Friday, August 24, 2018

Waziri Mahiga amuaga Balozi wa Ubelgiji nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza kwenye hafla ya kumuaga Balozi wa Ubelgiji aliyemaliza muda wa kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania Mhe. Paul Cartier (wa tatu kutoka kulia). Dkt. Mahiga alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuiwakilisha nchi yake vyema hapa Tanzania. Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani), Kaimu Mkurugenzi Idara ya  Ulaya na Amerika, Bw.Jestas  Nyamanga na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Hyatt Regency  jijini Dar es Salaam.
Balozi Paul Cartier naye alipata fursa ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ushirikiano aliokuwa akipata kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Mhe. Mwakyembe akisikiliza hotuba zilizokuwa zikitolewa na Dkt, Mahiga pamoja na Mhe.Cartier
Dkt. Mahiga akimkabidhi Balozi Cartier zawadi yenye mchoro wa Hifadhi ya  Mlima Kilimanjaro kama ukumbusho wa moja ya vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania
Waziri Mahiga (katikati), Balozi Cartier (wa nne kutoka kulia), Waziri Mwakyembe (wa tatu kutoka kulia), Bw. Nyamanga (wa tatu kutoka kushoto), Mke wa Balozi Cartier (wa nne kutoka kushoto) pamoja na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja.

 





Mikutano ya JPC ni Injini ya Maendeleo ya kiuchumi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Uganda zimepata mafanikio makubwa kupitia Mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyofanyika Arusha Aprili 2017 na sasa wa Kampala unaohitimishwa leo.

Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe .Dkt. Augustine Mahiga (Mb) na mwenzake wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa walipokuwa wanasoma hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.

Mafanikio yaliyoelezwa ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda na ushirikiano katika masuala ya elimu na mafunzo iliyosainiwa leo katika mkutano wa Kampala.

Mkutano huo ulijulishwa kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo unaridhisha na inalenga kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo ili kutimiza azma ya viongozi wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Museveni wa Uganda ya kukuza biashara kati ya nchi hizo.

Mikataba iliyosainiwa  inahusu uendelezaji wa miradi ya miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati ya Umeme, barabara hususan za mipakani, bandari, reli na usafiri wa anga.

Kufuatia mikataba hiyo miradi mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kikagati/ Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020. Aidha, Shirika la Ndege la Tanzania litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam hadi Entebbe mwishoni mwa mwezi huu kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga katika mkutano wa Arusha mwezi Aprili 2018

Miradi mingine ni ya ukarabati wa bandari za Bell na Bukasa na ukarabati wa meli za Kagawa na Pamba kwa upande wa Uganda ambayo italeta muunganiko mzuri katika usafirishaji hasa baada ya Reli ya Kisasa ya kiwango cha kimataifa inayojengwa na Tanzania itakapokamilika.

Waheshimiwa Mawaziri walisisitiza umuhimu wa Serikali za Tanzania na Uganda kuwekeza ipasavyo katika ushoroba wa kati ili kuleta muunganiko kwa ajili ya kukuza biashara. Aidha. Walisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kushughulikia changamoto za mipakani kwa haraka kadri zinavyojitokeza

Kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa miradi inayoafikiwa katika mikutano hiyo, pande zote mbili ziliwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu. 

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu walishiriki mkutano huo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kampala
23 Agosti 2018

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akisoma hotuba katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2918.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala kwa siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji akichangia jambo katika mkutano wa pili wa JPC kati ya Tanzania na Uganda.


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC0 kati ya Tanzania na Uganda.

Sehemu ya Waheshimiwa Mawaziri kutoka Uganda wakiwa katika mkutano huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi akichangia jambo katika mkutano huo.

Wajumbe wa Tanzania na Uganda wakiendelea na mkutano.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) na Waziri wa Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Peter T. Lokeris wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kuendeleza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda. Aliyesimam kushoto kwa Mhe. Mahiga ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akibadilishana Mikataba na  Waziri wa Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Peter T. Lokeris baada ya kusainiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu ya Juu wa Uganda, Mhe. J.C Muyingo wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kushirikiana katika masuala ya Elimu na Mafunzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu ya Juu wa Uganda, Mhe. J.C Muyingo wakibadilishna Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa kushirikiana katika masuala ya Elimu na Mafunzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akimkabidhi Hati za Viwanja va Ubalozi wa Tanania nchini Uganda Mhe. Dkt. Augustine Mahiga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi wakibadilishana taarifa ya masuala yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo.


