Wednesday, September 15, 2021

TPFS YARIDHISHWA NA JUHUDI ZA SERIKALI ZA KUKUZA SEKTA BINAFSI

 Na Mwandishi wetu, Dar

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imekiri uwepo wa ongezeko la biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ushoroba wa kusini zikiwemo nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula amesema kuwa ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zikiwemo Kenya, Burundi na Uganda umeongezeka na kwamba ushirikiano kati ya Tanzania na Mataifa hayo umezidi kuimarika ukiashiria kukua kwa diplomasia ya uchumi.

“Sasa hivi ukiangali ukuaji wa biashara chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, Serikali inaishirikisha ipasavyo Sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini,” amesema Bi. Ngalua

Ameongeza kuwa ushirikiano ambao Serikali imekuwa ikiutoa kwa sekta binafsi umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na ushoroba wa kusini ikihusisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Bi. Ngalula amepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuamua kuambatana na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika Taasisi ya Sekta Binafsi kwa kuwa hatua hiyo imesaidia kuwakutanisha na kuwaunganisha na wenzao wa Mataifa mengine tofauti na nyakati zilizopita ambapo kila mfanyabiashara alijitafutia fursa peke yake.

Kwa uapnde wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameihakikishia Taasisi ya Sekta Binafsi ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini kwa kuwa Serikali inaamini uwepo wa sekta binafsi imara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi imara wa Nchi.

Balozi Mulamula ameitaka TPSF kuhakikisha kuwa inakuwa na kanzi data ili kurahisisha azma ya Serikali ya kuiunganisha sekta hiyo na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka katika mataifa mengine ulimwenguni.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan Oswald aliyefuatana na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo ya Uchumi.

Dkt. Oswald amemuambia Balozi Mulamula kuwa Tanzania imekuwa ni Nchi ya kwanza kwa viongozi hao wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani kuifanya na hiyo imetokana na ishara ya  mabadiliko ya kidiplomasia na ushirikiano wa Maendeleo na Mataifa mengine duniani iliyooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa mazungumzo kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan na Kansela wa Ujerumani Mhe Angela Merkel ambayo yalilenga kutoa kipaumbele cha uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yamekuwa kichocheo cha Viongozi hao kufanya ziara hapa nchini.

Dkt.Stefan amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania pamoja na Nchi za Afrika kuzisaidia kuimarisha uchumi kutokana na kuathiriwa na UVIKO 19.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yaligusia masuala la ulinzi na usalama katika ukanda wa maziwa makuu na kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wa Burundi.   

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata  akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata  akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula yakiendelea 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan Oswald aliyefuatana na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ujerumani  


Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi Dkt. Stefan Oswald yakiendelea



UFARANSA KIUANZISHA SAFARI YA NDEGE KUJA ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la ndege ‘Fance Airline’ inategemea kuanzisha safari mpya ya ndege kutoka Ufaransa moja kwa moja hadi Zanzibar kuanzia 19 Oktoba 2021.

Hayo yamebainishwa na Balozi Mteule wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Nabil Hajlaouvi wakati alipokuwa anawasilisha nakala ya Hati za utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi Nabil amemhakikishia Mhe. Waziri Mulamula kuwa Airfance inaanzisha safari ya ndege ya moja kwa moja kutoka Ufaransa kuja Zanzibar –Tanzania ambapo katika uzinduzi wa safari hiyo utaongozwa na Waziri wa mambo ya Nje uwa Ufaransa tarehe 19 Oktoba 2021.

Pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amepokea nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Somalia hapa nchini mhe. Zahra Ali Hassan ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Zahra amemhakikishia Waziri Mulamula kuwa Somalia itaendelea kuhakikisha kuwa mahusiano yake na Tanzania yanazidi kuimarika.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umaja wa Ulaya hapa nchini mhe. Manfredo Fanti wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu pamoja ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Balozi Mulamula pia amekutana na kufanya mazungumzo baadhi ya Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini ambao ni Balozi wa Denmark, hapa nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjoberg

Kwa upande wake Balozi wa Denmark, hapa nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet amemhakikishia Waziri Mulamula kuwa pamoja na kuwa Denmark imesema kuwa itafunga ubalozi wake hapa nchini ifikapo 2024, bado nchi hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania na katika kukuza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo baina ya mataifa hayo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Aidha, Waziri Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Sweden hapa nchini Mhe. Anders Sjoberg ambapo viongozi hao wamejadiliana masuala mbalimbali ya kukuza na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na mataifa yao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi Mteule wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Nabil Hajlaouvi mara baada ya kuwasilisha nakala ya Hati za utambulisho katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



 

Monday, September 13, 2021

BALOZI SOKOINE AFUNGUA KIKAO KAZI CHA WADAU WA IORA

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kinachofanyika mjini Zanzibar

 

Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Aboud S. Jumbe (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine katika kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) 

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agness Kayola akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA)kinachofanyika mjini Zanzibar

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar Balozi Masoud A Balozi (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agness Kayola wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kinachofanyika mjini Zanzibar


Wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimsikiliza Mratibu wa masuala ya IORA Tanzania Balozi Agness  Kayola kinachofanyika mjini Zanzibar
Wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika picha ya Pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine baada ya ufunguzi wa kikao kazi chao kinachofanyika mjini Zanzibar


 Na mwandishi wetu, Zanzibar

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amefungua kikao kazi cha wadau wa ndani wa Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) na kuwataka washiriki wa kikao hicho kutoa msukumo na kipaumbele kwa shughuli zinazoratibiwa na Jumuiya hiyo.

Balozi Sokoine amesema hayo mjini Zanzibar alipokuwa akifungua kikao kazi hicho na kuongeza kuwa kufanya hivyo watakuwa wanalinda kwa vitendo maslahi ya Taifa na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania, Nchi Wanachama na Washirika wa Mazungumzo na hivyo kuleta tija kwa Tanzania.

Amesema uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya diplomasia, ushirikiano wa kikanda na kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa inakutanisha nchi mbalimbali kubwa zilizoendeleana kwamba  Tanzania inaweza kutumia fursa ya Jukwaa la IORA kuimarisha ushirikiano wa nchi na nchi na Washirika wa Mazungumzo ambao wana nguvu kiuchumi na wameendelea kisayani na kiteknolojia.

Amewataka wadau hao kuandaa Mapendekezo ya Miradi yenye sifa na vigezo vya kupatiwa ufadhili kwenye Mfuko Maalum wa Jumuiya ya IORA ili kusaidia kuwezesha, kuhudumia wananchi na kuwezesha  jamii inayozunguka maeneo ya ukanda wa bahari,  uhifadhi wa mazingira ya bahari, uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari, uwezeshaji wananchi kiuchumi na maeneo mengine mtambuka yenye tija na maslahi kwa wananchi.

Awali akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Agness Kayola alisema Kikao Kazi hiko kina lengo la kuimarisha ushiriki wa Nchi kwenye Jumuiya ya IORA; kuimarisha ushirikiano wa kisekta kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuimarisha vikundi kazi ili kuweza kunufaika na uanachama wa Tanzania katika IORA.

Alisema kwa sasa, IORA ina vikundi kazi vinane (8) ambavyo vinafanya kazi chini ya Uratibu wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda - Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Amevitaja vikundi hivyo kuwa ni Ulinzi na Usalama; Biashara na Uwekezaji; Kazi cha Utalii na Utamaduni; Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi; Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu; Uvuvi; Maafa na Uchumi wa Bluu  

Kikao kazi hicho kinajadili mada zinazohusiana na upatikanaji wa fursa za uwekezaji zilizopo kwenye uchumi wa bluu; sheria, kanuni na taratibu za kuvuna na kuhifadhi rasilimali zilizopo kwenye bahari hususan kwenye ukanda wa bahari kuu; sera na mwongozo wa kufanikisha utekelezaji wa masuala ya uchumi wa bluu pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari kwa maendeleo endelevu na usalama wa eneo la bahari.

