Picha ya pamoja |
Tuesday, June 14, 2022
WAZIRI MULAMULA ZIARANI NCHINI FINLAND
Helsinki, 14 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amewasili nchini Finland kwa ziara ya siku 3 kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic (NORDIC-AFRICA) unaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.
Mkutano
huo umeanza na hafla ya ufunguzi iliyofanyika tarehe 13 Juni 2022, ambapo mgeni
rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto.
Akiwakaribisha
wajumbe wa mkutano huo Mhe. Haavisto alisisitiza umuhimu wa kuimarisha
ushirikiano katika kujiletea maendeleo baina ya nchi hizo marafiki.
Aidha,
mkutano huu utahusisha nchi 5 za Nordic ambazo ni Finland mwenyeji wa mkutano
wa sasa, Sweden, Norway, Iceland na Denmark na nchi za Afrika 25 marafiki wa
Nordic.
Mkutano
huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utahusisha Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika
zinazowakilisha katika nchi za Nordic na Mabalozi wa nchi za Nordic
wanaowakilisha katika Nchi shiriki za Afrika.
Wazo la
kuanzisha mkutano huu lilianza mwaka 2000 ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika
nchini Sweden mwaka 2001. Baada ya hapo mikutano kama hii inafanyika kwa
kupokezana kutoka Bara la Afrika na upande wa Nordic.
Mwaka
2019 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huu ambapo nchi takribani 34
zilishiriki katika mkutano.
Wakati
huo huo Mhe. Waziri Mulamula ametumia fursa ya ziara hiyo kutembelea Makao
Makuu ya Ofisi ya Mpango wa usimamizi wa migogoro nchini Finland na kukutana na
uongozi wa mpango huo. Lengo la likiwa kujadili masuala ya amani na usalama
katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa kusini mwa Afrika.
Katika
mazungumzo yake Waziri Mulamula ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa mstari
wa mbele katika kusimamia masuala ya amani na usalama ili kuwezesha nchi za
ukanda huo kufanya shughuli za kiuchumi na kuinua maendeleo ya taifa na
wananchi kwa ujumla.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Saturday, June 11, 2022
MAKATIBU WAKUU WANAOSIMAMIA SEKTA MBALIMBALI WA NCHI ZA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA
Makatibu Wakuu wanaosimamia sekta mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki wakifurahia jambo kwenye Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini |
Meza Kuu kutoka kulia ni; Bw. Severin Mbarubukeye Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Vijana Michezo na Utamaduni kutoka Burundi, Bi. Edith Mwanje Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Bw. Saitoti Torume CBS, Katibu Mkuu wa Hazina na Mipango kutoka Kenya, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Bw. Adrea Aguer Ariik Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Sudan Kusini wakiwa kwenye Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini |
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha. |
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha. |
Mkutano wa 42 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Arusha |
Friday, June 10, 2022
ITALIA KUANZISHA UPYA SAFARI ZA NDEGE ZANZIBAR
Na Mwandishi wetu, Dar
Katika kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi Serikali ya Italia imeahidi kuanzisha upya safari za ndege za moja kwa moja kutoka nchini humo hadi Zanzibar kuanzia tarehe 29 Juni 2022.
Ahadi hiyo imetolewa na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Natalia amesema kuwa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar zitasaidia kukuza biashara na utalii baada ya kusitishwa kwa safari hizo tangu mwaka 2019 kutokana na changamoto ya Uviko 19.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuanzishwa upya kwa safari hizo kutachangia kukuza pato la taifa kwani awali kabla ya janga la Uviko 19, Zanzibar ilikuwa inapata watalii 200,000 kwa mwezi kutoka nchini Italia.
“Safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia kuja Zanzibar zinategemea kuanza rasmi tarehe 29 Juni, 2022 na tunaamini kuwa kuanzishwa kwa safari hiyo kutachangia kukuza sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Balozi Mbarouk
Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, utalii, viwanda, maji, kilimo, nishati, pamoja na maendeleo ya sekta binafsi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimueleza jambo na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle wakati alipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Inspekta Jenerali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Balozi Natalia Quintavalle baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
BALOZI MULAMULA AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA RAIS SAMIA KWA RAIS WA MISRI
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amewasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi Jijini Cairo.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula aliwasilisha salamu za Mhe. Rais Samia kwa Rais El-Sisi, alisisitiza umuhimu wa kuendelea uhusiano wa kihistoria na ushirikiano katika sekta mbalimbali, za kimkakati hususan Ulinzi na Usalama, Elimu, Nishati na Mifugo.
Aidha, baada ya mazungumzo na Mhe. Rais El-Sisi alikutana na kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Shoukri na kisha alifanya mahojiano na waandishi wa habari.
Moja wa Masuala ya msisitizo ni kuiunga mkono Misri kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mazingira COP27 utakaofanyika katika Jiji la Sharma Al Sheikh mwezi Novemba, 2022 na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika sekta za Afya, Elimu na nyinginezo kwa manufaaa ya Nchi hizi mbili.
