Monday, October 17, 2022

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA WADAU MBALIMBALI KUBORESHA SEKTA YA MAJI NCHINI

Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya maji na usafi wa mazingira nchini ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama. 

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 17 Oktoba 2022 alipotembelea Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi nchini humo.

 

Mhe. Dkt. Tax ambaye alikutana na Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na wamiliki wa kampuni mbalimbali za Poland zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maji nchini, amesema, sekta ya maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele nchini, kwani zinagusa maisha ya wananchi wote wa mijini na vijijini na kwamba  wanahitajika wawekezaji makini na wenye tija kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuiboresha.

 

Amesema miji mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam inaendelea kukua kwa kasi hivyo upo umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama lakini pia kuendelea kutunza mazingira.

 

“Maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa   Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali ili kuhakikisha sekta hii inaboreshwa zaidi hususan kwenye teknolojia ya kisasa ya usimamizi wa maji  ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu” alisema Dkt. Tax.

 

Pia amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na  Taasisi mbalimbali zinazosimamia sekta ya maji nchini ikiwemo Wizara ya Maji ili kwa pamoja kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.

 

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri chuoni hapo, Mkuu wa Chuo, Prof. Michal Zasada amesema chuo hicho ambacho kimejikita katika ufundishaji wa Teknolojia mpya ya usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, kipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sekta hiyo kutoka nchini.

 

“Tumefarijika kutembelewa na wewe Mhe. Waziri na ujumbe wako kutoka Tanzania. Chuo chetu kinatoa kozi mbalimbali za Shahada na Shahada ya Uzamili katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta ya maji. Tayari wataalam kadhaa kutoka sekta ya maji wamewahi kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo hapa chuoni. Tunaendelea kuwakaribisha Watanzania kujiunga na program mbalimbali za mafunzo hususan za sekta ya maji zinazotolewa chuoni hapa” alisema Prof.  Zasada.

 

Wakati wa Mkutano huo Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na sekta ya maji na usafi wa mazingira za Poland ikiwemo ile ya Asseco ziliwasilisha mada na kueleza utayari wao wa kuwekeza katika sekta ya maji kwa kuanza na miji ya Dodoma na Dar es Salaam.

 

Akiwa chuoni hapo Mhe. Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea maabara za kisasa za usimamizi wa maji pamoja na  kujionea mradi wa maji unaotumia teknolojia ya kisasa unaotekelezwa na chuo hicho.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland, Prof. Michal Zasada mara baada ya kuwasili Chuoni hapo leo tarehe 17 Oktoba 2022. Pamoja na ambo mengine Mhe. Waziri Tax alizungumza na menejimenti ya chuo hicho kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya elimu na maji pamoja na kutembelea miradi ya maji inayotekeelzwa na chuo hicho. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022


Mhe Waziri Dkt. Tax akizungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw cha nchini Poland kuhusu masuala ya ushirikiano katika sekta za elimu na maji. Kushoto kwake ni Prof. Zasada, Mkuu wa Chuo hicho akifuatiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Marta Mendel na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Mhe. Krystof Buzalski. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland, Mhe. Balozi Abdallah Possi
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Zasada akizungumza kumkaribisha Mhe. Dkt Tax alipotembelea Chuoni hapo

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia) akiwa pamoja na Wajumbe kutoka Tanzania walioambata na Mhe. Waziri Tax nchini Poland.

Sehemu ya Wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw na wamiliki wa Kampuni zinazojishughulisha na masuala ya maji wakifuatilia kikao
 
Sehemu nyingine ya Wajumbe kutoka Tanzania
 
Sehemu ya washirki kutoka Chuoni hapo
Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania
 
Mkutano ukiendelea
 
Sehemu ya wajumbe kutoka Chuoni hapo
 
Sehemu nyingine ya washiriki
 
Mada kuhusu masuala ya maji na usafi wa mazingir aikiwasilishwa na mmoja wa washiriki kutoka Poland
 
Mhe. Dkt. Tax akimweleza Prof. Zasada kuhusu zawadi  kutoka Tanzania kabla ya kumkabidhi. Zawadi hiyo ni mkusanyiko wa bidhaa za Tanzania zikiwemo Kahawa, Korosho, batiki, Vikoi na Viungo vya chakula.
 
