Wednesday, February 21, 2024

AFRIKA YASHAURIWA KUWA NA SERA YA LUGHA ZA ASILI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezishauri nchi za Afrika kuwa na sera ya lugha za asili ambayo itazingatia mchango wa lugha za asili katika kukuza uchumi.

Ushauri huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kufunga Kongamano la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni.

Katika Hotuba hiyo Dkt. Mwinyi, amesema Bara la Afrika ndilo bara lenye idadi kubwa ya vijana duniani na linategemewa kuwa na nguvu kazi ya dunia hivyo ni lazima kujiandaa kuona Afrika inaandaa nguvu kazi yenye ustadi na maarifa inayosimamia utamaduni na lugha zake za asili.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa kuna umuhimu wa kujadili maarifa kupitia lugha za asili yanavyoweza kupatikana na jamii zikaweza kutumia ili kunufaika katika kulinda maliasili na kuendeleza shughuli za uzalishaji kama vile kilimo, uvuvi na utamaduni wa ufinyanzi, ususi na nyenginezo.

“Katika jamii za kiafrika, mfungamano uliopo baina ya lugha za asili na maisha ya kazi, ya ubunifu  na ya ugunduzi wa biashara siyo wa kinadharia, bali ni ukweli tunaoishi nao. Kuwapo kwa lugha hizi za asili na hasa matumizi yake ni lazima kuchangie katika maendeleo ya kiuchumi ambayo yatakuwa endelevu,” alisema Dkt. Mwinyi katika hotuba yake.

Kadhalika, Dkt. Mwinyi amewataka wataalamu wa lugha kuongeza ushawishi na mchango katika kuhakikisha Kiswahili kinakuwa daraja muhimu la kukuza diplomasia ya uchumi na kiutamaduni katika ukanda wa Afrika kwa kuzingatia nafasi yake miongoni mwa lugha za asili za kiafrika.

Kongamano hilo limeshirikisha wataalamu wa lugha na watafiti, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, watu mashuhuri na Viongozi Wastaafu na mahiri katika kutumia lugha adhimu ya Kiswahili ikiwa ni miongoni mwa lugha za asili ambayo inazidi kupata mafanikio.

Rais Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia nafasi ya lugha, matumizi ya kidijiti na uchumi wa buluu ambapo alisema kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana  wanaotarajiwa kuwa mstari wa mbele katika ubunifu, ugunduzi na matumizi ya vifaa vya kidijiti.

“Tunapaswa kujiuliza ni kwa namna gani wingi wa lugha za asili za kiafrika unavyoweza kutumika kujenga uchumi wa mataifa yetu na kuona kwa vipi tutatumia tofauti za rasilimali tulizonazo na lugha katika kujifunza mifumo ya ikolojia ya bahari ya hindi ili kukuza uchumi wa buluu,” alisema Dkt. Mwinyi. 

Katika hatua nyingine Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano ametembelea makumbusho ya Taifa na Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es salaam. 

Akizungumza baada ya kutembelea makumbusho ya Taifa, Mhe. Chissano amesema kuna haja ya kuendelea kuhifadhi historia zinazohusu waafrika ili kuonesha ulimwengu juu ya maendeleo yaliyofikiwa na waafrika kabla ya ukoloni.

Mhe. Chissano alikuwa nchini kuhudhuria Kongamano  la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni. lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 20 na 21 Februari 2024.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akiwasilisha hotuba ya kufunga Kongamano la kwanza la Kimataifa kuhusu dhima ya lugha za asili katika kukuza na kujenga Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Jijini Dar es Salaam

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Utamaduni wa Makumbusho ya Taifa, Bi. Anthonia Mukama wakati alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi Makumbusho ya Taifa alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano akimsikiliza mmoja kati ya maafisa wa Kijiji cha makumbusho wakati alipotembelea makumbusho hiyo Jijini Dar es salaam





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.