Mhe. Abdallah Kigoda, Waziri wa Viwanda na Biashara akizungumza kwenye jukwaa la masuala ya biashara la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CBF), jana nchini Sri Lanka.
Tanzania yang`ara eneo bora kiuwekezaji
Tanzania inang’ara na kupanda chati kama eneo bora kiuwekezaji, kufuatia kujijengea heshima iliyoletwa na ziara ya Rais wa China Xi Jinping na Barack Obama wa Marekani, ambao ni viongozi wanaoheshimika kote duniani .
Haya yalisemwa nchini Sri Lanka kwenye jukwaa la masuala ya biashara la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CBF). Jumuiya hiyo inaundwa na yaliyokuwa makoloni ya Uingereza.
Kadhalika jukwaa hilo lilithibitishiwa kuwa imekuwa rahisi kwa Tanzania kutambulika kama taifa shindani kiuwekezaji linaloweza kuchuana na majirani zake na mataifa mengine ya Afrika.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda, alitoa maelezo hayo wakati akizungumza na wajumbe wa jukwaa hilo na kuongeza kuwa faida iliyopatikana kwenye miradi ya uwekezaji inayoendeshwa na kampuni za ndani na za kigeni imebakizwa nchini kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji.
Hata hivyo, si Waziri Kigoda wala Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar Mwinyikai, alitaja kiasi cha faida hiyo iliyopatikana na kubakizwa nchini kwa ajili ya uwekezaji zaidi.
Aliwaambia wajumbe kuwa serikali inatekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa pia inajizatiti kuimarisha maeneo ya taasisi za fedha, teknolojia ya habari na mawasiliano na maboresho ya kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC) kukifanya kuwa na uwezo kwa kutoa huduma na mahitaji yote ya wawekezaji.
Sri Lanka pamoja na Tanzania zinaangalia uwezekano wa kuwa na ushirikiano kwenye kuboresha miundombinu na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hiyo inakuja wakati Sri Lanka inajenga bandari ya kisasa iitwayo ‘Colombo port city’ ambayo baadhi ya wadau wanaikosoa kuwa itakuwa tishio kwa bandari nyingi ikiwamo Singapore ambayo ni bandari huru na kubwa duniani iliyoko kwenye bahari ya Hindi, ikiunganisha mataifa ya Mashariki na Magharibi .
Akizungumza kwenye jukwaa hilo Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Juliet Kairuki, alisema Tanzania ina uwezekano mkubwa wa kupata wawekezaji zaidi baada ya kuthibitika kuwa ni taifa lisilo na migogoro ya kisiasa.
Alitoa mfano kuwa TIC imepokea maombi ya uwekezaji kwenye nishati ya joto la asili la ardhini (geothermal) kutoka kampuni ya Marekani wenye thamani ya Dola milioni 28 (sawa na Sh. bilioni 45.5).
Source: The Guardian
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.