Monday, September 17, 2018

Uzinduzi wa ziara ya kitabibu Wilayani Kondoa




Dkt. Gwajima azindua ziara ya kitabibu Wilayani Kondoa

Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akihutubia kwenye uzinduzi wa ziara ya Madaktari Wauguzi kutoka taasisi binafsi ya Health Education Development (HEAD INC) ya watanzania waishio nchini Marekani ya kutoa huduma za kitabibu  kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa. Dkt. Gwajima alitumia fursa hiyo kuwapongeza taasisi hiyo kwakuona umuhimu wa kuja nyumbani kutoa huduma za afya kwa watanzania wenzao. Dkt. Gwajima hakusita kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Diaspora kwa kuwezesha kufanikisha Ziara ya Madaktari na Wauguzi hao kutoka Nchini Marekani ambapo inaonyesha namna mwitikio wa Watanzania waishio nje ya nchi katika kuchangia maendeleo nchini.  Madaktari na Wauguzi hao watakuwa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa siku nne (4) wakitoa huduma za Afya kwa wagonjwa mbalimbali. 
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta (wa kwanza kushoto), na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Anisa Mbega wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa ziara ya Madaktari na Wauguzi kutoka (Head Inc)
Sehemu ya Watumishi kutoka wilaya ya Kondoa wakimsikiliza kwa makini Dkt. Gwajima alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na wauguzi 
Sehemu ya Wananchi waliojitokeza kwenye Ufunguzi huo wakimikiliza kwa makini Dkt. Gwajima
Mkuu wa Wilaya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta naye alipata fursa ya kuwakaribisha Madaktari na Wauguzi hao kwenye Wilaya ya Kondoa na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote cha siku nne watakachokuwa wanatoa huduma za Afya katika Hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya NJe na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbega naye alipata Fursa ya kuwasalimia wananchi wa Wilaya ya Kondoa walio jitokeza kwenye Uzinduzi wa Ziara hiyo ya Madaktari na Wauguzi, pia alitumia fursa hiyo Kuwashukuru wanadiaspora kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya nchini kwa namna mbali mbali ikiwemo kuleta ujuzi wao,  kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Pia aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Kondoa kupitia Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makutta kwa maandalizi na mapokezi mazuri ya ziara hiyo. 

 Juu na chini sehemu ya wananchi wakiendelea kusikiliza hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye uzinduzi huo.

 Juu na chini sehemu ya wananchi wakianza kupata huduma za kiafya mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi huo

Picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi
Balozi Anisa Mbega akiagana na Dkt. Gwajima mara baada ya kumaliza ufunguzi wa Ziara ya Madaktari na Wauguzi.










Sunday, September 16, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mabalozi wa India na Qatar waliopo nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Mhe. Sandeep Arya. Katika mazungumzo yao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ya manufaa kwa nchi zote mbili.

Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda alikutana na Balozi wa Qatar nchini na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Qatar.

Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day) yafanyika Kenya

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day)

Bonde la mto Mara linalounganisha Tanzania na Kenya linashikilia uhai sio wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee, bali uhai wa nchi za Sudan, Ethiopia na Misri nazo kwa kiasi kikubwa unategemea bonde hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na viongozi mbalimbali walioshiriki sherehe za maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika katika Kaunti ya Narok, Kenya siku ya Jumamosi tarehe 15 Septemba 2018. 

Maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu "Mto Mara unatuunganisha wote" hufanyika kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya kila mwaka tarehe 15 Septemba kwa madhumuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya bonde la mto Mara.
 “Siku ya Mara hailengi chochote, isipokuwa kutukumbusha jukumu letu la kutunza mazingira”, Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe Samuel Oletunai alisema katika maadhimisho hayo.

Mhe. Samuel Oletunai aliwaasa Wakenya kutunza msitu wa Mau ambao ndio chanzo kikuu cha maji yanayotiririka mto Mara na kuiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa mgogoro katika msitu huo unapatiwa ufumbuzi haraka. 

