Tuesday, January 23, 2024
Monday, January 22, 2024
NAIBU WAZIRI MKUU WA CHINA MHE. LIU ATEMBELEA JKCI
Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong ametembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) leo tarehe 21 Januari 2024 na kupokelewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel.
Akiwa katika Taasisi hiyo, Mhe. Liu alipokea taarifa ya utendaji kazi iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge pamoja na kutembelea chumba cha upasuaji mdogo na mkubwa wa moyo na chumba cha wagonjwa mahututi wa moyo.
JKCI imejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China kuanzia mwaka 2006 na kukamilika mwaka 2014 kwa ajili ya kutoa matibabu ya moyo nchini.
Taasisi ya JKCI inashirikiana
na Taasisi za afya za China katika maeneo ya kubadilishana ujuzi na utaalam,
utafiti, vifaa tiba na huduma za upasuaji wa moyo.
Naibu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama
cha Kikomunisti cha China,
Mhe. Liu akieleza jambo wakati wa ziara hiyo. |
Ziara ikiendelea. |
Picha ya pamoja, Mhe. Liu (wa tano kutoka kulia), Mhe. Dkt. Mollel (wa sita kutoka kulia), Dkt. Kisenge na ujumbe kutoka Serikali ya China na wafanyakazi wa Taasisi ya JKCI |
NAIBU WAZIRI MKUU WA CHINA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI
Naibu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama
cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Gozhong, amewasili nchini kwa ziara ya siku
tatu (3) kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024 na kupokelewa na Naibu Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri waNishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko
(Mb.)
Ziara hii
inafanyika ikiwa ni jitihada za makusudi kati ya Tanzania na China katika kuimarisha
ushirikiano wa kihistoria na kidugu ulioasisiwa na kujengwa na waasisi wa mataifa
hayo mawili mwaka 1964; Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong wa China na
kuimarishwa na awamu zote za uongozi zilizofuatia katika mataifa hayo mawili.
Pamoja na mambo mengine, akiwa nchini Mhe. Liu atatembelea; Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI ), Makumbusho ya Taifa, Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kadhalika atatembelea eneo la makaburi ya wataalamu wakichina waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA.
Mmoja wa Wajumbe walioongozana na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Liu Guozhong akichukua matukio wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo nchini. |
Sunday, January 21, 2024
TANZANIA, OMAN KUIMARISHA UTAMADUNI NA KUMBUKUMBU
DIPLOMASIA YA TANZANIA YAZIDI KUNG’ARA KIMATAIFA
Diplomasia ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa kufuatia viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema tarehe 22 Januari 2024 atawasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini tarehe 22 - 24 Januari , 2024.
“Mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.),” alisema Waziri Makamba.
Amesema Kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 – 25 Januari, 2024. Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba.
Waziri Makamba, amesema Mheshimiwa Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.
Kiongozi mwingine anayetarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda atakayewasili nchini kwa ziara ya kikazi tarahe 8 – 9 Februari 2024.
Akiwa nchini, Mheshimiwa Duda atakutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland.
Amesema Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji, usimamizi wa mazingira, utalii, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.
Aidha, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.
Mbali na viongozi wakuu wa mataifa tajwa kufanya ziara nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 – 26 Januari 2024, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo. Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Agosti 2023.
“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” aliongeza Waziri Makamba.
Kadhalika, Waziri Makamba amewaeleza waandishi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia pia kufanya Ziara ya Kitaifa Vatican tarehe 11 – 12 Februari, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis.
Waziri Makamba ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Mhe. Pietro Parolin. Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini.
Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya. Kwenye ziara hiyo Mhe. Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo.
Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway, tarehe 13-14 Februari 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja. Ameongeza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Mfalme Herald. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kongamano la Nishati la Oslo,” alisema Waziri Makamba
Tanzania na Norway zinashirikiana kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.
Kuanzia mwaka 2010, Serikali ya Norway imekua ikishirikiana na Tanzania kwenye programu mbalimbali za maendeleo zilizo gharimu takribani TZS. 300 bilioni. Programu hizo zimesaidia na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Nishati; Sekta ya Elimu; Sekta ya Mafuta na Gesi; Mpango wa Usimamizi wa Fedha za Umma; programu za Mabadiliko ya Tabianchi; na programu za Usimamizi wa Misitu.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaandika historia kupitia ziara hii nchini humo kwani mara ya mwisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa Ziara ya Kitaifa ilikua mwaka 1976.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam |
Saturday, January 20, 2024
VITU LAZIMA VITOKEE, WAZIRI MAKAMBA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Veronica Macamo |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. . Dkt. Mohamad Maliki Bin Osman |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno
Eduardo Rodriguez Parrilla |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Mhe. Do
Hung Viet |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Shoukry |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Musalia Mudavadi. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Christophe Lutundula |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Simalia, Mhe. Ali Mohammed Omar |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Uhamiaji na Bima ya Taifa wa Bahamas, Mhe. Alfred Sears. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Aberzaijan, Mhe. Jeyhun
Bayra. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Mesganu Moach. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mhe. Nasser Bourita |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Philipino, Mhe. Enrique
A. Manalo, |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb), akibadilishana mawasiliano na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Mhe. Omer Ahmed Berzinji. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo |
Thursday, January 18, 2024
BALOZI NAIMI AZIZI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO UNIDO
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller. |
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller. |
Wednesday, January 17, 2024
Tuesday, January 16, 2024
TANZANIA, ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO KUONGEZA USHIRIKIANO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoleana visa kwa wenye hati/pasi za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika leo Zanzibar.
