Tuesday, October 10, 2023

RAIS DKT. SAMIA ATUNIKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI INDIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mwanamke wa kwanza kutunikiwa  Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa Watoto  wa  kike wanaoishi  katika  mazingira magumu nchini.


Akiipokea Shahada hiyo, ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini,  Rais  Samia amesema anakishukuru Chuo  hicho kwa heshima hiyo ambayo ni kubwa na kwamba anaitoa kwa watoto wa kike wa Tanzania  wanaoishi katika mazingira magumu na pembezoni  mwa nchi ambapo amewaka  kutokukata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.



"Mimi ni matokeo ya jozi nyingi za macho na mikono ya watu walioona uwezo ndani yangu wakanilea na kunishika mkono," amesisitiza Rais  Dkt. Samia.



Ameeleza kuwa ameitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa.

 

Pia amesema anawashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.

 

“Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani  na baba mwalimu. Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa" amesema Rais Dkt. Samia.



Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Santishree Dhulipudi Pandit amesema Chuo hicho kimetunuku Mhe. Rais Samia  Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe.  Dkt. Subrahmanyam Jaishankar ameielezea Shahada hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India.

 

Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa, Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wawili tu ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo, Rais wa Russia Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe. 


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunikiwa Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India, Prof. Santishree Dhulipudi Pandit. Mhe. Rais Dkt. Samia ameitoa Shahada hiyo kwa watoto wa kike nchini ili kuwapa moyo wa kuendelea na jitihada mbalimbali kwa ajili ya mafanikio yao ya baadaye. Mhe. Rais Dkt. Samia anakuwa  mwanamke wa kwanza kupata shahada hiyo kutoka Chuo hicho.

Mhe. Rais Dkt. Samia akizungumza mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Sehemu nyingine ya viongozi
Sehemu ya ujumbe wa India


Sehemu nyingine ya ujumbe wa India




Monday, October 9, 2023

TANZANIA NA INDIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Tanzania na India zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo ya kimkakati ambayo yana manufaa  kwa wananchi wa pande zote mbili ikiwemo maji, kilimo, nishati, teknolojia, afya, ulinzi na usalama, utamaduni na michezo, uchukuzi  na biashara na uwekezaji.

 

Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari  mara baada ya mazungumzo ya faragha kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi tarehe 09 Oktoba 2023.

 

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe. Rais Dkt. Samia ameipongeza Serikali ya India kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Tanzania hususan kwenye maeneo ya kimkakati kama maji, afya, kilimo, teknolojia, ulinzi na usalama, na baiashara na uwekezaji.

 

Pia amesema Tanzania inapongeza uamuzi wa Serikali ya India wa kuanziasha kampasi ya kwanza la Taasisi ya Teknolojia ya India nje ya nchi hiyo ambayo itaanzishwa hivi karibuni Zanzibar na kuutaja uamuzi huo kama heshima na upendeleo kwa Tanzania kwani utawanufaisha watanzania, Afrika Mashariki na Kati.

 

Akizungumzia biashara baina ya nchini hizi, Mhe. Rais Samia amesema, thamani ya ufanyaji biashara kati ya Tanzania na India imeendelea kuongezeka ambapo kwa takwimu zilizopo nchini biashara kati ya nchi hizi mbili imeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani  Bilioni 3.1 mwaka 2022 kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.6 mwaka 2017.

 

Kwenye medani za ushirikiano wa kimataifa, Mhe. Rais Samia amempongeza Waziri Mkuu Modi kwa kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Wakuu wa Nchi za G20 uliofanyika nchini hapa mwezi Septemba 2023 ambapo Afrika kupitia Umoja wa Afrika imefanikiwa kuwa mwanachama wa kudumu wa Umoja huo.  

 

“Siwezi kusita kuipongeza India kwa kufanikiwa kuandaa Mkutano wa G20 ambao ulishuhudia Afrika inakuwa mwanachama kamili wa G20, nampongeza Waziri Modi kwa kutetea mpango wa kupunguza madeni kwa mataifa madogo na kutangaza mpango wa dharura wa kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya nchi zinazoendelea ili kuwezesha upatikanaji wa teknolojia ya nishati safi ifikapo mwaka 2050” amesema Mhe. Rais Samia.

 

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Modi ameitaja Tanzania kama mshirika wake wa karibu na  mkubwa katika  maendeleo barani Afrika na kwamba nchi hizo zimekubaliana kuupeleka ushirikiano uliopo katika viwango vya juu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na India.

 

Amesema India itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya kukuza ujuzi, usambazaji maji, teknolojia ya habari na mawasiliano na uhusiano wa watu wa India na Tanzania, nishati safi na ulinzi na usalama.

 

Pia ameongeza kusema nchi hizo zimekubaliana kuwa na mpango wa miaka mitano wa ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama hususan katika maeneo ya kujenga uwezo, mafunzo na ulinzi baharini.

 

Akizungumzia ushirikiano katika biashara, Mhe.  Modi amesema nchi hizo zimekubaliana kuangalia uwezekano wa kuongeza biashara kwa kutumia sarafu za nchi zao kwa lengo la kupunguza gharama na matumizi ya Dola za Marekani.

 

Wakati wa Mkutano huo, Mhe. Rais Samia na Mhe. Modi walishuhudia ubadilishanaji wa Hati Sita za Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Hati 14 na Mkataba mmoja zilizosainiwa kati ya Tanzania na India wakati wa ziara hii. Hati hizo zinagusa sekta za Uchukuzi, Utamaduni, Michezo, Uwekezaji, TEHAMA na Elimu.

 

Mhe. Dkt. Rais Samia yupo nchini India kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yao  yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023

Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi  akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  wa India, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa pamoja na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi, wakiwashuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba  na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Subrahmanyam Jaishankar wakibadilishana moja ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano zilizosainiwa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini India
Uadilishanaji wa Hati za Makubaliano ukiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (kulia) akiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega wakifuatilia Mkutano wa Mhe. Rais Dkt. Samia na Mhe.Modi na waandishi wa habari uliofanyika jijini New Delhi wakati wa ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini India

Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023

Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023