 
Prof. Zasada naye akimkabidhi zawadi Mhe. Waziri Dkt. Tax
Picha ya pamoja
Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Wojciech Sas alipofika kukitembelea kituo hicho na kujionea maabara mbalimbali za maji

Mhe. Dkt Tax na ujumbe wake wakipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa mitambo na teknolojia mbalimbali za maji Prof. Adam Kiszko


Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya maji alipotembelea maabara hiyo

Mhe. Dkt. Tax akiangalia bwawa lililochimbwa kitaalam bila kuharibu mazingira na viumbehai  alipotembelea Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za maisha cha Warsaw, Poland




 

TANZANIA YATWAA TUZO KATIKA MAONESHO YA UTALII NCHINI KOREA KUSINI ’THE 23RD BUSAN INTERNATIONAL TRAVEL FAIR’

 


MAKAMPUNI YA JAPAN YAVUTIWA NA KAHAWA YA TANZANIA

Makampuni ya Japan yameonesha kuvutiwa na kahawa ya Tanzania katika maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yajulikanayo kama 2022 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition yaliyofanyika jijini Tokyo tarehe 12 – 14 Oktoba, 2022. 

Maonesho hayo ambayo yalishirikisha taasisi zipatazo 235 zinazoshughulika na kahawa kutoka kote duniani, yaliandaliwa na kusimamiwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ). 

Kutokana na mapokeo mazuri ya kahawa ya Tanzania miongoni watumiaji na makampuni ya Japan katika maonesho hayo, soko la kahawa ya Tanzania nchini humo linatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 32 ya sasa, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu 15,000,000 zinazounzwa nchini humo kwa mwaka. Kiwango hiki kimeelezwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu duniani zinazouza kahawa kwa wingi nchini Japan.

Maonesho hayo imekuwa ni fursa adhimu katika kukuza wigo wa soko na kujihakikishia soko la kudumu la kahawa ya Tanzania nchini Japan, ikiwa ni miongoni mwa kahawa pendwa nchini humo iliyopewa jina maarufu la kibiashara “Tanzania Kilimanjaro Coffee”.Ujumbe wa Tanzania katika maonesho hayo uliongozwa na Bodi ya Kahawa Tanzania ikiwa imeambatana na wawakilishi wa vyama viwili vya ushirika na makampuni matatu ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji na uuzaji wa kahawa ikiwemo; Kagera Cooperative Union (KCU), Karagwe District Cooperative Union (KDCU), Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD),Kampuni ya Acacia na Kampuni ya Touton Tanzania Ltd
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe.Balozi Baraka Luvanda (wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa ubalozi na wadau wa zao la kahama kutoka Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika jijini Tokyo

Sehemu ya walaji wa kahawa wa nchini Japan wakionja bidhaa hiyo kutoka Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa yaliyofanyika jijini Tokyo hivi karibuni
Wadau wa kahawa wa nchini Japan wakifuatilia wasilisho (presentation) kuhusu kahawa inayozalishwa hapa nchini lililowasilishwa na wataalam wa Bodi ya Kahawa Tanzania 

Wadau wa kahawa wa nchini Japan wakifuatilia wasilisho (presentation) kuhusu kahawa inayozalishwa hapa nchini lililowasilishwa na wataalam wa Bodi ya Kahawa Tanzania 

Saturday, October 15, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZASAINI MKATABA WA KUBADILISHANA WAFUNGWA NA MKATABA WA UTATU WA CHEMBA ZA BIASHARA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia zimesaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa na Mkataba wa Utatu kati ya Chemba za Biashara za nchi hizo wakati wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliomalizika tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka.

Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa ulisainiwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.

Wakati huo huo, Mkataba wa Utatu kati ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC) za Tanzania na Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda (ZACCI) ya Zambia ulisainiwa na Rais wa TCCIA, Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa TCCIA na Bw. Nerbat Mwapwele kwa niaba ya Mwenyekiti wa ZNCC. Pia kwa upande wa Zambia mkataba huo ulisainiwa na Mtendaji Mkuu wa ZACCI, Bw. Phil Daka.

Aidha, Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri, ulitanguliwa na mkutano katika ngazi ya wataalam uliofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2022 na kufuatiwa na Mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe  13 Oktoba 2022. 

Pamoja na mambo mengine mkutano huo pia ulitathimini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema aliyofanya nchini Tanzania mapema mwezi Agosti 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) akihutubia wakati wa kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika tarehe 11 hadi 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia wakisaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa kati ya nchi zao leo tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo wakionesha Hati zilizosainiwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo wakishuhudia Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda, Bw. Phil Daka wakisaini mkataba  wa ushirikiano kati ya chemba hizo.

Mtendaji Mkuu wa TCCIA, Bw. Nerbat Mwapwele akisaini Mkataba wa ushirikiano wa Chemba za Biashara kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC) utiaji saini huo pia ulishuhudiwa na Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Kabubo.

Kulia Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Naibu Waziri Wizara ya  Ujenzi na Uchukuzi, Bw. Atupele Mwakibete wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Yahya Simba na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimpa zawadi ya picha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.




Friday, October 14, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZAKUBALIANA KUBORESHA MIFUMO KUTATUA CHANGAMOTO YA MIGOMO YA MADEREVA MPAKANI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia zimekubaliana kuimarisha mifumo ya utendaji kazi ili kumaliza changamoto ya migomo ya madereva katika mpaka wa Tunduma - Nakonde unaozitenganisha nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa  leo tarehe 14 Oktoba 2022 katika Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.

Akifungua mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax ameeleza dhamira ya wazi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa kufanya maboresho na usimamizi wa karibu katika sekta za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

“Tunatakiwa kuchukua hatua na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta za umma na binafsi ili kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji ili kuinua uchumi wa nchi zetu; kuboresha utendaji wa kampuni ya reli ya TAZARA na kuboresha mtandao wa barabara  kati ya Tanzania na Zambia ili kuifanya Kapiri Mposhi kuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo nchini Zambia kwa kushirikiana na Bandari ya Dar es Salaam (TPA).

Aidha, Mhe. Tax ameeleza umuhimu  wa kuwa na mikakati ya pamoja na ya kudumu ya kutatua migomo ya madereva mpakani; kuimarisha utendaji kazi katika kituo cha pamoja cha mpakani Tunduma/Nakonde (OSBP) kwa kukiwezesha kituo hicho kuwa na huduma bora na rafiki kwa usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria; kufufua mradi wa bomba la mafuta la TAZAMA ambapo mradi huo utaenda sambamba na mradi wa kuunganisha umeme wa nchi za Tanzania na Zambia (TAZA).

Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo alieleza kuwa Serikali ya Zambia inathamini ushirikiano uliopo baina ya Zambia na Tanzania ambao umewezesha Marais wa nchi zote mbili kukutana jijini Dar es Salaam na kupelekea kutoa maelekezo ya kufanyika kwa mkutano huo unaojadili na kutoa maamuzi ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu Kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika mwaka 2016.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye ameambatana na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Bw. Atupele Mwakibete, Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia Ngazi ya Mawaziri unaofanyika tarehe 14 na 15 jijini Lusaka, Zambia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa ameambatana na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Bw. Atupele Mwakibete katika Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia unaofanyika  tarehe 14 na 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Mhe. Waziri Tax (kulia) akisistiza umuhimu wa kutatua migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza mpakani Tunduma/Nakonde ili kuimarisha ushirikiano na kuweka mazingira wezesha ya biashara kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Zambia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Zambia Ngazi ya Mawaziri unaofanyika tarehe 14 na 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia mkutano huo.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu akifuatilia ufunguzi wa mkutano wa Kumi wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Zambia Ngazi ya Mawaziri unaofanyika tarehe 14 na 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.