Jumuiya ya Nchi zilizopo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi inaundwa na nchi 23 ambazo ni Australia,  Afrika Kusini, Bangladesh, Comoro, India, Indonesia, Iran, Kenya, Madagascar, Malaysia, Maldieves, Msumbiji, Mauritius, Oman, Seychelles, Singapore, Somalia, Sri Lanka, Tanzania na Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen na Ufaransa kupitia Visiwa vya Reunion ambavyo inavimiliki.

 

 

KAMATI YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA (NUU) YAPIGWA MSASA

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeipiga msasa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa kuipatia mafunzo maalumu yenye malengo mbalimbali hasa katika kutetea maslahi ya Taifa.

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo pia yatajikita  katika masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi  ili kuwajengea uwezo wabunge wa kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya Kamati na Bunge kikamilifu.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tano Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa kupitia mafunzo hayo kamati itapata ujuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Kamati maslahi ya Taifa, masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi  ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yenu ya Kamati na Bunge kikamilifu.

“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa mtapata fursa ya kuelimishwa juu ya mambo Uchumi wa Buluu, mada itakayotolewa na Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa uchumi wa buluu kutoka Zanzibar ambayo imepiga hatua katika utekelezaji wake,” Amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Wizara inaamini kuwa wajumbe wa Kamati na washiriki wote wa mafunzo wataendelea kutumia ujuzi watakaoupata kuishauri Wizara na kuwa Mabalozi wazuri ndani na nje ya Bunge katika kulinda taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Niihakikishie Kamati kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nanyi kikamilifu hasa katika kipindi hiki tunapoandaa Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tunaamini kuwa ushiriki wenu utaiwezesha nchi yetu kuwa wa sera iliyosheheni masuala muhimu yatakayoiwezesha nchi kunufaika,” ameongeza Balozi Mulamula

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu amesema kamati anayoiongoza inafanya kazi kuwa kwa maslahi mapana ya nchi na kuahidi kuwa vichocheo vya maslahi ya nchi vinalindwa kwa maslahi mapana ya nchi.

“Kamati inatoa ushauri ‘cross-cutting’ kwa maana inagusa kila eneo kwa taifa letu, jambo lolote lile linalohusiana na masuala ya foreign huwa tunashauri, mambo ya ulinzi na usalama…..kwa hiyo inatoa mambo yak echini kwa chini kwa malengo ya kuisaidia serikali,” Amesema Bw. Zungu

Mafunzo haya muhimu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Chuo cha Diplomasia na yatafanyika kuanzia tarehe 13 – 17 Septemba 2021 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akijadili jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu (Mb) Jijini Dar es Salaam


Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) hayupo pichani

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi. Agnela Nyoni akitoa hotuba kabla ya kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula kuongea na wajumbe wa Kamati ya NUU


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba ya ufunguzi wa mafunzo maalum ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Jijini Dar es Salaam



Sunday, September 12, 2021

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujengwa Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Shirika la Elimu, Utamadani na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Amir Fehri alipotembelea Ofisi ya Ubalozi nchini Uholanzi.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akimpa zawadi ya kahawa ya Tanzania Balozi Fehri

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea barua kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Shule ya Kimataifa ya Wakimbizi kujngwa Tanzania

 

Balozi wa Shirika la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu (The Arab League Educational, Cultural and Scientific Organization-ALECSO), Mhe. Amir Fehri anakusudia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili aombe ridhaa ya kujenga shule ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania.

Balozi huyo kijana (17) na maarufu duniani, raia wa Tunisia alibainisha hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju.

“Naomba kupatiwa nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ili kumuomba nasaha zake (moral support) katika kampeni yangu ya kusambaza salaam ya Amani na Uvumilivu duniani, lakini zaidi kuomba ridhaa ya Mheshimiwa Rais ili niweze kujenga shule yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania”, Balozi Fehri alisema.

