TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Italia
yaiahidi Afrika Ushirikiano wa kiuchumi
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika wameazimia
kukuza na kuimarisha Ushirikiano katika nyanja mbalimbali, hususan biashara na
uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya kweli barani Afrika.
Mawaziri hao walifikia azimio hilo wakati wa
mkutano wa pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika uliofanyika Farnesina,
Italia tarehe 25 Oktoba 2018 na kuhudhuriwa na Mawaziri wa zaidi ya nchi 40 akiwemo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).
Mawaziri hao walikutana kwa madhumuni ya kujadili kwa
pamoja changamoto zinazohusu usalama, uhuru, amani, demokrasia na namna wadau
wa Italia (wenye viwanda, Wafanyabiashara, wanazuoni na taasisi zisizo za
kiserikali) watakavyoweza kushiriki katika kukuza uchumi barani Afrika hasa
katika sekta ya uwekezaji na biashara.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo ambao
ulifunguliwa na Rais wa Italia, Mhe. Sergio Mattarella, Mhe Waziri Mahiga alisisitiza suala la amani
kuwa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Aidha,
alieleza umuhimu wa Jumuiya za Kikanda katika kusuluhisha migogoro mbalimbali
inayotokea kwenye Bara la Afrika. Katika hilo, alijulisha jitihada zinazofanywa
na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) katika kusuluhisha mgogoro nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo.
Sanjari na mkutano huo, Waziri Mahiga alipata fursa
ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe
Enzo Moavero na Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo
(IFAD), Bw. Gilbert F. Houngbo.
Kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Italia, Viongozi hao walikubaliana kuwa, kuandaliwe Hati ya Makubaliano (MoU) kati
ya Tanzania na Italia ya kufanya majadiliano ya mara kwa mara yenye lengo ya
kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii,
elimu na utamaduni.
Kuhusu mazungumzo na Rais wa IFAD, wawili hao
walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Mfuko huo kwenye maeneo
makuu mannne ambayo ni Huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kuwajengea uwezeo
vijana ili waweze kufanya kilimo kama sehemu ya ajira, kuboresha sekta ya
mifugo pamoja na masuala ya lishe bora.
Aidha, Rais wa IFAD alimuahidi Mhe Waziri kuwa
mfuko huo utaendelea kushirikiana vizuri na serikali ya Tanzania hata kwenye
miradi inayoendelea ikiwemo Programu ya Miundombinu ya masoko, uongezaji wa
thamani na kuwawezesha wakulima wadogo wa vijijini kifedha (Marketing
Infrastructure, Value Addition and Rural Finance-MIVRAF). Madhumuni ya programu
hiyo ni kupunguza umasikini na kuharakisha ukuaji wa uchumi vijijini ili kuboresha
kipato na usalama wa chakula kwa jamii ya watu wa vijijini.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
29 Oktoba 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.