Tuesday, January 23, 2024

TANZANIA YANADI SEKTA YA UCHUMI WA BULUU KWA CHINA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuwekeza katika Sekta ya Uchumi wa Buluu na sekta nyingine za kimkakati.

Waziri Mkuu ametoa mwaliko huo alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Tanzania ina rasilimali za kutosha ambazo wawekezaji kutoka China wanaweza kuja kuwekeza kwa manufaa ya pande zote mbili kiuchumi hususan katika sekta ya uchumi wa buluu. 

“Kupitia uhusiano uliopo  nchi hizo mbili, Tanzania imedhamiria kuongeza thamani ya mazao ya biashara ili kuiwezeesha kuhimili ushindani katika soko la kikanda na kimataifa,” Alisema Mhe. Majaliwa

Wakati huohuo, Mhe. Majaliwa ameishukuru China kwa kuiondolea Tanzania ushuru katika mazao ya kilimo ambayo ni maharage ya soya, mihogo, parachichi na pia ameiomba China kuangalia uwekezano wa kuongeza mazao mengine ya biashara katika utaratibu huo mfano asali, mahindi ya njano na Maharage mabichi (Green Beans).

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong amesema Tanzania ni rafiki wa China kwa miaka takribani 60 hivyo, China itaendelea kuwekeza zaidi Tanzania katika sekta mbalimbali za kimkakati.

“China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha kuwa mazao ya biashara yanaingia katika masoko yake,” alisema Guozhong.

Kuhusu uchumi wa buluu, kiongozi huyo ameahidi kuwa atawaeleza wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China juu ya fursa zinazopatikana katika ukanda wa pwani na furza za kuwekeza kwenye sekta ya uchumi wa buluu.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde (Mb) pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania na China.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko



Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong akifuatilia mazungumzo ya kikao baina yake na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akifuatilia mazungumzo ya kikao chake na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk 

Mazungumzo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong yakiendelea 

Mazungumzo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong 


Mazungumzo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Dotto Biteko (Mb.) katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali 


WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE WA INDONESIA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akipeana mkono na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury jijini Jakarta wakati Waziri Makamba alipotembelea Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia jijini Jakarta, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba katika picha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury jijini Jakarta wakati Waziri Makamba alipotembelea Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na ujumbe wake (kulia) katika kikao na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury na ujmbe wake (kushoto) jijini Jakarta wakati Waziri Makamba alipotembelea Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amekutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Pahala Mansury jijini Jakarta, ikiwa ni hatua za mwisho za maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika kuanzia tarehe 24-26 Januari, 2024 nchini humo.



Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejiridhisha na maandalizi yanayoendelea ikiwemo ukamilishwaji wa hati saba za ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali zinazotarajiwa kusainiwa wakati wa ziara hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Waziri Makamba amesema ziara hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Ameongeza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia katika maeneo ya kımkakati ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, uchumi wa buluu na kilimo.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Mhe. Siregar amesema Indonesia iko tayari kumpokea Mhe. Rais Samia nchini mwao na kusisitiza kuwa Indonesia inathamini uhusiano wake na Tanzania na itaendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele na Mkurugenzi wa Afrika Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia

Tanzania na Indonesia zimekua na uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu tangu miaka ya 60, ambapo uhusiano ulijikita kwenye masuala ya ushirikiano baina ya nchi za Asia na Afrika ulioasisiwa na Mkutano wa Bandung mwaka 1955.

Kwenye awamu ya sita ya uongozi wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameimarisha zaidi uhusiano huu kwa kuelekeza nguvu zaidi kwenye kuongeza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.

Tanzania inaitazama Indonesia kama nchi rafiki wa muda mrefu , lakini pia kama lango la kufungua fursa nyingi zaidi za kibiashara baina yake na nchi za eneo la ukanda wa Kusini Mashariki mwa bara la Asia.

Mhe. Rais Samia anatarajiwa kuwasili kwa ziara hiyo ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 Januari 2024.

Monday, January 22, 2024

NAIBU WAZIRI MKUU WA CHINA MHE. LIU ATEMBELEA JKCI

 

Naibu Waziri Mkuu wa China, Mhe. Liu Guozhong ametembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) leo tarehe 21 Januari 2024 na kupokelewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel. 