Mwakilishi wa Serikali ya Tanzania katika maadhimisho hayo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb) alieleza kuwa maji hayana mbadala kama chakula ambapo ukikosa wali utakula ugali, hivyo aliwahakikishia wadau waliohudhuria sherehe hizo kuwa Serikali ya Tanzania haitakuwa kikwazo cha harakati za kuhifadhi ikolojia ya mto Mara.

Utunzaji wa ikolojia ya mto huo ilielezwa kuwa ni muhimu kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utalii na shughuli nyingine za kiuchumi ambapo Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) katika sherehe hizo alisema kuwa Tanzania na Kenya zinapata zaidi ya Dola milioni 300 kwa mwaka kutokana  na shughuli za kiuchumi katika mto Mara.

Tukio kubwa linalovutia watalii wengi duniani ni uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu zaidi ya milioni 1.2 baina ya mbuga ya Serengeti nchini Tanzania na Masai Mara nchini Kenya katika kipindi cha Julai hadi Oktoba ambapo mara zote wanyama hao hukatiza mto Mara.

Mwakilishi huyo wa USAID alitaja sababu zinazoharibu ikolojia ya mto huo kuwa ni pamoja na uharibifu wa misitu, matumizi makubwa ya maji, ujenzi wa miundombinu mbalimbali na mmomonyoko wa udongo. Hivyo, aliahidi kuwa USAID itaendelea kushirikiana na wadau kukabiliana na changamoto hizo kwa kusaidia miradi ya maji na utunzaji wa mazingira. Alisema mto huo lazima uhifadhiwe kwa sababu ni mali ya watu waliopita, wasasa na wajao.

Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, Mhe. Simon Chelugui aliwahakikishia waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa Serikali ya Kenya imejizatiti kulinda na kuhifadhi ikolokia ya mto Mara kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Kenya, alizitaja kuwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya maji na usafi katika mashule na aliutaja mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika kwenye mpaka wa Isebania ambao utawanufaisha pia Watanzania wanaoishi maeneo ya Sirari.

Sherehe hizo zilipambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma ambao uzalishaji wake unazingatia uhifadhi wa mazingira.

Aidha, kulikuwa na burudani za ngoma, michezo ya mpira wa miguu  mashairi, tunzo na ngojera ambazo zote zililenga kutoa ujumbe wa kuhimiza utunzaji wa mazingira. 
  
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Narok, kenya
16 Septemba 2018
Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara akitoa hotuba ya ufunguzi ambayo ilielezea mikakati mbalimbali inayochukuliwa ili kukabiliana na vihatarishi vya kutokomeza ikolojia ya Mto Mara.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mara yaliyofanyika kaunti ya Narok nchini Kenya
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Mara.

Gavana wa akaunti ya Narok, Mhe. Samuel Oletunai akihutubia watu mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo yalifanyika katika kaunti yake ya Narok.

Watu mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mara wakifuatilia hotuba za viongozi.

Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) akivalishwa vazi la kimasai kabla hajatoa hotuba yake katika maadhimisho hayo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima akitoa neno la mkoa katika maadhimisho hayo.

Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka moja ya banda la maonesho ya Siku ya Mara kuhusu utunzaji wa mazingira.

Mstari wa kulia kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka mmoja wa washiriki wa maonesho ya siku ya Mara namna anavyoshiriki katika shughuli za kutunza mazingira.

Kaimu Murugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Kijamii, Bw. Eliabi Chodota akiteta jambo na Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula.

Sehemu ya umati wa watu waliohudhuria maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara wakisikiliza hotuba za viongozi.

Burudani kutoka kwa wanafunzi wakihimiza umuhimu wa kutunza mazingira.

Mmoja wa wanaharakati wa kutunza Mazingira akipokea cheti cha kutambua mchango wake kutoka kwa Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe. Samuel  Oletunai. katikati ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Ally Said Matano.

