Tuesday, October 9, 2018

Tanzania kushiriki mazoezi ya kikosi cha dharura cha SADC nchini Malawi


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimejipanga kuzuia na kudhibiti madhara yanayosababishwa na machafuko ya kisiasa katika jumuiya hiyo na Bara la Afrika kwa ujumla. Wawakilishi wa nchi hizo wamekusanyika nchini Malawi kuanzia tarehe 1 Oktoba hadi 17 Oktoba 2018 kwa ajili ya kufanya mazoezi ya namna ya kutuliza ghasia pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika katika kipindi cha machafuko

Wawakilishi wa Tanzania kutoka Jeshi la Wananchi, Magereza na taasisi za kiraia ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni miongoni mwa watu 600 wanaoshiriki zoezi hilo lililopewa jina la EX UMODZI CPX 2018 na kaulimbiu ya Afrika ni Amani na Maendeleo (Africa for peace and prosperity).

Katika hafla ya ufunguzi wa mazoezi hayo iliyofanyika leo tarehe 08 Oktoba, 2018 katika Chuo cha Kijeshi cha Malawi kilichopo mji wa Salima takriban kilomita 120 kutoka Lilongwe, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Malawi, Mhe. Evaton Chemulirenji alisema mazoezi hayo ni utekelezaji wa maazimio ya SADC na Umoja wa Afrika (AU) wa kuandaa kikosi cha kukabiliana na machafuko barani Afrika (Standby Force-SF) ambacho kinatakiwa kiwe kimekamilika ifikapo Januari 2019.

Alisema madhumuni ya mazoezi hayo ni kuhakikisha kuwa kikosi cha SF kinapewa mafunzo ya vitendo ya kutosha ili kiwe na ujuzi na mbinu za kushiriki operesheni za kulinda amani na/au kuingilia kati na kuzuia machafuko (peace keeping and enforcement) pale yanapotokea barani Afrika. Aidha, alisema mazoezi hayo ni muhimu kwa kuwa yatasaidia kuimarisha ushirikiano na kuaminiana baina ya nchi wanachama wa SADC.

Mazoezi hayo yanajumuisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na majeshi  ya ulinzi,  askari polisi, askari magereza na raia wa fani tofauti kama vile za Utawala wa Sheria, siasa, mawasiliano, Utawala, haki za binadamu na jinsia ambao wana mchango mkubwa katila masuala ya operesheni za kulinda amani.

Wanajeshi watafanya zoezi la namna ya kutuliza machafuko na raia watajifunza namna ya kusaidia jamii punde tu machafuko yanapodhibitiwa na vikosi vya usalama.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Salima, Malawi

08 Oktoba 2018

Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Evaton Chimulirenji akitoa hotuba wakati wa hafla ya ufunguzi  rasmi wa mafunzo na mazoezi ya namna ya kutuliza ghasia pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika katika kipindi cha machafuko iliyofanyika tarehe 08 Oktoba, 2018 katika Chuo cha Kijeshi cha Malawi kilichopo katika mji wa Salima nje kidogo ya jiji la Lilongwe.Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya SADC yanajumuisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na majeshi  ya ulinzi,  askari polisi, askari magereza na raia wa fani tofauti kama vile za Utawala wa Sheria, siasa, mawasiliano, Utawala, haki za binadamu na jinsia ambao wana mchango mkubwa katila masuala ya operesheni za kulinda amani.

Mratibu wa Program ya Mafunzo yanayofanyika nchini Malawi akieleza mpangilio wa program ya mafunzo hayo kwa ujumla

Mratibu Mkuu wa Mafunzo hayo Meja Jenerali A.B Mhone naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Malawi  Mhe. Evaton Chimulirenji (kushoto) akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Malawi Generali Supini Phiri (kulia) pamoja na Mkuu wa Misheni ya mafunzo hayo, Mhe. Bi. Eunice Lumbia



Sehemu ya viongozi wa kijeshi wakifuatilia hotuba zilizokuwa zinatolewa wakati wa ufunguzi huo
Kikosi cha Tanzania kinachoshiriki mafunzo hayo kikiwa kimetulia wakati wa gwaride rasmi la ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo. Kikosi hicho kinajumuisha wanajeshi, askari magereza na raia kutoka fani mbalimbali za utawala, siasa na mawasiliano

Kikosi cha Malawi ambao ni wenyeji wa mafunzo hayo kikiwa kimetulia wakati wa gwaride la ufunguzi rasmi wa mafunzo
Kikosi cha Tanzania kikiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Zakarriya Kera (kushoto) ambaye pia ni kiongozi wa washiriki kutoka kundi la Raia kwenye mafunzo hayo akiwa katika picha na baadhi ya washiriki ambao ni wanajeshi na raia kutoka Tanzania.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.