Sunday, October 7, 2018

Dkt. Mahiga ashiriki Mkutano wa TICAD

Kufuatia  mwaliko wa Mhe. Taro Kono, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, (Tokyo International Conference for African Development-TICAD). Mkutano huo umeanza tarehe 6-7 Oktoba, 2018, Tokyo, Japan.

Mkutano huo ambao umewashirikisha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika, pamoja na masuala mengine, unajadili maazimio ya Mkutano wa Tano na wa Sita wa TICAD iliyofanyika mwaka 2013 na 2016, pamoja na kuandaa agenda za Mkutano wa Wakuu wa nchi wa TICAD VII unaotegemea kufanyika Yokohama, mwezi Agosti, 2019.
 
Masuala yaliyojadiliwa ni pamoja; Changamoto tangu kukamilika kwa TICAD VI mwaka 2016; Mageuzi ya kiuchumi na ukuaji shirikishi; Kuimarisha sekta ya Afya, Amani na Usalama katika jamii na; kuimarisha mawasiliano barani Afrika na duniani kote. Maeneo haya yanaenda sambamba na   Agenda 2030 ya Umoja wa Mataifa na Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika.
Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akisikiliza kwamakini wakati Mawaziri wengine wakichangia mada kwenye mkutano huo Tokyo, Japan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga mara baada ya kushiriki mkutano wa ngazi ya Mawaziri, alipata fursa ya kukutana na Waziri wa MAmbo ya Nje wa Japan Mhe. Taro Kono, katika mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Japani katika sekta mbalimbali. Aidha, Dkt. Mahiga aliishukuru serikali ya Japani kwa Mchango wake wa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo nchini Tanzania hususani miundombinu ya barabara.  Kwa upande wake, Mhe. Kono amesifia jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi, ushirikiano katika ngazi za kimataifa, na kuipongeza Tanzania katika kukuza na kulinda usalama barani Afrika na duniani 
Dkt. Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Mhe. Sameh Shoukry walipokutana kwenye Mkutano wa TICAD ngazi ya Mawaziri nchini Japan.
Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Bi Sadako Ogata, aliyekuwaga Mkurugenzi wa UNHCR mara baada ya kumalizika mkutano wa TICAD uliyofanyika Tokyo Japan.





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.