Friday, September 14, 2018

Prof. Mkenda na Balozi wa Kenya wakutana kujadili utatuzi wa changamoto za biashara mipakani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu walipokutana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya. Pamoja na mambo mengine walijadili changamoto za biashara hususan tukio la hivi karibuni la kukwamishwa kwa bidhaa za Tanzania kuingia Kenya kwa sababu mbalimbali ikiwemo vinywaji, mchele na unga wa ngano. Katika kikao hicho ilikubalika Tanzania kuitisha kikao cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki na Biashara na Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Tanzania na Kenya. Pia walikubaliana kuendelea kuratibu ziara za viongozi wa juu kati ya nchi hizi mbili kwa lengo la kukuza mahusiano.

Prof. Mkenda na Balozi Kazungu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo yao.

Thursday, September 13, 2018

Waziri Mahiga afungua rasmi Ofisi za Uwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani jijini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa pamoja na Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Detlef Waechter wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Ofisi Ndogo ya Uwakilishi wa Ubalozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani jijini Dodoma. Ofisi hiyo ni ya kwanza kwa Balozi za nje zilizopo Tanzania kufunguliwa Dodoma. Ufunguzi huo ni katika kuitikia wito wa Mhe. Rais baada ya Serikali kuhamia  rasmi Dodoma. Ofisi hizo ambazo zipo ghorofa ya nne katika Jengo la PSPF Barabara ya Benjamin Mkapa zitatoa huduma mbalimbali kwa Serikali, Bunge na Wananchi kwa ujumla huku zikisimamiwa na Bw. Richard Shaba ambaye ni Mtanzania. Pia Ofisi hizo zimejumuisha Mashirika ya Misaada ya Ujerumani ambayo ni GIZ na KFW.
Mhe. Waziri Mahiga kwa pamoja na Balozi Waechter wakifungua kitambaa kuashiria kuwa Ofisi Ndogo za Uwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani zimefunguliwa rasmi jijini Dodoma
Mhe. Waziri Mahiga akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo aliipongeza Serikali ya Ujerumani kwa uamuzi huo ambao ni ishara njema kwamba nchi hiyo inaunga mkono kwa dhati uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Pia alisema Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Ujerumani kwani nchi hiyo ina uzoefu wa kuhamisha makao makuu kutoka Bonn kwenda Berlin ambapo ilifanya hivyo miaka 30 iliyopita
Mhe. Waziri Mahiga akiendelea na hotuba yake. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (wa nne kushoto), Balozi Waechter (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga (kushoto), Msimamizi wa Ofisi Ndogo za Uwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani jijini Dodoma, Bw. Richard Shaba (wa tatu kushoto), Katibu wa Waziri, Bw. Gerald Mbwafu (wa pili kushoto na Wawakilishi kutoka GIZ na KFW. 
Mhe. Balozi Waechter nae akizungumza ambapo alisema wamefungua Ofisi hizo ili kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo katika nyanja mbalimbali kati ya Tanzania na Ujerumani
Mhe. Waziri Mahiga akiwa katika picha na Mhe. Balozi Waechter pamoja na viongozi wengine walioshiriki hafla hiyo
Mhe. Waziri Mahiga akimpongeza Balozi Waechter ufunguzi wa Ofisi Ndogo za Uwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani jijini Dodoma
Wageni waalikwa walioshiriki ufunguzi wa Ofisi hizo wakifuatilia matukio mbalimbali 
Mhe. Waziri Mahiga akizungumza na vyombo vya habari
Awali Mhe. Waziri Mahiga alisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi Ndogo za Uwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani zilizopo jijini Dodoma. Kushoto ni Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Detlef Waechter. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga
Mhe. Waziri Mahiga, Mhe. Balozi Waechter na Mkuu wa Dodoma Dkt. Mahenge wakiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo wakiwemo Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Picha ya pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Ujerumani nchini



