Makongamano
ya wadau yanayoendelea nchini kuhusu marekebisho ya Sera
ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 yanalenga
kukusanya maoni
yatakayosaidia kutengeneza Sera ya Mambo ya Nje Bora itakayoongoza ushirikiano
wenye tija baina ya Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na
kimataifa.
Hayo yamesemwa leo tarehe 10 Februari 2024 na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu - Zamzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir wakati
akisoma hotuba ya ufunguzi ya Kongamano la nne la wadau lililofanyika kisiwani
Pemba.
Makongamano hayo yanayoratibiwa kwa ushirikiano baina ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya
Rais-Zanzibar na Taasisi ya Uongozi yametajwa kuwa ni kielelezo cha utawala
bora ambao unahimiza ushirikishwaji wa wananchi katika utengenezaji wa Sera za
Taifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
(Mb) amesisitiza umuhimu wa wananchi walioshiriki kongamano hilo kutoa maoni yao
kwa uhuru bila woga. Alisema maoni yao yatasaidia kutengeneza
Sera ya Mambo ya Nje madhubuti itakayoifanya Tanzania kutetea maslahi yake
katika majukwaa ya Kimataifa na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika
dunia ya sasa.
Alisema mijadala
yao ya kurekebisha
Sera ya Mambo ya Nje itatoa mwelekeo wa kuboresha maeneo mapya yanayopendekezwa
ambayo ni pamoja na masuala ya uchumi wa Buluu, diaspora, mabadiliko ya
tabianchi, kubidhaisha Lugha
ya Kiswahili na kulinda mila na desturi za
Tanzania.
Balozi Mbarouk alimsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Sera ya Mambo
ya Nje ambao umesaidia
kuongezeka kwa ajira za Watanzania katika mashirika ya kikanda na Kimataifa,
masoko ya bidhaa za Tanzania Nje ya nchi, misaada na mikopo ya Maendeleo,
uenyeji wa taasisi za kimataifa nchini na ujenzi wa miradi ya Maendeleo katika
sekta mbalimbali za miundombinu, nishati, kilimo, elimu na afya.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa makongamano
yaliyofanyika Arusha, Dar Es Salaam na Unguja limehudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kusini-Pemba, Mhe. Matar Zahor Masoud; Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais-Zanzibar, Bw. Salehe Juma Mussa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shwaibu Mussa; baadhi
ya Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi; wawakilishi wa vyama vya siasa; asasi za
kiraia; jumuiya za kidini na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.