wa Zimbabwe akishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,

Wajumbe wa Sekretarieti ya SADC wakishirki Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,

Sehemu ya Washiriki wakati wa Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,

Mkutano ukiendelea











 

Wednesday, July 12, 2023

WAZIRI DKT. TAX APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA BALOZI MTEULE WA PAKISTAN NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Pakistan hapa nchini, Mhe. Siraj Ahmad Khan katika hafla fupi iliyofanyika leo tarehe 12 Julai 2023 katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

 

Katika mazungumzo yao, Mhe. Dkt. Tax amemkaribisha nchini Mhe. Khan na kumuahidi ushirikiano kutoka kwake binafsi, Wizara na Serikali kwa ujumla wakati wote atakaokuwa nchini akiiwakilisha nchi yake. 

 

Aidha, amesema kuwa, ushirikiano kati ya Pakistan na Tanzania ni mzuri na utaendelea kuimarika kupitia Balozi Khan kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.

 

Naye Mhe. Khan ameeleza furaha yake kuwa Tanzania na kwamba yupo tayari kutekeleza majukumu yake ya uwakilishi kwa kushirikiana na Wizara na Serikali kwa ujumla kwa maslahi mapana ya nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Pakistan nchini Mhe. Siraj Ahmad Khan. Hafla ya makabidhiano imefanyikatarehe 12 Julai 2023  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Mhe. Dkt. Tax akimsikiliza Mhe. Khan wakati wa mazungumzo yao.





Monday, July 10, 2023

MAWAZIRI SADC WAJADILI HALI YA AMANI DRC, MSUMBIJI

Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imefanya Mkutano wa Dharura kwa njia ya mtandao kwa lengo la kujadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo (DRC) na Msumbiji.

Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya  SADC, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi Ndaitwah ambapo pamoja na mambo mengine, amezisihi Nchi wanachama wa SADC kuendelea kushirikiana na DRC pamoja na Msumbiji na kuhakikisha kuwa hali ya amani inarejea.

“SADC imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inarejesha hali ya amani katika Mashariki ya DRC na Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Hivyo niendelee kuwasihi kuendelea kushirikiana na kuhakikisha hali ya usalama katika nchi hizo inapatikana. Amani na usalama ni bidhaa ghali hivyo yatupasa tuzilinde vyema," alisema.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano katika Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ambaye ameeleza kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mahitaji ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika harakati za kutafuta suluhu ya amani ya kudumu Mashariki mwa DRC na kulaani mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya waasi nchini humo.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazidi kulaani vitendo viovu vinavyotekelezwa na vikundi vyenye silaha dhidi ya raia wa DRC wasio na hatia. Hivyo, ni matarajio yetu kuwa mapendekezo yanayowasilishwa kuhusu uanzishwaji wa misheni hii yatasaidia kutatua changamoto hizo za kiusalama katika nchi za DRC na Msumbiji”

Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utafuatiwa na Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ-Troika) na kufuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 11 Julai 2023

Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ukiendelea 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiteta jambo na mmoja kati ya wajumbe walioshiriki katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha mchango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha mchango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 





Saturday, July 8, 2023

TANZANIA, INDIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya India zimekubaliana kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, nishati, elimu, maji, afya, tehama na ulinzi.

Makubaliano hayo yameafikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar (Mb.) katika Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya Mkutano huo, Dkt. Tax amesema wameona kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika eneo la biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa hayo kwa kuwa India ni mbia mkubwa wa Tanzania kibiashara akiwa katika nafasi ya nne na mbia pia wa uwekezaji akiwa katika nafasi ya tano. 

 “Tumeona kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa pande zote mbili, na tumelekeza changamoto zinazoikabili sekta ya bishara na uwekezaji zifanyiwe kazi kwa uharaka na kuondolewa,” aliongeza Dkt. Tax.

Dkt. Tax ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, kuna haja ya kuongeza ushirikiano katika eneo la biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa hayo.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Tax aliongeza kuwa uamuzi wa Serikali ya India kufungua tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT), Zanzibar utasaidia kujengea uwezo, ubunifu na teknolojia kwa Watanzania.

“Taasisi hii ni taasisi ya kwanza ya teknolojia kuanzishwa na India nje ya taifa lao. Taasisi hiyo itatusaidia kutujengea uwezo, ubunifu na teknolojia na ilikubalika hadi kufikia mwezi Oktoba utekelezaji uwe umeanza,” alisema Dkt. Tax.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Jaishankar amesema kuwa Mkutano wa 10 wa Tume ya pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India umetoa fursa ya kujadili na kuona maeneo mapya ya ushirikiano kati ya mataifa hayo. 