Akiwa katika Taasisi hiyo, Mhe. Liu alipokea taarifa ya utendaji kazi iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge pamoja na kutembelea chumba cha upasuaji mdogo na mkubwa wa moyo na chumba cha wagonjwa mahututi wa moyo. 

JKCI imejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China kuanzia mwaka 2006 na kukamilika mwaka 2014 kwa ajili ya kutoa matibabu ya moyo nchini.

Taasisi ya JKCI inashirikiana na Taasisi za afya za China katika maeneo ya kubadilishana ujuzi na utaalam, utafiti, vifaa tiba na huduma za upasuaji wa moyo.


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Gouzhong akipokelewa na Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel baada ya kuwasili katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete-JKCI tarehe 22 Januari 2024 jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Gouzhong (wa pili kushoto) akisikiliza taarifa ya utendaji kazi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete-JKCI (wa pili kulia), Dkt. Peter Kisenge alipotembelea taasisi hiyo tarehe 22 Januari 2024 jijini Dar es Salaam. 


Mhe. Liu akieleza jambo wakati wa ziara hiyo.

Ziara ikiendelea.

Picha ya pamoja, Mhe. Liu (wa tano kutoka kulia), Mhe. Dkt. Mollel (wa sita kutoka kulia), Dkt. Kisenge na ujumbe kutoka Serikali ya China na  wafanyakazi wa Taasisi ya JKCI


NAIBU WAZIRI MKUU WA CHINA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Gozhong, amewasili nchini kwa ziara ya siku tatu (3) kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024 na kupokelewa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri waNishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.)

Ziara hii inafanyika ikiwa ni jitihada za makusudi kati ya Tanzania na China katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidugu ulioasisiwa na kujengwa na waasisi wa mataifa hayo mawili mwaka 1964; Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong wa China na kuimarishwa na awamu zote za uongozi zilizofuatia katika mataifa hayo mawili.

Pamoja na mambo mengine, akiwa nchini Mhe. Liu atatembelea; Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI ), Makumbusho ya Taifa, Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kadhalika atatembelea eneo la makaburi ya wataalamu wakichina waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Liu Guozhong akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Doto Biteko alipowasili kwenye  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Liu Guozhong akisalimia wadau mbalimbali waliofika kumpokea mara baada ya kuwasili nchini kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari, 2024


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China,  Mhe. Liu Guozhong akiwa ameambatana na naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko mara baada ya kuwasili nchini kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari, 2024.
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Liu Guozhong akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza zaia ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024. Aliyesimama kulia kwa Mhe. Balozi Mbarouk ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Liu Guozhong akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Samwel Shelukindo alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Liu Guozhong akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari, 2024.

Mmoja wa Wajumbe walioongozana na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Liu Guozhong akichukua matukio wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo nchini.



 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk (kulia) akiwa na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (wa pili kulia) akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar (wa tatu kulia)  na wajumbe wengine kutoka Ubalozi wa China nchini wakati wa mapokezi ya Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Lio Guozhong ambaye amewasili nnchini kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Januari 2024.


Sunday, January 21, 2024

TANZANIA, OMAN KUIMARISHA UTAMADUNI NA KUMBUKUMBU

Tanzania na Oman zimekubaliana kuimarisha sekta ya utalii kupitia utamaduni na kumbukumbu za mambo ya kale ili kuongeza utalii na kukuza uchumi wa mataifa hayo mawili kwa maslahi ya pande zote mbili.

Makubaliano hayo yameafikiwa na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Urithi wa Mambo ya Kale na Utalii wa Oman, Mhe. Salim Mohammed Al Mahrouq kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Oman katika ukumbi wa Wizara hiyo. 
 
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadiliana na kukubaliana kuongeza fursa na ushirikiano katika nyanja za mafunzo na uzoefu kwa wataalam wa pande zote mbili. Adha, katika Utekelezaji wa mambo hayo, viongozi na wataalam wa Tanzania na Oman watakutana hivi karibuni kupanga mikakati ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano.

