Wednesday, February 14, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO NA MAONESHO YA 11 YA PETROLI AFRIKA MASHARIKI

Viongozi wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC (walioketi) wakisaini  taarifa ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 14 Februari 2024. Waliosimama ni Watendaji mbalimbali kutoka nchi wanachama wakishuhudia zoezi hilo.

Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.

Mbali na hayo mkutano huo umepitisha bajeti ya kiasi cha Dola za Marekani 1,842,467 kwa ajili ya maandalizi ya kongamano na maonesho hayo.

Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia. 

Katika hatua nyingine mkutano huo umetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.


Aidha, katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye pia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar umependekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.

Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara ameeleza kuwa Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo, pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikana wa nishati ya uhakika na salama. 


“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya. Hivyo umuhimu wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na sio la hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na kimataifa”. Alieleza Waziri Kaduara


Vilevile Mhe. Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuja nchini, kushuhudia na kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere, unaotarajia kuzalisha Megawatts 2115 utakaofanyika tarehe 25 Februari 2024.


Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu kuanzia 12-14 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam na Makatibu Wakuu.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye akifurahia jambo wakati akiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Viongozi na Watendaji wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumazika kwa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 14 Februari 2024, jijini Arusha.
Meza Kuu wakiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe kutoka Nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha

ASKOFU DKT. MALASUSA AONGOZA IBADA YA KUMUAGA LOWASSA

 

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa ameongoza ibada ya kumuaga Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam tarehe 14 Februari, 2024.

Akihubiri katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi Dkt. Malasusa ameeleza kuwa Hayati Lowassa pamoja na familia yake walipenda sana ibada katika maisha yao ya kila siku.

"Kuleta mwili wa mtu asiyependa ibada Kanisani ni kuutesa mwili wa mhusika na hivyo Hayati Lowassa amestahili kuletwa hapa kwakuwa ni sehemu aliyokuwa ameipenda kuja" alisema Dkt. Malasusa

Pia ameeleza ni muhimu kwa viongozi wenye wafuasi nyuma yao kuwa na utaratibu wa kusikiliza neno la Mungu kwa ajili ya kuendelea kuongoza watu wao vizuri na kuleta tija katika yale waliyopewa nafasi ya kuyasimamia.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Sinde Warioba, Waziri Ofisi ya Rais- Kazi Maalum, Mhe. George Mkuchika, Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene,  Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonaz, Kaimu Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu Tatu, Mama Anna Mkapa, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mama Esther Sumaye, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Viongozi wengine Waandamizi wa Serikali na  Kanisa.







 

RAIS SAMIA AINISHA MAENEO MUHIMU YA UWEKEZAJI NCHINI KWA WAWEKEZAJI WA NORWAY

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza nchini kwenye sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi na kukuza uchumi wa nchi ikiwemo nishati mbadala, kilimo, gesi na mafuta, mifuko ya uwekezaji na usafirishaji.


Mhe. Rais Samia ametoa wito huo alipohutubia Wajumbe walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway liliofanyika jijini Oslo, tarehe 13 Februari 2024


Mhe. Dkt. Samia ambaye aliongozana na Mwana Mfalme wa Norway Haakon kwenye Kongamano hilo amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wenye nia thabiti kuja kuwekeza  mitaji yao nchini  kwenye sekta  ambazo kwa kiasi kikubwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama vile chakula, umeme, mafuta na usafirishaji.


Amesema Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Norway kuwekeza mitaji yao kwakuwa Serikali imeboresha sheria mbalimbali za uwekezaji na kwamba kijografia Tanzania inafikika kwa urahisi na inapakana na nchi nane ambazo ni soko kubwa kwa wawekezaji na pia Tanzania ni nchi ya amani inayoamini katika usawa na utawala wa sheria.

Akizungumzia kilimo, Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji hao kwamba  bado sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania haijatumika ipasavyo kwenye sekta ya kilimo ambapo zipo Hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo Hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji 

Ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji wa zao la Alizeti na ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo bidhaa zake ikiwemo mafuta zinahitajika kwa wingi nchini na nchi jirani.

Kuhusu nishati mbadala, Mhe. Rais Samia amewahamasisha wawekezaji hao kuchangamkia fursa za umeme wa jua na upepo kwani bado Tanzania inahitaji kuwa na uhakika wa upatikaji wa nishati mbalimbali ikiwemo umeme wa uhakika.


Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuhamasisha wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi na namna ambavyo ameendelea kutambua mchango wa sekta binafsi kwenye uchumi na maendeleo ya nchi.


Mhe. Rais Samia yuko katika ziara ya kitaifa ya  siku tatu nchini Norway,  amefuatana na Mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nci, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Fedha, Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi mbalimbali.

Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya Wawekezaji na Wafanyabiashara 150 kutoka Norway na Tanzania. 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika jijini Oslo. Mhe. Rais Samia yupo nchini Norway kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari 2024 kwa mwaliko wa Mfalme wa Norway Herald V.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika Oslo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu
Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa Kongamano hilo.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Jan Christian Vestre naye akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
Kongamano likiendelea
Mhe. Rais Samia akizungumza kwenye Majadiliano ya Ngazi ya Juu kuhusu  Usawa wa Kijinsia na Siasa katika Biashara wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
Mshauri wa Rais, Siasa na Uhusiano na Jamii, Mhe. William Lukuvi nae akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji jijini Oslo. Wengine ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka (aliyesuka nywele)


Mratibu wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga akifuatilia Kongamano hilo
Mhe. Balozi Grace Olotu akishiriki Kongamano hilo na wajumbe wengine kutoka Norway
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa M.Khamis akishiriki Kongamano hilo
Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania
Afisa Mambo ya Nje Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Bw. Magabilo Murobi akishiriki Kongamano hilo
Sehemu ya ujumbe kutoka Norway wakishiriki Kongamano











 

Tuesday, February 13, 2024

MAKATIBU WAKUU WANAOSIMAMIA SEKTA YA NISHATI WA AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA JIJINI ARUSHA


Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akichangia hoja kwenye Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha

Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta ya Nishati katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la EAC unaoendelea jijini humo.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na mkutano wa Wataalam uliyofanyika tarehe 12 Februari 2024, umepitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya. Vilevile umepokea na kujadili taarifa za maendeleo ya sekta ya nishati katika maeneo ya umeme, mafuta na nishati jadidifu. 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki katika Jamhuri ya Kenya Bw. Abdi Dubati ameeleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za Wakuu wa Nchi wanachana wa Jumuiya, za kuhahikisha sekta ya nishati inaimarika ili kuchagiza maendeleo ya Jumuiya kutokana na mchango wake mkubwa katika kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na uzalisha wa bidhaa viwandani.

“Nitoe rai kwetu sote tuliopata nafasi na kuaminiwa kusimamia maendeleo ya sekta hii muhimu kuwa tujidhatiti katika kutoa michango na kushirikishana uzoefu wetu ili kwa pamoja kama Jumuiya tupige hatua katika upatikanaji wa nishati ya kutosha, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya yetu”. Alisema Dubati. 

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo ameleeza kuwa kikao hicho kinatoa fursa ya kuunganisha nguvu na kuweka mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo umeme. 

Vilevile alitoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kutumia fursa ya kuwepo jijini humo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. 

Makatibu Wakuu wengine kutoka Tanzania walioshiriki katika mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Balozi Stephen P. Mbundi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Joseph Kilangi Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi akichangia hoja kwenye Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la EAC katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia mkutano wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha
Mkutano ukiendelea


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen P. Mbundi akijadili jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhandisi Abdillah Mataka.

Meza Kuu wakiongoza mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliokuwa ukiendelea katika Makao Mkuu ya Jumuiya jijini Arusha.

Sehemu ya washiriki kutoka nchi wanachama wakifuatilia mkutano wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu wakuu uliofanyika jijini Arusha.

DKT. MPANGO AONGOZA WAKAZI WA DAR eS SALAAM KUMUAGA HAYATI LOWASSA

 



 











Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameongoza  waombelezaji  mbalimbali kutoka jijini Dar es Salam kuuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowassa katika shughuli iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee tarehe 13 Februari, 2024.

Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman  Abdullah, Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk aliungana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali, vyombo vya dola, viongozi wastaafu na wananchi katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Hayati Lowassa. 

Hayati Edward Lowassa anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Monduli, Arusha Februari 17, 2024 katika mazishi ya Kitaifa yanayotarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hayati Edward Lowassa alifariki dunia tarehe 10 Februari 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

 

 


Monday, February 12, 2024

MKUTANO WA 16 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA NISHATI WA AFRIKA MASHARIKI WAANZA JIJINI ARUSHA


Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Bw. Abdillah Mataka katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichangia hoja kwenye Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa EAC uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.

Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umenza leo tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha. 

Mkutano huo wa siku tatu kuanzia February 12 hadi 14, 2024 utafanyika katika ngazi tatu; ngazi ya Wataalamu tarehe 12 Februari 2024, ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 13 Februari 2024 na kuhitimishwa katika ngazi ya Mawaziri tarehe 14 Februari 2024.

Mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo ya sekta ya nishati katika Jumuiya. Vilevile kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na endelevu katika Jumuiya. 

Maeneo ya sekta ya nishati yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni; umeme, mafuta na nishati jadidifu. 

Awali akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa ngazi ya wataalamu Mwenyekiti wa Mkutano huo Bw. Petro Lyatuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati – Tanzania ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo bado mchango na weledi wa wataalamu hao unahitajika ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kufikia malengo yanayotarajiwa na Jumuiya. 

Bwana Lyatuu ametoa rai kwa watalamu hao kujikita katika kujadili na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu masuala muhimu yatakayojili katika mkutano huo kwa manufaa ya Jumuiya.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa ngazi ya wataalamu unaongozwa na Bw. Abdillah Mataka Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Mkutano huo unatarajiwa hutimishwa tarehe 14 Februari 2024 katika ngazi ya Mawaziri wanaosimamia sekta ya nishati umehudhiriwa na wajumbe kutoka Nchi zote saba (7) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati Bw. Petro Lyatuu akiongoza Mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati uliokuwa ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha




 Mkutano wa 16 Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati ukiendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha