Thursday, February 22, 2024

WAZIRI MAKAMBA; DUNIA INAHITAJI MFUMO MPYA WA MAAMUZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akichangia mada kwenye Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb), ameieleza Jumuiya ya Kimataifa kuhusu umuhimu wa kuwa na mifumo mipya ya kimataifa itakayo zingatia haki na usawa katika kufanya maamuzi hasa kwa Mataifa ya Afrika.

Waziri Makamba ameeleza hayo kwenye mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India. Mkutano huo unawakutanisha wabobezi wa diplomasia, watunga sera, wafanyabiashara, wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili na kutafuta majawabu ya changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazoikabili dunia.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Makamba ameeleza kuwa, Afrika imepoteza imani na baadhi ya mifumo ya sasa ya Kimataifa ambayo mara nyingi imekuwa ikifanya maamuzi yanaoegemea au kunufaisha wachache na kusahau maslahi ya pande zingine ikiwemo Afrika.

Ameitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni Umoja wa Mataifa pamoja Baraza la Amani na Usalama la umoja huo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa kufanya maamuzi yanayopendelea upande mmoja, hivyo kujenga hali ya kuto aminiana miongoni mwa Mataifa.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo wa Raisina 2024, Waziri Makamba ameutaja kuwa ni jukwaa muhimu ambalo linapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ni chachu katika kuleta mabadiliko ya namna ya kutafuta majawabu na suluhu ya changamoto mbalimbali za kiuchumi na kisiasa kwa haki na usawa.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amefanya mazungumzo na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India pembezoni mwa mkutano wa Raisina 2024. Mazungumzo hayo yalijikita katika kufuatilia utekelezaji wa suala mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini humo mwezi Oktoba 2023.

Mawaziri hao wameeleza kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa sehemu kubwa ya masuala yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili.

“Tumeridhishwa na hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa makubaliano na Wakuu wa Nchi zetu, mimi na mwenzangu Mhe. Jaishankar tumekubaliana kuendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kuhakisha masuala yote yaliyokubaliwa tunayatekeleza ndani ya muda uliopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili” Alisema Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba anatarijiwa kufanya mazungumzo na Mhe. Shri Piyush Goyal Waziri wa Masuala ya Walaji, Chakula na Usambazaji kwa Umma wa India (Minister for Consumer Affairs Food and Public Distribution) ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kufuatilia utekelezaji.
Mkutano wa Raisina 2024 ukiendelea jijini New Delhi, nchini India
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na washiriki wenzake wa majadiliano kwenye Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Anisa Mbega akifuatilia Mkutano wa Raisina 2024 unaofanyika jijini New Delhi, nchini India
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba kwenye picha ya pamoja na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa Raisina 2024
Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa kwenye mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India
Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe. Subrahmanyam Jaishankar akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.