Monday, May 15, 2017

Wapemba wapigwa msasa kuhusu Fursa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Stephen Mbundi akitoa mada kwenye semina ya mtangamano wa Jumuiya ya afrika Mashariki kisiwani Pemba ambapo alielezea namna Jumuiya hiyo ilivyoanzishwa, faida, fursa na changamoto mbalimbali zinazopatikana kwenye mtangamano wa Afrika Mashariki.
Bwa. Mbundi akiendelea kuelezea mada yake.
Bw. Othman Bakar Shehe akiuliza swali mara baada ya Bw. Mbundi (hayupo pichani) kumaliza kuwasilisha mada yake.
Bw. Mbundi akijibu swali lililoulizwa na Bw. Shehe (hayupo pichani).
Sehemu ya wajumbe na wajasiriamali wakisikiliza kwa makini majibu yaliyokuwa yakitolewa na Bw. Mbundi.

Friday, May 12, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yapokea magari ya msaada







Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) (katikati), akipokea funguo za Magari aina ya Toyota Land Cruiser  kutoka kwa  Balozi wa Kuwait hapa nchini, Mhe. Jasem Al-Najem. Anayeshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam leo. Waziri Mahiga alisema kuwa msaada huo umetolewa na Serikali ya Kuwait kwa ajili ya kusaidia masuala ya usafiri katika kipindi hiki cha mpito ambapo Serikali inahamia Dodoma. 
Waziri Mahiga akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Serikali na Wizara yake kwa ujumla mara baada ya kupokea msaada huo. 
Balozi Al-Najem naye akizungumza na kuishukuru Tanzania kwa ushirikiano anaoumpata kwenye utendaji kazi wake hapa nchini. Alisema Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wa pili kutoka kulia ni Afisa Ubalozi wa Kuwait haapa nchini.
Sehemu nyingine ya viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kutoka kulia ni Mhasibu Mkuu, Bw. Paul Kabale; Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi (wa pili kutoka kulia), Bw. Mapesi Manyama, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika,  Bw. Suleiman Saleh; Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, kutoka kushoto ni Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutoka kushoto ni  na wa pili kutoka kushoto ni Bw. Hangi Mgaka
Waziri akiendelea kuongea huku Watumishi wa Wizara yake wakimsikiliza kwa makini.

Picha ya pamoja mara baada ya shughuli kumalizika.

Wednesday, May 10, 2017

Rais wa Afrika Kusini awasili nchini kwa Ziara ya Kiserikali


Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma akiwa ameambatana na mkewe Mama Getrude SizakeleZuma wakishuka  kwenye ndege baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayotarajiwa kumalizika tarehe 11 Mei, 2017. 
Juu na chini Mhe. Rais Jacob Zuma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Mhe.  Jacob Zuma Rais wa Afrika Kusini akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi mara baada ya kuwasili  leo tarehe 10 Mei 2017.
Mhe.  Rais Jacob Zuma akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Saleh Kulia nia Mkuu wa Itifaki na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin. 
Mhe. Rais Zuma akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es salaam waliofika Uwanaja wa Ndege kwenye mapokezi rasmi yaliyoongozwa na Mhe. Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tanzania na Afrika kusini kuongeza maeneo ya ushirikiano ili kunyanyua uchumi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Mawaziri wa Kamisheni ya Pamoja ya Kitaifa kati ya Tanzania na Afrika Kusini, uliofanyika mapema leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake Mhe. Mahiga alieleza mkakati wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini katika kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika biashara na uwekezaji.
Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Maite Nkoana - Mashabane akihutubia katika mkutano huo ambao ulitanguliwa na mkutano wa siku mbili wa Makatibu wakuu. Pamoja na Mambo mengine, Mhe. Mashabane alieleza umuhimu wa kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya mataifa hayo mawili ili kuwaletea maendeleo wananchi wa mataifa yote. Pia  alitumia fursa hiyo kutoa salamu za rambirambi kwa taifa la Tanzania kwa kupatwa na msiba ambao umepunguza nguvu kazi na wataalamu wa kizazi kijacho.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akitoa utangulizi pamoja na kuratibu ratiba ya ufunguzi wa mkutano.
Sehemu ya Mawaziri wa Tanzania na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini wakifuatilia Mkutano.
Sehemu nyingine ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali ya Tanzania na Afrika kusini wakifuatilia Mkutano.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Afrika Kusini ambao pia walikua wenyeviti wa mkutano huo wakitoa ufafanuzi wa ratiba kwa Bi. Mindi wakati wa mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri.
Picha ya Pamoja ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini.

