Friday, October 26, 2018

Dkt. Ndumbaro awa Mgeni Rasmi maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Ubelgiji

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt. Ndumbaro awa Mgeni Rasmi maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Ubelgiji

 Kampuni 32 kutoka Ubelgiji zilizowekeza Tanzania ni chache ukilinganisha na uwingi wa fursa za uwekezaji zilizopo nchini ambazo kwa kiasi kikubwa bado hazijatumika kikamilifu.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Mfalme wa Ubelgiji iliyofanyika kwenye makazi ya Balozi jijini Dar Es Salaam tarehe 26 Oktoba 2018.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile; kilimo, ujenzi wa miundombinu, nishati, madini, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, viwanda vya uzalishaji, mafuta na gesi ambazo hazijatumika ipasavyo. Hivyo, Ubelgiji na Tanzania zikijizatiti zinaweza zikafanya biashara na kufanya uwekezaji mkubwa na wenye manufaa kwa pande zote mbili), Dkt. Ndumbaro alisema.

Alielezea matumaini yake kuwa ujio wa Makampuni makubwa ya Ubelgiji zaidi ya 40 ambayo yamekuwa na mazungumzo yenye tija na Makampuni ya Tanzania na sekta nyingine zinazohusika na uwekezaji kwa siku tatu zilizopita, utaleta ongezeko la uwekezaji na kuimarika kwa kiwango cha biashara kati ya Ubelgiji na Tanzania.

Kwa upande wa biashara kati ya Tanzania na Ubelgiji, Mhe. Naibu Waziri ameridhishwa na urari wa biashara uliopo, ingawa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, biashara kati ya Ubelgiji na Tanzania imefikia kiwango cha Dola milioni 332 huku Tanzania ikiuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 208 nchini Ubelgiji.

Dkt. Ndumbaro alihitimisha hotuba yake kwa kuishukuru Ubelgiji kwa kuendelea kuwa mshirika mkubwa wa jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Alitoa mfano wa programu mbalimbali za maendeleo nchini zinazogharamiwa na Serikali ya Ubelgiji kwa kiasi cha Euro milioni 20.

Programu hizo zinajumuisha upatikanaji wa maji safi vijijini na uendelezaji endelevu wa sekta ya kilimo katika mkoa wa Kigoma. Utekelezaji wa miradi hiyo imesaidia kuboresha usimamizi mzuri wa vyanzo vya maji, usimamizi wa rasilimali na mnyoro wa thamani katika kilimo, hususan kwa wakulima wadogo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter van Acker alisema kuwa Ubelgiji itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano za kubadalisha maisha ya watu masiikini. Alisema jitihada hizo pamoja na mambo mengine, zitaeendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania za kuleta utulivu wa kisiasa katika eneo la maziwa makuu ikiwemo usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
27 Oktoba 2018

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damasi Ndumbaro (Mb.) akihutubia kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya Mfalme wa Ubelgiji yaliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Ubelgiji jijini Dar Es Salaam jana. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya.  
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter van Acker akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Mfalme wa Ubelgiji yaliyofanyika katika makazi yake jana.  
Wageni waalikwa wakisikiliza kwa makini hotuba zilizokuwa zikitolewa  
Dkt. Ndumbaro akiendelea kuhutubia. 
Dkt. Ndumbaro akigonganisha glasi na Balozi Peter van Acker kwa kuwatakia afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Magufuli na Mfalme Philippe Leopold Louis Marie wa Ubelgiji.  
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb.) wa kwanza kulia akizungumza na Meneja wa mauzo wa Kimataifa wa kampuni ya Cardolite kutoka Ubelgiji Bw. Hans Carleer pamoja na Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Kamal (wa kwanza kushoto).

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.