Friday, October 24, 2014

Warsha kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika yahitimishwa Jijini Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe akitoa hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Magese Mulongo ya kufunga Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika na kufanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha.
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika na nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz kwa pamoja na Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Afrika Mhe. Konjit Sinegiorgis wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) alipokuwa akifunga Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika iliyowakutanisha Mabalozi, Wataalam wa masuala ya Amani na Wasuluhishi.
Sehemu nyingine ya Wajumbe wakimsikiliza Mhe. Nyerembe (hayupo pichani) akiwemo Rais Mstaafu wa Cape Verde, Mhe. Pedro Pires (kulia)
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akifuatilia kwa makini hotuba ya kufunga warsha ya amani na usalama iliyokuwa ikitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Nyerembe (hayupo pichani).
Wajumbe waliokuwepo wakati wa kufunga warsha ya amani na usalama.
Kamishna wa Amani na Usalama katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui akitoa neno la shukrani kwa Uongozi wa Mkoa wa Arusha na kwa Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuwa mwenyeji wa warsha hiyo ya siku tatu ambapo wajumbe wamenufaika na masuala yote yalijadiliwa pamoja na huduma nzuri.
Balozi Mstaafu, Prof. Joram Biswaro (kulia) akifuatialia hotuba  ya Balozi Chergui (hayupo pichani)

Bi. Shella Mbita, Mtoto wa Balozi Hashim Mbita nae pia alikuwa mmoja wa wajumbe waliohudhuria warsha ya amani na usalama jijini Arusha (Picha zote na Rosemary Malale)

===============================================

Na.  Ally Kondo, Arusha

Warsha ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika (AU) imehitimishwa jijini Arusha siku ya Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014. Warsha hiyo ambayo kaulimbiu yake ilikuwa “Silaha zisitumike kuuwa watu Barani Afrika ifikapo mwaka 2020” ilimalizika kwa wajumbe kutoa Rasimu ya Tamko la Arusha (Arusha Declaration). 

Katika Tamko hilo, kumebainishwa asili ya migogoro inayohusu nchi moja au baina ya nchi na nchi nyingine, vitu vinavyochochea migogoro na ukosefu wa utulivu Barani Afrika, wanaochochea na kudhamini migogoro pamoja na athari za maendeleo ya dunia kwa Bara la Afrika.

Aidha, Tamko hilo limeainisha juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na vitendo vya siasa kali, uhalifu wa kimataifa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika amani na usalama.

Tamko limebainisha pia kuwa migogoro mingi katika nchi za Afrika inasababishwa na ukosefu wa utawala bora katika Serikali, uwajibikaji, uwazi, uongozi shirikishi pamoja na kushindwa kutatua changamoto za umasikini na ukosefu wa usawa.

Kwa mujibu wa Tamko hilo, wajumbe kwa kauli moja walikubaliana na hoja kuwa ili nchi za Afrika ziondokane na matatizo hayo, hazina budi kutekeleza miongozo na maamuzi yanayotolewa na AU kuhusu amani, usalama na uongozi. Walisema kuwa maamuzi hayo yanatoa dira nzuri ya namna ya kukabiliana na changamoto za usalama Barani Afrika, isipokuwa nchi za Afrika hazina utamaduni wa kuyatekeleza.

Hivyo, wajumbe walisisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa AU kutekeleza maamuzi yote yanayofanywa na kuridhiwa na AU, Jumuiya za Kikanda na wadau wengine.

Aidha, walitoa wito kwa nchi wanachama wa AU, Kamisheni ya AU, Jumuiya za Kikanda, Baraza la Amani na Usalama la AU na wadau wengine kulipa kipaumbele suala la kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi hayo.

Sanjari na hayo, wajumbe walipongeza mabadiliko chanya yanayotokea Barani Afrika ikiwa ni pamoja na kupungua kwa migogoro ya kutumia silaha, kuongezeka kwa chaguzi za kidemokrasia, kukua kwa uchumi na ongezeko la kasi ya kupambana na vitendo vya ufisadi katika nchi nyingi za Afrika.

Licha ya maboresho hayo, wajumbe walielezea wasiwasi wao   kuhusu tishio linalotokana na changamoto mpya katika amani na usalama wa Bara la Afrika. Walihimiza umuhimu wa kutumia mbinu za kibunifu kukabiliana na changamoto hizo ambazo ni; uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uharamia, biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha na dawa za kulevya na biashara ya fedha haramu.