Wednesday, August 22, 2018

Mafanikio makubwa yamepatikana kupitia JPC, Balozi Mwinyi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda kwa ngazi ya Makatibu Wakuu. Katika hotuba hiyo, Balozi Mwinyi alieleza kuwa tokea JPC kati ya Tanzania na Uganda ilipoanzishwa mafanikio makubwa yamepatikana. Mafanikio hayo ni pamoja na kusainiwa kwa mikataba ya makubaliano mbalimbali ikiwemo mkataba wa kushirikiana katika ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kikagati/Murongo na makataba wa kushirikiana katika usafiri wa anga ambapo Tanzania inakusudia kuanza safari za moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam kwenda Kampala hivi karibuni. 

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini hotuba ya Balozi Mwinyi

Ujumbe wa Uganda ukifuatilia hotuba za ufunguzi zilizokuwa zinasomwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za Tanzania na Uganda.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akiongea na mwenyeji wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya kabla ya viongozi hao hawajafungua rasmi mkutano wa JPC kwa ngazi ya Makatibu Wakuu.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi akibadilishana mawazo na Balozi wa Uganda nchini Uingereza, Mhe. Leonard Mugerwa nje ya ukumbi wa mikutano.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Balozi Julius Onen akisoma hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika Kampala siku ya Jumatano tarehe 22 Agosti 2018.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko akichangia mada katika mkutano huo ambapo alisema kuwa Mamlaka ya Bandari imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zake

Mkurugenzi wa Shirika la kukuza Biashara katika nchi za Afrika Mashariki kwa upande wa Uganda (Trademark East Africa), Bibi Dawali Ssali akieleza mikakati ya inayofanywa na shirika hilo katika kuboresha mazingira ya biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. mikakati hiyo ni pamoja na kushirikiana na nchi za EAC kujenga vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani.


Wajumbe wa Uganda na Tanzania wakijadili mikakati ya kukuza na kuimarisha biashara kati ya nchi zao.


Tanzania na Uganda za azimia kukuza biashara kati yao

Tanzania na Uganda zimeazimia kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kukuza kiwango cha biashara kati yao ambacho kwa takwimu zilizopo sasa zinaonesha kipo chini mno.

Hayo yalibainishwa katika mkutano wa Jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo kando ya Mkutano wa pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) unaofanyika kwa silku tatu jijini Kampala tokea tarehe 21 Agosti 2018.

Mgeni Rasmi katika mkutano huo ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirikia ya Uganda, Balozi Julius Onen alieleza kuwa Tanzania na Uganda zina nafasi kubwa ya kukuza biashara endapo njia za usafiri zitaboreshwa, vikwazo visivyo vya kibiashara vitaondolewa pamoja na kuwa na mikakati ya pamoja ya kuweka viwango vya ubora vinavyotambulika katika nchi zote na kanda nzima kwa ujumla.

Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema kuwa Mamlaka ya Bandari imeboresha kwa kiasi kikubwa huduma zake ikiwemo kuanza upya kwa njia ya Dar Es Salaam- Mwanza hadi bandari ya Bell nchini Uganda. Alisema kufunguliwa kwa njia hiyo kumepunguza idadi ya siku za kusafirisha mizigo kutoka Dar Es Salaam hadi Uganda ambapo kwa sasa mizigo inasafirshwa kwa siku nne  na kwa kiwango kikubwa na gharama nafuu.

Jambo hilo liliungwa mkono na wafanyabiashara wa Uganda walioshiriki mkutano huo ambapo waliipongeza TPA kutokana na hatua inazozichukua kuboresha huduma katika Bandari ya Dar Es Salaam na walikiri kuwa kufunguliwa kwa njia ya Dar Es Salaam-Mwanza hadi Bandari ya Bell kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kufanya biashara pamoja na muda wa kusafirisha bidhaa zao.

Balozi Onen aliendelea kueleza kuwa licha ya changamoto zilizopo za kufanya biashara kati ya Uganda na Tanzania lakini vihatarishi vya kufanya biashara na Tanzania ni vichache ukilinganisha na nchi nyingine.  Hivyo, aliwsihi wafanyabiashara wa Uganda na Serikali kwa ujumla kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na nchi hiyo.

Alibainisha kuwa Tanzania na Uganda zinaweza kufaidika zaidi kibiashara kutokana na nchi zote kuwa kwenye eneo la Maziwa Makuu ambalo lina soko kubwa kutokana na idadi kubwa ya watu katika eneo hilo. Hivyo alizihimiza Serikali zaTanzania na Uganda kufanya uwekezaji mkubwa katika ushoroba wa kati (central corridor) ili kukuza biashara.