Wednesday, September 12, 2018

Tanzania ilivyoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara nchini Msumbiji

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi, (katikati), akikaribishwa katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM yaliyofanyika tarehe 27 Agosti hadi 2 Septemba 2018 Maputo nchini Msumbiji. Wengine ni Bw. Albert Philipo, Afisa wa Wizara, Idara ya Diaspora (kushoto) na ndugu Nelson Nkini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania (Diaspora) wanaoishi nchini Msumbiji  Ushiriki wa wafanyabiashara kutoka Tanzania uliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Carlos Agostinho do Rosário wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM alipotembelea banda la Tanzania na kukaribishwa na Bi. Getrude Ngweshemi, Kaimu Meneja - Masoko ya Ndani wa TanTrade na Bw. Albert Philipo, Afisa Idara ya Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje ambapo alipatiwa maelezo kuhusu bidhaa za viwandani pamoja na vivutio vya utalii wa Tanzania.
                                                                                                         

Balozi Rajabu Luhwavi akifafanua jambo kwa wafanyabiashara na washiriki kutoka mataifa mengine (hawapo pichani) waliofika katika banda la Tanzania wakati maonesho ya biashara ya 54 ya FACIM yakiendelea.  Wafanyabiashara wa Tanzania walikutana na wafanyabiashara wenzao kutoka mataifa zaidi ya 20 ambapo walibadilishana mawazo na kuzitangaza bidhaa na huduma za Tanzania katika maonesho hayo.
Balozi Rajabu Luhwavi akipokea maelezo kutoka kwa Afisa wa Wizara, Bw. Albert Philipo kuhusu bidhaa za Tanzania zilizoletwa na wafanyabiashara mbambali kutoka Tanzania wakati wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya 54 ya FACIM Maputo, Msumbiji. Wengine katika picha hiyo ni wafanyabiashara kutoka Kampuni mbalimbali nchini Tanzania.

Mheshimiwa Balozi Luhwavi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania walioshiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 54 ya FACIM mjini Maputo.
Gavana wa Nampula, Mheshimiwa Victor Borges akiwa na Mheshimiwa Balozi Rajabu Luhwavi kushoto kwake wakikata utepe wakati wa kufungua Maonyesho ya Biashara Nampula tarehe 20 Agosti 2018. Maonesho hayo yalihusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na wenyeji wa Msumbiji. 
Mheshimiwa Balozi Rajabu Luhwavi akitoa maelezo mafupi wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Biashara Nampula yaliyohusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania. Kwa upande wake Balozi Luhwavi, alieleza kuwa maonesho haya ni ya kimkakati kwa ajili ya kukuza na kuimarisha umoja, mshikamano na mahusiano ya kiuchumi yaliyojengwa na waasisi wetu hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar na hayati Samora Moises Machel, aliyekuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Msumbiji. Maonesho haya yalifungua fursa za masoko kwa bidhaa za viwanda vya Tanzania pamoja na kuendeleza juhudi za utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa vitendo na kukuza uchumi, hususan uchumi wa viwanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Juma Ali Juma aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kilele cha maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania mjini Nampula akiwa pamoja na Balozi Rajabu Luhwavi na Katibu Mkuu wa Jimbo la Nampula, Bi. Veronica Langa wakipata maelezo kuhusu teknolojia ya ufugaji samaki kutoka kampuni ya Dokaman ya nchini Tanzania.
Kutoka kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Juma Ali Juma, Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara TanTrade, Bi. Anna Bulondo wakipata maelezo kutoka kwa wawakilishi wa kampuni ya A - Z Textile Mills. 

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mheshimiwa Rajabu Luhwavi akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ndugu Juma Ali Juma wakipokea maelezo kuhusu bidhaa zinazotengenezwa na Kampuni ya Tanzania M/s Darsh Industries wakati wa maonesho ya bidhaa za viwanda mjini Nampula, Msumbiji.