Thursday, November 21, 2019

MKUTANO WA 39 BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC WAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeanza leo jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Februari, 2020.

Mkutano huo wa siku saba umeanza leo kwa ngazi ya maofisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu kisha kuhitimishwa na Mawaziri wa Wizara za Kisekta zinazohusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 27, 2019.

Ajenda za mkutano huo zinakadiriwa kuwa tisa ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda nyingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuishia mwezi Juni 2019.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini. 



Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi
Baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri ulioanza leo jijini Arusha kwa ngazi ya maofisa waandamizi

Wednesday, November 20, 2019

INDONESIA KUWEKEZA TANZANIA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Indonesia kuwekeza Tanzania
Dodoma, 20 Novemba 2019

Mkutano wa Jukwaa la Viwanda kati ya Tanzania na Indonesia utafanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro jijini Dar Es Salaam tarehe 21 Novemba 2019. Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo ambapo kampuni kubwa 21 za Indonesia zinazojihusisha katika masuala ya ujenzi wa miundombinu na usafirishaji; kilimo; usindikaji vyakula; utengenezaji wa nguo, vifaa tiba na madawa ya binadamu; na uchimbaji wa madini na taasisi zinazosimamia masuala ya uwekezaji Tanzania (TIC, TPSF, CTI, TCCIA) zitashiriki katika mkutano huo.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wadau mbalimbali wa Tanzania na Indonesia kubadilishana mawazo, uzoefu na ujuzi pamoja na kuweka mikakati ya kushirikiana katika sekta ya viwanda kwa faida ya pande zote mbili.  
Kutoka na nchi ya Indonesia kuwa ni kubwa kiuchumi Kusini-Mashariki mwa Asia na ipo nafasi ya 16 katika kundi la nchi 20 tajiri zaidi duniani (G20), na uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji nchini, ni dhahiri kuwa kongamano hilo litakuwa na matokeo mazuri katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.            

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 


Tuesday, November 19, 2019

UTURIKI KUWEKEZA UJENZI WA VIWANDA VYENYE THAMANI YA DOLA MILIONI 50 SIMIYU

. Kawasaki kutoka Japan nayo yaonesha nia ya kuanzisha kiwanda kitakachohudumia soko la Afrika na Nje ya Afrika

Katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi, Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki umeambatana na wawekezaji kutoka nchini humo kwa ajili ya kuwekeza katika viwanda mkoani Simiyu ambavyo vinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 2000.

Uwekezaji huo utajumuisha kiwanda cha nguo pamoja na kiwanda cha kutengeneza vyombo vya majumbani ambao una thamani ya dola za kimarekani milioni 50. Viwanda hivyo vitajengwa katika eneo la Isanga Mjini Bariadi Mkoani Simiyu na vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2020.

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo ambalo linatarajiwa kujengwa viwanda hivyo mkoani Simiyu, mwekezaji huyo kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram ameahidi kujenga viwanda viwili kimojawapo kikiwa ni cha nguo na kingine cha kutengeneza vyombo vya nyumbani ikiwemo vikombe, sahani na glasi.

Bw. Albayram amesema ameridhishwa na mazingira ya uwekezaji baada ya kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kuangalia mazingira wezeshi kwa uwekezaji wa viwanda, akiwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo mkoani Simiyu.

Aidha ameitaka serikali kutatua baadhi ya changamoto ili kuuwezesha uwekezaji huo kufanyika ikiwa ni pamoja na miundombinu yote muhimu hususani ya umeme ili uwekezaji huo uanze mara moja baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu zinazohitajika ikiwa ni pamoja na usajili wa kampuni na kutafuta hati miliki ya ardhi.

“Tumeamua kuwekeza Simiyu, kila kitu kikienda sawa kiwanda cha nguo kinaweza kujengwa na kufanya kazi ndani ya miezi tisa mpaka mwaka mmoja, kiwanda cha vyombo vya nyumbani miezi nane baada ya usajili wa kampuni nitarudi tena Simiyu kukamilisha masuala ya hati miliki ya ardhi, sitaki kumuangusha Mhe. Balozi maana amefanya mengi kwa ajili yetu,” alisema Albayram.

Nae Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo amesema mwekezaji ameridhishwa na eneo hilo na kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kutoa ardhi ya kujenga viwanda hivyo huku akibainisha kuwa ombi kubwa la mwekezaji ni upatikanaji wa nishati ya kutosha kwa kuwa viwanda hivyo hutumia umeme mwingi.

Balozi Kiondo ameongeza kuwa, hayo ni matokeo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa vitendo, hivyo Ubalozi utaedelea kuhamasisha wawekezaji wengine zaidi kuja kuweza nchini, hatimaye kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alimhakikishia mwekezaji huyo upatikanaji wa mahitaji yote muhimu na kuahidi kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika kuhakikisha anapata huduma zote kwa wakati na pasipo urasimu wowote.