Waziri Makamba amesaini hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi. Aidha, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesaini hati ya ushirikiano katika sekta ya afya
Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo, Waziri Makamba alisema Tanzania na Angola zina uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na viongozi wakuu wa Kitaifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Agostinho Neto walianzisha uhusiano huo kwa matarajio yao kuwa uhusiano huo utoe manufaa kwa nchi zote mbili.
“Leo kupitia mkutano wetu tumesaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola. Hati hizo ni pamoja na hati ya makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, Hati ya makubaliano ya kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya,” alisema Waziri Makamba.
Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa kisiasa, ulinzi, elimu, afya, mafuta na gesi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, kubadilishana visa, kusafiri bila visa kati ya nchi zetu mbili na hatimaye tumeingia makubaliano ya ushirikiano.
Kuadhalika, viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali husasan uwepo wa ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya Kongamano la bishara na uwekezaji na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja walizokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupitia makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tuahidi kuyatekeleza yale yote tuliyokubaliana katika mkutano wetu ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi António.
Aidha, kuhusu kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya kongamano la biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wananchi wetu kubadilisha uzoefu na kuendelea kukuza sekta binafsi kwa mataifa yote mawili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi leo Zanzibar |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakionesha Hati za Makubaliano ya Ushirikiano baada ya kuzisaini leo Zanzibar |
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakifuatilia mkutano |
Meza Kuu katika Picha ya pamoja, katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António. Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (wa pili kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye Kamba ya njano shingoni) na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Mhe. Sandro de Oliveira. |
Sunday, January 14, 2024
MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA ANGOLA WAANZA ZANZIBAR
Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola umeanza tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar.
Mkutano huo unafanyika katika ngazi mbili za maafisa waandamizi unaofanyika tarehe 14 — 15 Januari 2024 na ngazi ya mawaziri utafanyika tarehe 16 Januari 2024.
Mkutano huo unalenga kujadili mambo mbalimbali muhimu ya ushirikiano ya siasa, diplomasia, ulinzi, usalama, Sheria, kilimo, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji.
Maeneo mengine ni pamoja na maendeleo ya miundombinu, ujenzi, uchukuzi, nishati, madini, tehama na huduma za kijamii za afya, elimu, sayansi, na teknolojia ya Habari na mawasiliano. Mkutano huo pia unalenga kuibua maeneo mapya ya ushikiano ili kuchagiza maendeleo kati ya Tanzania na Angola.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa amebainisha kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo uchumi hususan biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, miundombinu na fedha.
“Katika mkutano wetu tunategemea kujadili masuala ya uchumi hususan msingi wa diplomasia ya uchumi. Mkutano huu utatoa mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili,” Alisema Balozi Mussa.
Balozi Said aliongeza kuwa mkutano huo unajenga na kuendeleza misingi madhubuti ya mashirikiano katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Angola unaendelea kuimarika zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias amesema mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano itaendelea kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya ushirikiano katika nyanja za diplomasia, usalama, ulinzi na uboreshaji wa huduma za kijamii,” alisema Balozi Sardinha Dias.
Mkutano huu umejumuisha Mabalozi, Watendaji Wakuu na Maafisa mbalimbali wa Serikali kutoka Tanzania na Angola.
Mkutano wa kwanza ulifanyika mwezi Oktoba, 1988 Jijini Dar es Salaam. Kufanyika kwa mkutano huu wa Pili kunafuatia kusainiwa kwa Hati mbili za Makubaliano (MoUs) za kuhuisha/kufufua Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola mwezi Februari 2023 Addis Ababa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar |
Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias akizungumza katika Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar |
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar |
Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye kamba ya njano shingoni) , Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto) pamoja na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Sandro de Oliveira (wa kwanza kulia). |
Viongozi wa Meza kuu katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola tarehe 14 Januari 2024 Zanzibar |