Wakati wa kufunga warsha hiyo ambayo iliwakutanisha Mabalozi, wasuluhishi, wajumbe maalum, wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na wasomi mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe alielezea matumani yake kuwa, washiriki walipata fursa nzuri ya kujadili kwa kina chanzo cha migogoro Barani Afrika na kupendekeza njia muafaka za kukabiliana nayo. Alisisitiza umuhimu wa mapendekezo hayo kuingizwa katika sera za kitaifa, kikanda na kimataifa ili yaweze kuwa na manufaa.

-Mwisho-


President Kikwete accorderd rousing Karibu, as China's President Xi Jinping formaly welcomes him to Beijing

President Xi Jinping of China welcomes President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete to the Great Hall of the People in Beijing this evening during the official formal reception at the climax of the State visit at the invitation of the Chinise Leader
President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete and the First Lady Mama salma Kikwete pose for an official photograph with their  host China's President Xi Jinping and his wife China's First Lady Peng Liyuan shortly after they arrived for an official formal reception at the Great Hall of the People in Beijing this evening

President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete and his host Chinese President Xi Jinping inspects a guard of honor mounted China's People Defense force in Beijing this evening during a formal reception at the Great Hall of the people. President Kikwete is on a State Visit to China invitation of  President Xi Jinping.
President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete and his host President Xi Jinping waves to the cheering crowd during a formal reception for the President and his delegation held at the Great Hall of  the People in Beijing at the climax of his State visit today 
President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete introduces former OAU/AU Secretary General Salim Ahmed Salim to China's President Xi Jinping during the formal reception held at the Great Hall of the People in Beijing this evening Left is the Minister for Foreign Affairs Mr Bernard Membe and second left is CCM Secretary General Abdulrahman Kinona.





==========================================================================

China ya yamwaga neema kubwa kwa Tanzania

Jamhuri ya Watu wa China leo, Ijumaa, Oktoba 24, 2014, imetangaza neema kubwa kwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutoa dola za Marekani milioni 85 kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kusaidia Tanzania kufanya mageuzi ya viwanda.

Neema hiyo kwa China kwa Tanzania imetangazwa na Rais Xi Jinping wa nchi hiyo katika mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati yake na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku sita katika China

Mazungumzo hayo kwenye jumba la The Great Hall of the People yamefanyika baada ya Rais Kikwete kukaribishwa rasmi katika Jamhuri ya Watu wa China kwa kupokelewa na Rais Xi Jinping katika eneo la East Plaza ya Jumba hilo.

Katika mapokezi hayo yakuvutia na kusisimua, Rais Kikwete amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la ukakamavu la Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China la People's Liberation Army.
Katika mazungumzo hayo, Rais Xi Jinping alitangaza kuwa China itaipatia Tanzania kiasi cha dola milioni 85 ikiwa ni mchanganyiko wa msaada na mkopo usiokuwa na riba, fedha ambazo Tanzania itaamua yenyewe jinsi gani yakuzituma.

"Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania kuboresha maisha ya wananchi wake, napenda kutangaza kuwa Jamhuri ya watu wa China itatoa kiasi cha RMB milioni 200 ikiwa ni msaada na RMB 200  milioni nyingine zikiwa ni mkopo ni mkopo usio kuwa na riba kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiasi cha RMB 100 milioni za msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zitatumika kwa kadri Serikali hizo mbili zitakavyoamua,'' amesema Rais Jinping.

Rais huyo wa China pia ametangaza kuwa nchi hiyo itaisaidia Tanzania katika uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji ya EPZ, uendelezaji wa miundombinu itaharakisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na itaingia katika shughuli za kutafuta gesi na mafuta katika ukanda wa Bandari ya Hindi katika eneo la Tanzania.

Rais Jinping pia ametangaza kuwa Serikali ya China imefanya uamuzi wa kuikarabati Reli ya Uhuru ya TAZARA inayounganisha Tanzania na Zambia na yenye urefu wa Kilometa 1,860 na kusaidia uendeshaji wa reli hiyo. "Ili kutekeleza uamuzi huu kwa haraka, napendekeza kuundwa kwa kamati ya pamoja ya wataalam kuandaa ramani ya namna ya kuitoa reli hiyo katika matatizo yake ya sasa.''

Rais Jinping ametangaza kuwa Serikali yake itatoa nafasi 100 za masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka Tanzania katika miaka mitano ijayo, itaongeza idadi ya madaktari ambao China inapeleka Tanzania, itahimiza makampuni zaidi ya China kuwekeza katika Uchumi wa Tanzania na kuzishawishi taasisi za kifedha za China kuanzisha shughuli zake katika Tanzania.