Kuhusu suala la Umeme Mtaka amesema katika Bajeti ya mwaka 2019/20 Wizara ya Nishati kupitia Shirika la umeme TANESCO imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme (substation) ambacho kitajengwa karibu na eneo la uwekezaji huo.

Mtaka ameongeza kuwa mtazamo wa mkoa wa Simiyu ni kuwa na viwanda vichache vitakavyoajiri maelfu ya watanzania badala ya kuwa na viwanda vingi vinavyoajiri watu wachache ili kuwezesha watanzania wengi kupata ajira.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa wakulima wa pamba kulima pamba kwa wingi kwa kuwa kiwanda cha nguo kitakuwa mkombozi wa kuongeza thamani ya zao la pamba na itauzwa kwa bei ya uhakika.

Naye Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema kujengwa kwa kiwanda cha nguo mkoani Simiyu kutasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika kuondoa changamoto ya bei ya pamba kwa kuwa kitapanua wigo wa soko la pamba, ambapo pamba inayotumika ni chini ya asilimia 20 - 25 ya pamba yote inayozalishwa nchini.

Katika tukio jingine kampuni ya Kawasaki Heavy Industries Ltd kutoka Japan imeonesha nia ya kuanzisha kiwanda nchini ambapo kiwanda hicho kitahudumia soko la Afrika na Nje ya Afrika.

Kawasaki Heavy Industries Ltd ni kampuni nchini Japan ambapo imewekeza katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya usafiri (anga, reli na majini)  nishati (cogeneration, energy plants, gas tuibines, gas engines), vifaa vya viwandani (hydraulic components and systems, robotics, industrial plants, environmental and recycling), pamoja na leisure (motorcycle, off-road four wheel,JET SKI).

Naibu Meneja wa Idara ya Mkakati wa Kimataifa, Kitengo cha Biashara cha Kampuni ya Kawasaki Bw. Michio Kambe anatarajia kufanya ziara nchini Tanzania kuanzia tarehe 21 hadi 26 Novemba 2019 ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akioneshwa pamba inavyochambuliwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) wakati walipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (katika) akiwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) pamoja na maafisa wa serikali pamoja na baadhi ya wafanyakazi wakitembea ndani ya kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka (katika) akiwa na mwekezaji kutoka Uturuki, Bw. Mustafa Albayram (mwenye shati jeusi) na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo (mwenye gauni la kijivu) wakati walipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery Ltd mkoani Simiyu. Wengine ni maafisa wa serikali pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.



USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA SHIRIKA LA AALCO KUENDELEA KUIMARIKA

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza wakati hafla ya Maadhimisho ya Miaka 63 ya kuanzishwa kwa  Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO) yaliyofanyika jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda [kushoto] akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Shirika la Mashauriano ya Masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika [AALCO], Prof. Kennedy Gastron wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019
Mhe. Balozi Luvanda akiwa  katika meza moja na viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya miaka 63 tangu kuanzishwa kwa Shiriko la AALCO
Wageni waalikwa wakiwa kwenye maadhimisho
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi pamoja na Maafisa Ubalozi  wa nchi wanachama wa AALCO  walioshiriki hafla ya  maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019.
=======================================================

Ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Mashauriano ya masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (AALCO) kuendelea kuimarika

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Baraka Luvanda amemwakilisha Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria na Rais wa sasa wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (Asia-Africa Legal Consultative Organization-AALCO) kwenye sherehe ya miaka 63 ya kuanzishwa kwake. Sherehe hiyo imefanyika Jijini New Delhi tarehe 15 Novemba 2019 na kuhudhuriwa na nchi wanachama wageni waalikwa, wenyeji na mashirika ya kimataifa yaliyopo New Delhi.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Mahiga, Balozi Luvanda alielezea uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na AALCO na kueleza kuwa utaendelea kudumishwa kwa manufaa ya pamoja.

AALCO ilianzishwa tarehe 15 Novemba 1956 kwa lengo la kuwa chombo cha ushauri na ushirikiano katika masuala ya sheria za kimataifa kwa nchi za Asia na Afrika. Toka kuanzishwa kwake AALCO imewezesha nchi wanachama kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya sheria za kimataifa na imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sheria za kimataifa.

Ushirikiano kati ya Tanzania na shirika hilo ulianza tangu mwaka 1965 ambapo Tanzania ilishiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AALCO kama nchi Mwangalizi na baadaye mnamo mwaka 1973 kama nchi mwanachama rasmi. 

Mpaka sasa Tanzania imeshaandaa Mikutano mikubwa 3 ya Mwaka ambapo Mkutano wa 25 wa AALCO ulifanyika mwaka 1986 jijini Arusha, Mkutano wa 49 ulifanyika Jijini Dar es Salaam mwaka 2010 na Mkutano wa 58 ulifanyika hivi karibuni, jijini Dar es Salaam tarehe 21 hadi 25 Octoba 2019.

