Sunday, October 28, 2018

UBALOZI WA TANZANIA, KOMORO WAADHIMISHA MIAKA19 YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

Balozi wa Tanzania Visiwani Komoro Mhe. Sylvester M. Mabumba akihutubia kwenye Kongamano la Mwalimu Nyerere, ambapo Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Diaspora ya Watanzania Visiwani Komoro (TADICO) pamoja na taasisi ya kijamii ya Komoro ijulikanayo kama Udjamaa wa Komori na Afrika Mashariki uliandaa Kongomano hilo la siku mbili kuanzia tarehe 26 – 27 Oktoba, 2018 kama sehemu ya kumenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Watanzania waishio Visiwani Komoro wakimsikilisha Mhe. Mabumba hayupo pichani.


Watanzania waishio Visiwani Komoro wakiwa kayika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa Kongamano hilo



UBALOZI WA TANZANIA, KOMORO WAADHIMISHA MIAKA19 YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
TAREHE 26 – 27 Octoba, 2018

Katika harakati za kuendeleza kukuza na kuhuisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Ubalozi wa Tanzania Visiwani Komoro kwa kushirikiana na Diaspora ya Watanzania Visiwani Komoro (TADICO) pamoja na taasisi ya kijamii ya Komoro ijulikanayo kama Udjamaa wa Komori na Afrika Mashariki uliandaa Kongomano la siku mbili kuanzia tarehe 26 – 27 Oktoba, 2018 kama sehemu ya kumenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kongomano hilo lilifanyika katika ukumbi wa Bunge la Taifa la Komoro ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu wa Komoro, Mhe. Salime Mohamed Abderemane. Aidha, kutoka Tanzania, Mhe. Pro. Mark Mwandosya alialikiwa kama mmoja ya watoa mada juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere.
Wageni wengine mashuhuri walioshiriki katika Kongomano hilo ni pamoja na Mhe. Mohamed Msaidie, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Komoro, Mhe. Balozi Ahmed Thabeet, mmoja ya waazilishi wa Chama cha Ukombozi cha Komoro kujilikanacho kama MOLINACO. Aidha, Balozi wa Tanzania Visiwani Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba naye pia aliweza kushiriki kikamilifu katika Kongomano hilo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ubalozi wa Tanzania Visiwani Komoro kusheherekea kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Visiwani hapa. Lengo la Kongomano hilo ilikuwa ni kuelezea mchango wa Mwalimu Nyerere na Tanzania kwa ujumla katika harakati za ukombozi wa Visiwa vya Komoro kuanzia 1962 – 1975. Aidha, Kongomano hilo lililenga pia kuikurubisha Komoro katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kuwa mda mrefu Visiwa hiyo vimeelekeza mahusiano yake katika nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati.
Watoa mada mbalimbali waliweza kuelezea kwa kina mchango wa Mwalimu Nyerere katika harakati za ukombozi wa Visiwa vya Komoro na Afrika kwa ujumla. Prof. Mwandosya kwa upande wake alielezea mchango wa Mwalimu katika harakati zake za kudumisha umoja na kuwasihi wa Komoro kudumisha umoja wao hasa katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inapitia mageuzi makubwa ya kisiasa.
 Kongomano la kumuenzi Mwalimu Nyerere lilifana sana na imekuwa ni chachu kwa Wakomoro kuona umuhimu wa kudumisha mahusiano ya (Kusini-Kusini), South-South Cooperation. Ubalozi umedhimiria kuendeleza Kongomano la Mwalimu kwani imeonekana yanachangia sana kudumisha mahusiano mazuri yaliopo baina ya Tanzania na Komoro.

Friday, October 26, 2018

Dkt. Ndumbaro awa Mgeni Rasmi maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Ubelgiji

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt. Ndumbaro awa Mgeni Rasmi maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Ubelgiji

 Kampuni 32 kutoka Ubelgiji zilizowekeza Tanzania ni chache ukilinganisha na uwingi wa fursa za uwekezaji zilizopo nchini ambazo kwa kiasi kikubwa bado hazijatumika kikamilifu.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Mfalme wa Ubelgiji iliyofanyika kwenye makazi ya Balozi jijini Dar Es Salaam tarehe 26 Oktoba 2018.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile; kilimo, ujenzi wa miundombinu, nishati, madini, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, viwanda vya uzalishaji, mafuta na gesi ambazo hazijatumika ipasavyo. Hivyo, Ubelgiji na Tanzania zikijizatiti zinaweza zikafanya biashara na kufanya uwekezaji mkubwa na wenye manufaa kwa pande zote mbili), Dkt. Ndumbaro alisema.

