Tanzania na Panama zimefungua mlango wa majadiliano wa kuanzisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za uchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. Miongoni mwa sekta zinazoangaziwa kwenye ushirikiano huo ni pamoja na utalii, biashara na uwekezaji, madini, Mabadiliko ya Tabia Nchi, na Kilimo.
Hayo yamejili katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia unaoendelea jijini New Delhi, India.
Waziri Makamba katika mazungumzo hayo alieleza kuwa licha ya uongozi imara, uwingi wa rasilimali, vivutio lukuki vya kipekee vya utalii, amani na utulivu wa kisiasa uliopo nchini, Tanzania ipo katika nafasi nzuri zaidi kijiografia inayoifanya kuwa lango la kuzifikia kwa urahisi nchi nyingi za jirani. Hali hiyo inawavutia wawekezaji na wafanyabishara wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuwekeza nchini.
“Serikali chini uongozi imara wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeboresha sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji ambazo zimefanya mazingira ya biashara kuwa rafiki zaidi. Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Panama kuwekeza mitaji yao kwakuwa kijografia, Tanzania ni lango la kuzifikia Nchi nane ambazo ni soko kubwa kwa wawekezaji na pia ni nchi ya amani inayoamini katika usawa na utawala wa sheria” Alisema Mhe. Makamba.
Kwa upande wake Waziri Tewaney ameeleza kuwa Panama inashauku kubwa ya kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kwa kuwa inatambua fursa zinazopatika katika pande zote mbili zikitumiwa ipasavyo zitaleta tija katika mandeleo ya uchumi ya pande zote.
Aidha, Waziri Tewaney ameongeza kuwa hatarajii kuishikia kwenye ushirikiano wa sekta za uchumi pekee, bali anaona ipo fursa kwa Nchi hizo mbili kufungua milango ya kuanza kuangazia namna kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kwa kuwa zina mtazamo unaoshahabiana katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje.
Pande zote mbili zimeazimia kuanza kwa utekelezaji wa haraka wa masuala yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Katika hatua nyingine Mhe.Waziri Makamba amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Uingereza anayesimamia Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika, Kusini mwa Asia, Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa Mhe. Tariq Mahmood Ahmad (Mb) yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa 9 wa Raisinia jijini New Delhi, India.
Mazungumzo yao yalijikita kujadili na kutafuta majawabu ya masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa hususani katika maeneo ya ulinzi na usalama na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Waziri Makamba yupo nchini India kushiriki katika Mkutano wa 9 wa Raisina (9th Raisina Dialogue)unaofanyika nchini humo terehe 21 – 23 Februari 2024. Mkutano huo umefunguliwa Februari 21, 2024 na Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi na Waziri Mkuu wa Ugiriki Mhe. Kyriakos
Mazungumzo yakiendelea |
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Panama Mhe. Janaina Tewaney (kushoto) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba. |
Mazungumzo yakiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.