Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewasihi washiriki wa Kongamano la lugha za asili kujielekeza kupanga mikakati itakayohakikisha lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za asili zinapata fursa katika uchumi wa kidijiti ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni linalofanyika kwa siku mbili (2) tarehe 20 - 21 Februari, 2024 Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais amesema Kongamano hilo linapaswa kuangazia namna ambayo Kiswahili na lugha nyingine za asili za Afrika zitakavyotumika kuendeleza teknolojia za asili, kuchochea uvumbuzi, uwekezaji na kukuza diplomasia.
Aidha, Makamu wa Rais ameongeza kuwa Kongamano hilo linapaswa kusaidia kuonesha fursa zilizopo katika matumizi ya lugha za asili ili kuwafanya vijana kujipatia stadi na maarifa mbalimbali katika kujiandaa kwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia ndani na nje ya bara la Afrika.
Makamu wa Rais amesema kupitishwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kumepanua wigo wa matumizi ya Kiswahili na kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kiutamaduni.
“Kongamano hili muhimu linabeba jukumu kubwa la kuibua fursa zaidi na kuendeleza historia ndefu ya Kiswahili katika kujenga uhusiano kati ya watu wa tamaduni, lugha na misingi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii,” alisema Dkt. Mpango.
Amesema Katika muktadha wa ukuaji na maendeleo ya Kiswahili, ni pamoja na kuhifadhi lugha nyingine za asili, sambamba na tamaduni na mifumo yake. Afrika Mashariki na Kati, wafanyabiashara wadogo na wanaoinukia “Wamachinga” wametoa mchango ambao hauna budi kutambuliwa na kuthaminiwa
Dkt. Mpango ameongeza kuwa lipo hitaji la kufanya utafiti wa kina ili kuona jinsi nchi za Kiafrika zinavyoweza kuendeleza mifumo inayozingatia ushiriki wa vijana na makundi kama ya wafanyabiashara waliojiajiri katika diplomasia ya uchumi na kukuza biashara.
Kadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika kukuza lugha ya Kiswahili, ambapo inalenga kuifanya lugha hiyo kuendelea kuleta umoja, amani na kuvumiliana katika bara zima la Afrika.
Aidha, Dkt. Mpango amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendelea kushirikiana na Vyuo na Taasisi za nje katika kukuza Kiswahili na kuendeleza diplomasia ya kiutamaduni.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Joaquim Chissano, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, Mabalozi wa nchi za nje nchini, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James G. Bwana, Watunga sera, Wafanyabiashara, Wajasiriamali na wenye Viwanda, Viongozi wa Dini, Wanataaluma na Wakuu wa Taasisi za Utafiti, Vijana, Wanawake na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kiraia.
Kongamano limeandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kwazulu-Natal cha Afrika Kusini.
Sehemu ya mabalozi wakifuatilia Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024 |
Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni lililofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 20 Februari 2024 |
Mmoja kati ya Washiriki akichangia jambo katika Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni |
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe.Uhuru Kenyatta akifuatilia mada katika Kongamano la Kimataifa la Dhima ya Lugha za Asili katika kuendeleza Diplomasia ya Kiuchumi na Kiutamaduni |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.