Alielezea matumaini yake kuwa ujio wa Makampuni makubwa ya Ubelgiji zaidi ya 40 ambayo yamekuwa na mazungumzo yenye tija na Makampuni ya Tanzania na sekta nyingine zinazohusika na uwekezaji kwa siku tatu zilizopita, utaleta ongezeko la uwekezaji na kuimarika kwa kiwango cha biashara kati ya Ubelgiji na Tanzania.

Kwa upande wa biashara kati ya Tanzania na Ubelgiji, Mhe. Naibu Waziri ameridhishwa na urari wa biashara uliopo, ingawa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, biashara kati ya Ubelgiji na Tanzania imefikia kiwango cha Dola milioni 332 huku Tanzania ikiuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 208 nchini Ubelgiji.

Dkt. Ndumbaro alihitimisha hotuba yake kwa kuishukuru Ubelgiji kwa kuendelea kuwa mshirika mkubwa wa jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Alitoa mfano wa programu mbalimbali za maendeleo nchini zinazogharamiwa na Serikali ya Ubelgiji kwa kiasi cha Euro milioni 20.

Programu hizo zinajumuisha upatikanaji wa maji safi vijijini na uendelezaji endelevu wa sekta ya kilimo katika mkoa wa Kigoma. Utekelezaji wa miradi hiyo imesaidia kuboresha usimamizi mzuri wa vyanzo vya maji, usimamizi wa rasilimali na mnyoro wa thamani katika kilimo, hususan kwa wakulima wadogo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter van Acker alisema kuwa Ubelgiji itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano za kubadalisha maisha ya watu masiikini. Alisema jitihada hizo pamoja na mambo mengine, zitaeendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania za kuleta utulivu wa kisiasa katika eneo la maziwa makuu ikiwemo usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
27 Oktoba 2018

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damasi Ndumbaro (Mb.) akihutubia kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya Mfalme wa Ubelgiji yaliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Ubelgiji jijini Dar Es Salaam jana. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya.  
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter van Acker akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Mfalme wa Ubelgiji yaliyofanyika katika makazi yake jana.  
Wageni waalikwa wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikitolewa  
Dkt. Ndumbaro akiendelea kuhutubia. 
Dkt. Ndumbaro akigonganisha glasi na Balozi Peter van Acker kwa kuwatakia afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Magufuli na Mfalme Philippe Leopold Louis Marie wa Ubelgiji.  
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb.) wa kwanza kulia akizungumza na Meneja wa mauzo wa Kimataifa wa kampuni ya Cardolite kutoka Ubelgiji Bw. Hans Carleer pamoja na Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Kamal (wa kwanza kushoto).

Balozi Dkt. Slaa awasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Rais wa Finland

Balozi wa Tanzania kwenye Nchi za Nordic, na Baltic Mhe. Wilbrod Slaa awasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Rais wa Finland, Mheshimiwa Sauli Niinistö  jijini Helsinki
Balozi Dkt. Slaa akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Sauli Niinistö.


Thursday, October 25, 2018

Ubelgiji yaambiwa iongoze uwekezaji nchini, Mhandisi Manyanya


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ubelgiji yaambiwa iongeze uwekezaji nchini, Mhandisi Manyanya

Ubelgiji imetakiwa kuongeza kiwango cha uwekezaji nchini ili kuchochea zaidi kasi ya azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb) alipokuwa anatoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Ubelgiji na Tanzania linalofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar Es Salaam.

“Kuna miradi 32 yenye thamanai ya Euro milioni 902 ambayo imeajiri wafanyakazi 1814 inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Ubelgiji nchini Tanzania. Hivyo, kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji huo kwa kuwa mazingira ya uwekezaji nchini ni mazuri na yanavutia”, Mhandisi Manyanya alisema.