Monday, November 18, 2019

TANZANIA YAKABIDHI SHEHENA YA KWANZA YA MBEGU ZA KOROSHO NCHINI ZAMBIA


Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia akihutubia adhira iliyojitokeza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mbegu za korosho jimbo la Mongu, Zambia  tarehe 16 Novemba, 2019
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi 
shehena ya mbegu za korosho kwa Serikali ya Jamhuri ya 
Zambia katika hafla iliyofanyika mjini Mongu nchini humo. 

Korosho hizo zimekabidhiwa kufuatia ahadi ya Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe 
Magufuli aliyoitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. 
Edgar Lungu kwenye uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha 
Huduma Mpakani (OSBP) Tunduma tarehe 5 Oktoba, 2019.

Katika tukio hilo Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Mhe. 
Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia, na

 kwa upande wa Zambia, Serikali aliwakilishwa na Waziri wa 

Jimbo la Mongu Mhe. Richard Kapita, Watendaji kutoka 

Serikalini na viongozi wa Kimila.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Kapita kwa naiba ya
 Serikali ya Jamhuri ya Zambia ametoa shukurani za pekee
 kwa Mhe. Rais Magufuli kwa  upendo aliouonesha
 kwa Zambia na kwa upekee kabisa kwa wananchi wa jimbo
 la Mongu.
 Aliongezea kusema wananchi wa Mongu 
wanamatumaini makubwa kuwa, mbegu hizo zitawapa 
chachu ya kuzalisha korosho kwa wingi na kunufaika 
kiuchumi kama ambavyo imekuwa kwa wananchi wa
 Tanzania
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia (kushoto) na Waziri wa Jimbo la Mongu Mhe. Richard Kapita (kulia) wakijadili jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa hafla ya kukabidhi na kupokea korosho iliyofanyika Mongu, Zambia 
Waziri wa Jimbo la Mongu, Zambia  Mhe. Richard Kapita 

akihutubia hadhira iliyojitokeza kwenye hafla ya 

mapokezi ya mbegu za korosho
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia, na Mhe. Mukela Manyindo Waziri Mkuu wa Jimbo la Mongu (katika ngazi ya kimila) wakikata utepe kuashiria mapokezi ya mbegu za korosho katika hafla iliyofanyika Mongu, Zambia 
Picha ya pamoja baada ya hafla ya kukabidhi mbegu za korosho
Mhe. Hassan Simba Yahaya Balozi wa Tanzania nchini Zambia (kushoto) na Afisa kutoka Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia wakifuatilia tukio lililokuwa likiendelea wakati wa hafla ya kukabidhi mbegu za korosho
Shemu ya wananchi wa Mongu, Zambia waliojitokeza kwenye hafla ya mapokezi ya mbegu za korosho 



Saturday, November 16, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE, PROF. PALAMAGAMBA KABUDI AKUTANA NA WATUMISHI WA WIZARA JIJINI DODOMA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) leo tarehe 16 Novemba 2019 amezungumza na Watumishi wa Wizara hiyo kwenye Mkutano uliofanyika jijini Dodoma. Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi amewapongeza Watumishi hao kwa kufanikisha majukumu makubwa ya kitaifa ikiwemo Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uiofanyika nchini mwezi Agosti 2019 pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika nchini mwezi Novemba 2019. Pia aliwaasa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujenga Umoja na mshikamano pamoja na kuwa na nidhamu na kutokata tamaa katika kutekeleza majukumu yao.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) nae akiungumza wakati wa Mkutano kati ya Mhe. Waziri na Watumishi wa Wizara.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akizungumza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri na Watumishi wa Wizara.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akichangia hoja wakati wa mkutano kati ya Waziri na Watumishi wa Wizara

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Issa Ng'imba akitoa neno kwa Watumishi wakati wa mkutano kati yao na Mhe. Waziri

Sehemu ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwasikiliza viongozi wa Wizara wakati wa Mkutano kati ya Waziri na Watumishi

Sehemu nyingine ya Wakurugenzi

Wakurugenzi wakifuatilia hotuba

Watumishi wa Wizara wakinukuu mazungumzo kati yao na Mhe. Waziri

Mkutano ukiendelea

Wakurugenzi wengine wakifuatilia mkutano

Watumishi wa Wizara wakiwa kwenye mkutano kati yao na Mhe. Waziri

Sehemu nyingine ya Watumishi wa Wizara kwenye mkutano

Pichani ni Watumishi wa Wizara wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mhe. Waziri (hayupo pichani) alipozungumza nao

Sehemu nyingine ya Watumishi

Balozi Mteule, Bw. Jestus Nyamanga akiwa amesimama ili kupokea pongezi kutoka kwa Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani) kwa niaba ya Watumishi wa Wizara kufuatia kuteuliwa kwake kwenye wadhifa wa Balozi hivi karibuni