Maeneo hayo ni pamoja na sekta za bishara na uwekezaji, sayansi na teknolojia, mafunzo, afya, kilimo, elimu na ulinzi kwa maslahi ya pande zote mbili. “India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu ulidumu kwa muda mrefu, hivyo ni imani yangu kuwa tutaendelea kushirikiana katika maeneo mapya,” alisema Dkt. Jaishankar 

 Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India – Zanzibar, Dkt. Jaishankar alisema kuwa kwa mara ya kwanza Serikali ya India imekusuadia kuanzisha tawi la taasisi hiyo Zanzibar ambayo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba 2023. 

“Tumefurahishwa sana na jambo hili kwani kwa mara ya kwanza Taasisi hii inaanzisha tawi lake nje ya India, kuanzishwa kwa tawi la taasisi hiyo Zanzibar ni imani yetu kuwa itasaidia kuboresha elimu na teknolojia nchini Tanzania,” alisema Dkt. Jaishankar

Makubaliano ya kuanzishwa kwa tawi la Taasisi ya Teknolojia ya India nchini Tanzania yalisainiwa tarehe 05 July 2023 kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar na Taasisi ya IITM pamoja na Wizara ya Elimu ya India.

Aidha, kabla ya Mkutano huo, Dkt. Jainshankar aliwasilisha Ujumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasilisha Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kadhalika, Dkt. Jainshankar ailifanya ziara Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine, alikutana kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Husein Ali Mwinyi na kukubaliana kuendelea kuimalisha ushirikiano katika sekta za elimu na maji.

Vilevile, aliwasilisha alipata fursa ya kutembelea miradi wa maji wa Kidutani – Zanzibar, na Kibamba Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Technolojia Dar es salaam (DIT).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akielezea hatua zilizofikiwa katika Mkutano wa 9 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika mwaka 2019

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar wakionesha makubaliano ya maeneo mapya ya ushirikiano (Agreed Minutes) wakati wa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India uliofanyika Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India ukiendelea 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India  

Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati Tanzania na India 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali za pande zote mbili



Friday, July 7, 2023

WATUMISHI WA WIZARA YA MAMBO YA NJE WASHIRIKI BONANZA LA MICHEZO


Timu ya mpira ya miguu ikiongozwa na nahodha wake Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi wakiwa kwenye picha ya pamoja muda mfupi kabla ya kuwakabili wapinzania wao kwenye bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma.

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 7/7/2023 kwa shauku na morali ya hali juu wameshiriki bonanza la michezo lililofanyika kwenye uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma.

Bonanza hilo ambalo limeandaliwa na Wizara limehusisha michezo mbalimbali kama vile mazoezi ya pamoja ya viungo, mpira wa miguu, mpira wa pete na riadha.

Bonanza hilo pamoja na masuala mengine lililenga kuhamasisha upimaji wa afya kwa watumishi wake hususani kwa Magonjwa Sugu Yasiyoabukiza (MSY), ikiwa ni miongoni mwa hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara katika utekelezaji wa Afua za VVU na MSY kwa mujibu wa Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza wa mwaka 2014. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Chiku Kiguhe ameeleza kuridhishwa kwake na namna watumishi walivyohamasika kushiriki zoezi la upimaji afya na michezo ya pamoja. Vilevile, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watumishi wa Wizara kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kushiriki michezo, kupima afya mara kwa mara na kuzingatia ushauri na miongozo inayotolewa na wataalam wa afya kuhusu masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha afya zao. 

Watumishi wa Wizara waliojitokeza katika bonanza hilo kwa nyakati tofauti wameeleza furaha yao kuhusu namna Uongozi wa Wizara unavyozigatia na kujali suala la utimamu wa afya ya Watumishi wake, hususani kwa kuandaa programu mbalimbali za mara kwa mara ikiwemo michezo, elimu kuhusu masuala ya afya na upimaji. 
Wachezaji wa mpira wa miguu wakiwania mpira kwenye bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma.
Wachezaji wa mpira wa pete wakiwania mpira 
kwenye bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma.
Washiriki wa michezo wakiwa katika hali ya furaha kwenye ufunguzi wa Bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi akianzisha mpira kwneye bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma
Washiriki wa michezo wakiwa katika hali ya furaha kwenye ufunguzi wa Bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Chiku Kiguhe akiwatoka wapinzani kwenye mpira wa pete katika bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja wa Dodoma Sekondari jijini Dodoma.
Mchezo wa mpira wa miguu ukiendelea







Wednesday, July 5, 2023

TANZANIA, MAREKANI KUIMARISHA USHIRIKIANO ZAIDI

Tanzania na Marekani zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi katika sekta za biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi baina ya mataifa hayo.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alipomwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni nyumbani kwa Balozi wa Marekani nchini Jijini Dar es Salaam. 

