Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewakaribisha
wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza nchini kwenye sekta zinazogusa maisha ya
wananchi wengi na kukuza uchumi wa nchi ikiwemo nishati mbadala, kilimo, gesi
na mafuta, mifuko ya uwekezaji na usafirishaji.
Mhe. Rais Samia ametoa wito huo alipohutubia Wajumbe walioshiriki Kongamano la
Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway liliofanyika jijini Oslo,
tarehe 13 Februari 2024
Mhe. Dkt. Samia ambaye aliongozana na Mwana Mfalme wa Norway Haakon kwenye
Kongamano hilo amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wenye nia thabiti kuja
kuwekeza mitaji yao nchini kwenye sekta ambazo kwa kiasi
kikubwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama vile chakula, umeme,
mafuta na usafirishaji.
Amesema Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Norway kuwekeza mitaji
yao kwakuwa Serikali imeboresha sheria mbalimbali za uwekezaji na kwamba
kijografia Tanzania inafikika kwa urahisi na inapakana na nchi nane ambazo ni
soko kubwa kwa wawekezaji na pia Tanzania ni nchi ya amani inayoamini katika
usawa na utawala wa sheria.
Akizungumzia kilimo, Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji hao kwamba
bado sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania haijatumika ipasavyo kwenye sekta ya
kilimo ambapo zipo Hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo Hekta
milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji
Ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji wa zao la Alizeti
na ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo bidhaa zake ikiwemo
mafuta zinahitajika kwa wingi nchini na nchi jirani.
Kuhusu nishati mbadala, Mhe. Rais Samia amewahamasisha wawekezaji hao
kuchangamkia fursa za umeme wa jua na upepo kwani bado Tanzania inahitaji kuwa
na uhakika wa upatikaji wa nishati mbalimbali ikiwemo umeme wa uhakika.
Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango
na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuhamasisha
wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi na namna ambavyo ameendelea kutambua
mchango wa sekta binafsi kwenye uchumi na maendeleo ya nchi.
Mhe. Rais Samia yuko katika ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini
Norway, amefuatana na Mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nci, Ofisi
ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein
Bashe, Waziri wa Fedha, Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya, Makatibu Wakuu na Watendaji
Wakuu wa Taasisi mbalimbali.
Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya Wawekezaji na Wafanyabiashara 150
kutoka Norway na Tanzania.
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika jijini Oslo. Mhe. Rais Samia yupo nchini Norway kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari 2024 kwa mwaliko wa Mfalme wa Norway Herald V.
|
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika Oslo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu
|
|
Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa Kongamano hilo.
|
|
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Jan Christian Vestre naye akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
|
|
Kongamano likiendelea
|
|
Mhe. Rais Samia akizungumza kwenye Majadiliano ya Ngazi ya Juu kuhusu Usawa wa Kijinsia na Siasa katika Biashara wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
|
|
Mshauri wa Rais, Siasa na Uhusiano na Jamii, Mhe. William Lukuvi nae akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji jijini Oslo. Wengine ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka (aliyesuka nywele)
|
|
|
Mratibu wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga akifuatilia Kongamano hilo
|
|
Mhe. Balozi Grace Olotu akishiriki Kongamano hilo na wajumbe wengine kutoka Norway
|
|
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa M.Khamis akishiriki Kongamano hilo |
|
Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania
|
|
Afisa Mambo ya Nje Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Bw. Magabilo Murobi akishiriki Kongamano hilo
|
|
Sehemu ya ujumbe kutoka Norway wakishiriki Kongamano
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.