Ujumbe kutoka Zambia.

Ujumbe wa Tanzania.

Picha ya pamoja Mawaziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tyume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.



TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA HISPANIA : DKT CHANA

Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa na Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa na Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam wakijumuika.

Waziri wa Maliasilia na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameihakikishia Serikali ya Ufalme wa Hispania kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi hiyo katika kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya nchi na watu wake.

Mhe. Dkt. Pindi Chana ametoa kauli hiyo katika hafla ya maadhimisho Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana  kwa karibu na Serikali ya Ufalme wa Hispania katika kukuza na kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi mapana ya nchi zetu na wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Pindi Chana.

Ameishukuru Hispania kwa kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia sekta za maji, afya, umeme vijijini na kilimo na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba ushirikiano huo utakuwa na kufikia sekta nyingine nyingi za kiuchumi.

Mhe. Dkt. Pindi Chana pia ameishukuru Hispania kwa kuijumuisha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazonufaika na Sera Maalum ya Nchi za Afrika iliyoanzishwa mwaka 2019.

Amesema Hispania imekuwa mstari wa mbele katika maeneo ya afya, lishe, elimu, mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia, maeneo ambayo ni ya kipaumbele pia kwa Tanzania na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba Tanzania na Hispania zitaendelea kushirikiana katika maeneo hayo kwa maslahi mapana ya nchi hizo.

“Kwa miaka mingi Serikali ya Hispania imekuwa mstari wa mbele katika maeneo ya afya, lishe, elimu, mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia, hay ani maeneo ambayo Tanzania ni kipaumbele chake pia nina uhakika kuwa Tanzania na Hispania zitaendelea kushirikiana katika maeneo hayo kwa maslahi mapana ya nchi zetu” alisema.

Akiongelea kuhusu uhusiano wa kibiashara Dkt. Pindi Chana ametoa wito wa kuongezwa kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo na kuongeza kuwa ujazo wa biashara kati ya nchi hizo kwa mwaka 2021 ulikuwa sawa na Shilingi Bilioni 183.3.

Akiongelea Utalii Dkt. Pindi Chana alisema watalii kutoka Hispania wamekuwa wakiitembelea Tanzania lakini watalii hao walipungua kutokana na janga la ugonjwa wa COVID 19 kutoka watalii 18,838 kwa mwaka 2019 hadi watalii 13,150 kwa mwaka  2021.

Alitoa wito kwa watalii wa Hispania kuja kwa wingi kuitembeleea Tanzania kutokana na kuwa na vivutio vya kipekee  duniani na hawatasahau ujio wao hapa nchini.
Awali akimkaribisha Dkt. Chana katika hafla hiyo Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez alisema Serikali yao ina nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuingiza maeneo mengi zaidi ya ushirikiano na kufanya kazi pamoja na kuiletea nchi maendeleo.

Alitaja mpango mradi wa upanuzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam ambao watakaoshirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kama mfano mmojawapo

“Tumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya nchi zetu, tunataka kushirikiana zaidi katika maeneo ya Maendeleo, mfano ni kupitia mradi wa upanuzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam ambako tunashirikiana na Benki ya Dunia na Serikali kufanya kazi hiyo,” alisema.

Thursday, October 13, 2022

WAZIRI WA MAMBO YA NJE AKUTANA NA WATUMISHI WA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ZAMBIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana na kufanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 katika ofisi za ubalozi huo Jijini Lusaka, Zambia.

Mhe. Tax amekutana na watumishi wa Ubalozi huo baada ya kuwasili nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022.