Mazungumzo hayo ni hatua ya utekelezaji wa Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab ya kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akizungumza na Waziri wa Urithi wa Mambo ya Kale na Utalii wa Oman, Mhe. Salim Mohammed Al Mahrouq kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Oman katika ukumbi wa Wizara hiyo



DIPLOMASIA YA TANZANIA YAZIDI KUNG’ARA KIMATAIFA

Diplomasia ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa kufuatia viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam. 

Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema  tarehe 22 Januari 2024 atawasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini tarehe 22 - 24 Januari , 2024.

“Mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.),” alisema Waziri Makamba. 

Amesema Kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 – 25 Januari, 2024. Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba. 

Waziri Makamba, amesema Mheshimiwa Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson.

Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.

Kiongozi mwingine anayetarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda  atakayewasili nchini kwa ziara ya kikazi tarahe 8 – 9 Februari 2024. 

Akiwa nchini, Mheshimiwa Duda atakutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland.

Amesema Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji,  usimamizi wa mazingira, utalii, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.

Aidha, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Mbali na viongozi wakuu wa mataifa tajwa kufanya ziara nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 – 26 Januari 2024, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo. Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Agosti 2023. 

“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” aliongeza Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba amewaeleza waandishi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia pia kufanya Ziara ya Kitaifa Vatican tarehe 11 – 12 Februari, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis.

Waziri Makamba ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Mhe. Pietro Parolin. Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini. 

Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya. Kwenye ziara hiyo Mhe. Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo. 

Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway, tarehe 13-14 Februari 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja. Ameongeza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Mfalme Herald. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kongamano la Nishati la Oslo,” alisema Waziri Makamba

Tanzania na Norway zinashirikiana kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.

Kuanzia mwaka 2010, Serikali ya Norway imekua ikishirikiana na Tanzania kwenye programu mbalimbali za maendeleo zilizo gharimu takribani TZS. 300 bilioni. Programu hizo zimesaidia na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Nishati; Sekta ya Elimu; Sekta ya Mafuta na Gesi; Mpango wa Usimamizi wa Fedha za Umma; programu za Mabadiliko ya Tabianchi; na programu za Usimamizi wa Misitu.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaandika historia kupitia ziara hii nchini humo kwani mara ya mwisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa Ziara ya Kitaifa ilikua mwaka 1976.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo vya Wizara.



Saturday, January 20, 2024

VITU LAZIMA VITOKEE, WAZIRI MAKAMBA

“Vitu lazima vitokee", ni msemo ambao ameutumia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) alipokutana na Mawaziri wenzake jijini Kampala, Uganda pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na Mkutano wa Kundi la Nchi 77+China tarehe 15 hadi 22 Januari 2024.

Waziri Makamba ambaye alishiriki kwa siku tatu katika Mikutano hiyo alikutana na Mawaziri 17 kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi hizo na kuweka mikakati ya kushirikiana kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.

Waziri Makamba aliifanya Mikutano hiyo ambayo imekusanya takriban theluthi mbili ya nchi zote duniani kama fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kidiplomasia na kujadili mikakati na nyenzo za kujiletea maendeleo na kutatua changamoto zinazoikabili dunia.

Mawaziri wa Mambo ya Nje waliokutana na Mhe. Makamba wanatoka nchi za Kenya, Msumbiji, Somalia, Malawi, Misri, Ghana, Morocco, Filipino, Ethiopia, Singapore, Vietnam, Cuba, Iraq, Bahamas, Venezuela, Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo na Azerbaijan.

Masuala muhimu ambayo Waziri Makamba ameyasisitiza kwa mawaziri wenzake ni kutumia nyezo za kawaida za kidiplomasia kukuza ushirikiano baina ya mataifa yao. Nyenzo hizo ni pamoja na Midahalo ya Kisiasa, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs), Mikutano ya Majukwaa ya Kiuchumi, Tume za Pamoja za Mawaziri (JMCs) na ziara za viongozi wa kitaifa.

Mhe. Makamba amesema kuwa endapo vyombo hivyo vitatumika ipasavyo vitatoa fursa kwa pande husika kukuza biashara, uwekezaji, utalii pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa masuala ambayo pande husika zimekubaliana.