Kiongozi huyo wa China pia ametangaza kuwa nchi yake itajenga Chuo kikubwa cha mafunzo ya ufundi katika Tanzania na itaendeleza kushirikiana na Tanzania katika eneo la uimarishaji wa ulinzi na usalama.

Rais Jinping amesema kuwa urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania ni mfano unaong'ara wa uhusiano mzuri na mwema duniani na kuwa china iko tayari kutoa uzoefu wake wa maendeleo kwa Tanzania bila wasiwasi wowote.

Rais Kikwete amemshukuru sana Rais Jinping na Jamhuri ya watu wa China kwa misaada yake ambayo baadhi yake haikutarajiwa.

Imetolewa na: 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikuli - Dar es salaam     

Thursday, October 23, 2014

Fly Dubai yazindua rasmi safari zake nchini.

Ndege ya Shirika la Ndege la Fly Dubai ikiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere ikiwa katika uzinduzi wake uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, Ndege hiyo itafanya safari zake za moja kwa moja kutokea Dubai mpaka Dar es Salaa, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar.
Watatu kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, na wapili kutoka kushoto ni Balozi mdogo wa Tanzania, Dubai Omar Mjenga, wakwanza kushoto ni Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Pius Msekwa na wakwanza kulia ni Bajeti meneja wa Fly Dubai wa nchini Tanzania Bw. Riyaz Jamal wakiitazwa Ndege ya Fly Dubai ilipokuwa inawasili.  
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu akisalimiana na Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan mara baada ya kuwasili na Ndege hiyo katikati ni Bajeti meneja wa Fly Dubai Tanzania Bw. Riyaz Jamal.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Simba Yahaya akisalimiana na Bw. Screedharan   
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai Omar Mjenga akisalimiana na Bw. Screedharan
Mhe. Suluhu akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ndege hiyo itakayoanzisha safari zake moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka Dubai 
Wakwanza kushoto ni Bw. Shabani Baraza akimwakilisha Balozi wa Tanzania UAE, wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara katika Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Bw. Cleophas Luhumbika Watatu kutoka Kushoto ni Afisa Mambo ya Nje Bw. Hangi Mgaka pamoja na wajumbe wengine wakimsikiliza Mhe. Suluhu
Makamu Mkuu Bw. Screedhana (wakwanza kulia), wa kwanza kushoto Balozi Mdogo Mhe. Mjenga na (katikati) ni Bw. Riyaz Jamal wakimsikiliza Mhe. Waziri alipokuwa akizungumza.  
 Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan akizungumza katika hafla hiyo mara baada ya uzinduzi wa safari za Ndege ya Shirika lake la Fly Dubai, alisema safari za ndege zao zinatumia ndege mpya za kisasa aina ya Boeing zipatazo 100.  
Wajumbe mbalimbali wakimsikiliza Bw. Screedharan alipokuwa akizungumza
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai akizungumza na kuushukuru uongozi wa Fly Dubai kwakukubali kuanzisha safari za moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka dubai, Balozi mdogo Mjenga alisema kwa kuanza kwa safari ya ndege hiyo inategemewa kuongezeka kwa idadi ya Watalii nchini kutokea Milioni 1 kwa mwaka mpaka Milioni 2, fursa za ajira kwa Watanzania.
Sehemu ya wajumbe wengine wakimsikiliza Balozi Mdogo.
Picha ya pamoja

Picha na Reginald Philip


==============================================================


Na Reginald Philip

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu (Mb.) ameupongeza Uongozi wa Shirika la Flydubai la Dubai kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Dubai na Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar kwa gharama nafuu.

Akizindua huduma hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, jijini Dar es Salaam, Jumatano tarehe 22 Oktoba, 2014, Mhe. Suluhu alimwambia Makamu Mkuu wa Shirika la Flydubai, Bw. Sudhir Sreedharan, kuwa  kuja kwao Tanzania kutafungua njia za kiuchumi na nchi nyingine za Kiafrika.

Alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo pia kutatoa fursa ya ajira kwa watanzania, na akawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo.