Akiongea katika kikao na watumishi hao Mhe. Waziri Tax ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ni wa kihistoria na kidugu uliojengwa kupitia ujirani mwema na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Mataifa hayo mawili Hayati Baba wa Taifa la Tanzania Mw. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Keneth Kaunda wa Zambia. Kupitia kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Tax ameelekeza Ubalozi kuendelea kuwa kiungo katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa kufuata misingi iliyowekwa na Waasisi wa Mataifa hayo.

“Fanyeni kazi kwa bidii hususan wakati huu tunapotekeleza diplomasia ya uchumi ili ushirikiano wetu uweze kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa maslahi mapana ya nchi yetu”alisema Mhe. Waziri Tax.

Naye Balozi wa Tanzania nchi Zambia anayemaliza muda wake Mhe. Hassan Yahya Simba akisoma taarifa ya utekelezaji, ameeleza kuwa ubalozi unaendelea kusimamia ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwa kuhakikisha unafatilia kwa karibu maslahi ya Taifa na maslahi ya Watanzania wanaoishi na kuingia nchini Zambia kwa shughuli mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax ametumia nafasi hiyo kutembelea majengo yanayomilikiwa na ubalozi wa Zambia pamoja na ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia.

Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umekuwa ofisi ya kwanza ya uwakilishi kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi huo tarehe 13 Oktoba 2022.

Mhe. Dkt, Tax (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Mheshimiwa Waziri Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia tarehe 13 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia, kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya.

Maafisa wa Ubalozi wakifuatilia kikao hicho.

Kutoka Kulia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakipokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati wa jengo la ofisi na nyumba za Serikali ya Jamhuri ya Tanzania zilizopo nchini Zambia kutoka kwa Mhe. Balozi Hassan Yahya Simba alipotembelea nyumba za watumishi wa Ubalozi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi huo Bw. Humphrey Shangarai (kushoto) alipotembelea nyumba za watumishi wa ubalozi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika ofisi za Bandari ya Dar es Salaam (TPA) zilizopo jijini Lusaka, Zambia tarehe 13 Oktoba 2022. Aliyesimama ni Mwakilishi wa TPA nchini Zambia, Bw. Hamis Chambali.

Picha ya pamoja.





Wednesday, October 12, 2022

TANZANIA NA ZAMBIA ZAAZIMIA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA NA USAFIRISHAJI

Tanzania na Zambia zimedhamiria kumaliza changamoto za kibiashara na usafirishaji zinazowakabili wafanyabiashara ili kuruhusu biashara na usafirishaji wa bidhaa ufanyike bila vikwazo baina ya nchi hizo.

Hayo yamebainishwa katika hotuba ya ufunguzi iliyosomwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakati wa Mkutano 10 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 12 Oktoba 2022 jijini Lusaka Zambia.

Balozi Sokoine aliwasisitiza watendaji kutumia mkutano huo kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na binafsi ili ziweze kufanya uwekezaji utakaoleta maendeleo endelevu kwa ajili ya maslahi mapana ya kiuchumi kwa pande zote mbili.

“Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wake wa kindugu na kihistoria na Zambia ili kuendeleza jitihada zilizoasisiwa na waasisi wa mataifa yetu kwa kuweka na mfumo rasmi wa ushirikiano unaowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji katika masuala ya ushirikiano” alisema Balozi Sokoine.

Aidha, alieleza kuwa ushirikiano imara na wenye mafanikio ni ule unaojengwa kwa mfumo rasmi ambao unaruhusu kukutana na kufanya majadiliano ya mara kwa mara hivyo, alieleza kuwa ana amini kupitia mkutano huu maeneo yote ya ushirikiano yenye changamoto yatajadiliwa kwa kina kwa maslahi ya nchi zote mbili na wananchi wake.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula alieleza kuwa ni muhimu majadiliano yakaangalia kwa kina maeneo muhimu yatakayowezesha pande zote mbili kuwa na mchango katika maendeleo ya mtangamano wa kikanda.