Mkutano wa JPC unatarajiwa kufungwa rasmi Alhamisi kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi. Isack Kamwele (Mb) na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu (Mb) watashiriki mkutano huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kampala
22 Agosti 2018

Tuesday, August 21, 2018

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Wanawake amewasili Nchini leo.

Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alipowasili Ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo.
Mhe. Balozi. Dkt Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Mhe Bi. Phumzile Mlango.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake, Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Katika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Celestine Mushy mara baada ya kumpokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya zaira ya kikazi Nchini kuanzia tarehe 21 hadi 24 Agosti, 2018


Mhe. Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka  akimweleza jambo Balozi Mushy wakati wa mazungumzo yao mara baada ya kuwasili nchini


Tanzania ya tia fora kwenye Tamasha la Michezo la Afrika Mashariki jijini Bujumbura


Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania (waliovalia jezi nyeupe) ikichuana na timu ya wanawake ya mpira wa miguu ya Burundi katika uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi. Katika pambano hili timu ya Taifa ya Tanzania iliibuka na ushindi mnono wa magoli 8-1 dhidi ya timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Burundi.

Kufuatia ushindi huu timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake  ya Tanzania inatarajia kukutana na Timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Kenya katika mchezo utakaofanyika siku ya Alhamis terehe 23 Agosti 2018 kwenye uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi.

Aidha, timu ya mpira wa pete ya Taifa ya Tanzania pia iliibuka na ushindi mnono wa magoli 79-14 dhidi ya timu ya mpira wa pete ya Burundi. Kufuatia shindi huo timu ya Taifa ya mpira wa pete inatarajia kukutana na timu ya mpira wa pete ya Uganda hapo kesho tarehe 22 Agosti, 2018 katika viwanja vya Chuo cha Ualimu cha ENS jijini Bujumbura

Vilevile timu ya mchezo wa Karate ya Taifa nayo imeanza kushiriki mchezo huo katika hatua mbalimbali, ambapo hadi sasa mwenyeji wa tamasha hilo Burundi ndiye anayeongoza kushida kwenye vipengele vingi vya mchezo huo.

Tanzania katika Tamasha hili inashiriki katika michezo minne tofauti ambayo ni Riadha (mashindano bado hayajaanza), mpira wa miguu (kwa timu ya wanawake pekee), karate na mpira wa pete.

Tamasha la kwanza la Michezo la Afrika Mashariki lilianza  kufanyika tarehe 15 Agosti na litafikia tamati Agosti 30, 2018 nchini Burundi.

Moja wa msambuliaji wa timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania akiwachambua mabeki wa timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Burundi. Katika mchezo huo Tanzania iliibuka na ushindi wa magoli 8 - 1

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania ikicheza dhidi ya timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Burundi katika uwanja wa mpira wa Gitega, Burundi.
Timu ya  mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania ikishangilia ushindi pamoja mashabiki waliojitokeza kushuhudia shindano hilo

Ufunguzi wa Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Uganda jijini Kampala

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda unaofanyika jijini Kampala kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018. Balozi Mugoya katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kuboresha miundombinu na kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na Uganda

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya maafisa waandamizi akisoma hotuba katika ufunguzi wa mkutano wa JPC. Bw. Mbilinyi alisema kuwa Mkutano huo pamoja na mambo mengine utathimni utekelezaji wa masuala yaliyokubalika wakati wa mkutano wa kwanza wa JPC uliofanyika Arusha mwezi Aprili 2017 na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa masuala ambayo hayajakamilika.
Balozi Mugoya na Bw. Mbilinyi wakiwa katika meza kuu kabla hawajasoma hotuba za ufunguzi.
Kutoka kushoto ni Bw. Mbilinyi, Bw. Innocent Luoga, Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Bi. Tuma Abdallah Kaimu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) wakiwa katika meza kuu.

Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia hotuba za ufunguzi wa Mkutano wa JPC. Kutoka kushoto ni Bi. Mwadawa Ali kutoka kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN), Bw. Paul Makelele kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Karim Msemo wa Wizara ya Mifugo.





Sehemu ya ujumbe wa Uganda ukifuatilia ufunguzi wa mkutano wa JPC. 


Mhandisi Robert Marealle kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiongea jambo katika mkutano wa JPC.


Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Erick Ngilangwa na Bi. Elizabeth Rwitunga ambao ni sehemu ya sekretarieti ya mkutano huo wakinukuu masuala muhimu yanayozungumzwa.

Ujumbe wa Tanzania

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvator Mbilinyi wakibadilishana mawazo baada ya ufunguzi wa mkutano wa JPC kukamilika.

Picha ya Pamoja