mazungumzo yakiendelea |
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na ujumbe wa wabunge na maseneta kutoka Canada walipokutana naye ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma |
Baadhi ya Wabunge na Maseneta wa Canada wakimsikiliza Naibu Waziri Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana naye ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amekutana na Ujumbe wa Jumuiya ya Maseneta na Wabunge wa Canada (Africa Parliamentary Association (CAAF) ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma Februari 20, 2024.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Mbarouk ameelezea kuridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Canada, hususan katika sekta za sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.
Amesema Serikali ya Canada imekuwa mdau mkubwa katika harakati za kusaidia uboreshwaji na uimarishwaji wa mifumo ya afya nchini kwa kusaidia kuimarisha huduma za afya ya uzazi na vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini.
“Canada imekuwa mdau wetu mkubwa katika sekta ya afya nchini, imetupatia Dola za Canada zipatazo Milioni 15 kupitia mfuko wa bajeti ya afya, msaada huu una maana kubwa kwa Tanzania, unasaidia sana kuboresha sekta ya afya nchini,” alisema
Amesema Canada pia imekuwa ikisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ambapo imetoa msaada wa Dola za Canada milioni 53 ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuboresha kiwango cha elimu hasa kwa watoto wa kike nchini.
Kuhusu Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mbarouk amesema kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi kinaendelea kuimarika na kuongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 26 kiwango cha mauzo ya Canada kwa Tanzania kimeongezeka kwa asilimia 9.27 kutoka Dola milioni 16.1 za Canada hadi kufikia Dola Milioni 194 za Canada kwa mwaka 2023, na mwaka huo huo, Tanzania iliiuzia Canada bidhaa zenye thamani ya Dola za Canada Milioni 19.9.
Amewahakikishia Wabunge na masenator hao kutoka Canada kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kutoka Canada kuja nchini kuwekeza mitaji yao hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina soko kubwa kutokana na uanachama wake katika jumuiya za kikanda za EAC na SADC.
Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa wabunge na masenata, Bi Brenda Shanahan (MP) amesema kuwa ziara hiyo inalenga kuwajengea uwezo wabunge hao katika nchi wanazozitembelea na kuona jinsi ambavyo Serikali yao inavyoshirikiana na Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Ujembe huo upo nchini kwa ziara ya kikazi tangu tarehe 18 Februari 2024 na umeshatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukutana na Spika wa Bunge hilo ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt Tulia Ackson pamoja na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama. Ujumbe huo pia unatarajiwa kwenda Zanzibar tarehe 21 Februari 2024 ambapo pamoja na mambo mengine utakutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Canada hususan baina ya Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Canada.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.