Pia Balozi Mulamula alitumia mazungumzo hayo kuishukuru Misri kwa misaada mbalimbali inayoipatia Tanzania katika sekta za kimkakati pamoja na kuiunga mkono Tanzania katika mipango yake ya maendeleo kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Katika Mazungumzo hayo, Balozi Mulamula na Mhe. Shoukri walikubaliana kufanya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) utakaofanyika Nchini Tanzania mwezi Desemba, 2022 baada ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP-27).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi Jijini Cairo |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi Jijini Cairo |
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi Jijini Cairo akisoma Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifuatilwa na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Dkt. Emmanuel Nchimbi. |
OACPS YATENGA EURO MILIONI 157 KUKOPESHA WAKULIMA KUONGEZA MNYORORO WA THAMANI MAZAO YA KILIMO
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumzia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mkutano huo. |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (aliyekaa katikati) akiwa na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 202. Kushoto aliyekaa ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia aliyekaa ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi Agnes Kiama. |
Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) umetenga kiasi cha Euro milioni 157 kukopesha wadau wa kilimo katika nchi wanachama kwa masharti nafuu ili kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema hilo ni azimio mojawapo lililofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Amesema kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wanaotaka mikopo hiyo ya masharti nafuu watatakiwa kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kuweza kushiriki kikamilifu katika mkakati huo wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo
“ Mkutano
umeazimia kuanzisha mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya
kilimo, na ili kufanikisha azimio hilo Jumuiya imetenga Euro milioni 157 ambazo
zitatoka kama mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima ndani ya jumuiya yetu ya
OACPS” alisema Balozi Sokoine na kuongeza kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania
wataweza kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.
Amesema kuwa Ubalozi ukikamilisha taratibu za uombaji na utoaji wa mikopo hiyo utatoa kwa walengwa ili wafanye maombi ya mikopo hiyo.
Akiongelea mazimio mengine, Balozi Sokoine amesema kuwa ni kuidhinishwa kwa Tanzania katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya masuala ya Uvuvi kwa miaka miwili kuanzia 2022 hadi 2024 na hivyo kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa masuala Uvuvi unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.
“Hatua hii ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kusimamia utekelezaji wa ajenda yake ya uchumi wa buluu na kukuza ushirikiano baina ya nchi za OACPS katika sekta ya uvuvi” alisema.
Amesema Mkutano huo umejadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ndani ya jumuiya wakati wa kuingiza bidhaa katika soko la Ulaya na kuja na mikakati ya kutatua changamoto hizo kwa kufaya tathmini ya kina ili kuzielewa changamoto husika na kuanzisha mfumo wa utoaji tahadhari mapema kwa wafanyabiashara.
Amesema azimio lingine ni kuanzisha Jukwaa Maalum la Wafanyabiashara ndani ya Jumuiya kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara, kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa masoko ya bidhaa na huduma na kuongeza kuwa Mkutano pia umeazimia kuunganisha nguvu ya Diaspora kwa kuanzisha jukwaa maalum la kuwezesha Diaspora kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala mbalimbali ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Jumuiya na kutoa maoni na kufanyiwa kazi.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa OACPS ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya hiyo ambacho kinahusika na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kwa Nchi wanachama na hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kutoka katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.
Thursday, June 9, 2022
TANZANIA YAIKARIBISHA JUMUIYA YA OACPS KUADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI
Katibu Mkuu Balozi
Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia lugha ya Kiswahili Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mwenyekiti wa Mkutano wa 114 wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS Mhe. Slyvie Baipo Temon uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 |
Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia kiswahili Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede wakati wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS jijini Brussels |
Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia kiswahili Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS Bw. Georges Robelo Pinto Chikoti wakati wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (waliokaa katikati) katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022. Waliokaa kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia ni mwakilishi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi. Agnes Kiama. |
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022. |
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 wakiendelea na mkutano huo. |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amezikaribisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 7 2022.
Akitoa mwaliko huo katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, Balozi Sokoine amesema Lugha ya Kiswahili imeendelea kukua na hivyo kuwa na wazungumzaji wengi katika sehemu nyingi duniani.
Amesema Tanzania inajivunia uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa kuitambua na kuipa Siku Maalum lugha ya Kiswahili hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa Tanzania.
Amesema Maadhimisho hayo yanatarajiwa kukuza zaidi na kuongeza matumizi ya lugha hiyo duniani.
"Leo hii Kiswahili sio lugha ya Taifa ya Tanzania pekee au katika nchi nyingine za Afrika bali pia ni lugha inayozungumzwa na watu wengi katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini," alisema Balozi Sokoine.
Ameongeza kuwa Kiswahili sasa kinafudishwa katika zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani na ni miongoni mwa lugha za kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika.
"Kwa niaba ya Ubalozi wa Tanzania hapa Brussels na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu tunawaalika rasmi nchi wanachama wa OACPS kuungana na Tanzania na wadau wengine wa Kiswahili kuadhimisha kwa mara kwanza Siku ya Kiswahili duniani," alisema Balozi Sokoine.
Tanzania na Balozi zake zitaungana na wadau wa Kiswahili duniani kuadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kiswahili duniani.
Katika Mkutano huo Balozi Sokoine alipata fursa ya kukabidhi vitabu vya awali vya kujifunzia lugha ya Kiswahili vilivyoungwa na Baraza la Kiswahili Tanzania kwa Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Mhe. Slyvie Baipo Temon na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede.
Julai 7 ya kila mwaka ilitangazwa na UNESCO kuwa siku maalum ya Maadhimisho ya Kiswahili duniani.