Tuesday, May 9, 2017

Balozi Fatma awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho nchini Qatar

Mhe. Fatma Mohammed Rajab, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar akiwa katika mazungumzo na Mhe. Sultan bin Saad Al Muraikhi, Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje wa Qatar. Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho. Wawili hao walizungumza masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar.

Balozi Mteule wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Fatma Mohammed Rajab akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Sultan bin Saad Al Muraikhi, Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje wa Qatar ofisini kwa Mhe. Waziri. Mhe. Fatma Rajab anakuwa Balozi Mkazi wa kwanza kuiwakilisha Tanzania katika Taifa la Qatar. Mhe. Balozi alipowasili kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Doha alipokelewa na Idara ya Itifaki ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar. Aidha, wawakilishi wa Watanzania wanaoishi nchini humo walifika Uwanja wa Ndege kumlaki

Mhe. Balozi Fatma Mohammed Rajab, akiwa na viongozi wa Watanzania wanaishi nchini Qatar.

Monday, May 8, 2017

Tanzania na Afrika Kusini za dhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Tume ya Marais ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Makatibu Wakuu nao wakifuatilia kwa makini Hotuba ya ufunguzi iliyokuwa ikitolewa na Dkt. Mlima.

Dkt. Mlima akiendelea kuzungumza
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward XolisaMakaya naye akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo.
Dkt. Mlima pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (wa kwanza kulia), wakimsikiliza kwa makini Bw. Makaya (hayupo pichani).
Sehemu nyingine ya Maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Maafisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa Mkutano huo.
Sehemu ya washiriki kutoka Tanzania na Afrika Kusini walioshiriki katika ufunguzi huo wakiendelea kuwasikiliza viongozi (hawapo pichani)walikuwa wakitoa hotuba zao wakati wa ufunguzi huo.
Wakiwa katika picha ya pamoja, mara baada ya kumaliza ufunguzi.
Dkt. Mlima akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ufunguzi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akielezea jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo kukamilika.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Tanzania na Afrika Kusini za dhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.



Wataalamu wa Tanzania na Afrika Kusini wapo katika mkutano wa siku nne wa kuandaa mpango bora wa kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi hizo.

Mkutano huo unaojulikana kama Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) umefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima jijini Dar Es Salaam leo.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa kuwa licha ya nchi zetu kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri tokea enzi za ubaguzi wa rangi, lakini bado utakuwa chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo tutakayokubaliana na wenzetu” Balozi Mlima alisema.  

Balozi Mlima alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini BNC ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC.  Tokea uwekaji saini wa makubaliano hayo, chombo hicho hakikuweza kukutana licha ya kuwa,  makubaliano hayo ndiyo yatakuwa mwongozo katika majadiliano yatakayoendelea hadi tarehe 11 Mei 2017.

Kwa mujibu wa Balozi Mlima, uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda. Kwa takwimu zilizopo takribani makampuni 226 ya Afrika Kusini yamewekeza nchini mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 803.15 na kuajiri zaidi ya watu 20,917. Alisema idadi ya makampuni inaweza kuongezeka kwani kuna makampuni mengi mapya kutoka Afrika Kusini yameshaonesha dhamira ya kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward Makaya alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini hazijafanya vya kutosha kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kijamii. Alisema hadi wakati huu nchi hizo zimesaini makubaliano na mikataba takribani 14 ambayo ni michache ukilinganisha na urafiki na udugu uliopo baina ya nchi hizo.

Hivyo, alisistiza umuhimu wa kikao hicho kufanya majadiliano yatakayowezesha uwekaji saini wa mikataba mingi zaidi. Alisisitiza umuhimu wa mikataba hiyo kuzingatia maslahi ya pande zote. 



-Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 08 Mei, 2017

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kufanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu Ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini Mhe. Jacob Zuma, ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku 3. Pamoja na mambo mengine,  Rais Zuma pia atatembelea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha tiba ya ugonjwa wa moyo (Jakaya Kikwete Cardiac Institute), na pia kufungua rasmi Ubalozi wao hapa nchini.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Suleiman Salehe, akimsikiliza Waziri Mahiga (Hayupo pichani) katika mkutano na waandishi wa Habari
Sehemu ya waandishi wa habari wakinukuu maeneo mbalimbali yaliyotajwa na Waziri Mahiga kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini



1.      UTANGULIZI

(i)      Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini, kuanzia tarehe 10 hadi12 Mei 2017, kwa mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(ii)     Ziara hii inafanyika baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

(iii)    Mheshimiwa Rais Zuma anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 10 Mei 2017, jioni na kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli.