Wakati wa mazungumzo na Mawaziri wa nchi za Singapore, Vietnam na Filipino, Mhe. Makamba alisema nchi hizo ni mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea duniani kutokana na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi kifupi.

Alikubaliana na mawaziri wa nchi hizo kushirikiana katika mafunzo, hususan, kueendeleza rasilimali watu, utalii na kilimo.

Jambo lingine lililojitokeza ni ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu na usafiri wa anga wa moja kwa moja baina ya mataifa. Waheshimiwa Mawaziri walijiridhisha bila shaka kuwa ukosefu wa miundombinu unakwamisha ufanyaji wa biashara na kuongeza gharama katika uzalishaji, hivyo wamesisitiza kutumia rasilimali za nchi zao kujiletea maendeleo.   

Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu kwa njia za kidiplomasia panapotokea migogoro ya kisiasa na aliwahakikishia viongozi wenzake kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani duniani.

Waziri Makamba katika kusimamia msemo wake wa “Vitu lazima vitokee" alikubaliana na viongozi wenzake kufufua makubaliano ya ushirikiano waliyojiwekea ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kunzisha ushirikiano rasmi na nchi ambazo Tanzania haina mikataba rasmi ya ushirikiano.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf. Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) uliofanyika Kampala, Uganda tarehe 15 hadi 20 Januari 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Mhe. Veronica Macamo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. . Dkt. Mohamad Maliki Bin Osman
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Eduardo Rodriguez Parrilla

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam, Mhe. Do Hung Viet

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Shoukry
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Musalia Mudavadi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Christophe Lutundula
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Simalia, Mhe.  Ali Mohammed Omar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Uhamiaji na Bima ya Taifa wa Bahamas, Mhe. Alfred Sears.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Aberzaijan, Mhe.  Jeyhun Bayra.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Mesganu Moach.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mhe. Nasser Bourita
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Philipino, Mhe. Enrique A. Manalo,

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb), akibadilishana mawasiliano na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Mhe. Omer Ahmed Berzinji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Nancy Tembo



Thursday, January 18, 2024

BALOZI NAIMI AZIZI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO UNIDO


Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Austria, Mheshimiwa Naimi Aziz amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Mhe. Gerd Müller, tarehe 18 Januari, 2024. Katika mazungumzo yao, wamekubaliana kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNIDO hususan katika maendeleo ya viwanda.


Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  Austria, Mhe. Naimi Aziz akiwa kwenye picha ya pamoja na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Mhe. Gerd Müller.


Tuesday, January 16, 2024

TANZANIA, ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO KUONGEZA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoleana visa kwa wenye hati/pasi za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika leo Zanzibar.

Waziri Makamba amesaini hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi. Aidha, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesaini hati ya ushirikiano katika sekta ya afya

Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo, Waziri Makamba alisema Tanzania na Angola zina uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na viongozi wakuu wa Kitaifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Agostinho Neto walianzisha uhusiano huo kwa matarajio yao kuwa uhusiano huo utoe manufaa kwa nchi zote mbili.

“Leo kupitia mkutano wetu tumesaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola. Hati hizo ni pamoja na hati ya makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, Hati ya makubaliano ya kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya,” alisema Waziri Makamba.

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa kisiasa, ulinzi, elimu, afya, mafuta na gesi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, kubadilishana visa, kusafiri bila visa kati ya nchi zetu mbili na hatimaye tumeingia makubaliano ya ushirikiano.

Kuadhalika, viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali husasan uwepo wa ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya Kongamano la bishara na uwekezaji na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja walizokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupitia makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tuahidi kuyatekeleza yale yote tuliyokubaliana katika mkutano wetu ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi António. 

Aidha, kuhusu kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya kongamano la biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wananchi wetu kubadilisha uzoefu na kuendelea kukuza sekta binafsi kwa mataifa yote mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi leo Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakionesha Hati za Makubaliano ya Ushirikiano baada ya kuzisaini leo Zanzibar

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakifuatilia mkutano

Meza Kuu katika Picha ya pamoja, katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António. Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (wa pili kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye Kamba ya njano shingoni) na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Mhe. Sandro de Oliveira.