“Nchi zetu zimepiga hatua kiuchumi na katika maendeleo ya jamii tangu kumalizika kwa mkutano wa tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya ushirikiano baina yetu, hivyo ni vyema majadiliano yakaendana na uhalisia wa mabadilika hayo” alisema, Bw. Mbula.

Pamoja na mambo mengine mkutano huu utapitia na kujadili utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tisa wa Tume ya Kudumu ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika tarehe 25 na 26 Februari 2016 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioanza tarehe 11 Oktoba 2022 kwa ngazi ya Wataalam, utafuatiwa mkutano wa Makatibu Wakuu na utahitimishwa kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022 jijini humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Bw. Ally Gugu na Balozi wa Tanzania nchini Zambia anayemaliza muda wake, Mhe. Hassan Simba Yahya wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Zambia

Ujumbe kutoka Tanzania.

Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka Tanzania.

Maafisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano, kutoka kushoto ni  Bi. Lilian Mukasa na Bw. Makama D. Makamba.

Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutoka kulia ni Bi. Clementine Msafiri na Bi. Happiness Lyandala wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo.

Ujumbe kutoka Tanzania ukifuatilia ufunguzi wa mkutano, kulia ni Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Laila Kagombora.

Ujumbe kutoka Tanzania.

Picha ya Pamoja Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (wa nne kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw. Chembo Mbula (wa tatu kutoka kulia) pamoja na viongozi na maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zambia unaofanyika kuanzia tarhe 11 hadi 14 Oktoba jijini Lusaka Zambia.



TUENDELEE KUMUENZI MWALIMU NYERERE- MHE MAKINDA



Kamishna wa Sensa ya mwaka 2022 Mhe. Anne Makinda amewasihi Watanzania kuendelea kuenzi fikra na mitazamo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mhe. Makinda ametoa rai hiyo katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam alipofungua Kongamano la kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea 1999 jijini London.

Amesema Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, ni muasisi wa siasa za kutokufungamana na upande wowote, Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika hasa zile za Kusini pamoja na kutokukubaliana na fikra za ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote na kusisitiza kuwa ni lazima tuendelee kumuenzi kwa mambo makubwa aliyotufanyia

“Mwalimu alikuwa muasisi wa vitu vingi ambavyo nchi yetu inajivunia hadi sasa, alikuwa muasisi wa siasa za kutofungamana na upande wowote, kusimamia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kupinga ukoloni na ubaguzi wa aina yoyote ile, haya mambo ni makubwa sana lazima tuendelee kuyaenzi kwa nguvu zote,” alisema.

Amefafanua kuwa Hayati Mwalimu alitamani kuchelewesha uhuru wa Tanganyika kutokana na imani yake ya ukombozi wa nchi zote za Afrika kwakuwa aliona ukombozi wa mmoja hauna maana kama nchi nyingine hazitakuwa huru.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga amewashukuru watoa mada na washiriki wa kongamano hilo kwa michango yao ambayo imefanya kongamano hilo kufanikiwa na kutoa elimu kwa wengi.

“Watoa mada wetu wamesema mengi ya muhimu sana na tumejifunza kwa kina. Nawashukuru wote kwa mawasilisho yenu muhimu katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambalo limetukumbusha mambo mengi yaliyofanywa na Hayati Mwalimu Nyerere,” alisema Balozi Mindi.

Balozi Mindi pia amekipongeza Chuo cha Diplomasia kwa kuandaa Kongamano hilo kwa ajili ya kukumbuka miaka 23 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na hivyo kuwakutanisha wadau mbalimbali na kuwakumbusha, kujadili na kujifunza mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kujenga Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia ya Tanzania.

Kongamano hilo lilijadili mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika Kuendeleza Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia nchini liliwakutanisha mabalozi wastaafu na wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia na wanafunzi wa shule ya Sekondari Jitegemee ya Dar es Salaam.