Na Ally Kondo, Kuwait
Nchi za Afrika na Kiarabu zimehimizwa kutumia
idadi kubwa ya watu wanaoishi katika nchi hizo kama rasilimali ya kujiletea
maendeleo ya kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili. Kauli hiyo ilitolewa na
Mwakilishi wa Umoja wa Nchi za Kiarabu wakati alipokuwa anatoa hotuba katika
ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Ushirikiano baina ya Nchi za
Afrika na Kiarabu ulioanza nchini Kuwait siku ya Alhamisi tarehe 14 Novemba,
2013.
Wakati alipokuwa anafungua rasmi mkutano huo,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait alieleza kuwa, Serikali ya Kuwait
inazithamini na kuzipa kipaumbele nchi za Afrika akitolea mfano namna Mfuko wa
Maendeleo wa Kuwait unavyofadhili miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya miundombinu
katika nchi za Afrika.
Naibu Waziri alieleza kuwa theluthi mbili ya nchi
za Kiarabu zipo barani Afrika, hivyo alisisitiza umuhimu wa nchi hizo
kushirikiana kiuchumi, hususan katika uwekezaji na biashara. Aidha, alisisitiza
umuhimu wa mkutano huo kuweka malengo na mikakati thabiti ya utekelezaji ili
kukidhi matarajio ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa
Libya ambaye nchi yake ilikuwa Mwenyekiti wa mkutano uliopita, alipongeza
ripoti ya pamoja iliyoandaliwa na Sekretariet ya Umoja wa Kiarabu na Kamisheni
ya Umoja wa Afrika kwa namna ilivyochambua utekelezaji wa malengo ya Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ushirikiano baina ya Nchi za Afrika na Kiarabu uliofanyika
Sirte, Libya mwaka 2010. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya utekelezaji
wa malengo hayo pamoja na kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa katika ripoti
hiyo ili kuwe na tija kwa wananchi.
Mwakilishi wa Mabalozi wa Umoja wa Afrika naye
aliwasihi wajumbe wa mkutano huo kujadili kwa kina suala la uhamaji ambalo
linaonekana kuwa ni changamoto kubwa duniani hivi sasa. Alisisitiza umuhimu wa
mkutano huo kutoa mapendekezo ya kukomesha tatizo hilo bila kuathiri maisha ya
watu.
Mkutano wa Maafisa Waandamizi, ambao lengo lake
kuu ni kuandaa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Kiarabu, utamalizika tarehe 15
Novemba, 2013. Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, unatarajiwa kujadili
namna ya kuoanisha vyombo vya kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mpango
Kazi iliyopitishwa kwenye Mkutano wa Pili wa Ushirikiano baina ya Nchi za Afrika
na Kiarabu na pia Kubuni mikakati ya kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya pamoja ya ushirikiano huo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.