Shirika hilo, ambalo ndege zake zina bei nafuu- kutokea Dar es salaam kwenda dubai na kurudi (DSM-DXD-DSM) kwa bei ya dola za Kimarekani 399 tu (budget Airline) litafanya safari zake kati ya Dar es salaam, KIA na Zanzibar. Baadae, shirika hilo litaongeza safari zao kutokea Mbeya kuelekea Dubail.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyoandaliwa na shirika la Flydubai kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Suluhu aliipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa kuratibu uanzishwaji wa safari za bei nafuu kupitia kwa Balozi  Mdogo wa Tanzania nchini Dubai, Mhe. Omar Mjenga, ambaye alihudhuria hafla ya uzinduzi.

Baada ya Dar es Salaam, hafla nyingine ya uzinduzi ilifanyika Zanzibar baadaye hiyo jana, Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

-Mwisho-

AU yawatunuku Dkt. Salim na Balozi Mbita Tuzo za Juu za Mwana wa Afrika



Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim akipokea Tuzo ya Juu ya Umoja wa Afrika ya Mwana wa Afrika kwa Mwaka 2014 kutoka kwa Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Smail Chergui. Tuzo hiyo  ilitolewa mjini Arusha pembezoni mwa Warsha ya Tano ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama Bararani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika inayoendelea mjini humo. Tuzo hiyo pia imetolewa kwa Balozi Mstaafu na Mpigania Uhuru Mahiri Barani Afrika, Balozi Hashim Mbita. Tuzo hizo zimetolewa kwao kutokana na mchango mkubwa walioutoa Barani Afrika na kwa Umoja wa Afrika ambapo Dkt. Salim alikuwa Katibu Mkuu wa saba wa OAU kuanzia mwaka 1989 hadi 2001. Kwa upande wake Balozi Mbita alikuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Ukombozi Barani Afrika chini ya OAU kuanzia mwaka 1974 hadi 1994 ilipomaliza kazi yake baada ya Uhuru wa Afrika Kusini.
Balozi Chergui akimkabidhi Cheti cha Tuzo hiyo Dkt. Salim
Dkt. Salim akipongezwa na Balozi Chergui
Balozi Chergui akimkabidhi Tuzo ya Juu  ya Umoja wa Afrika ya Mwana wa Afrika ya Mwaka 2014, Binti wa Balozi Hashim Mbita, Sheila Hashima Mbita ambaye aliipokea Tuzo hiyo kwa niaba ya Baba yake ambaye hakuweza kufika kutokana na matatizo ya kiafya.
Balozi Chergui akimkabidhi Cheti Bi. Sheila Hashim Mbita kwa niaba ya Balozi Mbita

Balozi Chergui akimpongeza Bi. Sheila Hashim Mbitaaliyepokea Tuzo kwa  kwa niaba ya Balozi Mbita
Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Balozi Naimi Aziz wakipiga picha ya pamoja na Dkt. Salim Ahmed Salim na Bi. Sheila Hashim Mbita mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hizo.

Dkt. Salim akipongezwa na Balozi Augustine Mahiga huku Rais Mstaafu wa Cape Verde (kulia) akushuhudia.
Dkt. Salim akipongezwa na wajumbe mbalimbali waliokuwepo wakati wa hafala ya utoaji Tuzo.
Dkt. Salim katika picha ya pamoja na Balozi Naimi Aziz
Dkt. Salim katika picha ya pamoja na Bi. Zuhura Bundala, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Balozi Aziz katika picha ya pamoja na Bi. Sheila Mbita
Balozi Aziz akiwa na Balozi Mahiga katika picha ya pamoja na Bi. Sheila Mbita.



Tuesday, October 21, 2014

Warsha kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika yafunguliwa rasmi Mjini Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akifungua rasmi Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika. Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano huo unaofanyika  Jijini Arusha kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2014 na itawahusisha Wajumbe Maalum, Wasuluhishi, Mabalozi na Wataalam wa masuala ya Amani. Kaulimbiu ya warsha hiyo ni "Silencing the Guns-Owning the Future" na inalenga kujadili changamoto za usalama Barani Afrika na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Amani iliyotolewa na Makamu wa Rais,  Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto) kwa pamoja na aliyewahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na  Msuluhishi wa Mgogoro wa Syria, Dkt. Lakhdar Brahim wakisikiliza hotuba ya Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia hotuba hiyo akiwemo Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Mhe. Filberto Ceriani Sebregondi (kushoto)
Balozi Mstaafu Augustine Mahiga (kushoto) na Mhe. Sirpa Maenpaa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. Balozi Mahiga aliwahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akiwa na Balozi Mstaafu Walidi Mangachi wakati wa warsha hiyo ya amani na usalama.