Akielezea kuhusu matarajio yake hayo, alisema, shule hiyo itakuwa inatoa vyeti vya kimataifa ili kuwasaidia watoto hao ama kupata kazi nchini Tanzania au wakirejea katika nchi zao. Aidha, Mhe. Fehri ameomba apatiwe nafasi ya kukutana na wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali nchini Tanzania ili kuwaelimisha kuhusu unyanyasaji unaofanyika mashuleni (bullying) na madhara yake pamoja na njia za kukabiliana na kadhia hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alimpongeza Mheshimiwa Fehri kwa jitihada zake thabiti na kumshukuru kwa mapenzi yake juu ya Tanzania, lakini zaidi kwa dhamira yake ya kujenga shule ya wakimbizi nchini Tanzania.

Alisema ni kweli kwamba, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kwa zaidi ya miaka 40 na moja ya changamoto kubwa inayojitokeza ni pale ambapo wakimbizi hao wanaporejea katika nchi zao kwa hiari, wanashindwa kujumuika ipasavyo na jamii zao kutokana na ukosefu wa elimu stahiki itakayowawezesha pamoja na mambo mengine kupata ajira. 

 

Balozi Kasyanju alitumia fursa hiyo pia kumpongeza sana Balozi Fehri kwa umaarufu wake duniani kama vile; kuteuliwa kuwa Balozi wa Francophonie ulimwenguni; kuweza kuchapisha vitabu 4 akiwa na umri wa miaka 12, ambavyo vilimpa tuzo 25 za kimataifa katika fasihi kama Sanaa na Barua za Tuzo ya Kimataifa ya Ufaransa, 2014; na kuzungumza lugha saba (Kikurdi-Kifaransa-Kichina-Kiingereza-Kijerumani-Kiarabu-Kilatini) sifa iliyomuwezesha kuwasiliana na viongozi wakubwa duniani. 

 

Balozi Fehri anashirikiana na Rais wa Tume ya Ulaya, kupitia Mfuko wa Amir Fehri (Amir Fehri Foundation) kufungua shule ya kwanza ya Kimataifa huko Mossoul, Iraq. Shule hiyo itakuwa ishara halisi ya elimu kwani itajengwa ndani ya kambi za wakimbizi na itatoa nafasi mpya kwa watoto wote wakimbizi.

 


 

Friday, September 10, 2021

VACANCY ANNOUNCEMENT AT THE OACPS SECRETARIAT


 

MTOTO BARKA SEIF MWENYE KIPAJI CHA MPIRA WA MIGUU ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI


Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akisaini kitabu cha Wageni katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Uholanzi. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.

Mtoto Barka Seif mwenye umri wa miaka 7 ambaye anakipaji cha kucheza mpira wa miguu,akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Uholanzi Mhe. Erine Kasyanju alipotembelea ubalozini hapo. Barka Seif yuko Nchini Uholanzi katika klabu ya Ajax.
 

Thursday, September 9, 2021

UINGEREZA IMEIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA, UWEKEZAJI, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Uingereza imeipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, Haki za Binadamu na Utawala Bora, jambo ambalo limeimarisha ushirikiano baina ya Nchi hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge, ukiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ya awali kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri huyo alipofanya ziara hapa nchini

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kutokana na mazungumzo hayo Uingereza na Tanzania zimekubaliana kufanya kongamano kubwa litakalojumuisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uingereza ili kuja kuwekeza hapa nchini. 

Pia Balozi Mulamula ameishukuru Uingereza kwa kuiunga mkono Tanzania katika bodi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jambo lililoiwezesha Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na adhari za UVIKO 19.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami, ambapo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulisaidia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari.

“Ili shirika hili liendelee kuhudumia vyema wakimbizi ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa ikaendelea kutoa mchango wake, hasa kwa kuwaongezea bajeti UNHCR ambayo itawawezesha kutimiza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi” alisema Mheshimiwa Balozi Mulamula 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami kwa niaba ya Shirika hilo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa muda mrefu katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi. 

Ofisi ya Kikanda ya UNHCR iliyopo Kasulu, Kigoma inahudumia nchi Kumi na Moja (11) ambazo ni; Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, South Sudan, Tanzania and Uganda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami yaliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Gerald Mbwafu baada ya kumaliza mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara na Watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi.

Wednesday, September 8, 2021