Na
Ally Kondo, Kuwait
Mkutano
wa Ushirikiano baina ya Nchi za Afrika na Kiarabu (Afro – Arab Summit) umeanza
nchini Kuwait siku ya Jumatatu tarehe 11 Novemba, 2013 kwa Mfuko wa Maendeleo
wa Kuwait (Kuwait Fund) kuandaa Kongamano la Uchumi na Uwekezaji. Mkutano huo
unafanyika katika ngazi mbalimbali ukianzia na mkutano wa ngazi ya maafisa
waandamizi baadaye Mawaziri na
kuhitimishwa na Mkutano wa Ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali ambao umepangwa
kufanyika tarehe 19 na 20 Novemba, 2013.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal
atamwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano wa ngazi ya Wakuu wa
Nchi na Serikali.
Mkutano
wa mwaka huu wa Afro –Arab Summit ni watatu kufanyika ambapo wa kwanza
ulifanyika Misri katika miaka ya 70 na wa pili ulifanyika mjini Sirte, Libya
mwaka 2010. Katika Mkutano wa Libya, Wakuu wa Nchi na Serikali walijiwekea
malengo mbambali ambayo utekelezaji wake utatathiminiwa katika mkutano wa mwaka
huu nchini Kuwait.
Mkutano
wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo “Wabia katika Maendeleo na Uwekezaji”
unadhamiria kuweka mikakati madhubuti ya kushirikiana baina ya nchi za Afrika
na Kiarabu katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo, bishara, uwekezaji, siasa
na masuala ya kijamii.
Kwa
upande wa sekta ya kilimo, nchi hizo zinakusudia kuimarisha ushirikiano ili
kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa kutumia ardhi kubwa na yenye
rutuba iliyopo katika nchi za Afrika ambazo hazina mitaji yakutosha kama
zilivyo nchi za Kiarabu. Lengo kubwa la mkakati huo ni kukomesha njaa ya mara
kwa mara inayozikumba nchi za Afrika pamoja na kuondoa hali ya wasiwasi wa
tishio la njaa linaloweza kutokea katika nchi za Kiarabu.
Katika
mkutano huo pia nchi za Afrika na Kiarabu zitajadili namna zitakavyoweza kushirikiana
kwa pamoja katika kukabiliana na kudhibiti majanga ya asili ambayo yanapotokea husababisha
uharibifu mkubwa wa maisha ya watu na mali zao.
Sanjari
na mkutano huo, Serikali za Tanzania na Kuwait zinatarajia kuweka saini
Mikataba miwili ya Kukuza na Kulinda Vitega Uchumi; na Ushirikiano katika Sekta
ya Utalii. Mikataba hiyo itakaposainiwa itahamisisha uwekezaji pamoja na
kuongeza idadi ya watalii kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.