Mhe. Naibu Waziri aliwahamiza wawekezaji hao ambao ni wafanyabiashara wakubwa nchini Ubelgiji kuwekeza katika sekta za kilimo, hususan kwenye maeneo ya viwanda vya nguo, sukari, mafuta ya kupikia, maziwa, ngozi, nyama, mbegu, matunda na maua,

Sekta nyingine aliyoitaja ni ya nishati hasa katika miundombinu ya kuzalisha na kusambaza gesi asilia na nishati jadilifu.
Maeneo mengine yaliyosisitizwa na Mhe. Naibu Waziri ni pamoja na sekta ya utalii, madini, uvuvi katika bahari kuu, miundombinu, maeneo maalum ya viwanda (industrial parks) na ujenzi wa majengo hususan katika mji mkuu wa Dodoma ambapo mahitaji ni makubwa.

 Uzalishaji wa dawa za binadamu na wanyama, vifaa tiba na uzalishaji wa samani za kisasa ni maeneo ambayo Mhe. Naibu Waziri aliwasihi wawekezaji hao kuyapa jicho la pekee.

Mhe Manyanya alisema wawekezaji watakaoamua kuwekeza nchini hawatajutia uamuzi wao kwa kuwa Tanzania kuna mazingira mazuri. Mazingira hayo ni pamoja na amani na usalama, rasilimali za kutosha na uhakika wa soko kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na hatua zinakamilishwa kuwa na eneo huru la biashara barani Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. John Mathew Mnali aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa TIC itatoa msaada unaohitajika kupitia kituo chake cha kutoa huduma kwa pamoja (One Stop Centre) kwa mfanyabiashara yeyote mwenye dhamira ya kuwekeza nchini. Alitaja msaada wanaotoa kupitia kituo hicho ni pamoja na msaada wa kupata vibali vya kazi na makazi, kupata ardhi ya kuwekeza, miongozo ya kodi ikiwemo kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipa Kodi (TIN), kuthibitisha bidhaa kutoka Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Dawa na masuala ya kupata vibali vya mazingira (environment clearance).

Bw. Mnali alibainisha kuwa kuna bandari kubwa tatu nchini zinaunganisha nchi jirani ambazo hazina bandari. Aidha, Tanzania inaongoza kikanda kupokea miradi ya moja kwa moja ya uwekezaji kutoka nje (FDI) na pia ni miogoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani. Alisema sababu hizo ni vigezo tosha vya kuichagua Tanzania kuwa kimbilio la uwekezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Wafanyabiashara la Umoja wa Ulaya nchini, Bi. Marie Strain alisema kuwa nchi za umoja huo zinashika nafasi ya pili kwa kufanya biashara na Tanzania. Hivyo kundi hilo linatoa huduma mbalimbali kwa Wafanyabiashara zikiwemo za ushauri, taarifa za masoko na maeneo ya uwekezaji pamoja na kufanya majadiliano na Serikali namna ya kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.

Katika mahojiano na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga alisema kuwa ujio wa wawekezaji hao unatokana na juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji za kuvutia wawekezaji. Alisema Ubalozi umefanya hivyo, huku ukitambua kuwa takwimu zinaonesha kuwa Ubelgiji ni moja ya nchi kumi duniani zinazoongoza kwa kufanya uwekezaji nje ya nchi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
25 Oktoba 2018

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye kongamano la biashara kati ya Tanzania na Ubelgiji. kongamano hilo lilifanyika katika Hoteli ya Serena jini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bw. John Mathew Mnali akiongea katika kongamano hilo.
Wafanyabiashara kutoka Ubelgiji na Tanzania na wageni waalikwa wakimsikiliza Naibu Waziri wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano la biashara katika Hoteli ya Serena

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga (kulia) pamoja na wafanyabiashara kutoka Ubelgiji wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri Manyanya
Wafanyabiashara katika kongamno
Wafanyabiashara na wajumbe wengine wakiendelea kumsikiliza Naibu Waziri.
Wafanyabiashara wa Tanzania na Ubelgiji wakiwa katika majadiliano ya ana kwa ana.

Majadiliano ya ana kwa ana kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Ubelgiji

Majadiliano yanayoonesha dalili ya kuzaa matunda ya ushirikiano kati ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Ubelgiji

Majadiliano yanaendelea

Tunataka tushirikiane ili tuweze kuwekeza nchini Tanzania

mjadiliano ya ana kwa ana

Njoo uwekeze Tanzania mazingira ni mazuri.