Dkt. Shelukindo alisema Tanzania na Marekani zimekuwa zikifanya kazi pamoja katika kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, ambapo Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji na wauzaji bidhaa kutoka Marekani na Tanzania imekuwa ikisafirisha bidhaa za nguo kwenda Marekani chini ya Mpango wa Ukuzaji fursa za kiuchumi Afrika (AGOA).

“Takwimu zinaonesha kuwa uagizaji wa bidhaa kutoka Marekani umeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 201.8 mwaka kwa 2017 hadi Dola za Marekani milioni 215 mwaka 2022. Pia, katika miaka ya hivi karibuni, mauzo ya nje kutoka Tanzania kwenda Marekani yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 9.7 mwaka 2017 kufikia Dola za Marekani milioni 49.5 mwaka 2022,” alisema Dkt. Shelukindo. 

Balozi Shelukindo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia zaidi wafanyabiashara na wawekezaji nchini na kuwawezesha Watanzania kufanya biashara katika mazingira mazuri na rafiki. 

“Kuanzia mwaka 1997 hadi 2023, Marekani imefanya uwekezaji nchini Tanzania wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.8 katika sekta za Kilimo, Nishati, Taasisi za Fedha, Rasilimali Watu, Uzalishaji Asili, Maliasili, Madini, Mawasiliano, Utalii na Uchukuzi, uwekezaji huo umezalisha ajira zaidi ya 54,900 nchini,” alisema Balozi Shelukindo. 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Shelukindo aliwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Marekani kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati mbadala, viwanda vya magari, viwanda vya dawa, mafuta ya kula, viwanda vya pamba na nguo, kilimo, utalii, mifugo, uvuvi, Samaki, madini na miundombinu.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle alisema ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania ni wa muda mrefu na umekuwa imara tangu ulipoanzishwa.

Mhe. Balozi Battle aliongeza kuwa wakati Marekani inasherekea maadhimisho ya miaka 247 na miaka 62 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati yake na Tanzania ni vyema kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo na kuhakikisha wananchi wanapata mambo ya msingi hususan elimu, kazi, afya, ulinzi, usalama, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na diplomasia inayounganisha kwa manufaa ya baadae ya wananchi wote.

“Marekani tumedhamiria kufanya biashara na uwekezaji na Tanzania kwa maslahi mapana ya nchi zetu. Uwekezaji katika sekta hiyo bila shaka utachangia kuboresha zaidi uchumi wa Tanzania,” alisema Mhe. Balozi Battle 

“Uhusiano wetu na Tanzania umedumu kwa takribani miaka 62…..tulisimama na Tanzania, tumesimama na Tanzania na tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyakati zote,” aliongeza Mhe. Balozi Battle. 

Tanzania na Marekani zimekuwa zikishirikiana katika sekta za Afya, Kilimo, Nishati, Taasisi za Fedha, Rasilimali Watu, Uzalishaji Asili, Maliasili, Madini, Mawasiliano, Utalii na Uchukuzi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akihutubia katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni nyumbani kwa Balozi wa Marekani nchini Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle akizungumza katika maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania yaliyofanyika tarehe 04 Julai 2023 jioni Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle baada ya kuwasili nyumbani kwa Balozi huyo Jijini Dar es Salaam

sehemu ya Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na wananchi mbalimbali wakifuatilia maadhimisho ya miaka 247 ya uhuru wa Marekani na Miaka 62 ya Ushirikiano wa Marekani na Tanzania Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle




BALOZI KAYOLA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA MALAWI

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Agnes Kayola amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera, tarehe 04 Julai 2023 Ikulu, Jijini Lilongwe Malawi.

Julai 1, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu alimteua Balozi Kayola kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi. 

Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Agnes Kayola tarehe 04 Julai 2023 Ikulu, Jijini Lilongwe Malawi

Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera akimpongeza Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Agnes Kayola mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho, Ikulu Jijini Lilongwe

Picha ya Pamoja