(iv)    Ziara hii itatoa fursa kwa Viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara. Ujio wa Mheshimiwa Rais Zuma ni fursa nzuri sana ya kuendelea kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri naya kihistoria kati ya nchi zetu mbili.

(v)     Mheshimiwa Rais Zuma anafuatana pia na wafanyabiashara takribani 80. Hii ni fursa muhimu sana katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Hivyo, tarehe 11 Mei 2017, kutakuwepo na Kongamano la Wafanyabiashara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JINCC).

(vi)    Ziara ya Mheshimiwa Rais Zuma inaenda sambamba na vikao vya Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission - BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Mkutano wa Marais umepangwa kufanyika tarehe 11 Mei, 2017. Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 10 Mei, 2017 na kikao cha Makatibu Wakuu kitafanyika tarehe 8 na 9 Mei, 2017.



2.0.    RATIBA

(i)      Wakati wa ziara hiyo, tarehe 11 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma atakutana na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli kwa mazungumzo ya faragha kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili.

(ii)     Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa Mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano.

(iii)    Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Rais Zuma atashiriki chakula cha mchana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini katika Hoteli ya Hyatt Regency. Pia, Mheshimiwa Rais Zuma na Mheshimiwa Rais Magufuli watashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

(iv)    Aidha, jioni ya siku hiyo, Mheshimiwa Rais Zumana ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mheshimiwa Rais Magufuli.

(v)     Tarehe 12 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma anarajiwa kufungua rasmi Jengo jipya la Ubalozi wa Afrika Kusini nchini pamoja na kutembelea Taasisi ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

(vi)    Mheshimiwa Rais Zuma na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Afrika Kusini.



3.0.    MAHUSIANO BAINA YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

(i)      Mahusiano ya Tanzania na Afrika Kusini ni mazuri na ni ya muda mrefu tangu wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini zilizoongozwa na Chama kikongwe cha African National Congress (ANC). Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kikanda na hasa ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Kwa sasa, Afrika Kusini ni Mwenyekiti wa SADC na Tanzania ni Mweyekiti wa SADC Organ, hatua inayotoa nafasi ya kushirikiana zaidi.

(ii)     Aidha, ushirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika kila mara kwa Viongozi wakuu kutembeleana na viongozi wa ngazi za juu Serikalini kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu mbili. Kama mtakumbuka Julai 2011, Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifanya Ziara ya Kiserikali nchini Afrika Kusini ambayo ndiyo iliyozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Tume ya Marais ambayo ndiyo iliyotuwezesha kukutana leo.



(iii)    Uhusiano wa Vyama vya Siasa vya CCM na ANC

Vyama vya ANC na CCM vina mahusiano mazuri na Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati yao.



(iv)    Mikataba ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hadi sasa, Tanzania na Afrika Kusini tayari zimetia saini Mikataba ya Ushirikiano (MoU) kumi na tano (15), ambayo inagusa sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi na teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo.



(v)    Ushirikiani katika Utatuzi wa Migogoro katika Kanda

Tanzania na Afrika Kusini zimeendelea kufanya kazi pamoja katika juhudi za utatuzi wa migogoro na kuhakikisha kwamba Afrika inakuwa sehemu salama. Nchi hizi mbili zimeshiriki katika kutatua migogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Sudan Kusini. Tanzania na Afrika Kusini zote zimechangia Askari katika Brigedi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Amani na Usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (United Nation Force Intervention Brigade-FIB) kwa lengo la kutuliza uvunjifu wa amani Mashariki mwa Kongo. Vile vile, nchi hizi mbili kwa pamoja zimekua zikishirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sudan Kusini.



(vi)   Uhusiano katika Nyanja za Uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini



Ø Uhusiano ya uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huo mzuri umezidi kuchochea na kurutubisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na wa kihistoria.



Ø Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazochangia idadi kubwa ya wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre-TIC) kimesajili jumla ya miradi 226 kati ya mwaka 1990 hadi 2016. Miradi hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 803.15 na imetoa ajira zipatazo 20,916.