Mtumishi mpya wa Wizara akijitambulisha

Mhe. Waziri Kabudi na meza kuu wakiwaongoza Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) kuimba wimbo wa ….Tuna imani na Mhe. Rais

Watumishi wa Wizara wakiimba wimbo huo kwa furaha


Friday, November 15, 2019

TAKUKURU yakabidhiwa jalada la kufanyia uchunguzi upotevu wa fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia


Na Mwandishi wetu,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeikabidhi TAKUKURU  jalada la kulifanyia uchunguzi upotevu wa fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe amekabidhi jalada hilo kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo katika ofisi ndogo za Wizara jijiji Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja kutokana na jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kupambana na kuzuia rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za uma.

Uchunguzi huo unafanyika baada ya kubainika upotevu/matumizi mabaya ya fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.

Kuhusu kiwango cha fedha kilichopotea Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe, amesema kitajulikana mara baada ya Takukuru kukamilisha uchunguzi huo wa jalada walililokabidhiwa.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dkt. Faraji Mnyepe akimkabidhi Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo jalada la upotevu wa fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia leo jijini Dar es Salaam

Wednesday, November 13, 2019

DOUBLE TROIKA YA SADC YAKUTANA KUJADILI HALI YA AMANI NA USALAMA DRC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akifungua mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje pamoja na Mawaziri wa Ulinzi na vyombo vya ulinzi na usalama (double Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto wake ni Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax na anayefuatia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe.

Baadhi ya wajumbe wa Double Troika wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika mkutano Jijini Dar es Salaam



Baadhi ya wajumbe wa Double Troika wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika mkutano Jijini Dar es Salaam



Mawaziri wa mambo ya Nje, Mawaziri wa Ulinzi wa SADC wakutana kujadili hali ya Usalama na Amani DRC 

Mawaziri wa Mambo ya nchi za Nje pamoja na Mawaziri wa Ulinzi na vyombo vya ulinzi  vya Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) ijulikanao kama DOUBLE TROIKA wamekutana kwa dharura kujadili hali ya kisasa na amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha amani katika nchi hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa dharura wa DOUBLE TROIKA inayojumuisha Troika ya siasa na Troika ya Ulinzi na Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa lengo la mkutano huo wa dharura ni kuweka mikakati itakayosaidia kuimarisha amani nchini Congo DRC na kumaliza migogoro inayotishia ustawi wa nchi hiyo iliyodumu kwa miongo mingi.


Aidha, Waziri Kabudi amebainisha kuwa mkutano huo utasaidia nchi za SADC zenye vikosi vya ulinzi na usalama nchini DRC yaani Tanzania, malawai na Afrika Kusini kuimarisha amani na DRC kwa kufanya tathmini na kukubaliana hatua za kuchukua ili vita na migogoro ya mara kwa mara inayoibuka Nchini Congo DRC ifikie tamati na amani ya kudumu ipatikane.

“Mkutano huu wa leo ni wa Troika ya Siasa na Troika ya ulinzi na usalama ambapo kupitia mkutano huu tunaamini kuwa tutafanya tathimini ya hali ya amani DRC na kukubaliana ni hatua gani za kuchukua,” amesema Prof. Kabudi

Katika hatua nyingine Prof. kabudi ameongeza kuwa ndani ya mwaka huu amani na demokrasia vimezidi kuimarika katika nchi wanachama wa SADC, kutokana na baadhi ya nchi wanachama kuendesha chaguzi za kidemokrasia zilizomalizika kwa amani katika nchi za Msumbiji na Botswana. 

Aidha Prof. Kabudi amesema Tanzania na Nchi 16 wanachama wa SADC bado zinaendelea kupaza sauti kwa jumuiya za kimataifa na nchi ambazo zimeiwekea vikwazo Zimbabwe kuviondoa mara moja kutokana na vikwazo hivyo kutokuwa na uhalali jambo linalosababisha mateso kwa raia wan chi hiyo hususani akina mama na watoto .

"Katika hili la Zimbabwe lazima sisi kama SADC tushikamane na kusafiri pamoja ili tufike kwa umoja wetu" Amesema Prof. kabudi.

Awali akitoa hutuba katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC), Stergomena Tax amesema kuwa ana matumaini makubwa na mkutano huo unaofanyika jijini Dar es salaam utatathimini na kutoa mapendekezo ya muda mfupi na mrefu kuhusu hali ya usalama, amani na siasa katika nchi ya Congo DRC  na ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ili kuhakikisha ukanda huo unakuwa salama na amani

Ameongeza kuwa amani na usalama ni nyenzo mojawapo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na hivyo kupata maendeleo yanayohitajika kwa ajili ya mataifa ya Afrika.