Thursday, February 15, 2024

RAIS SAMIA AWATAKA DIASPORA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUITANGAZA TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi yaa Diaspora kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuitangaza nchi kwenye maeneo waliyopo ili kuvutia watalii, wawekezaji na wafanyabishara kwa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.

 

Mhe. Rais Samia ametoa wito huo kwenye Mkutano wake na Watanzania waishio Norway na nchi nyingine za jirani uliofanyika hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kitaifa nchini humo.

 

Mhe. Samia amesema Serikali inatambua na kutahamini mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na kuwahimiza kuendelea kuitangaza nchi kwa kusema yale mazuri yanayopatikana nchini ikiwemo vivutio vya utalii na fursa za biashara na uwekezaji.

 

Pia amewahimiza Diaspora hao kuendelea kuweka akiba nyumbani, kufundisha watoto wao mila na desturi nzuri za Tanzania ikiwemo Lugha ya Kiswahili, kupendana na kushirikiana na kufuata sheria na taratibu za nchi walizopo ili kujiepusha na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwasababishia matatizo wao binafsi na kuiabisha nchi.

 

Akizungumzia hali ya siasa na uchumi nchini, Mhe. Rais Samia amewaeleza Diaspora hao kuwa, hali ya uchumi ni nzuri na inaendelea kuimarika baada ya kushuka katika kipindi cha janga la ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo kwa sasa uchumi umekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4 miaka mitatu iliyopita na unatarajiwa kukua hadi asilimia 6.5 ifikapo mwaka 2027.

 

“Tunaendelea na jitihada mbalimbali za kukuza uchumi wetu hata ziara yangu nchini Norway ni kati ya jitihada hizo za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tanzania inapiga hatua katika maendeleo na tayai imetajwa na Shirika la Fedha la Kimataifa kuwa ni kati ya Nchi 20 zinazokua vizuri kiuchumi duniani” amesema Mhe. Rais Samia.

 

Kuhusu siasa, Mhe. Rais Samia amesema kuwa hali nchini ni shwari ambapo vyama vyote vya siasa vinaendelea na shughuli zao za kichama kwa uhuru na nchi ina amani na utulivu.

 

Kuhusu ajira,   Mhe. Rais Samia amesema bado ni tatizo hata hivyo Serikali yake imeendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwasaidia vijana na wanawake wa mijini na vijijini ili kuwawezesha kujiajiri na kujipatia kipato kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo biashara ndogondogo.

 

Amesema, kwa upande wa mijini, Serikali imeendelea kuwajengea masoko bora vijana ambao wengi wanajishughulisha na biashara ndogondogo maarufu kama machinga,  kuwatafutia mfuko wa kupata mitaji na kuanzisha taasisi yao ambayo inafanya vizuri na hata wameweza kuanzisha gazeti na Televisheni yao.

 

Kuhusu vijana wa vijijini, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imeanzisha program inayoitwa Jenga Kesho Bora (BBT) ambayo imejikita kuwwezesha vijana hao katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji. Amesema tayari kundi la kwanza la zaidi ya vijana 800 wamepewa Ekari 10 kila mmoja yenye miundombinu ya umwagiliaji na kuwakopesha mitaji na ruzuku kwa ajili ya pembejeo za kilimo.

 

Kuhusu sekta ya elimu na afya nchini, Mhe. Rais Samia amewaeleza Diaspora hao kuwa, hali ni nzuri ambapo kwa sasa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi kidato cha sita wanasoma bure huku Serikali pia ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi.

 

Akizungumzia Hadhi Maalum, Mhe. Rais Samia amesema anatambua umuhimu wake kwa Diaspora na kwamba  Serikali inafanyia kazi baadhi ya taratibu za kisheria kwenye masuala ya ardhi na uhamiaji ili kukamilisha suala hilo.

 

Awali akizungumza, Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden anayewakilisha pia  Nchi za Scandinavia na Baltic, Mhe. Grace Olotu amesema Diaspora katika eneo lake la uwakilishi wapo 3,973 ambapo kwa upande wa Norway ni Diaspora 1,407, Sweden 1,815, Denmark 1,001, Finland, 725, Iceland 11, Estonia 11 na Ukraine 4. Diaspora hao wamegawanyika katika makundi ya wafanyabiashara, wafanyakazi na wanafunzi.

 

Kwa upande wao Diaspora ambao waliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi, Bi. Margaret Adaa wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada mbalimbali anazozifanya nchini katika kujenga umoja na mshikamano nchini na kuinua uchumi kwa kuitangaza nchi kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Jumuiya ya Diaspora wa Tanzania wanaoishi Norway alipokutana nao wakati wa ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini humo kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari 2024

Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe, Grace Olotu akizungumza wakati wa mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora

Mwakilishi wa Diaspora na Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano kati ya Mhe. Rais Samia na Diaspora akisoma risala ya Jumuiya ya Diaspora mbele ya Mhe. Rais Samia (hayupo pichani)
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya viongozi wa Serikali wakishiriki Mkutano wa Mhe. Rais  Samia na Diaspora. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. Selemani Jafo na kulia ni Katibu wa Rais, Bw. Waziri
Mhe. Balozi Olotu akiwana Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (kushoto)
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Viongozi kutoka Serikalini walioshiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diapora wa Norway.
Sehemu ya ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki mkutano wa Mhe. Rais na Samia na Diaspora. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bw. Justine Kisoka akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani, Balozi Swahiba Mndeme na Mkurugezni wa Idara ya Sheria, Dkt. Kweka

Mkurugezni wa Idara ya Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akishiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Norway wakishiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Mhe. Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wake na Diaspora nchini Norway
Mhe. Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na wajukuu ambao ni watoto wa wana Diaspora walioshiriki mkutano wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi akimkabidhi zawadi Mhe. Rais Samia kwa kutambua mchangio wake katika maendeleo ya kiuchumi nchini

Mhe. Rais Samia akipokea zawadi ya jezi namba 10 kutoka kwa kiongozi wa Timu ya Diaspora ya Kilimanjaro FF kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini

Kikundi cha burudani kinachojiita Wamasai wa Norway kikitumbuiza wakati wa mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora.
















 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.