(vii)  Uhusiano katika Sekta ya Biashara



Ø Kiwango cha biashara (volume of trade) imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Mwaka 2007 ilikuwa Tsh Milioni 976,331 na mwaka 2016 ni Tsh 2,402,211.20. Hili ni ongezeko kubwa na linaleta matumaini ya ushirikiano zaidi.



Ø Bidhaa ambazo Tanzania inauza nchini Afrika Kusini ni pamoja na maua, kahawa, wanyama hai, chai, nguo, pamba, vito vya thamani, tumbaku na mafuta ya kupikia. Bidhaa zinazoagizwa kutoka Afrika Kusini ni pamoja na maziwa na mazao yote ya maziwa, matunda aina ya apple, mbegu za mahindi, mafuta ya soya, sukari kwa matumizi ya viwanda, juisi za matunda, mafuta ya kulainisha mitambo, bidhaa za vileo, Acrylic polymers, lami, magari, pampu za maji, bidhaa za chuma, vitabu, mashine, na trela.

(vii)  Mchango wa Madawati wa Afrika Kusini kwa Serikali ya Tanzania



Ø Katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, kwa kupitia Ubalozi wake hapa nchini, Serikali ya Afrika Kusini iliweza kuchangia jumla ya madawati 1100 kwa shule za Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma. Madawati hayo yalikabidhiwa kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.



Ø Pamoja na hayo, Serikali ya Afrika Kusini inatarajia kuanzisha programu mahsusi ya kubadilishana walimu na uzoefu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuinua sekta ya elimu.



4.0.    TAARIFA FUPI KUHUSU TUME YA USHIRIKIANO YA MARAIS (BI-NATIONAL COMMISSION) KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI



Sasa naomba niwape taarifa fupi kuhusu Mkutano wa Tume ya Ushirikiano ya Marais



(i)      Tanzania na Afrika Kusini zilisaini Mkataba wa kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) tarehe 19 Julai 2011 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tume ya Ushirikiano ya Marais imechukua nafasi ya Tume ya Uchumi ya Pamoja ya Marais (Presidential Economic Commission-PEC) iliyoanzishwa mwaka 2005. Kama nilivyosema awali, Mkataba huu ulisainiwa wakati wa ziara ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tano, Mhshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.



(ii)     Mkataba wa kuanzisha BNC umeainisha maeneo kumi (10) ya ushirikiano ambayo ni Biashara na Uwekezaji (Trade and Investment), Maendeleo ya Miundombinu (Infrastructure Development), Kilimo (Agriculture), Elimu, Sayansi na Teknolojia (Education, Science and Technology), Ulinzi na Usalama (Defence and Security), Habari, Utamaduni na Michezo (Infrastructire, Culture and Sports), Afya (Health), Nishati na Madini (Energy and Minerals) na Maliasili na Utalii (Natural Resources and Tourism).



(iii)    Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Mashirikiano ya Marais (BNC) unatarajiwa kufanyika kuanzia leo, tarehe 8 hadi 11 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utatanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu tarehe 8 na 9 Mei, 2017 ukifuatiwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 10 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utafanyika tarehe 11 Mei, 2017 ambapo Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma watakuwa Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo. 



(iv)    Wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Marais, Mikataba ifuatayo inatarajiwa kutiwa saini:-



(a) Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Masuala ya Bio Anuwai na Uhifadhi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini (Memorandum of Understanding between the Government of the United Republic of Tanzania and the Government of the Republic of South Africa on Cooperation in the Field of Biodiversity Conservation and Management);



(b)Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Maji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini; na



(c) Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Uchukuzi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini;



(v)     Pia kuna Mikataba mingine inaendelewa kufanyiwa kazi na mara itakapokamilika, Mawaziri wa sekta husika watasaini. Mikataba hiyo ni pamoja na wa Sekta ya Utalii, Sekta ya habari, Sekta ya kilimo, sekta ya afya, niitaje hiyo tu kwa sasa.



(vi)    Tofauti na Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (BNC) inashirikisha Marais wa Nchi mbili ambapo katika JPC inaishia katika ngazi ya Mawaziri.  Ushiriki wa Marais katika Tume ya Pamoja ya Ushirikiano unatoa uzito wa pekee katika utekelezaji wa maeneo ya mashirikiano yaliyoafikiwa.





-Mwisho-



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 08 Mei, 2017