Mwenyekiti wa Warsha hiyo ambaye ni Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui nae akizungumza wakati wa Warsha hiyo.
Wajumbe wakati wa ufunguzi wa warsha.
Sehemu nyingine ya wajumbe wakati wa warsha iliyojadili masuala ya amani na usalama Barani Afrika
Wajumbe zaidi
Warsha ikiendelea na wajumbe wakifuatilia kwa makini
Warsha ikiendelea
Waziri Membe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kuhusu Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika. Picha zote na Rosemary Malale
=================================================

Na Ally Kondo, Arusha.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa, licha ya machafuko yanayoendelea hivi sasa katika Bara la Afrika, nchi za Afrika hazina budi kuunganisha nguvu ili ziweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka ambazo zinatishia amani, usalama na utulivu wa Bara hili.  Changamoto hizo ni pamoja na ugaidi, uharamia, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, biashara ya dawa za kulevya, na biashara haramu ya binadamu.

Hayo aliyasema jijini Arusha siku ya Jumanne tarehe 21 Oktoba 2014 alipokuwa akifungua Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika ambayo itafanyika kwa siku tatu hadi Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014.

Makamu wa Rais alieleza kuwa ugaidi ni changamoto kubwa katika Afrika kwa sababu hakuna hata nchi moja ambayo imesalimika na uovu huo. Alisema kuwa, licha ya nchi za Afrika kulengwa na mashambulizi ya kigaidi pia zinatumika na magaidi kufanya mashambulizi yanayolenga maslahi ya nchi za kigeni, kujificha, kuandaa na kusajili magaidi wapya pamoja na kuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao hizo haramu.

Aidha, Dkt. Bilal alibainisha kuwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita Bara la Afrika limeshuhudia likikumbwa na zaidi ya migogoro 20 ambayo imelifanya bara hilo kutambulika na sifa ya kuwa eneo la vita. Ukweli huo unadhihirishwa na idadi kubwa ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ambapo kati ya vikosi 17 duniani, vikosi 9 vipo Barani Afrika. Aidha, asilimia 60 ya agenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinajadili namna ya kurejesha na kuimarisha amani Barani Afrika.

Dkt. Bilal alihimiza nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili ziweze kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro katika Bara la Afrika kwa kuwa athari zake ni kubwa. Athari hizo ni pamoja na kudumaza uchumi wa nchi na kuharibu miuondombinu ya kijamii ambayo ilijengwa kwa miaka mingi; kukwamisha juhudi za kupunguza umasikini; ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuzalisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo, Dkt. Bilal alisifu juhudi zinazofanywa na AU na washirika wake ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kupunguza migogoro Barani Afrika. Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, Bara la Afrika limeshuhudia kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, usuluhishi wa migogoro ya muda mrefu na migogoro ya baada ya uchaguzi katika nchi za Angola, Liberia, Sierra Leone, Rwanda, Burundi, Cote d’Ivoire na Madagascar.

“Kutokana na kuimarika kwa amani barani Afrika, uchumi wa bara hilo umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kati ya nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita nchi sita zinatoka barani Afrika.  Aidha, matarajio katika kipindi cha muongo mmoja ujao, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara uchumi wake utakua kwa kiwango cha asilimia saba” alisema Dkt. Bilal.

Makamu wa Rais aliendelea kueleza kuwa Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto za kiusalama kama ilivyo katika nchi za Libya; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Sudan; Somalia; Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Kwa upande wa Sudan Kusini, alisema kuwa Serikali imekubali ombi la Rais wa nchi hiyo, Mhe. Salvar Kiir la kusaidia usuluhishi wa mgogoro huo. Hivyo, Chama cha Mapinduzi tokea tarehe 12 – 18 Oktoba 2014 kimekuwa kikifanya majadiliano na vyama hasimu nchini Sudan Kusini kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Alisema kuwa majadiliano hayo hayataingilia au kuharibu majadiliano yanayoendelea nchini Ethiopia ambayo nayo yanalenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Warsha kuhusu amani na uslama Barani Afrika inayoendelea jijini Arusha ni ya tano kufanyika ambapo warsha zilizotangulia zilifanyika katika nchi za Misri na Cote d’Ivoire. Warsha hizo ambazo huwa zinawakutanisha Wajumbe Maalum, Mabalozi, Wataalamu wa masuala ya usalama zinalenga kujadili changamoto za usalama na namna ya kukabiliana nazo barani Afrika. 

-Mwisho-